KITABU-MALIPO NI HAPAHAPA
SIMULIZI-DADA YANGU
ILIPOISHIA
“Mimi na Upendo ni marafiki wakubwa sana na huyu binti ni msichana
ambaye anajiheshimu sana tokea nilipomfahamu, nimempenda sana
kutoka moyoni mwangu natamani awe mama wa watoto wangu. Kwa vile
sijawahi kumtamkia lolote juu ya suala la mapenzi kwa kipindi chote cha
kufahamiana kwetu, nahisi nikimdokeza tu pengine anaweza akachukia.”
Aliwaza James huku akitamani kumwambia Upendo kuhusu alilonalo
moyoni mwake.Zilipita siku kadhaa kila James akionana na Upendo akawa anataka
kumwambia lakini alikuwa anasita. Siku moja alipanga kumtoa Upendo
ili kwenda naye sehemu tulivu apate fursa nzuri na adimu ya kumwambiaUpendo juu ya mapenzi aliyonayo moyoni mwake. ITAENDELEA USIKOSE UHONDO WA SIMULIZI HII
INAPOENDELEA
Ilikuwa siku ya Ijumaa James aliyopanga kumtoa Upendo jioni yake
kwenda katika matembezi. Alipomweleza Upendo juu ya azima yake ya
kutoka naye alikubali bila pingamizi. Ilipofika jioni ya saa kumi na
mbili
hivi James alikwenda Hosteli ya Mabibo na gari yake aina ya Benzi
kumchukua Upendo. Alipofika Hosteli block
A chumba namba 228
alimkuta Upendo akiwa tayari amejitayarisha kwa ajili ya matembezi ya
jioni. Upendo alivalia vazi la kutokea jioni ambalo lilimkaa barabara
likionyesha vizuri jinsi Mungu alivyompendelea kimaumbile. Alipendeza
sana kiasi kwamba James alijiona ni mwanamume mwenye bahati kama
angefanikiwa kumpata kimapenzi.
James aliendesha gari kuelekea Sinza eneo liitwalo Madukani katika
Mgahawa uitwao “Fast Food
and Take Away” ambao ulikuwa na utulivu na
hali ya hewa nzuri. Walichagua sehemu nzuri na kwenda kukaa pamoja.
James alimpa Upendo uhuru wa kuagiza chochote alichopenda kula na
kunywa. Waliletewa vinywaji na kuanza kunywa huku wakisubiri chakula.
Muda wote mapigo ya moyo wa James yalikwenda mbio akiwaza namna
ya kuanza kumwambia Upendo suala la mapenzi. Baada ya kama dakika
ishirini hivi za maongezi ya kawaida James aliamua kumwaga sera zake.
“Upendo umependeza sana leo hilo gauni ulilovaa limekupendeza sana.”
James alianza kwa kumsifia Upendo.
“Asante James mbona hata wewe umependeza.” Wote wakacheka na
kugonganisha mikono. James alivuta kiti chake na kusogea karibu na Upendo huku moyo wake ukiwa bado unamdunda macho yakiwa na rangi nyekundu kwa hofu ya
kumwambia Upendo kuwa anampenda. James alijikaza na kumshika
Upendo mkono. “Upendo kuna kitu kinanisumbua sana moyoni mwangu, kitu hicho
kimekuwa kinanitesa kwa muda mrefu sana tangu tufahamiane.” Aliongea
James huku midomo ikimtetemeka kidogo.
“James! Ni kitu gani hicho jamani?” Aliuliza Upendo kwa sauti ya
mahaba
na macho yake ya kurembua. “Ni kitu cha kawaida sana lakini…”
“Lakini nini?” Alimkatisha Upendo akiwa ananyanyua glasi ya soda na
kuinywa huku akimwangalia James usoni. “Nitakwambia kitu hicho jioni hii ya leo ingawa kitu hicho kinaweza kuharibu au kuboresha urafiki wetu.” Aliongea James kwa kujihami ili apate ujasiri wa kusema. “We sema tu James, ni jambo gani hilo ambalo unasita kuniambia wakati kuna mambo mengi sana tumekwishaongea mimi na wewe tangia tufahamiane.” Upendo aliongea kana kwamba anampa uhuru wa kusema
linalomsumbua James.
“Upendo! Aliita James kwa sauti ya chini sana huku akijitahidi
kuyakwepa
macho ya Upendo. Abee!” Aliitikia Upendo. “Ahhm! Tangu tufahamiane nimetokea kukupenda zaidi ya urafiki tulionao.” James alitulia kidogo huku safari hii akimwangalia Upendo usoni. Kabla Upendo hajasema kitu James aliendelea kumwaga sera zake
huku Upendo akiwa kimya. “Ningependa uwe mpenzi wangu na baadaye Mungu akitujalia uwe mama wa watoto wangu.” Aliongea James akimkazia macho Upendo.
Upendo aliyekuwa ametulia akimsikiliza aliutoa mkono wake mikononi
mwa James ambaye alikuwa amemshika, huku akiinama na kuminyaminya
vidole vyake kwa aibu.
“Mh! We James! Ina maana hadi sasa hauna mwanamke kijana mzuri kama
wewe acha hizo bwana mbona si kitu cha kawaida.” Alihoji Upendo.
Ni kweli Upendo lazima utafikiria hivyo, ila nakwambia ukweli kutoka
moyoni mwangu, sina mwanamke yeyote. Ila niliwahi kuwa na mpenzi
zamani kidogo tukakorofishana na kwa sasa ameolewa. Nilikuwa
nampenda sana ila aliniumiza moyo wangu nikajikuta sitamani kuwa na
mwanamke tena maishani mwangu. Lakini tulipoanza urafiki mimi na
wewe nimegundua kuwa nahitaji kuyaanza maisha yangu upya.
Nimekupenda sana Upendo nipe nafasi katika moyo wako.” Alibembeleza
James.
“Je, kwa sasa huyo aliyekuwa mpenzi wako anaishi wapi?” Aliuliza
Upendo. Alikuwa anaishi hapahapa Dar lakini baada ya kuolewa alihamia Mbeya
na mume wake. “Mmmh!! Hapana James kwa sasa, naona tuendelee kuwa marafiki, ila
nitakujibu kuhusu ombi lako siku yoyote.” Alimjibu Upendo huku akitafakari kitu.
“Nikupe muda gani Upendo.” Alihoji James huku akishusha pumzi kwa
nguvu. Kisha akaendelea kuongea.
“Nashindwa hata kusubiri. Ila sawa nitakupa muda ili uweze
kunifikiria,
fahamu kuwa nakupenda na ni wewe pekee unaye utesa moyo wangu kwa
sasa. Natumaini nitapata jibu zuri. Au siyo?” Aliuliza James huku
akitabasamu na kuweka mkono wake wa kulia begani kwa Upendo.
“Jamani mbona una haraka hivyo usijali tutaona itakavyokuwa.” Alijibu
Upendo huku akitabasamu kama alivyofanya James lakini akiuondoa
mkono wa James uliokuwa juu ya bega lake.
Baada ya hapo chakula kilikuwa tayari kimeletwa, walikula na
kuendelea
kunywa vinywaji vyao na kuzungumza mambo mbalimbali. Ilikuwa tayari
imetimia saa tatu za usiku. “Heh! Kumbe muda umeenda hivi hebu nirudishe hostel James, nina kaziza chuo sijazimaliza.” Alitamka Upendo. “Acha hizo Upendo yaani saa tatu tu ndo muda umeenda. Mimi ningependa twende na disko lakini kwa vile umesema kuwa una kazi za kufanya, sina namna ngoja tu nikupeleke. Ila tumalizie vinywaji
kwanza.” Alishauri James.
Baada ya kumalizia vinywaji waliondoka kuelekea hosteli. Wakiwa
njiani,
James aliendelea kubembeleza na kusisitiza juu ya ombi lake.
“Please (nakuomba) usiache kunifikiria nakupenda sana Upendo.”
Alisisitiza James.Upendo alinyamaza kimya huku akimwangalia James bila kumjibu
chochote. Walipofika hosteli kabla hajashuka katika gari James
alimshika
mikono yote miwili kisha akamkumbatia na kumbusu shavuni.
“Nakupenda sana Upendo. Nakutakia usiku mwema na ndoto njema.”
Aliongea James wakati akiendelea kumbusu huku Upendo akijaribu
kumzuia. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio Upendo, huku akijitoa kifuani kwa
James. “James asante kwa yote nakutakia usiku mwema nawe.” Alishukuru
Upendo kisha akashuka kwenye gari na kuingia hosteli huku James
akiondoka kuelekea Kinondoni. Usiku kucha Upendo aliwaza sana akimwaza James moyoni mwake.
“Mmh! Mmh! James ni kijana mtanashati siwezi kumpoteza nampenda
pia. Lakini wanaume nao hawatabiriki, leo ananibembeleza sana akidai
kuwa ananipenda halafu akinipata ataniacha. Ikitokea hivyo ataniumiza
moyo wangu sana. Mmh! lakini sidhani kama James atakuwa hivyo,
natamani awe baba wa watoto wangu. Sijui nimpigie simu ni mwambie
sasa hivi! Lakini hapana! Aa! Hebu ngoja nimpigie sasa hivi.”
Alichukua
simu yake na kuanza kumpigia simu James.
Wakati simu ikiwa inaita Upendo alikuwa na hofu kubwa. “Haloooo! Alipokea simu James. “Yaani nilitaka kukupigia simu muda huu umeniwahi, niambie mpenzi
wangu.” Aliongeza James bila kumpa nafasi upendo ya kuongea. “Aha vipi James uko wapi? Unafanya nini saa hizi? Unajua kuna kitu nataka nikwambie ila basi, nitakwambia kesho, usiku mwema.” Akakata simu Upendo. “Aah! Kakata simu.” Aliwaza James kisha akaamua kupiga yeye.
“Halooo! Mbona umekata simu kabla hatujamaliza maongezi? Aliuliza
James “Haya niambie ulichotaka kuniambia kwani natamani sana kusikia kutoka
kwako la sivyo utanifanya nisilale.” Aliomba James.
“Hakuna kitu jamani James nilikuwa nataka kujua kama umefika salama.”
Alijibu Upendo. Usiku ule Upendo hakumwambia chochote James akabaki akijilaumu
baada ya kukata simu huku akiwaza; “Hivi kweli nimeshindwa kumjibu! Ila kesho tukionana nitamwambia.” Upendo aliendelea kumwaza James hata kusoma kulimshinda usiku ule akaamua kulala.
Kesho yake ilikuwa ni siku ya Jumamosi, asubuhi Upendo aliingia
darasani
kujisomea kama kawaida yake. Ilipofika saa sita na nusu aliamua
kurudi
hosteli. Akiwa chumbani na rafiki yake Grace aliamua kutoka nje ili
apate
muda mzuri wa kutafakari kuhusu ombi la James. Alimuaga Grace na
kumwambia kuwa atakuwa chini ya mti mkubwa ulio nyuma ya hosteli
akijipumzisha.
Baadaye James alikuja pale chumbani kwa Upendo bila taarifa, baada ya
kugonga mlango na kuruhusiwa kuingia alimkuta Grace akiwa amejilaza
kitandani akisoma gazeti.
“Habari gani dada!” Alisalimia James.
“Nzuri kaka karibu kiti.” Alijibu Grace.
“Asante dada. Aaahmm! Nimemkuta Upendo?” Aliuliza James huku
akitabasamu. “Ndiyo! Ila yupo nje amekaa chini ya mti mkubwa nyuma ya jengo hili.”
Alijibu Grace huku akiamka na kukaa vizuri kitandani.
“Haya asante hebu nimfuate.” Aliaga James na kuondoka. ITAENDELEA HADI MWISHO USIKOSE UHONDO.
Maoni 1 :
Hadithi zako Adela ni nzuri sana' ilaunachelewa sehemu ya 2 naomba hii usiicheleweshe
Chapisha Maoni