Jumatano, Novemba 21, 2012

SIMULIZI YA MAMA MDOGO SURA YA .........16.........




ILIPOISHIA:“He! we Jamal una kichaa nini? Yaani unataka kumwambia nini baba yako? Sasa naona unataka kuuwasha moto ambao kuuzima hutaweza. Ehe! na ukisha mwambia unatarajia nini?” Aliongea mama mdogo kwa kufoka. “Natarajia vyovyote itakavyokuwa, liwalo na liwe.” Alijibu Jamal. Mama yake mdogo alishindwa kuelewa Jamal amepatwa na maswaibu gani akasema.


INAPOENDELEA:“Kwani kuna nini kilichokufanya ukafikia uamuzi huo mpenzi wangu?” Alihoji mama mdogo. “Sikiliza kwa makini sana. Mimi siwezi kuendelea kuwa mjinga kiasi hiki. Haya mambo lazima niyaweke wazi. Nitaishi kwa wasiwasi hadi lini?” Aliongea Jamal kwa uchungu na kuondoka. “Hivi Jamal anataka kuwa kichaa au? Yaani amwambie Mzee Said kuwa mimi na yeye ni wapenzi na tumezaa mtoto? Sidhani kama atakuwa mzima hili ni tatizo.” Aliwaza mama mdogo. Siku zilivyozidi kwenda Jamal alikuwa akiota ndoto za kutisha sana. 

Mara nyingi alikuwa akimwona mama yake akimwambia aseme ukweli wa mambo yote yaliyotokea. Aliishi kwa shida sana, kwani hata usingizi alikuwa hapati. Hatimaye alianza kuwa mlevi ili asahau ndoto anazoota hivyo alianza kunywa pombe sana na kutumia dawa za kulevya kama bangi kwa nia ya kupoteza mawazo. Kumbe ndiyo alikuwa akizidi kuharibikiwa.

Baada ya kuwa mtumiaji wa vilevi alianza kufeli sana katika masomo yake ya chuo na baadaye akiwa mwaka wa tatu aliacha chuo na kuanza kuzurula mitaani. Kutokana na hali yake ya kutumia dawa kukithiri, baba yake alihuzunika na kuchukia sana baada ya kupata taarifa ya matatizo aliyopata mtoto wake. Huko nyumbani mama yake mdogo alikuwa na mawazo sana kwani alikuwa anatamani sana kumwona Jamal na hasa alipopata taarifa za kuwa anavuta bangi.


“Jamani ni kitu gani kimempata Jamal? Mbona alikuwa mzima tu na hajawahi kutumia dawa za kulevya? Inabidi leo baba yake akirudi nimwambie amtafute popote alipo ili arudi nyumbani.” Aliwaza mama mdogo. Baada ya muda mfupi baba Jamal alifika na kumkuta mkewe amekaa chumbani. “Vipi mke wangu mbona unaonekana mnyonge sana leo?” Aliuliza baba Jamal.“Unajua baba Jamal mimi nashangaa kwanini huhangaiki kumtafuta mtoto wako na unajua kabisa ana matatizo. Je akifa huko barabarani?” Alihoji mama mdogo.

“Yaani mimi nihangaike na mtu aliyejitakia kuwa mwendawazimu? Unanichekesha kweli. Mimi siwezi kuhangaika naye muache dunia imfundishe ipo siku atarudi mwenyewe.” Alijibu baba Jamal huku akivua koti lake na kulitundika. “Hapana baba Jamal, huyu ni mtoto wako bora umtafute apelekwe hospitali ili akafanyiwe uchunguzi lazima atakuwa ana tatizo kubwa. Na kama hautofanya hivyo basi utakuwa una roho mbaya sana!” Alitamka mama mdogo.

“Sawa basi nitatafuta watu wamkamate apelekwe hospitali sijui ni kitu gani kimemfanya atumie hizo dawa, kwa kweli amenikera sana.” Alijibu baba Jamal baada ya kukaa kimya kwa muda. “Eh! Sasa lini utawaomba wamtafute?” Aliuliza mama mdogo akiwa na
furaha. “Nadhani kesho asubuhi nitawatuma vijana wamtafute popote alipo. Ninaimani watampata tu kwani nasikia huwa anaonekana sana maeneo ya Kijitonyama.” Alijibu baba Jamal.

Kesho yake asubuhi baba Jamal aliwatuma vijana waende kumkamata. Wale vijana walizunguka sana huku na kule na ndipo ilipofika jioni alionekana maeneo ya studio Kinondoni akiwa amelala chini hajitambui amechafuka sana. Walimsogelea na kumbeba kisha kumpandisha katika gari walilokuwa nalo alikuwa ameishiwa nguvu kabisa. Walimtaarifu baba yake kwa simu na kumpeleka moja kwa moja hadi hospitali ya Muhimbili ambapo daktari alimchoma sindano na kumlaza katika chumba cha peke
yake.

Baada ya muda mfupi baba yake akiwa ameongozana na mama yake mdogo walifika pale hospitali na kuingia ndani katika chumba alichokuwepo Jamal. Baba yake alipomwona katika hali ile roho ya imani ilimjia. “Masikini kijana wangu ndiyo amekuwa hivi siwezi kuamini dokta naomba umsaidie apone.” Baba Jamal alimwambia daktari.
Wakati huo mama yake mdogo machozi yalikuwa yakimtoka kwa uchungu. “Daktari fanya lolote na kwa gharama yoyote Jamal apone.” Alisisitiza USIKOSE SURA YA ....17........
mama mdogo.

Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

Asante kwa hadithi, ni nzuri sana ila unaweka fupi jamani, ongeza kidogo Adela

Bila jina alisema ...

nikweli nifupi Adela sisi wengine tupo mbali hatuwezi kuvipata hivyo vitabu batunafurahi sana unavyotuandikia ubarikiwe

Bila jina alisema ...

HONGERA DADA MAANA KWA HAKIKA NAPATA KUELIMIKA....

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom