Ijumaa, Mei 30, 2014

MAFUTA YANAYOANIKWA JUANI NI HATARI KIAFYA


Mkaguzi wa Chakula wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TDFA) Kanda ya Kati,  Albert Deule, amewataka wananchi kuacha kununua mafuta ya kula yanayouzwa juani kutokana na kuwa na athari kubwa ya kiafya, ikiwamo kusababisha ugonjwa wa saratani.

Deule alitoa tahadhari hiyo wakati akijibu swali la mshiriki wa mafunzo kwa wajasiriamali wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa, wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.

Alisema ni vyema wauzaji wa mafuta hayo wakayaweka mbali na jua kwani kitendo cha kuuza yakiwa yameanikwa juani yanakuwa na athari kubwa za kiafya kwa watumiaji.

Alifafanua kuwa, jua husababisha mafuta kuchacha na kutengeneza sumu inayoweza kuleta madhara mwilini ikiwamo kusababisha saratani.
Alisema mafuta ambayo tayari yamechacha na kisha kwenda kuchemshwa madhara yake ni makubwa zaidi mwilini.



“Mafuta yanayoanikwa juani ni hatari kiafya, njia sahihi kwa watumiaji ni kuyakataa, kutokana na  watu wengi wanapata magonjwa ya tumbo na hata kusababisha saratani kwa kutumia mafuta hayo yasiyofaa, ni vema yakawekwa mahali salama wakati yanapouzwa” alisema Deule.

Pia alisema ni muhimu kwa wajasiriamali kutafuta namna nzuri ya kufungasha mafuta na siyo kama ilivyo sasa ambapo hata chupa za maji zilizotumika zimekuwa zikitumika kuuzia mafuta.

Alisema pamoja na kuwa vifungashio ni tatizo kwa wajasiriamali, lakini ni lazima wajali afya za walaji na wateja kwa upande wao wahakikishe wanakagua bidhaa muda zilipotengenezwa na muda wa mwisho wa matumizi ya bidhaa hizo ili kulinda afya zao.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom