Jumatatu, Januari 07, 2013

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA SURA YA .....10......

 
 
ILIPOISHIA “Wewe! Wewe! John! Muogope Mungu ulinichukua kwetu Arusha na kunidanganya kuwa unanipenda leo hii unaniona sifai. Eti kichaa! Baada ya kunidanganya na kuniharibia maisha yangu leo unaniona kichaa. Ungeniambia ukweli haya yote yasingetokea, kumbe ulikuwa una mke na mtoto. Sawa! mimi nitaondoka ila Mungu ndiye atakayenisaidia nakutakia maisha mema.” Alifoka Julieth kwa mfululizo bila hata kumpa John fursa ya kujibu huku akibubujika machozi.USIKOSE SURA YA ...10......
 
 
INAPOENDELEA 
Wakati akizungumza maneno hayo mama Philipo alibaki kimya akitafakari kisha akaungana na John kumshambulia Julieth; “Hebu tuondolee kilio hapa ufanye uhuni wako upate mimba halafu uje hapa na vitoto vyako nani akupokee, kamtafute baba wa watoto wako. Unataka kunigombanisha na mume wangu toka mjinga wewe.” Alitamka mama Philipo huku akimsukumiza Julieth na watoto wake nje. Julieth alitoka akiwa analia sana.

Julieth alirudi kwa mama Janeth na kumwelezea yote aliyokutana nayo. Mama Janeth alisikitika sana na hakuwa na namna nyingine ya kumsaidia zaidi ya kumpa nauli na pesa kidogo za matumizi ili arudi kwao Arusha; “Julieth wewe nenda tu nyumbani ukamweleze mama yako hali halisi kwani ukiendelea kuishi hapa utateseka sana na ipo siku huyo John atakutafuta. Nakutakia kila la heri Mungu atakusaidia utawalea watoto wako vizuri.” Mama Janeth alishauri.

 “Nashukuru sana mama Janeth kwa msaada wako, tangu siku nilipoumwa uchungu hadi sasa. Umekuwa msaada mkubwa sana kwangu. Mimi nitakwenda nyumbani na hata huko nyumbani sijui wanaendeleaje kwani sijawasiliana nao kwa muda mrefu. Kuna siku nilimpigia mama simu ikawa haipatikani sijui wana hali gani.” Mama Janeth akampa simu ajaribu kumpigia tena mama yake lakini haikupatikana. Julieth  aliwaza  moyoni mwake; “Jamani mama atakuwa ana matatizo gain? Labda simu itakuwa imepotea au imeharibika.”


 “Julieth unaondoka watoto hatujawapa majina, mimi ningependa huyu wa kiume aitwe Dominiki na huyu wa kike aitwe Domina au unasemaje.” “Sawa hakuna shaka ni majina mazuri najisikia fahari nakufarijika sana kwa wewe kuwapa majina watoto wangu kwani bila wewe pengine wasingekuwepo.” Alijibu Julieth huku akiwa na mawazo mengi. Waliendelea na mazungumzo wakala chakula cha usiku na muda wa kulala ulipofika wote walikwenda kupumzika ili kesho yake asubuhi na mapema Julieth aanze safari ya kwenda Arusha.

Kesho yake asubuhi na mapema saa kumi na moja Julieth alijiandaa na kusindikizwa na mama Janeth hadi kituo cha mabasi cha Nyegezi. Basi liitwalo Jordan liliwasili, waliagana harakaharaka na safari ilianza kuelekea Arusha.

 Akiwa kwenye basi alikuwa amekaa karibu na mama mmoja ambaye alimsaidia kumshika mtoto mmoja. Safari ilianza huku Julieth akiwa na mawazo mengi moyoni mwake;
“Nikifika sijui nitaanzaje kumweleza mama. Kwa matatizo yake ya moyo (shinikizo la damu) sijui atalipokeaje swala hili.” Aliendelea kuwaza huku gari likichanja mbuga.

Safari iliendelea hatimaye walifika Arusha saa kumi na mbili za jioni. Julieth alipoteremka tu alianza kuangalia huku na kule akishangaa mabadiliko ya mji ule kama mgeni. Alichukua teksi na kwenda moja kwa moja nyumbani kwao mtaa wa Kaloleni katika nyumba aliyomwacha mama yake. Wakati anamlipa dereva teksi, mara dada mmoja aliyetokea nyuma yake akamwita kwa mshangao;
“He! Julieth! Julieth! Umerudi Julieth!” Akamkumbatia yeye na watoto wake pamoja.
“Jamani za siku nyingi.” Aliendelea kumsemesha Julieth. Mwanzo Julieth hakumtambua lakini alivyozidi kumwangalia akamkumbuka.
“Oh! Kumbe Zubeda! Mambo vipi rafiki yangu? Nimefurahi sana kukuona habari za hapa?” Zubeda alikuwa ni rafiki yake Julieth, kwani walikuwa wakiuza chapati pamoja wakati Julieth akiwa Arusha. Domina alianza kulia, haraka Zubeda alimchukua Dominiki ili Julieth amnyonyeshe Domina. USIKOSE SURA YA 11

Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

Mmh! Story zako zinanoga Adela . Mungu akujaalie afya njema na akupe maisha marefu inshallah.

Bila jina alisema ...

Jamani I wish ningepata Kbs kitabu vile hadithi ilivyo nzr! Bless u swt hrt.xxx

ADELA KAVISHE alisema ...

ASANTENI KWA KUENDELEA KUWA NAMI

ADELA KAVISHE alisema ...

ASANTENI KWA KUENDELEA KUWA NAMI

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom