Jumapili, Novemba 25, 2012

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA SURA YA .....6.......



ILIPOISHIA“Mimi mama nipo tayari kuolewa naye kwani kwa kipindi cha wiki tatu tangu nimfahamu ameonyesha moyo wa kutusaidia.” Alijibu Julieth huku akimwangalia John kwa macho ya kusisitiza.

“Sawa! Kwa sababu yeye ameridhia hata nikimkatalia ni kazi bure. Ila nawaomba mfuate taratibu zote za kimila na kufunga ndoa rasmi ili mpate baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa wazazi pia.” Alishauri mama Julieth. USIKOSE SURA YA ......5........


INAPOENDELEA
“Huo ni ushauri mzuri mama, lakini namwomba niende naye Mwanza nikamtambulishe kwa wazazi wangu halafu atarudi ili tufanye taratibu hizo kama ulivyoshauri.” Aliomba John. “Kumbe kwenu ni Mwanza?” Aliuliza Mama Julieth. “Ndiyo mama.” Alijibu John. “Na je maisha yenu yatakuwa wapi?” Aliuliza mama Julieth. “Baada ya taratibu zote za kufunga ndoa kukamilika tutakwenda kuisha Mwanza.” Alijibu John. “Sasa baba kama mtaishi mbali na mimi nani atanihudumia, maana Julieth ndiyo alikuwa akinisaidia. 

Mimi mwenyewe hali yangu si nzuri sana naumwa mara kwa mara na Julieth anajua.” Alihoji mama Julieth. “Hapana mama usijali mimi na mwenzangu tumekwisha jipanga namna ya kukusaidia. Kwanza nataka uondoke hapa uhamie kwenye nyumba nzuri nitakayokupangishia. Pia nitakuachia pesa ili uweke msichana wa kazi ambaye atakusaidia kazi mbalimbali. Kuhusu pesa isiwe tatizo kabisa mambo yote yatakaa sawa.” John aliongea na kuahidi kwa kujiamini huku akimwangalia Julieth ambaye alikuwa akitabasamu muda wote wa maongezi.

“Sawa mimi nashukuru kama mmejipanga hivyo. Mungu akubariki sana mimi sina kipingamizi tena alimradi mmependana na kufuata taratibu za kufunga ndoa ili mpate baraka za Mungu. Pia ninaomba mkishaanza maisha muwe mnakuja huku kutusalimia mara kwa mara.” Mama Julieth alishauri huku akimkazia macho Julieth na baadaye John. “Hilo halina tatizo kabisa mama hapa ni nyumbani tutakuja bila shaka kwani nyumbani ni nyumbani, hata hivyo kwa sasa akishawaona wazazi wangu tu atarudi ili kukamilisha mambo ya ndoa kama ulivyoshauri.” Alijibu John.

********************************************************************
Mikakati ya kuondoka ikaanza, mama Julieth akahamishwa kutoka nyumba waliyokuwa wanakaa na kuhamia katika nyumba kubwa ambayo ilikuwa na kila kitu ndani. Kisha alitafutwa msichana kwa ajili ya kazi za ndani. Halafu nje ya nyumba alimfungulia duka dogo ambalo mama Julieth alikuwa akiuza bidhaa ndogondogo kama sabuni, sukari, unga na vinginevyo. Mwisho John alimnunulia mama Julieth simu kwa ajili ya mawasiliano ili kukitokea tatizo lolote atoe taarifa mapema. Mama Julieth alifurahi sana.


Siku ya kuondoka ilikaribia Julieth alionekana mwenye huzuni kwa ajili ya kumwacha mama yake. Mama Julieth yeye alikuwa katika hali ya kawaida akisisitiza kuwa Julieth akumbuke yote aliyomwambia. Safari ya kwenda Mwanza ilianza hatimaye walifika salama na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa John, maeneo ya Igoma. Julieth alishangaa sana kuona nyumba aliyokuwa akiishi John ilivyokuwa kubwa, nzuri na ya kifahari iliyojaa vitu vya thamani.

“Mpenzi nyumba yako ni nzuri sana, yaani nyumba yote hii unakaa mwenyewe?” Aliuliza Julieth. “Hapa ni kwako mama, nilikuwa nakaa mwenyewe na vijana wa kazi lakini sasa nina mke aitwaye Julieth naamini nyumba hii itakuwa nzuri zaidi hasa ikiwa na watoto na mke mzuri kama wewe.” John alijibu kwa kiburi na majivuno. Julieth alitabasamu huku akizunguka huku na kule akishangaa uzuri wa nyumba ile ya kifahari. John alipeleka mizigo chumbani na kumwelekeza kila kitu kilichomo na matumizi yake.

John na Julieth waliishi maisha ya raha na furaha. John alimtembeza Julieth sehemu mbalimbali ili kumwonyesha utofauti wa mazingira ya Mwanza na Arusha. Katika kuishi kwake Arusha Julieth alikuwa hajawahi kufika Mwanza, aliupenda sana mji wa Mwanza hususan samaki aina ya sato na sangara wanaopatikana katika mji huo ambao huvuliwa katika Ziwa la Viktoria. Kwa ujumla Julieth alifurahia sana maisha yake mapya. Baada ya wiki moja kupita Julieth alitaka kuwafahamu wazazi wa John, lengo kuu la safari yao ilikuwa kwanza kwenda kuwafahamu wakwe zake.

“Vipi mpenzi lini tutakwenda nikawafahamu wakwe?” Aliuliza Julieth. “Usijali mpenzi wangu tutakwenda tu kwani una wasiwasi gani, si upo na mimi kuna kazi tu zimenibana kwa sasa ila tutapanga mapema wiki ijayo.” Alimjibu John.
“Sawa John hakuna tatizo nilikuwa nataka kujua ili nimjulishe mama Arusha.” Alijibu Julieth. Mazungumzo yaliendelea baadaye walichoka na kwenda kupumzika.
*****Baada ya mwezi mmoja****
Wazazi wa John walikuwa wakiishi Bukoba na siyo Mwanza kama John alivyosema akiwa Arusha. Kila mara Julieth alipomwambia suala la kwenda kuwafahamu wazazi wa John aliambiwa kuwa watakwenda asiwe na wasiwasi. Baadaye kutokana na raha alizokuwa anazipata Julieth, alijisahau kabisa kama hajafunga ndoa na John. Mama yake Julieth alipokuwa akimpigia simu na kumuuliza vipi kuhusu ndoa alimjibu hakuna tatizo mipango inaendelea vizuri. Kumbe ilikuwa ni uongo wao walikuwa wakijirusha na kusahau mambo ya ndoa na taratibu nyingine za kimila.

********Baada ya miezi mitano**************

Baada ya mapenzi na raha kushamiri, Julieth alipata ujauzito ambao hakugundua kama ana mimba. Aligundua baada ya kwenda hospitali kupima afya yake kutokana na kutojisikia vizuri ikiwa ni pamoja na kusikia kichefuchefu. Suala la mimba lilimfurahisha sana Julieth. “Huu ndio wakati mwafaka wa kufunga ndoa, najua John atafurahi sana nikimzalia mtoto. Akija leo nitamwambia tufanye haraka tufunge ndoa.” Aliwaza Julieth. USIKOSE SURA YA ......7.........

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom