Jumatatu, Januari 27, 2014

KUELEKEA BUNGE LA KATIBA HAYA NI MASUALA MUHIMU YA WANAWAKE YA KUZINGATIA KATIKA KATIBA MPYA

Haki za wanawake kubainishwa kwenye katiba mpya:Haki za msingi za wanawake ziendelee kubainishwa zaidi katika tamko la msingi wa Haki za Binadamu, ili wanawake waendelee kupata haki sawa za uraia, siasa uchumi na ustawi wa jamii zinazolindwa kikatiba.

Sheria Kandamizi zibatilishwe:Katiba mpya iendelee kubatilisha sheria zote za ubaguzi wa jinsia, ikiwa ni pamoja na kukataza mwendelezo wa tabia, taratibu za mila zenye kubagua na kudhalilisha wanawake na watoto wa kike chini ya mfumo dume unaotawala jamii zetu.

Utu wa wanawake ulindwe:Katiba mpya iendeleze misingi inayolinda utu wa mwanamke, ikiwa ni pamoja na kulinda wanawake dhidi ya vitendo vya kikatili dhidi yao kama ukatili wa kijinsia ukiwemo ubakaji ndani na nje ya ndoa, unyanyasaji wa kisaikolojia, ukeketaji, ndoa za utotoni na vitendo vingine vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.


Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu haki za Wanawake: Katiba mpya iwajibishe serikali kutekeleza mikataba yote ya kimataifa iliyoridhia kuhusu haki za wanawake.

Haki sawa katika nafasi ya uongozi:Katiba mpya ibainishe  misingi itakayozuia kuhodhiwa kwa madaraka katika mihimili mikuu ya utawala kwa jinsi moja kwa mfano:Taasisi ya Urais, Makamu,Waziri Mkuu, Mwanasheria mkuu, Spika na Naibu Spika, wakuu wa mikoa, Manispaa na umma, na viongozi mpaka ngazi ya chini kabisa. Hivyo Basi uwepo uwiano wa kijinsia (50/50%) na ujenwe katika ngazi zote za uongozi na maamuzi na siyo kwenye nyanja za siasa tu.

Haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na kumiliki Rasilimali ya Nchi. Kwa kuzingatia kwamba rasilimali ya nchi yetu ni ya mtanzania  kama madini, ardhi na vitu vyote vilivyoko nchi kavu na majini katiba mpya iweke bayana wanawake wa kitanzania wana haki sawa za kufikia kumiliki na kufaidika na rasilimali za nchi yetu.

Haki ya Uzazi Salama: Katiba mpya ihakikishe kuwa afya ya uzazi na uzazi salama kwa kila mwanamke inalindwa kikatiba, serikali iwajibishwe kuwekeza katika afya ya uzazi kwa ujumla, pamoja na uzazi wa mpango ili kumpunguzia mwanamke mzigo  mkubwa anaobeba katika kuendeleza kizazi cha Tanzania. Katika kutimiza jukumu la uzazi katika jamii wanawake hukumbana na changamoto nyingi zinazotishia haki yao ya msingi ya kuishi.

Haki ya wanawake wenye Ulemavu:Katiba mpya iainishe haki za wanawake wenye ulemavu kwa kutambua kwamba kundi hili huathirika  mara dufu na mfumo dume. Katiba mpya iwajibishe serikali  kuchukua hatua  za kisera  na kisheria ili kulinda wanawake wenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili na kufikia huduma za msingi za kukimu  maisha kama vile huduma za afya, elimu, hifadhi ya jamii na fursa sawa katika ajira

Haki za watoto wa kike:Katiba mpya iweke msingi utakaolinda haki za mtoto  wa kike katika kufikia na kufaidi huduma za jamii ikiwa ni pamoja na elimu yenye kuwawezesha kudai na kulinda haki zao. Kumlinda mtoto wa kike juu ya ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni

Tume ya Haki za Wanawake: Katiba mpya iunde chombo maalumu  kitakachowajibisha  serikali na taasisi mbali mbali nchini katika kutekeleza  haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii kisiasa na kiuchumi.

Mahakama ya Kifamilia:Katiba mpya iainishe bayana uundwaji wa mahakam ya kifamilia itakayokuwa na jukumu la kuendesha  na kuratibu kesi zote   zenye mashauri ya msingi ya kifamilia.Mahakama hii itasaidia  kuleta ufanisi  na kurahisiha  upatikanaji wa haki za mwanafamilia. Hasa wale wanyonge wakiwemo wanawake.

Mtandao wa wanawake na katiba Tanzania unahusisha mashirika yanayotetea Haki za Wanawake na Binadamu.  moojawapo ni Women Fund Tanzania WFT, Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) nk.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom