Ijumaa, Desemba 27, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA "DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

ILIPOISHIA
 “Hivi nimefanya nini mimi huyu msichana ana mimba yangu na hataki
kuitoa na mimi nafunga ndoa hivi karibuni. Sijui itakuwaje ila ngoja
nimwache siwezi kumpoteza Upendo nampenda sana na ndio mke
wangu, sitaki mawasiliano na huyu mwanamke tena.”
Basi naye aliendelea na mambo yake huku akiwa anajiandaa na harusi
yake. Wakati huo Upendo alipanga safari ya kwenda Morogoro kwani
ilikuwa imebaki kama mwezi mmoja afanyiwe sherehe ya kuagwa na
wazazi wake

INAPOENDELEA

Baada ya wiki kadhaa kupita mawasiliano kati ya James na Esta yalikwisha
kwani kila Esta alipojaribu kupiga simu James alikuwa hapokei. Na
ikitokea amepokea alimtaka asiendelee kumpigia simu tena. Upendo
aliondoka na kwenda Morogoro kwa ajili ya kuandaa sherehe. Akiwa
Morogoro mdogo wake alikuwa bado yupo chuoni, hivyo wazazi wake
walimpigia simu na kumwambia ni lazima awepo kwenye sherehe ya dada
yake.

Zikiwa zimebaki kama wiki mbili kufanyika sherehe ya kumuaga Upendo,
Eliza alirudi Morogoro kwa wazazi wake ili kusherekea pamoja na dada
yake. Siku Eliza alipofika, wazazi wake hawakuwepo ila Upendo pekee.
Upendo alipomwona mdogo wake alifurahi sana, alimpokea begi wote
wakaingia ndani.

“Jamani hatujaonana siku nyingi sana my young sister (mdogo wangu)
mbona umenenepa hivyo ulikuwa unasoma kweli wewe?” Alisema
Upendo.
Eliza alimwangalia sana dada yake:
“Dada Upendo kuna kitu nataka nikwambie, ila iwe siri yako sitaki mama
wala baba wafahamu hili.“ Aliongea Eliza kwa kusihi.

Upendo alishtuka na kuwaza moyoni mwake: “Je, atakuwa ana tatizo
gani?”Aliwaza Upendo. Hebu niambie tafadhali.
“Upendo mwenzio nina mimba hapa nilipo ndio maana unaniona
nimenenepa.” Alianza kueleza Eliza.
“Acha utani wako wewe una mimba ya nani.” Upendo alihoji kwa
mshangao.

“Nina mimba ya kijana mmoja anaitwa Juliasi sijui hata nitampatia wapi
najua anakaa Dar es Salaam, lakini sijui nitaanzia wapi kumpata.” Alisema
Eliza huku akiwa ameinama.
“Inamaana wewe umepata mimba ya mtu ambaye hata ha umjui vizuri,
kweli mdogo wangu umechezea maisha yako.” Aliongea Upendo kwa
kejeli.
Eliza machozi yakiwa yanamtoka,
“Nisaidie dada yangu mimi sijui nifanyeje hapa nilipo kwani hata
mwanamume mwenyewe nikimpigia simu hapokei na ameshakataa hii
mimba ameniambia niitoe na mimi siwezi kufanya hivyo”.
“Haiwezekani! Hiyo mimba usitoe kumbuka nilikuonya mdogo wangu
uwe makini na hawa wanaume. Wengi wao ni matapeli sasaa… ngoja,
tutajua cha kufanya kesho lakini usijali sana kwani tayari jambo limetokea,
kulia siyo sulihisho.” Aliendelea kumbembeleza na baadaye alimtaka
akaoge ajiandae kwani wazazi wao wangerudi muda huo.

Wazazi wao walikuwa wamekwenda kuwachukua ndugu wengine, lakini
walikuwa wanafahamu kuwa Eliza anakuja siku hiyo. Baada ya dakika
kadhaa kupita wakiwa wanaendelea na mazungumzo Baba na Mama yao
pamoja na ndugu wengine walifika. Upendo aliwakaribisha wageni, na
kuwaelekeza sehemu za kukaa.

“Karibuni sana, wengine wakae pale na wengine hapa, waswahili husema
sherehe ni watu’, na watu wenyewe ni ninyi, sisi na wengine watakao kuja.”
Upendo aliwaelekeza wageni. Baba Upendo (Mzee George) alimtuma
Upendo akamwite mdogo wake aje awasalimie wageni. Upendo aliinuka
haraka na kuelekea chumbani.
“Eliza unaitwa na baba ili ukawasalimie baba, mama na wageni.
Nakuomba uvae gauni kubwa ili wasielewe mabadilko uliyonayo, kwani
mimba uliyokuwa nayo imeanza kujionyesha.” Alishauri Upendo.
Eliza alijiandaa kama alivyoshauriwa na Upendo kisha wote wakaelekea
sebuleni. Alipofika aliwasalimia wazazi na shangazi yake na wageni
wengnie waliokuwepo

”Jamani ni wewe wajina wangu Esta umekuwa mkubwa hivi”. Shangazi
yake alishangaa kuona Eliza amekuwa mkubwa.
“Yaani dada, hilo jina la Esta mwenzio halitumii anatumia jina la Eliza,
wamekuwa wakubwa sana. Hata sisi hatujawaona siku nyingi. Huyu yupo
chuoni Arusha anaingia mwaka wa mwisho.“ Alifafanua Baba Upendo
huku akimwangalia shangazi yake Eliza na kucheka.
“Kweli siku zinakimbia na hilo jina la Esta ha ulitumii unapenda kuitwa
Eliza mama jamani watoto wa siku hizi.” Aliendelea kushangaa na kucheka
shangazi yake Eliza.
“Hapana shangazi, huwa nalitumia mara moja moja.” Alijibu Esta huku
akiinamisha kichwa chini kwa aibu.
“Lakini bora usilitumie kwani haya majina ya kurithi wakati mwingine sio
mazuri unaweza ukampa mtoto jina la mtu mwenye mikosi na mtoto
akajikuta anakuwa na mikosi katika maisha kwa sababu ya majina ya
kurithi.” Alisema shangazi yake huku watu wote wakiangua vicheko.
“Hakuna wifi hizo ni imani tu za watu.” Alijibu mama Upendo huku
akiinuka kuelekea jikoni.

“Haya jamani huku jikoni vipi?” Aliuliza mama Upendo.
“Tayari mama hakuna tatizo.” Alijibu Upendo.
Waliendelea na mazungumzo pale sebuleni na baadaye baada ya kupata
chakula cha usiku wote walikwenda kupumzika. Hatimaye siku ya sherehe
ilifika, sherehe, iliandaliwa pale nyumbani kwa kina Upendo. Kulikuwa na
uwanja mkubwa ambao ulipambwa vizuri sana. Ama kweli ilikuwa ni siku
ya furaha kwa Upendo.

Kwa upande wa mdogo wake Eliza mambo hayakuwa mazuri kwani muda
wote alikuwa akiwaza sana kuhusu Juliasi kwa nini hapokei simu yake.
“Eliza hii ni siku ya furaha ya maisha yangu naomba uwe na furaha
mdogo wangu. Halafu leo pia ni siku mwafaka kwa wewe kumwona
shemeji yako ambaye hujawahi kumwona, nadhani utampenda kwani
nampenda sana.” Upendo alimfariji mdogo wake huku akimpigapiga
mgongoni na kiganja cha mkono wake wa kulia.
“Nitafurahi sana kumfahamu shemeji yangu nadhani alikuwa akinisikia
tu.” Kwa tabasamu la upole Eliza alimjibu dada yake.“
“Ndiyo nilikuwa nikimsimulia sana kuhusu wewe mdogo wangu kwamba
upo chuoni kwa hivyo leo mtafahamiana au siyo mdogo wangu.” Alisema
Upendo.
“Asante nitashukuru sana kumwona shemeji, sijui atavaa suti, jinsi na
tisheti au atakuwa katika pamba za namna gani.” Aliongea Eliza huku
akitabasanu na kumwangalia dada yake Upendo.

Mipango iliendelea na hatimaye sherehe ilikaribia kuanza. James na wazazi
wake walitokea hotelini na kuelekea nyumbani kwa akina Upendo maeneo
ya Kihonda ambapo sherehe ilikuwa ikifanyika. Walipofika walipokelewa
kwa vigelegele na shangwe nyingi walipelekwa sehemu ya kukaa na
baadaye James alifichwa katika umati wa watu ili Upendo aje kumtafuta.
Upendo alitoka ndani huku matarumbeta yakipigwa na shangwe nyingi
zikitawala akiwa sambamba na mdogo wake Eliza.

Upendo akiwa sambasamba na Eliza alielekea sehemu ile kwenye umati
wa watu ambako James alifichwa ili akamfichue. James akiwa katikati ya
umati alimwona Upendo akiwa anatoka na pembeni akiwa na Esta
alishtuka sana kumwona Esta.
“Mungu wangu yule si Esta? Anafanya nini hapa na mbona yupo karibu
na Upendo? Kuna nini kinaendelea hapa?” James aliwaza na kujiuliza
maswali mengi yaliyokosa majibu. ITAENDELEA HADI MWISHO WAKE USIKOSE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom