Alhamisi, Oktoba 31, 2013

SIMULIZI INAYOITWA DADA YANGU KUTOKA KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA

KITABU- MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI- DADA YANGU
hii ni simulizi ya pili kutoka katika kitabu cha Malipo ni hapahapa baada ya simulizi ya kwanza.

Mapenzi ni kitu ambacho kina nafasi kubwa sana katika maisha
ya watu kote duniani. Mapenzi haya yanaweza kuleta furaha sana endapo
mtu atampata mtu sahihi ambaye atakuwa ni muwazi, mwenye mapenzi
ya kweli na kuheshimu uhusiano huo. Lakini mapenzi yanaweza kuleta
karaha au kukosa amani kabisa kama kutakuwa na migogoro ambayo
unakuta inasababishwa na kukosa uaminifu na kuleta ugomvi kati ya
wawili wapendanao. Mapenzi haya yanaweza yakasababisha ndugu
kugombana, marafiki kukosana na hata kuuana.
*****
Eliza na Upendo ni wasichana warembo waliozaliwa katika familia ya
kitajiri mkoani Morogoro. Wasichana hawa waliishi katika maisha ya
kifahari kutokana na Baba yao Mzee Bondi kuwa na uwezo mkubwa sana
kifedha. Mzee Bondi aliwapenda sana mabinti zake na alipenda wasome
kwa bidii ili baadaye waje kuwa na maisha bora. Eliza na Upendo walisoma
katika hali nzuri sana hadi kufikia elimu ya chuo, ambapo Upendo alikuwa
akisoma Chuo Kikuuu cha Dar es Salaam na Eliza Chuo cha Uhasibu
Arusha. Kutokana na masomo walitengana na kuonana mara chache
kipindi cha likizo.

Baadaye Eliza na Upendo walijikuta wakijiingiza katika uhusiano wa
kimapenzi wote wawili kwa kijana mmoja mtanashati aliyeitwa James bila
kujijua. Uhusiano wa kimapenzi kwa mwanamume mmoja ulileta
migogoro katika familia yao.
*********
Baada ya kumaliza Kidato cha Sita Upendo alipangiwa kwenda kuendelea
na masomo ya Chuo Mkoa wa Dar es Salaam. Baba yake alifurahi sana na
kumuahidi kuwa angempa zawadi nono kama angefanya vizuri akiwa
Chuo. Kabla ya kujiunga na chuo Upendo alifanyiwa sherehe kubwa ya
kumpongeza, ambayo ilihudhuriwa na watu wengi sana ndugu jamaa na
marafiki. Wakati huo mdogo wake Eliza alikuwa Kidato cha Sita kwani
walipishana mwaka mmoja tu na kwa jinsi walivyokuwa, walionekana
kama mapacha. Wakati mwingine ilikuwa ni vigumu kwa watu ambao
walikuwa hawajawaona kujua mkubwa ni yupi na mdogo ni yupi.
Siku zilipokaribia za kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Upendo
alijiandaa barabara kwa ajili ya kuanza masomo ya Chuo. Siku moja kabla
ya kuondoka Mama na Baba yake walimwita na kuzungumza naye
mazungumzo ili kumwasa na kumpa ushauri.


“Upendo tumeishi wote kutoka ukiwa mdogo, hujawahi kuishi mbali nasi
kuanzia masomo ya elimu ya shule ya msingi hadi elimu ya Sekondari.
Umesomea Morogoro, sasa unakwenda Dar es Salaam kuanza maisha
mapya ya kuishi mbali na sisi. Ninakuomba ukasome kwa bidii ili ujiandalie
maisha yako ya baadaye.” Mzee Bondi alimaliza kutoa nasaha zake, huku
Upendo akisikiliza kwa makini kabisa.


“Umsikilize baba yako kwa makini kwa sababu dunia ya sasa imeharibika
mwanangu. Magonjwa ni mengi na ukifika huko sio ndio ukasahau
kilichokupeleka. Kumbuka kinachokupeleka ni masomo na sio starehe.
Nadhani umenielewa.” Alisisitiza Mama yake.
“Jamani Mama nitasoma kwa bidii mbona unaongea hivyo.” Upendo
alihamaki “Lazima niongee mwanangu vijana wa sasa mnakutana na
mambo mengi na vishawishi vingi usipokuwa makini utapoteza kabisa
mwelekeo na malengo yako.” Mama upendo aliendelea kutoa nasaha.
“Baba na Mama nimewasikia, kamwe sitoenda kutenda yasiyo sahihi,
nitasoma na nitawafurahisha siku zote wazazi wangu.” Upendo alijibu kwa
unyenyekevu.
Baada ya maongezi hayo wote walisimama na kuelekea kulala ili Upendo
akaanze kujiandaa na safari. Upendo aliingia chumbani na kuanza kupanga
vitu vyake akisaidiana na mdogo wake Eliza.
“Ndugu yangu si nilikuwa nimekaa na Mama na Baba sebuleni wananipa
wosia namna ya kuishi huko Chuo.” Alisema Upendo.
“Eheh! Ilikuaje? Kwa sababu Mama naye akiamua kuongea ni balaa
wamesemaje hao wazee?” Alidadisi Eliza.
“Mwenzangu, Baba na Mama wameniambia nikienda nisisahau
kilichonipeleka nisiendekeze starehe.” Alisema Upendo.
“Heh! Hao wazee nao inamaana ukakae tu unasoma hata disko
usijichanganye? Aka mwaya sisi bado vijana lazima tujirushe we ngoja mi
nimalize Kidato cha Sita nikienda chuo nitajirusha sana kwani hapa
nyumbani hawa wazee wanatubania sana.” Alizungumza Eliza.
“Usiseme hivyo mdogo wangu mimi naona Baba na Mama wapo sahihi,
kwani nikianza kujiingiza kwenye starehe nitajikuta nafeli mitihani halafu
malengo yangu ya kuwa mwanasheria yasitimie, we mwenzangu unawaza
kujirusha tu.” Alijibu Upendo.

“Kujirusha ni wajibu na kusoma nitasoma tu, haya bwana tufanye haraka
tuwahi kulala hao wazee watakuamsha mapema kesho.” Alimaliza Eliza.
Kesho yake asubuhi na mapema Mama yake Upendo alimwamsha na
kumshauri Upendo ajiandae kwani safari ingeanza saa nne asubuhi. Eliza
siku hiyo hakwenda shule ili amsindikize dada yake. Walikunywa chai kwa
pamoja na tayari baba yao alikuwa amejiandaa kwa safari. Waliondoka na
usafiri wao binafsi hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumwacha
Upendo. Upendo alimwaga mama yake na mdogo wake akiwa na huzuni
kutokana na kuanza maisha mapya. Upendo alipangiwa kuishi katika
hosteli za mabibo ambazo zipo kandokando ya barabara ya Mandela
upande wa kulia kutokea Ubungo kuelekea Buguruni.

Akiwa chuoni Upendo alikukutana na watu mbalimbali. Alijitahidi sana
kusoma kwa bidii akiwa na uwezo mzuri darasani aliweza kufaulu vizuri
mitihani yake.
Eliza naye alimaliza Kidato cha Sita na kupangiwa kwenda kusoma Chuo
cha Njiro Mkoa wa Arusha wakati huo Upendo alikuwa amebakiza mwaka
mmoja ili amalize Chuo. Upendo aliishi vizuri na alipendwa sana na
wanafunzi kutokana na juhudi zake katika masomo na tabia yake nzuri
aliyokuwa nayo, hivyo alikuwa na marafiki wengi na pia walimu
walimpenda sana.

Wakati akikaribia kumaliza chuo Upendo alipata rafiki wa kiume aliyeitwa
James ambaye alikuwa ni mfanyabiashara. James naye alisoma Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma lakini aliamua kufanya kazi zake
binafsi kutokana na ajira kuwa ngumu. Kadiri siku zilivyozidi kwenda
urafiki wa James na Upendo ulikua na kuimarika sana kiasi kwamba watu
waliokuwa wakiwaona pamoja walijua ni mke na mume.
Siku moja James akiwa amekaa nyumbani kwake maeneo ya Kinondoni
aligubikwa na wazo zito kuhusu Upendo.

“Mimi na Upendo ni marafiki wakubwa sana na huyu binti ni msichana
ambaye anajiheshimu sana tokea nilipomfahamu, nimempenda sana
kutoka moyoni mwangu natamani awe mama wa watoto wangu. Kwa vile
sijawahi kumtamkia lolote juu ya suala la mapenzi kwa kipindi chote cha
kufahamiana kwetu, nahisi nikimdokeza tu pengine anaweza akachukia.”
Aliwaza James huku akitamani kumwambia Upendo kuhusu alilonalo
moyoni mwake.

Zilipita siku kadhaa kila James akionana na Upendo akawa anataka
kumwambia lakini alikuwa anasita. Siku moja alipanga kumtoa Upendo
ili kwenda naye sehemu tulivu apate fursa nzuri na adimu ya kumwambia

Upendo juu ya mapenzi aliyonayo moyoni mwake. ITAENDELEA USIKOSE UHONDO WA SIMULIZI HII

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom