Jumanne, Juni 10, 2014

Ni vyema sheria ikachukua mkondo wake "Waliomtesa `mtoto wa boksi` kushitakiwa kwa mauaji"

Gari ya Polisi iliyobeba watuhumiwa wa kesi ya mtoto wa boksi, Nasra Rashid ikiwasili Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Morogoro, imelazimika kuahirisha kesi ya washtakiwa watatu dhidi ya unyanyasaji kwa mtoto marehemu Nasra (4) (mtoto wa boksi), baada ya kesi iliyokuwa ikiwakabili washtakiwa kubadilika na kuwa ya mauaji.

Akiahirisha kesi hiyo jana, Hakimu wa mahakama hiyo, Mary Moyo, alisema mahakama imeamua kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 12, mwaka huu, kufuatia shtaka la kesi hiyo kubadilika na kuwa la mauaji baada ya mtoto huyo kufariki dunia.

Hakimu huyo alisema kuwa, washtakiwa hao wanatakiwa kupelekwa kituo kikuu cha polisi cha mkoa huo kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo upya jana, ili yatumike wakati wa kusoma mashtaka hayo mapya keshokutwa wakati washtakiwa hao watakapopandishwa tena kizimbani.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, washtakiwa walipandishwa kwenye teksi na kupelekwa kituo cha polisi kuhojiwa upya.

Hata hivyo, licha ya kuwapo askari polisi mahakamani hapo, wananchi walionekana kuwa na hasira kutokana na kuendelea kuguswa na tukio la utesaji mtoto huyo hadi kufariki, walitaka kuwashambulia watuhumiwa baada ya kulizingira gari walilopanda.

Washtakiwa wa kesi hiyo mama mkubwa wa mtoto huyo, Maria Saidi na baba mkubwa Mtonga Saidi, pamoja na baba mzazi, Mohamed Nasoro Mvungi, walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashtaka mawili; la kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.

Awali ilidaiwa kuwa, washtakiwa wa kwanza na wa pili walifanya ukatili wa kutisha dhidi ya marehemu tangu akiwa na umri wa miezi tisa kwa kumuweka kwenye boksi na kuibuliwa miaka minne baadaye na kuanza kufanyiwa matibabu na hatimaye kufariki dunia kwa ugonjwa wa pneumonia akiwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Juni Mosi, mwaka huu, wakati akipatiwa matibabu.

UMATI
Kesi hiyo ilifiikishwa mahakamani hapo kwa mara ya pili, ilijaza umati wa watu ukitaka kuwapiga washitakiwa, baada ya kufikishwa mahakamani hapo kutoka mahabusu. Hata hivyo, hali hiyo ilidhibitiwa na askari polisi.

Hakimu Moyo aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ambayo ilipangwa kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali, alikubaliana na ushauri uliotolewa na upande wa mashtaka ulioongozwa na waendesha mashtaka watatu wa Serikali, Sunday Hyera, S Edgar Bantulaki na Inspekta wa Polisi Zablon Msusi.

Hyera aliieleza Mahakama juu ya kifo cha mtoto Narsa na kwamba kutokana na hali hiyo, washtakiwa wote watatu, Mariam, Mtonga na Mvungi wanapaswa kuhojiwa upya na kufanyiwa uchunguzi upya na kuomba tarehe ya karibu ili kesi hiyo ifikishwe mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Hyera aliiomba mahakama kuruhusu washitakiwa hao kurudishwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Mjini Morogoro kwa ajili ya mahojiano mapya, ombi ambalo llilikubaliwa na Hakimu Moyo.

Washtakiwa hao waliondolewa na Polisi kwa gari ndogo la binafsi, lililozungukwa na umati mkubwa wa watu, wengi wao wakiwa ni kina mama, ambao waliwazomea washtakiwa na walikimbiza gari hilo huku wakitoa maneno ya kuwashutumu kwa madai kuwa walihusika na kifo cha mtoto huyo kutokana na kumtesa.

Mshtakiwa wa kwanza na wa pili walikuwa mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminiwa watakaokuwa wamesani dhamana ya maandishi ya Sh. milioni tano kila mmoja, huku mshtakiwa wa tatu akitimiza masharti na kuwa nje kwa dhamana.

Katika maelezo ya awali ya mashtaka, washtakiwa hao walidaiwa kula njama na kumfanyia ukatili mtoto huyo, ambaye mama yake mzazi alifariki dunia na jukumu la malezi kuachiwa mama yake mkubwa ambaye ni mshtakiwa wa kwanza.

Shitaka lingine ni kumfungia kwenye boksi na kunyima huduma za msingi kama mtoto ikiwemo chakula, tiba, mavazi na malazi, hali iliyosababisha apate magonjwa ya pneumonia, utapiamlo, maumivu ya kifua na kuvunjika kwa mifupa ya miguu na mikono.

CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom