Jumanne, Machi 11, 2014

SIMULIZI FUPI NISAMEHE MAMA

NA ADELA D.KAVISHE
Unaambiwa waheshimu Baba na Mama ili upate heri na baraka za kuishi maisha mengi zaidi duniani, lakini bado kuna baadhi ya watoto wanawadharau wazazi kwa namna tofauti, Embu tizama Mama amekubeba tumboni miezi tisa amepambana na wewe katika maisha hadi umekuwa mtu mzima, leo hii unakuta kijana anamdharau Mama yake na kumuona hafai. "Kuna msichana mmoja alitokea katika kijiji kimoja ambapo alikuwa akiishi na Mama yake aliyemlea katika shida na raha, kwani Mama huyu alimlea mtoto wake peke yake baada ya Baba wa mtoto kumtelekeza hivyo Mama alijitahidi kwa hali na mali kufanya kazi mbalimbali ili mtoto wake aweze kupata elimu.

 Alijitahidi sana hadi alipomaliza kidato cha nne, kwa bahati mbaya binti huyu hakufanikiwa kuendelea na kidato cha tano, kutokana na kutofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne. Mama yake alisikitika sana kwani alitamani mtoto wake asome ili baadaye aje kuwa na mafanikio mazuri katika maisha yake. Mama huyu alikuwa na ndugu yake jijini Dar es salaam ambaye alikuwa ni mjomba wake na yule binti. Kaka huyu aliamua kumsaidia dada yake na kumchukua  binti huyu aliyekuwa anaitwa Chichi.


 Hatimaye Chichi alihamia jijini Dar es salaam na mjomba wake alimtafutia chuo, Alifanikiwa kupata chuo cha uhasibu, ambapo alianza masomo yake na kutokana na umbali wa chuo na nyumbani mjomba alimua kumtafuti Hostel. Baada ya miezi sita kupita tokea chichi aanze masomo yake alianza kubadilika kutokana na makundi aliyokuwa nayo, alianza kuvaa mavazi ambayo alikuwa hajawahi kuvaa kama nguo fupi na suruali za kubana kwani siku zote alikuwa akivalia sketi ndefu. Chichi alikuwa ni msichana mrembo sana, sura yake nzuri, na macho yake ya upole pamoja na umba lake namba nane, vilimfanya kila aliyekuwa akimtizama kumsifia kwa uzuri wake. 

Maisha yaliendelea akiwa pale chuo Chichi alianza kusahau maisha yake ya kijijini na kujiona wa mjini, Na hata marafiki zake  aliwaambia kuwa mjomba wake ndiyo baba yake mzazi na hata siku moja hakuwahi kusema kuwa Mama yake anaishi kijijini. Baada ya mwaka mmoja kupita Mama yake na Chichi alikuja  Dar es salaam na moja kwa moja  alikwenda kumtembelea mtoto wake. Alipofika, aliwakuta baadhi ya wanafunzi na kuwauliza, wale wanafunzi walibaki wakimshangaa baada ya kujitambulisha kama mama yake mzazi na Chichi, ndipo mmoja kati ya wale wanafunzi alikwenda kumuita Chichi alikuja huku akiwa amevalia kigauni kifupi kilichokuwa kimeacha sehemu kubwa ya mapaja yake wazi. 

Mama yake aliyekuwa amejifunga kanga mbili alisikitika sana kumuona Chichi alivyovaa. Chichi alimsogeza pembeni na kumuambia Mama yake asijitambulishe kama Mama yake mzazi aseme kuwa yeye ni bibi yake. Mama yule aliendelea kushangaa na kusema 'Mungu wangu, hivi kweli ni wewe mwanangu unanikana, na kuniona mimi ni bibi yako, yaani umenidharau kiasi hiki, hapana haiwezekani, kwanza angalia mavazi uliyovaa na rangi yako umekuwa kama mzungu, mmmh,mmh ni kitu gani kimekupata wewe" Mama yule aliongea kwa uchungu huku machozi yakiwa yanamlengalenga, Chichi hakujali na kusema "Mama acha ushamba huku ni mjini bwana watu tunakwenda na wakati, kwanza wewe ondoka rudi nyumbani unanitia aibu, embu tizama hizo nguo ulizovaa ,ondoka bwana mimi nitakuja kukusalimia nyumbani' Yule Mama alisikitika sana na kuondoka akisema "Sawa mwanangu mimi naondoka, siamoni kama unaweza kubadilika kiasi hiki, leo hii unanitizama mimi nakuniona mchafu, asante mwanangu".

 Mama yule aliondoka na alipofika nyumbani kwa kaka yake hakumueleza chochote alinyamaza kimya na kesho yake alirudi kijijini.Siku zilienda huku Chichi akiendelea kujichanganya katika kumbi mbalimbali za starehe ilifikia kipindi akagombana na mjomba wake na sasa alianza kuishi maisha kwa kuetegemea wanaume yaani alibadilisha wanaume kama nguo. Baada ya miezi michache alipata ujauzito. Ndipo alipochanganyikiwa kwani hakujua ile mimba ni ya nani.Alirudi nyumbani kwa mjomba wake kumuomba msamaha baada ya maisha kuwa magumu sana, lakini mjomba wake alitaka arudi kijijini kwa mama yake na kwa wakati huo mimba ilikuwa ina umri wa miezi saba.

Ilikuwa imepita miaka miwili bila kuwasiliana na Mama yake. Alipofika alipiga magoti chini huku akilia kwa uchungu na kumuomba msamaha Mama yake ambaye alibaki akimtizama huku machozi yakibubujika katika paji la uso wake "Leo hii unarudi kwangu kuniomba msamaha baada ya kuona umetenda kosa, mwanangu nilikuwa napenda usome ili uje kuwa na maisha mazuri, lakini wewe umechagua maisha ya starehe sasa tiza umebeba ujauzito, huyo mtoto hata baba yake humjui inaniuma sana. Nimekusame mimi ni Mama yako na nitabaki kuwa Mama yako." Alimkumbatia huku wote wakilia kwa uchungu. Maisha ya Chichi yalibaki kuwa ni ya pale kijijini baada ya kujifungua. Siku zote alikuwa akimuheshimu Mama yake na kujutia makosa aliyotenda.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom