Ijumaa, Julai 06, 2012

SIMULIZI YA MAMA MDOGO SURA YA ...7....


KITABU  MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE

...ILIPOISHIA.....Siku moja Jamal alitoka katika matembezi na kuchelewa kurudi nyumbani, ilikuwa ni saa tatu za usiku. Alimkuta baba yake pamoja na mama yake mdogo wamekaa sebuleni.
 “Shikamoo baba!” Aliamkia Jamal
 “Umetokea wapi usiku huu, unarudi muda unaotaka siku hizi?” Aliuliza Mzee Said kwa hasira bila hata kujibu salamu.
“Nilikuwa na marafiki zangu samahani kwa kuchelewa.” Alijibu Jamal huku akimuomba baba yake radhi na kuondoka.

Baba yake alichukia na kumpiga kibao cha usoni.
“Mjinga sana wewe unaweza kunijibu huku ukiwa unaondoka? Tabia gani hii? Ndiyo mnayojifunza shuleni eeh?” Alifoka Mzee Said. “Samahani baba naomba unisamehe sintorudia tena.” Alijibu Jamal huku akirudi kukaa kwenye kiti.
“Lakini baba Jamal usimfokee mtoto hivyo mbona hajachelewa sana, huyu ni mtoto wa kiume muache awe huru na marafiki zake.” Aliongea Sophia kwa kumtetea Jamal.

“Watoto wa siku hizi wanakua vibaya sana nitamvunjavunja! Mimi sitaki ujinga kabisa!” Alifoka zaidi Mzee Said huku anamgeukia Jamal.
“Toka hapa na sitaki kusikia hata siku moja umechelewa kuingia ndani nadhani tumeelewana.” Aliongeza Mzee Said.
“Sawa baba!” Alijibu Jamal kwa woga na wasiwasi mwingi.
Jamal aliondoka na kuelekea chumbani kwake huku akiwa na dukuduku moyoni mwake.
“Baba amenipiga mimi inaniuma sana na huyu mwanamke wake anajidai kunitetea anafikiri anaweza kuwa kama mama yangu? Hajui kama namchukia sana?” Aliwaza Jamal lakini haikusaidia.


Wakati akiendelea kuwaza mara alisikia mlango unagongwa alipokaribisha aliingia mama yake mdogo akiwa amebeba chakula.
“Jamal nimekuletea chakula pole kwa yaliyotokea.” Sophia alimfariji Jamal na kumletea chakula. Jamal alimtazama halafu akacheka kwa dharau.
“Acha unafiki wewe, kwanza sijisikii kula nimeshiba.” Alijibu Jamal.
“Kwanini unasema hivyo Jamal? Mimi sina nia mbaya na wewe.” Alijibu Sophia.
“Nenda zako huko, mimi najua unachotaka kutoka kwa baba yangu. Nacho si kitu kingine ila ni pesa zake tu. Kuna cha zaidi?” Alihoji Jamal huku akimwangalia kwa dharau.


“Sawa kama umeshiba vizuri, lakini mimi sina nia mbaya usiku mwema.” Alijibu Sophia halafu akatoka nje.
“Nenda zako huko tapeli mkubwa ingekuwa ni uwezo wangu
ningekufukuza binti mdogo unaolewa na mzee.” Aliwaza Jamal kisha alifunga mlango wake na kupanda kitandani kulala.
Kesho yake asubuhi aliamka mapema na kutokana na jana alilala bila ya kula alikuwa akisikia njaa sana. Alielekea jikoni na kuanza kujipikia mayai
ili ale pamoja na mkate. Akiwa jikoni Sophia alikuja na kumkuta akiwa
anapika.
“Habari za asubuhi Jamal.” Alisalimia Sophia.
“Nzuri shikamoo!” Aliitikia Jamal.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Jamal kumsalimia lakini Sophia hakuitikia na kusema.
“Vipi mbona unapika mwenyewe ngoja nikusaidie.” Alitamka Sophia.
“Wala usijali nitapika mwenyewe kitu ninachotaka kula we mpikie mume
wako.” Alijibu Jamal huku akiendelea kupika.
Mama yake mdogo ilimbidi anyamaze kimya na kumuacha akiendelea kujipikia. Baadaye alikula na kuondoka.
Maisha ya Jamal yalibadilika sana, alikuwa hana furaha katika nyumba ya baba yake. Ilipofika mwezi wa kumi na mbili Aisha alirudi likizo,. Jamal alifurahi sana na baba yao akamtambulisha Aisha kwa mama yake mdogo.
Kwa Aisha ilikuwa ni tofauti kutokana na ukarimu alioonyesha Sophia alimpenda na kumuheshimu kitu ambacho kilikuwa kikimkera sana Jamal.
Siku moja Jamal alikuwa amekaa na Aisha nyuma ya nyumba yao wakibarizi saa za jioni. Waliongea mambo mengi kuhusu maisha yao mapya wakiwa na mama yao mdogo.

“Aisha mdogo wangu kuwa makini sana na huyu mama mdogo wetu, mimi simwamini hata kidogo naona mpo naye karibu sana.” Alitahadharisha Jamal.
”Lakini kaka mbona mimi naona hakuna tatizo kabisa. Angalia
anavyonipenda ananinunulia zawadi nyingi. Mimi binafsi sina tatizo naye nampenda na ni mama yetu.” Alijibu Aisha.
“Wewe mpumbavu sana tena nisikusikie unasema ni mama yetu, mjinga mkubwa mama yetu alishafariki na kamwe huyu hawezi kuchukua nafasi ya mama anataka tu pesa za baba.” Alifoka Jamal huku akimwonyeshea kidole Aisha.
“Sasa tufanyeje kaka kwani Baba ndio ameshamwoa.” Alisema Aisha huku akimfunga Jamal kishikizo cha shati.
“We subiri utaona nitajua cha kufanya.” Aliongeza Jamal huku akisimamana kumuashiria Aisha waende ndani. USIKOSE SURA YA NANE SASA UTAENDELEA KUPATA MFULULIZO WA SIMULIZI ZA KUSISIMUA

Maoni 1 :

neema alisema ...

mi naona jamal yuko sawa kabisa, sophia yuko kwa ajili ya mali tu. maskini usilolijua ni kama usiku wa giza

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom