Pages

Jumatano, Oktoba 09, 2013

ENDELEA KUSOMA SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA

SIMULIZI- MALIPO NI HAPAHAPA
KITABU- MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI- ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA
Julieth alirudi kwa mama Janeth na kumwelezea yote aliyokutana nayo.
Mama Janeth alisikitika sana na hakuwa na namna nyingine ya kumsaidia
zaidi ya kumpa nauli na pesa kidogo za matumizi ili arudi kwao Arusha;
“Julieth wewe nenda tu nyumbani ukamweleze mama yako hali halisi
kwani ukiendelea kuishi hapa utateseka sana na ipo siku huyo John
atakutafuta. Nakutakia kila la heri Mungu atakusaidia utawalea watoto
wako vizuri.” Mama Janeth alishauri.“Nashukuru sana mama Janeth kwa msaada wako, tangu siku nilipoumwa uchungu hadi sasa. Umekuwa msaada mkubwa sana kwangu. Mimi nitakwenda nyumbani na hata huko nyumbani sijui wanaendeleaje kwani sijawasiliana nao kwa muda mrefu. USIKOSE MUENDELEZO WA SIMULIZI HII ITAENDELEA HADI MWISHO.

INAPOENDELEA
Kuna siku nilimpigia Mama simu ikawa haipatikani.” Mama Janeth akampa simu ajaribu kumpigia tena mama yake lakini haikupatikana. Julieth aliwaza moyoni mwake; “Jamani mama atakuwa ana matatizo gain? Labda simu itakuwa imepotea au imeharibika.”

“Julieth unaondoka watoto hatujawapa majina, mimi ningependa huyu
wa kiume aitwe Dominiki na huyu wa kike aitwe Domina au unasemaje.”
“Sawa hakuna shaka ni majina mazuri najisikia fahari nakufarijika sana
kwa wewe kuwapa majina watoto wangu kwani bila wewe pengine
wasingekuwepo.” Alijibu Julieth huku akiwa na mawazo mengi.

Waliendelea na mazungumzo wakala chakula cha usiku na muda wa kulala
ulipofika wote walikwenda kupumzika ili kesho yake asubuhi na mapema
Julieth aanze safari ya kwenda Arusha. Kesho yake asubuhi na mapema saa kumi na moja Julieth alijiandaa na kusindikizwa na mama Janeth hadi kituo cha mabasi cha Nyegezi. Basi liitwalo Jordan liliwasili, waliagana harakaharaka na safari ilianza kuelekea Arusha.


Akiwa kwenye basi alikuwa amekaa karibu na mama mmoja ambaye
alimsaidia kumshika mtoto mmoja. Safari ilianza huku Julieth akiwa na
mawazo mengi moyoni mwake; “Nikifika sijui nitaanzaje kumweleza mama. Kwa matatizo yake ya moyo (shinikizo la damu) sijui atalipokeaje swala hili.” Aliendelea kuwaza huku gari likichanja mbuga. Safari iliendelea hatimaye walifika Arusha saa kumi na mbili za jioni.

Julieth alipoteremka tu alianza kuangalia huku na kule akishangaa
mabadiliko ya mji ule kama mgeni. Alichukua teksi na kwenda moja kwa
moja nyumbani kwao mtaa wa Kaloleni katika nyumba aliyomwacha
mama yake. Wakati anamlipa dereva teksi, mara dada mmoja aliyetokea
nyuma yake akamwita kwa mshangao; “He! Julieth! Julieth! Umerudi Julieth!” Akamkumbatia yeye na watoto wake pamoja.

“Jamani za siku nyingi.” Aliendelea kumsemesha Julieth. Mwanzo Julieth
hakumtambua lakini alivyozidi kumwangalia akamkumbuka.
“Oh! Kumbe Zubeda! Mambo vipi rafiki yangu? Nimefurahi sana
kukuona habari za hapa?” Zubeda alikuwa ni rafiki yake Julieth, kwani
walikuwa wakiuza chapati pamoja wakati Julieth akiwa Arusha.
Domina alianza kulia, haraka Zubeda alimchukua Dominiki ili Julieth
amnyonyeshe Domina.

“Habari za hapa ni nzuri kiasi.” Aliongea Zubeda huku akimshika vizuri
mtoto. “Nzuri kiasi!” Alihamaki Julieth huku akimkazia macho Zubeda.
“Ndiyo! Nzuri kidogo.” Alisisitiza Zubeda huku akiyakwepa macho ya
Julieth. “Vipi mwenzangu mbona ulikuwa kimya sana? Wakati mama yako akiwa anaumwa tulikupigia simu mara nyingi lakini haikupatikana na …”
“Ehe! Sasa anaendeleaje?” Julieth alimkatisha Zubeda na kuuliza akiwa
katika hali ya kushtuka.

Zubeda aliwachukua watoto wa Julieth na kukaa nao pembeni wakati yule
dereva akiondoka. Julieth alitaka kuingia ndani moja kwa moja lakini
Zubeda alimzuia.
“Julieth wadogo zako na mama yako hawapo hapa.” Zubeda alianza
kueleza.

Kama nilivyokudokeza mama yako aliugua sana, tulikutafuta kwenye simu
yako ili utume fedha za matibabu bila mafanikio. Kwa vile mama yako
alikuwa hana pesa ikabidi auze simu yake ili apate pesa za matibabu.”
“Oh! Samahani sana. Simu yangu iliharibika nikawa na simu nyingine.
Lakini namba ya mama ninayo, ila nilishawahi kumpigia lakini
haikupatikana. Labda ndo kipindi alipoiuza. Aliongea Julieth kwa
masikitiko.”

“Lakini mbona hata mume wako tulimpigia simu hakupokea, tuliamua
kumtumia ujumbe lakini hakujibu. Hivi kwa nini mlikuwa mnafanya hivi?”
Aliendelea kuhoji Zubeda huku Julieth akimsikiliza kwa makini sana.
“Ni histora ndefu hebu nitulie kwanza nitakusimulia siku nyingine wewe
ni rafiki yangu sitakuficha kitu. Eh! Hebu niambie mama na wadogo zangu
wanaishi wapi sasa?” Julieth alihoji zaidi.

“Wadogo zako waliondoka kutokana na kushindwa kulipa kodi ya
nyumba, kwa sasa sijui watakuwa wapi.” Alijibu Zubeda.
“Eh! Na mama?. Aliuliza Julieth.
Zubeda alimwangalia usoni Julieth ambaye alikuwa akionyesha uso wenye
maswali mengi sana. Kwa muda wa dakika moja hivi Zubeda aliwaza na
kutaka kumdanganya Julieth kuhusu aliko mama yake. Lakini mwisho
aliamua kumwambia ukweli.

“Baada ya kuugua kwa muda mrefu mama yako ali…” Alisita kidogo
Zubeda.
“Alifanya nini?.” Julieth aliuliza.
“Alifariki dunia.” Zubeda alijibu huku akimpa pole Julieth.
Julieth aliyekuwa amesimama alipiga kelele na kuanguka chini puu! Huku
nguvu zikimwishia. Alilia sana kama mtoto aliyeungua moto.
“Mamaaa! Mamaaa! Mama yangu wee! Upo wapi mama! Siamini nipeleke
nikamwone. Nipeleke! Nipeleke!” Aliendelea kulia, kugagaa chini na
kutamka maneno mbalimbali kwa uchungu sana. Hata hivyo haikusaidia
kitu mama yake alikuwa ameshafariki na kuzikwa siku nyingi sana.

Julieth alikuwa ameishiwa nguvu kabisa hivyo Zubeda aliwabeba watoto
wote. Ilikuwa yapata kama saa mbili hivi za usiku, Julieth alinyanyuka kwa
nguvu za ajabu na kugonga geti la nyumba aliyokuwa akiishi mama yake
huku akiita ;
“Mama fungua mimi mtoto wako Julieth nimerudi.”
“Hapo kuna mpangaji mwingine Julieth unawasumbua watu bure.”
Zubeda alimkataza Julieth. Lakini Julieth hakutaka kumsikiliza. Kutokana
na geti kugongwa kwa nguvu alitoka kaka mmoja na kufungua.
“Vipi dada una matatizo gani?” Aliuliza yule kaka.

“Yuko wapi mama yangu, namtaka mama yangu.” Aliuliza Julieth huku
akilia na akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa.
Yule kaka hakumwelewa anachozungumza akabaki anamshangaa. Ghafla
Julieth alianguka chini na kuzimia. Yule kaka na Zubeda walisaidiana
kumnyanyua Julieth na kumwingiza ndani kisha wakamlaza chini huku
feni ikimpepea. Yule kaka akamuuliza Zubeda aliyekuwa amewabeba
watoto wa Julieth.
“Vipi huyu mwenzio ana matatizo gani?” Aliuliza yule kaka.  JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SIMULIZI HII HADI MWISHO WAKE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom