Natumaini wajukuu zangu ni wazima wa afya, mkiwa bado baadhi yenu mnaendelea na mfungo wa Ramadhan. Leo wajukuu zangu nina mada nyepesi ambayo naamini inawagusa wengi.Kabla ya kuanza mada yetu ya leo ni vizuri tukafahamu maana ya uvivu.
Uvivu ni neno ambalo limezoeleka katika vinywa vyetu, lakini naamini wengi wenu hamfahamu maana ya neno hili.
Uvivu ni ile hali ya kutotaka kufanya kazi. Ukihisi una tabia ya kutotaka kufanya kazi bila shaka wewe ni mvivu.
Wapo baadhi ya watoto wanaamini eti, uvivu ni ugonjwa ambao mtu anaweza kutibiwa hospitali. La hasha hilo si kweli. Uvivu ni tabia tu ambayo mtu anajizoesha na baadaye anajikuta linakuwa jambo la kawaida kwake.
Baadhi ya watoto huwa wanaanza tabia ya uvivu kwa kukwepa kufanya kazi za nyumbani na kama mzazi hajagundua hilo mapema mtoto huyo ataendelea na tabia hiyo hata katika masomo yake darasani.
Mwanafunzi mwenye tabia ya uvivu hatoweza kufanya mazoezi aliyoagizwa na mwalimu na hasara ya kwanza atakayoipata ni kushindwa kujipima katika mitihani kwa kile alichosoma na hatimaye lazima atafeli mitihani yake.
Pia inaweza kupeleka mwanafunzi mwenye tabia hiyo ya uvivu kuwa mtoto au kuacha kabisa shule kwa sababu hapendi kubughudhiwa kama hajaandika au kukwepa kufanya mazoezi darasani.
Mtoto mwenye tabia ya uvivu kama hatokemewa na kuacha tabia hiyo anaweza kuwa mvivu hata katika mambo ya msingi katika maisha yake ya kila siku. Mfano anaweza kuwepa kuchota maji yake ya kuoga sababu tu ya uvivu umemtawala na matokeo yake anapata magonjwa ya ngozi kwa kukosa kuoga.
Ni vyema wazazi mkahakikisha watoto wenu wasiwe na tabia ya uvivu ili waweze kujiepusha na madhara kama hayo. Ni vizuri wazazi wakajenga tabia ya kuhakikisha watoto wanashiriki kazi za nyumbani ipasavyo na kushirikiana kwa karibu na walimu ili kujua tabia za watoto wenu kama kuna tatizo muweze kulitatua mapema.
Pia wazazi mnatakiwa kuhakikisha watoto wanafanya mazoezi ya viungo ni njia nzuri ya kumfanya mtoto aondokane na uvivu. Mazoezi yatawasaidia pia wawe na afya bora na kuwa wakakamavu na wachapakazi wazuri. Nina imani wajukuu zangu wote mliokuwa na tabia ya uvivu mtaiacha tabia hiyo na mtaanza mazoezi ili msiwe wavivu tena.
Imeandaliwa na Hafidhi Hamisi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni