Jumanne, Januari 28, 2014

SIMULIZI FUPI "WIFI MTATA"


Alipomaliza chuo tu Justa aliolewa na Mfaume kijana huyu alikuwa ni mfanyabiashara,  ambaye alikuwa akimpenda sana Justa. Mfaume alikuwa akiishi na mdogo wake wa kike aliyekuwa anaitwa Leti kwa kipindi hicho Leti alikuwa bado anasoma chuo. Baada ya Justa kuolewa sasa alihamia na kuishi pamoja na mume na wifi yake, maisha yalikuwa mazuri kwani Mfaume alikuwa anampenda sana mke wake. Kwa kipindi hicho Justa alikuwa bado hajafanikiwa kupata kazi hivyo alikuwa ni Mama wa nyumbani huku akiwa anaendelea kutafuta kazi. 

Siku zote Mfaume alikuwa akiacha pesa za matumizi pale nyumbani na  alikuwa akimpa mdogo wake pesa hizo yaani hata pale mke wake alipokuwa na shida ilimbidi amweleze wifi yake kwani mume wake alikuwa akimpatia pesa zote za matumizi ya pale nyumbani mdogo wake.Hali ile ilikuwa inamuumza sana Justa na ndipo alipoamua kumwambia mume wake kuwa hapendezewi na tabia yake  lakini mwanaume huyo hakutaka kumsikiliza. Siku zilivyozidi kwenda Justa alikuwa anakosa amani kabisa katika nyumba yake kwani alikuwa hana uhuru wowote kutokana na kila kitu alikuwa akipewa wifi yake. 


Kutokana na kuchoka na hali hiyo siku moja Justa aliamua kumweleza ukweli wifi yake na hapo ndipo matatizo yalianza kwani Leti alianza kumchukia Justa na wakati mwingine alikuwa akimtukana "Wewe mwanamke umekuja hapa kwa kaka yangu kula vya bure, yaani unatia kichefuchefu, kazi yako kula tu. kila siku unataka hela nenda katafute kazi upate na wewe hela zako" Alikuwa anaongea Leti huku akibidua midomo yake. Justa alinyamaza kimya lakini kadiri siku zilivyokuwa zinaenda aliona maisha yanzidi kuwa magumu kwani Mfaume alikuwa akimtetea mdogo wake kwa kila jambo na Leti alizidisha  dharau.

 Baadaye Justa aliamua kuwashirikisha wazazi ambao waliamua kuwaweka kikao ndipo mfaume aliomba radhi mbele ya wazazi wa pande zote mbili huku Leti akionekana kukasirika baada ya Baba yake mzazi kumtaka aondoke kwenye nyumba ya kaka yake na sasa alirudi nyumbani na kumuacha Justa akiishi kwa furaha na amani na mume wake.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom