Jumatano, Desemba 04, 2013

ENDELEA KUPATA UHONDO, SIMULIZI YA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

KITABU-MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI-DADA YANGU
MTUNZI-ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA
Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa lakini baadaye ilipokelewa.
“He! We Eliza mbona umechelewa kupokea simu?” Aliuliza Upendo.
“Mh dada samahani nilikuwa bafuni, ehe niambie.” Alijibu Eliza.
“Ndugu yangu natamani ungekuja huku unisaidie katika mipango ya
harusi yangu vipi mnafunga lini chuo?” Aliuliza Upendo.
“Makubwa! Kweli mapenzi yamepamba moto ndio unaolewa na huyo
shemeji hata simjui jamani?” Alihamaki Eliza. ITAENDELEA

INAPOENDELEA
“Wewe nawe! Utakuja kumwona siku ikifika. Kwanza yupo huko Arusha
lakini ametingwa sana sijui kama mtaweza kuonana.” Alisema Upendo.
“Hee! Jamani kweli shemeji yangu yupo huku halafu huniambii? Vibaya
hivyo dada yangu, sasa kuhusiana na mimi kuja huko kukusaidia hiyo
mipango yako ya harusi kwa sasa itakuwa vigumu kwani najiandaa na
mitihani itakayoanza mwezi ujao.” Alijibu Eliza.

“Jamani Eliza mwenzio natamani ungekuwepo ila hakuna tatizo kwani
masomo nayo ni muhimu. Mh mdogo wangu hebu niambie sijapata
shemeji mmasai huko?” Aliuliza Upendo huku akicheka.
“Mmh! mwenzangu nimepata mchumba nampenda sana, mambo yakiwa
sawa nitakufahamisha.” Alijibu Eliza.
Basi waliendelea kuzungumza na baadaye kila mmoja aliendelea na
mambo yake.

James kipindi chote akiwa Arusha alikuwa akimsaliti Upendo na kustarehe
na Esta. Baada ya siku kadhaa kupita hatimaye siku za James kurudi Dar
es Salaam zilikaribia. Esta alimfuata James hotelini ili kuzungumza naye
kuhusiana na hatma ya uhusiano wao watakapokuwa mbali.
“Juliasi karibu utaondoka kwenda Dar hivi kweli utanikumbuka? Na jinsi
warembo walivyo wengi huko Dar?” Aliuliza Esta huku akimpapasa uso
James.


“Hapana siwezi kukuacha mpenzi wangu tutawasiliana usijali. Arusha
nitakuja hata wewe utakuwa unakuja Dar es Salaam.” Alijibu James huku
akimbusu Esta katika shavu la upande wa kushoto.
“Sawa hakuna tatizo mimi naomba tuendelee kuwasiliana nakupenda sana
mpenzi wangu.” Alijibu Esta huku akiwa amemkumbatia na kumbusu
James.
******************
Huko Dar es Salaam Upendo alikuwa anaandaa mapokezi ya kumpokea
mchumba wake James ambaye walikuwa hawajaonana yapata miezi minne.
Alifanya usafi wa mazingira ya nyumba na kubadilisha baadhi ya vitu ili
kuonekane tofauti. Alikuwa na furaha sana siku hiyo ambapo kesho yake
James ndiyo alikuwa akirud.i Alinunua maua mazuri ya rangi nyekundu
pamoja na mvinyo.
Kesho yake James alirudi, Upendo alikwenda kumpokea uwanja wa ndege
yapata saa moja jioni. James alishuka kwenye ndege na kuelekea sehemu
za mapokezi na kumkuta Upendo aliyempokea kwa furaha sana.
Darling (mpenzi) umependeza sana, umezidi kuwa mweupe, nimefurahi
sana kuwa nawe tena” Aliongea James huku akiwa amemkumbatia
Upendo.
“Yaani James nimefurahi sana umerudi nilikuwa mpweke sana.” Alijibu
Upendo huku akimpokea James begi.
Walielekea Kinondoni nyumbani kwa James. James alishangaa sana kuona
mabadiliko ya nyumba yake na jinsi ambavyo Upendo alikuwa amepamba.
“Mpenzi unafaa sana katika mambo ya upambaji nyumba imekuwa tofauti
kabisa nimefurahi kweli wewe ni mke mzuri.” Aliongea James kwa furaha
huku akikaa kwenye sofa.
“Asante mpenzi wangu nenda ukaoge uje tule chakula halafu unipe habari
za Arusha.” Upendo alimsihi James. Usiku ule ulikuwa ni usiku wa furaha
kwa wote wawili walikula na kunywa na kulala huku wakiwa na mikakati
ya kufunga ndoa haraka.

Hatimaye maandalizi ya kumuaga Upendo yalikamilika na wakati huo
wazazi wa James walikuwa wakiandaa harusi. Mawasilianao ya Esta na
James yalipungua sana. Kila Esta akimpigia simu alikuwa akimdanganya
kuwa ametingwa sana, kitu ambacho kilikuwa kikimuumiza sana Esta.
Hata hivvyo Esta aliendelea kujipa moyo kuwa Juliasi anampenda bila
kujua kuwa alikuwa ni tapeli wa mapenzi. Baada ya miezi miwili kupita
Esta aliugua homa na kwenda hospitali ambapo alipimwa na kukutwa
akiwa na ujauzito wa miezi miwili. Kutokana na hali hiyo Esta
alichanganyikiwa sana.

“Mungu wangu nina mimba ya Juliasi nitafanyaje mimi na huyu
mwanamume sijui ana mpango gani na mimi. Nafikiria kuitoa mimba
lakini naogopa sana. Hapana lazima nimfahamishe hali halisi kwa sababu
sijui nifanyeje. Kwani nyumbani baba akijua ataniua na ndugu zangu
watanifikiriaje, nikifika chuo ni lazima nimpigie simu leo.” Aliwaza Esta
huku machozi yakimlengalenga.

Esta aliondoka pale hospitali akiwa na mawazo mengi sana. Alipofika
chuoni aliingia chumbani kwake na kupiga simu. Simu iliita muda mrefu
bila kupokelewa. Aliendelea kupiga kama mara mbili bila mafanikio hadi
alipojaribu tena ndipo simu ilipokelewa na James aliyekuwa kazini kwake
muda huo.
“Haloo vipi Juliasi mbona nakupigia simu yangu hupokei?” Auliza Esta.
“We mwanamke mjinga kweli inamaana niache kazi zangu nipokee simu
yako? Je, hujui kwamba huu ni muda wa kazi? Je, unasemaje?” Aliuliza
James kwa sauti iliyojaa hasira .

“Samahani mpenzi kwa usumbufu nimekupigia nikwambie leo
nimekwenda hospitali kupima nina mimba yako ya miezi miwili.” Esta
alimfahamisha James. “Hee! Nini? Mimba! Ya nani!” Alihamaki James
huku akionyesha kama mtu aliyekanganyikiwa.
“Kweli Juliasi unaweza kuniuliza kuhusu mimba hali unajua ni yako?
Halafu unaniuliza ya nani?” Aliuliza Esta huku amebana pua kumuigiza
James.
“Sikiliza nikwambie Esta, mimi sina mpango wa kuwa na mtoto sasa hivi,
kama wewe ulitaka mtoto ni juu yako ninachoweza kukusaidia ni pesa ya
kutoa hiyo mamba.” Alisema James kwa sauti ya kutetema tofauti na siku
nyingine.
Esta hakuamini maneno anayoambiwa na James”

“Sikujua kama utanifanyia hivi Juliasi, unajua ni kiasi gani nakupenda,
nashukuru sana ila hii mimba sitaitoa na huyu mtoto ni wako na nitamleta
huko huko Dar es Salaam.” Kisha akakata simu na kulia kwa uchungu
huku akijilaumu moyoni mwake na kujipa matumaini”
“Nilijua Juliasi ni mwanaume mkweli kumbe yuko hivi au kwa sababu ya
hii mimba imekuja ghafla, sijui nifanyeje naamini mambo yatakwenda
sawa, ngoja nimwache kwanza kwa sasa.” Alijipa moyo Esta.
Esta aliendelea kuwaza sana na baadaye akamua kuendelea na shughuli
zake za kawaida. James naye alibaki akiwaza moyoni mwake.

“Hivi nimefanya nini mimi huyu msichana ana mimba yangu na hataki
kuitoa na mimi nafunga ndoa hivi karibuni. Sijui itakuwaje ila ngoja
nimwache siwezi kumpoteza Upendo nampenda sana na ndio mke
wangu, sitaki mawasiliano na huyu mwanamke tena.”
Basi naye aliendelea na mambo yake huku akiwa anajiandaa na harusi
yake. Wakati huo Upendo alipanga safari ya kwenda Morogoro kwani
ilikuwa imebaki kama mwezi mmoja afanyiwe sherehe ya kuagwa na

wazazi wake.ITAENDELEA. WADAU MNIWIE RADHI MAJUKUMU KIDOGO NDIYO MAANA SIMULIZI IMECHELEWA, KUHUSU BADO MIMI NA KOSA LANGU NI LIPI MSIHOFU, KILA KITU KIPO SAWA. ASANTENI KWA KUWA NAMI WAKATI WOTE. 

Maoni 1 :

SUFI JR alisema ...

Hakika simulizi iko kwa msimuliaji, Hadithi nzuri sasa dada

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom