Ilipoishia: Alipofika alikuwa na wasiwasi mkubwa akifikiria jinsi atakavyokabiliana na uso wa John baada ya kuachana kwa takribani miezi mitatu. Alisogea jirani, akagonga taratibu na kusubiri afunguliwe. Mara mlango ulifungulwa na mwanamke mwenye uso wa kujiamini kisha akaanza kumsemesha Julieth: “Habari za leo dada! Alisalimia. “Salama dada yangu! Habari za hapa?” Alijibu na kuuliza Julieth. “Karibu dada nikusaidie nini?” Aliuliza bila hata kujibu swali aliloulizwa.Julieth alishtuka sana na kuingiwa na hofu kubwa kumwona yule mwanamke aliyefungua mlango. USIKOSE SURA YA 9...........
INAPOENDELEA
“Samahani
namuulizia John.” Yule mwanamke alimwangalia Julieth kuanzia
kichwani hadi kwenye vidole vya miguu, kisha akamkaribisha: “Karibu
ndani.” Alimkaribisha Julieth huku akitangulia ndani haraka bila hata
kuangalia nyuma. Julieth aliingia na kukaa katika sofa lililokuwa jirani kabisa na
mlango huku moyoni mwake akijiuliza: “Huyu mwanamke ni nani?”
Wakati huo yule mwanamke alikuwa amekaa katika sofa lililokuwa karibu na
mlango wa kuingia chumbani, huku mtoto wa kiume mwenye umri kati
ya miaka mitano na sita hivi akichezea kijigari kidogo.
Kwa
takribani dakika tatu au nne hivi walibaki kimya huku kila mmoja akimwangalia mwenzie kwa kuibia. Ghafla yule mwanamke alivunja ukimya kwa
kutaka kujua Julieth alikuwa na shida gani; “Samahani
dada unamtaka John wa nini?” Aliuliza yule mwanamke. Julieth alitaka
kumjibu lakini alisita. Baada ya dakika moja hivi Julieth alijipa ujasiri mkubwa na
kumweleza kilichomleta pale ndani, wakati huo John alikuwa yupo
chumbani asiyejua chochote juu ya nini kinachoendelea pale sebuleni:
“Mimi ni
mchumba wa John, nilikuwa naishi hapa na nimetoka hospitali nimejifungua
hawa watoto mapacha.” Alijieleza Julieth kwa ujasiri wa kuigiza.
Yule mwanamke alishtuka na kusimama ghafla huku ameshika kiuno na
kunyoosha shingo yake kama fisi aliyesikia harufu ya mzoga. “Wewe
dada! Unajua unachoongea? Una uhakika ni nyumba hii au umekosea
nyumba? Aliuliza na kuhoji yule mwanamke. “Dada
yangu sijakosea kabisa ni hapahapa.” Alijibu Julieth akiwa katika hali ya
kujiamini kidogo.
Yule mwanamke
alimuangalia Julieth, akainama chini akitafakari jambo kisha
akaendelea kufoka; “Hapa ni
nyumbani kwangu, na huyo John unayemsema ni mume wangu.” Huku
akimnyooshea kidole yule mtoto aliyekuwa anachezea kijigari. “Na yule
pale ni mtoto wetu anaitwa Philipo. Je, huo uchumba wenu mliufanyia
mbinguni? Mbona wewe dada unanishangaza sana?” Aliendelea kufoka. “Kama wewe
umezaa naye mtoto, mimi nimezaa naye watoto, nakuomba niitie
John niongee naye.” Alifoka Julieth huku akionyesha kujiamini zaidi kuliko mwanzo.
Baada ya
kuona Julieth anavyoongea kwa kujiamini yule mwanamke alisimama
haraka na kuingia chumbani akimwacha Julieth na watoto wake pale
sebuleni. Julieth
aliinama na kuwaza kitu; “Nakumbuka siku John aliponifukuza alisema
mke na mtoto wake wanakuja je, atakuwa ndio huyu? Nahisi kama naota.
Lakini ni kweli yamenikuta nitafanya nini mimi?” Julieth aliendelea kuwaza na
kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Ni dhahiri
yule mwanamke alikuwa ni mke wa John kwani alikuwa akiishi Dar es
salaam akiwa masomoni katika moja ya vyuo vikuu vilivyoko huko.
John
alikuwa akisafiri mara kwa mara kumtembelea na sasa alikuwa amerudi
baada ya kumaliza masomo. Wakati huo wote John alikuwa anaishi na
Julieth huku akimdanganya kuwa alikuwa anasafiri kikazi kumbe tayari
alikuwa na mke aliyefunga naye ndoa pamoja na mtoto sasa sijui Julieth
atafanya nini. Julieth
aliendelea kukaa pale sebuleni akimsubiri John. Alitumia fursa hii kukagua
sebule yote. Alitazama ukutani na kuona picha kubwa ya harusi iliyomwonyesha
John akiwa na yule mwanamke aliyemkaribisha. Alishtuka na
kuishiwa nguvu huku machozi yakimtoka asiamini anachokiona.
Mara
mlango wa chumbani ulifunguliwa ghafla huku yakisikika maneno kama vile
watu wanafokeana. John alitokeza huku yule mwanamke akimfuata
kwa nyuma na kumkuta Julieth; “Nani
kakuruhusu kuja hapa kwangu wewe mbweha mkubwa?” John alifoka na
kutukuna bila hata salamu. Kisha akamgeukia mama Philipo; “Hivi mama
Philipo umeanza kukaribisha vichaa humu ndani?” Aliendelea kufoka
John.
“Hapana
mume wangu mimi huyu amekuja anakutafuta wewe kwani unamfahamu
vipi? Alihoji mama Philipo kwa upole tofauti na alivyokuwa akiongea
na Julieth. “Huyu
mwanamke ulipokuwa Dar es Salaam mke wangu, alikuwa ni mfanyakazi
wangu wa ndani hapa nyumbani. Mimi nilipokuwa nasafiri alikuwa
analeta wanaume hapa nyumbani taarifa nikawa nazipata. Baadaye alikuja
akapata mimba na kuanza kusambaza maneno mimi ni mume wake nilimfukuza
na nashangaa anataka nini tena hapa na pesa yake nilishampa siku
nyingi” Bila ya aibu na hata huruma alisema John huku akimtaka Julieth na
watoto wake waondoke na asirudi tena.
“Wewe!
Wewe! John! Muogope Mungu ulinichukua kwetu Arusha na kunidanganya
kuwa unanipenda leo hii unaniona sifai. Eti kichaa! Baada ya
kunidanganya na kuniharibia maisha yangu leo unaniona kichaa. Ungeniambia
ukweli haya yote yasingetokea, kumbe ulikuwa una mke na mtoto.
Sawa! mimi nitaondoka ila Mungu ndiye atakayenisaidia nakutakia maisha
mema.” Alifoka Julieth kwa mfululizo bila hata kumpa John fursa ya kujibu
huku akibubujika machozi.USIKOSE SURA YA ...10......
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni