Pages

Ijumaa, Juni 13, 2014

BAJETI 2014/2015 KASHESHE

Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya akionyesha mkoba uliobeba Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Dar es Salaam. Kinyume na matarajio ya wananchi walio wengi ya kupata unafuu katika kodi za bidhaa mbalimbali, Bajeti ya Serikali iliyosomwa jana imekuwa ya maumivu kwao ikipendekeza wakamuliwe zaidi lakini ikaja na mikakati ya kudhibiti misamaha ya kodi na kupunguza matumizi.
Kinyume na bajeti ya mwaka jana iliyoonekana ni ‘majanga’ kwa kila eneo, mwaka huu Serikali imetoa ahadi za kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika ununuzi na misamaha ya kodi ili kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye shughuli muhimu za maendeleo na huduma za jamii.
Hayo yamo katika hotuba ya Bajeti iliyosomwa bungeni, Dodoma jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Hata hivyo, uamuzi huo kama njia ya kupate fedha zaidi umeelezwa kuwa ni ‘mzuri wenye tatizo la jinsi gani ya kupima utekelezaji wake’.
Mhadhiri wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Goodluck Urassa alisema kuna matatizo makubwa ya uwajibikaji yanayoweza kuzorotesha nia njema ya kubana matumizi na kudhibiti misamaha ya kodi.
Pia, katika hotuba hiyo kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi kutaka kupunguziwa kodi kwenye mshahara hadi chini ya asilimia 10, kimeendelea kuwa kitendawili baada ya Serikali kupunguza kwa asilimia moja tu, kutoka 13 hadi 12 huku Kima cha Chini cha Mshahara (KCC), kikielezwa kwamba kitaongezwa lakini bila kuwekwa wazi kwa kiwango gani.
Hotuba hiyo pia haikubainisha vyanzo vipya vya mapato vilivyoainishwa, suala ambalo awali, lilizua mvutano mkali kati ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Badala yake, imeendelea na utamaduni uleule wa kuzikamua kodi bidhaa zilezile zikiwamo soda, pombe, sigara na magari.
Hata hivyo, Waziri Mkuya alisema Bajeti yake imelenga kupunguza gharama za maisha ya wananchi kwa kuendelea na jitihada za kudhibiti na kupunguza mfumuko wa bei, kuboresha huduma za jamii, miundombinu ya barabara, umeme na umwagiliaji.
Kudhibiti matumizi
Mkakati kabambe aliokuja nao Waziri Mkuya ni wa kuimarisha zaidi usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, kuongeza nidhamu ya matumizi na uwajibikaji kwa wadau wote wanaotekeleza Bajeti ya Serikali.
Pengine jambo muhimu katika mkakati huo ni kuunganisha matumizi yote ya Serikali, yaani wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa, mamlaka za Serikali za mitaa na wakala na taasisi za Serikali chini ya mfumo mmoja wa udhibiti wa fedha za umma unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali.
Katika kutekeleza hilo, kuanzia sasa hakuna taasisi yoyote ya umma inayokusanya maduhuli itakayoruhusiwa kutumia fedha walizokusanya kabla ya bajeti yao kupitiwa na kuidhinishwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali na fedha zote zinazozidi bajeti iliyoidhinishwa zitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Utaratibu huu unatumiwa na nchi nyingine duniani zikiwamo nchi jirani na kwa hapa Tanzania utaratibu huu unatumika kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania,” alisema Waziri Mkuya.
Ili kuondoa tatizo la utekelezaji wa miradi ya chini ya viwango,  Serikali imenunua vifaa vya kuhakiki ubora wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inawiana na uwekezaji katika miradi husika na kuwabaini makandarasi dhaifu katika ujenzi wa miundombinu na kuwachukulia hatua.
Vile vile Waziri wa Fedha alitangaza mpango wa Serikali wa kufanya ununuzi wa pamoja (bulk procurement) kutoka kwa wazalishaji badala ya kutumia wakala kama ilivyo sasa na hatua imeanza kuchukuliwa ili ununuzi wa magari na vyombo vya Tehama ufuate utaratibu huo.
Alisema katika mwaka ujao, vitabu vya kumbukumbu (diaries) na kalenda za kila mwaka, zitachapishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu tu na kuondokana na utaratibu wa sasa wa wizara, idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za Serikali, mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa kila moja kuchapisha kwa utaratibu wake.
Ukiacha eneo la matumizi, waziri alisema Serikiali inalenga kuongeza mishahara ya watumishi wa umma, kuendelea kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, kuongeza fursa za ajira na kuimarisha utawala bora.
Kuhusu Kodi
Waziri huyo alisema kodi katika vinywaji baridi, ushuru kwenye maji ya matunda (juisi), mvinyo na sigara vinatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh124, 2 milioni.
Katika magari, Serikali inatarajiwa kuongeza kodi kwa yale yatakayoingizwa nchini yakiwa yametumika kwa zaidi ya miaka minane baada ya kubadilisha ukomo wa umri wa magari yasiyo ya uzalishaji (non-utility vehicles) na magari ya uzalishaji na yasiyobeba abiria (non-passanger utility vehicles), kutoka miaka 10 hadi minane.
Katika suala la misamaha ya kodi ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi na wabunge, Waziri Mkuya aliainisha baadhi ya mabadiliko katika Sheria ya Kodi na Uwekezaji yakiwamo ya kuondoa saruji katika orodha ya bidhaa zinazofikiriwa kuwa za mtaji, kufuta misamaha ya kodi iliyokuwa inatolewa kwa kampuni za simu, kuongeza mtaji wa wawekezaji wanaotoka nje kutoka Dola za Marekani 20 milioni hadi Dola 50 milioni.CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom