Jumatatu, Novemba 05, 2012

SIMULIZI YA MAMA MDOGO SURA YA 12 ENDELEA KUPATA UHONDO WA SIMULIZI

KITABU MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE

ILIPOISHIA....“Mume wangu hii bahasha ndani ina ujumbe kuna msichana ameiletanimpe Jamal nimefungua nikasoma niliyokutana nayo nimeshindwa kuamini macho na akili yangu nimeona nikupe kwanza uisome uone mambo anayofanya mtoto wako.” JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA 12


INAPOENDELEA 
Jamal alichukua ile barua na kutoa karatasi yenye ujumbe
uliosomeka hivi:
“Kwako mpenzi Jamal ni matumaini yangu umzima wa afya, vipi
unaendeleaje na maisha? Kwa nini umenitupa hivyo? Je, unajua ni
kwa kiasi gani niliteseka nilipotoa ile mimba yako? Sawa bwana! Ila
mimi bado nakupenda mpenzi wangu. Vipi shule utakwenda lini?
Naomba tuonane kabla hujaondoka ili nikupe ile zawadi uipendayo.
Ni mimi mpenzi wako Maria.”
Alipomaliza kusoma ule ujumbe baba Jamal alikunja uso na kuitupa ile
barua chini huku akisimama na kufoka kwa hasira.
“Hivi huyu mtoto amekuwa mwendawazimu kiasi hiki! Yaani mimi
nahangaika kutafuta fedha ili nimpeleke shule akasome yeye anawaza
mapenzi!” Alifoka baba Jamal.

“Ndiyo hali halisi mume wangu, Jamal hawezi kusoma kabisa. Kwa hiyo
utajijua mwenyewe kusuka au kunyoa. Nionavyo mimi hapa utapoteza
fedha zako bure. Kama ameshindwa kufanya vizuri Kidato cha Nne ndo
atamudu Kidato cha Tano?” Alitamka na kuuliza mama mdogo kwa
dharau. “Nashukuru sana kwa taarifa, nadhani sasa siwezi kupoteza fedha zangu kwa huyu mjinga. Kwanza yuko wapi sahizi?” Aliongea baba Jamal na
kuuliza. “Nadhani atakuwa huko chumbani kwake akiangalia mikanda ya video, si ndio kazi yake.” Alijibu mama mdogo. “Jamal! Jamal!” Aliita baba Jamal kwa sauti.

“Naam baba!” Aliitikia Jamal huku akisimama na kuelekea sebuleni.
Alipofika tu kabla hata hajaongea chochote baba yake alimpiga Jamal
kibao cha usoni. Jamal alipepesuka hadi kwenye sofa huku akishangaa na
kutoelewa kinachoendela. Jamal alishindwa kuelewa sababu ya kupigwa.“
“Baba mbona unanipiga bila sababu? Kosa langu ni nini?.” Aliuliza Jamal
huku akibubujika machozi. Baba yake alichukua ule ujumbe na kumtupia Jamal huku akifoka kwa hasira.

“Unataka kujua umefanya nini? Leo lazima nikumalize mjinga mkubwa
wewe! Mimi nakupeleka shule kusoma unakwenda kujifunza mapenzi!
Sasa nataka uniambie kwa nini umefanya hivi?” Aliendelea kufoka baba
Jamal kwa hasira.
Jamal aliokota ile karatasi na kusoma ule ujumbe. Alibaki akishangaa sana
kuona ujumbe ambao hakujua aliyeandika, na ulimlenga nani.
“Baba mbona mimi sielewi huyu Mary ni nani, mimi simjui baba sidhani
kama huu ujumbe utakuwa ni wa kwangu.” Aliongea Jamal kwa kujiamini.
“Nitakuua Jamal unataka kusema mimi mjinga, sasa sikiliza hutakwenda
shule utakaa hapa nyumbani hadi akili yako itakapokaa sawa, na tena hii
hali ikiendelea nitakufukuza hapa nyumbani.” Alifoka baba Jamal huku
amemshika Jamal shingoni kana kwamba anataka kumnyonga.

“Lakini baba unanionea mimi sijafanya hivyo na pia napenda kusoma
baba hata mama aliniambia nisome kwa bidii ili niweze kusimamia mali
alizoacha.” Aliongea kwa huruma Jamal.
“Hivi wewe ujasiri wa kujibizana na mimi umeupata wapi? Kosa umetenda
kidhibiti hiki hapa unakataa nini?Sasa nenda kamfuate mama yako
kaburini umwambie akusomeshe mpumbavu mkubwa unabishana na
mimi.” Aliongea baba Jamal huku hasira zikimpanda.
Baba Jamal aliendelea kumpinga Jamal hadi nguvu zilipomwishia. Mama
yake mdogo alitabasamu na kucheka muda wote wakati Jamal anapigwa.
Jamali alifanikiwa kupata kaupenyo na kukimbilia nje hadi mtaa wa tatu.
Jamal alitembea asijue wapi anaelekea hadi alipofika katika gogo moja kavu
akaamua kukaa akiendelea kulia kwa uchungu na mawazo mengi sana.
“Laiti mama angekuwepo! Hivi kwa nini mama umetuacha? Angalia
mwanao ninateseka bila sababu.” Aliwaza kwa uchungu Jamal.
Baada ya saa mbili kupita Jamal aliamua kurudi nyumbani. Alipofika baba
yake hakuwepo sebuleni. Alikaa kimya hadi mama yake mdogo
alipomletea chakula akala na kwenda kulala. Usiku ule ulikuwa ni usiku
wa majonzi sana kwa Jamal.

Siku za kwenda shule Jamal ziliwadia, lakini baba yake hakuhangaika
kumtafutia shule. Wanafunzi wanaoingia Kidato cha Tano walianza
kwenda katika shule mbalimbali. Jamal alijaribu kumwomba baba yake
ampeleke shule, lakini baba yake hakutaka kusikia kabisa. Hivyo aliendelea
kukaa nyumbani bila shughuli yoyote akitafakari hatima ya maisha yake
na mdogo wake Aisha endapo hatakwenda kusoma.

“Wenzangu wameshakwenda shule mimi bado nipo nyumbani na yote
haya ni kwa sababu ya mama mdogo. Baba naye amebadilika sana hataki
kunisikiliza kabisa, sijui nifanyeje. Natamani sana niendelee na shule.”
Aliwaza Jamal.
Wakati akiendelea kuwaza ghafla aliingia rafiki yake Goodluck.
“Jamal habari za asubuhi” Alisalimia Goodluck.
“Habari siyo nzuri ila afya yangu safi.” Alijibu Jamal.
“Kwanini siyo nzuri?” Aliuliza Goodluck.
“Si unajua matokeo yangu ya mtihani siyo mazuri sana, hivyo
sikuchaguliwa kuendelea na Kidago cha Tano.” Alieleza Jamal.
“Lakini kwa daraja la tatu ulilopata unaweza kwenda shule binafsi.”
Alishauri Goodluck.”
“Ndiyo lakini baba amekataa katakata kunisomesha, sababu ni huyo mama
mdogo anamshauri vibaya. Na chanzo ananitaka kimapenzi mimi
ninakataa. Hivyo alishasema eti kwa sababu ninajifanya mjanja hata hiyo
shule sitasoma. Huwezi amini ananizushia mambo ya ajabu kiasi kwamba
baba naye anaamini na sasa ameghaili kunisomesha.” Aliongea Jamal kwa
huzuni na hisia kubwa.
“Pole sana rafiki yangu lakini mbona hiyo ni kazi ndogo sana. Ningekuwa
ni mimi ningemkubalia ilimradi tu amshauri baba anipeleke shule.
Kumbuka muda ni huu wa kusoma ukichelewa basi hata huyo mdogo
wako utamsaidiaje?” Alishauri Goodluck.
“Kwa nini hukunishauri hivi muda wote huu?” Aliuliza Jamal.
“Hukuniambia Jamal, ningejuaje kama unatatizo?” Aliuliza Goodluck.
“Nakushukuru sana Goodluck, nadhani sasa itanibidi nikubaliane na ombi
la mama mdogo kwani ndiyo kikwazo. Halafu nikishakwenda shule
baadaye nitajua cha kufanya. Jamal uamuzi huu ni mgumu sana, lakini sina
namna inaniuma sana, Mungu anisaidie.” Jamal alitamka.
Baada ya maongezi hayo Goodluck aliaga na kuondoka kuelekea kwao
akimwacha Jamal akiwa na mawazo mengi kuhusu mama yake mdogo.
Siku iliyofuata yapata saa nne asubuhi wakati babake akiwa kazini Jamal
alimfuata mama yake mdogo sebuleni ili azungumze naye kuhusu swala
la kupekekwa shule. Alipoingia tu alimkuta amekaa katika sofa akifuma
kitambaa. USIKOSE SURA YA 13 muendelezo utaendelea hadi mwisho

Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

Nimefurahi sana leo kuiona tena hadithi hii! Mana nilimtuma mtu aninunulie pale salamander alikuta vimekwisha! Usichoke kuiweka kwani inavutia na haichoshi kuisoma! Mpaka hapa nakupa mia kwa mia 100%. Nakutakia afya njema ili utuwekee kila siku hadithi hii.

ADELA KAVISHE alisema ...

PAMOJA SANA MUENDELEZO UTAENDELA HADI MWISHO

Bila jina alisema ...

Asante sana kwa kunijibu! Naisubiri namba 13 ili nione kilitokea nini! Ukipata muda niwekee mshabiki wako namba 1 nifurahi na moyo wangu.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom