SEHEMU YA TATU
Niliendelea kumsihi Nadia asiendelee kulia kilio
kikuu namna ile. Laiti kama angechomoka katika mikono yangu bila shaka
angefanya kitu kimoja kibaya sana, ndio! Nilihisi ni kibaya lakini sikujua ni
kitu gani angeweza kuongozwa na hasira zake kukifanya.
Hatimaye alitulia akabaki kulia kwa kwikwi tu binti
yule aliyekeketwa katika safari yake ya kutafuta ndoa. Ndoa ya hayawani!!
“Unajua Nadia, sometime you have to let it go…ukiwa
mtu wa….” Kabla sijamaliza akiwa amelala chali aliyaingilia maongezi yangu.
Wakati huu sikupata nafasi ya kukishika kifaa changu cha kuinasa sauti yake.
Hivyo nikaweka umakini kumsikia anachotaka kusema. Huenda katika kauli yangu
fupi kuna kitu alikumbuka.
“Desmund! Alikuwa na lafudhi mbaya kweli, hakujua
hata ‘give me some water’ ina maanisha nipe maji ya kunywa, sikupenda kuonekana
nipo juu yake kwa kila kitu, nikamwanzishia kozi ya kujifunza kiingereza.
Wanafunzi wenzake walimcheka alivyoshindwa kujitambulisha iwapo yeye ni ‘boy’
ama ‘girl’ nikasimama kidete kumshauri juu ya hilo nikampa moyo asonge mbele.
Akanielewa akazidi kujituma, mwishowe akaanza kukijua kiingereza.
Wakati huo
sijui hata kama atakuja kukitumia kila kiingereza vibaya kwa kuniambia ‘you
bitch pack your things and leave! My house!!’….sasa niende wapi na kwa kosa lipi
sijui, halafu ilke nyumba kodi yote nilikuwa nimelipa mimi lakini akadai ni
nyumba yake nichukue kilicho changu niondoke. Hakuishia hapo akaniuliza swali
ambalo lilinifanya nimuone mpuuzi na mwendawazimu, eti ‘don’t you understand
English?’ ..sasa mimi nimemchukua akiwa hakijui hata hicho kiingereza lakini
leo hii ananiuliza eti iwapo sijui kiingereza was he crazy!!!” hapa Nadia kwa
mara ya kwanza tangu tuanze safari alifanya kicheko kidogo, kasha akaendelea
“wanaume huwa mnakuwa wapumbavu sana mkishashika pesa kidogo halafu mkagundua
kuwa mnapendwa mnavimba sana vichwa. Basi Desmund akawa ana kiburi
kilichopitiliza, eti hapo kisa tu nilimwambia yeye ni kila kitu kwangu. Desmund
akayatumia madhaifu yale kunifanya apendavyo.
Unajua kaka…katika haya maisha hakika tunatenda
maovu mengi sana, mengine yanasameheka lakini kwa akili ya kibinadamu mengine
yanakuwa magumu sana kusamehe, ujue kucheza na akili ya mwanadamu mwenzako ni
kitu kibaya sana maana hujui ataathirika kiasi gani akijua kuwa unamchota
akili. Fikiri kuhusu Desmund yaani na miaka yake thelathini na mbili, alikuwa
ananidekeza sana. Nitake nini Desmund asinifanyie, mara apike uji mara anibembe
mgongoni. Nikinuna kidogo ananibembeleza na kila alivyonikumbusha kuwa
ananipenda sana mwanaume alitoa machozi, alilia haswaa. Chozi lake nililiona la
thamani sana lakini nikagundua baadaye kuwa anacheza na hisia zangu, niliumia
alivyokuwa analia lakini yeye alikuwa akinitukana kuwa niache kujilizaliza.
Niache kujiliza wakati nimeumizwa kabisa, Desmund hakuliona chozi hili
akawasaidia wale wanawake kunitawanya miguu yangu kisha wembe mkali ukanifyeka,
nikakeketwa Nadia mie. Nikakeketwa ili niolewe.
Wakati mwingine najilaumu mimi mwenyewe halafu
nahisi ni laana hii inaniandama kakangu, hii itakuwa laana tu. Ujue mama alilia
sana siku ambayo baba alikuwa ananifukuza nyumbani, wadogo zangu walilia sana
kaka, wote wakanisihi kwa kiarabu kuwa nibadili maamuzi yangu. Tayari alikuwa
amechaguliwa mchumba wa kiarabu kutokea Jedah kwa ajili yangu nikimaliza chuo.
Mchumba ambaye alinivumulia tangu nikiwa mdogo hadi nikiwa chuo kikuu, huyo
nikaona hana maana nikakabidhi maisha yangu kwa Desmund. Mama alisema maneno
mengi huku akigalagala chini, alilia sana, na kwa mara ya kwanza katika maisha
yangu mzee wangu Ramadhani licha ya ukorofi wake uliokithiri na usiomithirika
alitokwa na chozi katika jicho moja. Nikaondoka na sikutaka kuangalia nyuma.
Nikaenda kwa Desmund ambaye alikuwa kila kitu kwangu. Nikaamini kuwa nipo
katika njia sahihi kabisa, wala sikujilaumu!!
Elimu ilinipotosha hakika, bila elimu sidhani kama
ningeyajua mambo ya kujichagulia mume wa kunioa, mimi nilifunguliwa na elimu
nikajichagulia Desmund labda kweli elimu ni ufunguo wa maisha lakini kwangu
mimi el;imu ilinifungua na kasha ikanifunga katika utumwa wa mapenzi.
Mdogo wangu alinipigia simu kwa mara ya mwisho
akanieleza taarifa mbaya sana ambayo nd’o naiita laana maishani. Hakika ilikuwa
laana, mdogo wangu alikuwa analia na akaniambia waziwazi kuwa familia nzima
inanichukia tena inanichukia sana. Hakunipa nafasi ya kuongea neon lolote
aliendelea kuzungumza akinirushia lawama kuwa nimemuua mama, hapa nikahisi
kuzizima kabisa, Kassim akaniambia kuwa mama alikufa akinilaumu kwa kila neno,
na neno lake la mwisho alisema ‘Nikifa mnitupe baharini ama mnichome moto simtaki
Nadia kaburini kwangu, sitaki kuisikia sauti yake, kama ataweza aiombe bahari
initapike kama ataweza ayaombe majivu yaungane tena aweze kuniona. Msinizike
aje kulowanisha kaburi langu na machozi yake yaliyolaaniwa, sitaki kelele za
kilio chake zinisumbue katika usingizi wangu wa milele. Mwambieni namchukia
kupita watoto wangu wote kwa yote aliyonifanyia na kunifedhehesha!!!’. Maneno
yale yalikuwa makali sana, kisha simu ikakatwa. Nilipojaribu kupiga
haikuwezekana.
Simu ilipigwa kutoka katika vibanda vya simu Jeddah
Saudi Arabia.
Huo ukawa mwisho wa kuwasiliana na ndugu zangu,
ndugu pekee alibaki kuwa Desmund, na nilimweleza yote haya kuwa mama yangu
amekufa akinilaani, nikamsihi Desmund awe mkweli kwangu ili mama yangu popote
alipo atambue kuwa huyu alikuwa mwanaume sahihi, najua roho ya mama inanizomea
kwa wakati huu kwa sababu nimeaibika tayari. Nilimvumilia Desmund ili mama
asijue kama tuna matatizo katika familia lakini haikuwa hivyo kwa upande wangu,
kwa maana hiyo Desmund aliona sawa tu nilivyochukiwa na familia, aliona sawa tu
mama yangu mpenzi alipokufa akinilaani, yaani kwa ufupi kila lililo baya
Desmund aliona sawa tu….aliona Nadia alizaliwa ili ateseke…Desmund u mwanaume
gani sasa wewe…eeh Desmund..” kilio kikamzidi…akajilaza tena, nikampiga piga
begani bila kusema naye lolote. Huku nikidhani kuwa amenyamaza na hatazungumza
tena kumbe alikuwa akijifuta machozi kisha akaendelea, sasa alikuwa anakaripia.
Ni kama mbele yake alikuwapo huyo wa kuitwa Desmund….hapa nilikumbuka kurekodi.
“Mbona alifanya hivyo Desmund!! Naamini alifanya
yeye japo sina uthibitisho lakini Desmund alinitafutia sababu maksudi, kivipi
mwanamke ambaye nimeamua kupoteza kila kitu kwa ajili yake ashindwe
kunisikiliza na kujifanya anamuamini sana Frank, Frank si amekutana naye akiwa
ameng’ara tayari, wanajifanya wanajua sana wanaongea kiingereza cha kipumbavu,
kiingereza nilichoongea darasa la pili wao wanakuja kukiongea mbele yangu na
kujifanya wananificha wanachozungumza. Yaani rafiki yako anakueleza kuwa mkeo
ni Malaya nawe unatabasamu unasema ndio ndio….Desmund hivi ulirogwa. Walikuroga
Desmund!!! Umuulize basi niliufanya wapi, si ni huyu nilikwambia anavyonitazama
sipendi maana anaonyesha matamanio, mwanzoni ukanielewa leo hii anakuletea
ujinga kwamba mimi nilikuwa Malaya SAUT (Saint Augustine University Of
Tanzania) na wewe unaamini Desmund, ama hakika walikuroga wewe si bure nasema,
sio wewe ulifanya mapenzi na mimi mara ya kwanza nikikueleza kuwa sijawahi
kushirikiana na mwanaume tangu nizaliwe, sio wewe nilikueleza kuwa nilikuwa
nangojewa na bweana wa kiarabu anioe huku nikiwa na bikira yangu, huo umalaya
niliufanyia mdomoni we fala!! Nakuuliza niliufanyia mdomoni mimi, au
niliufanyaje sasa hadi ukanikuta na bikira yangu. Desmund kumbe u mpumbavu
kiasi kile, mimi nikawa mpuuzi nikafanya sherehe kubwa kukutambulisha kwa
rafiki zangu kama mchumba wangu. Marafiki wakakutukana kabisa kwa kunong’ona
kuwa wewe si saizi yangu, wakakucheka na kimwili chako kilichokondeana, hivi
ningekuwa wa kuitwa Malaya wewe nawe ulikuwa mwanaume wa kushiriki nami
mapenzi…..au kwa kuwa nilikusifu kuwa unaniridhisha kila siku Desmund.
Sikukusifu bure, sikufanya maigizo yoyote mimi, lakini aaah Desmund ukaja
kusema mimi ni mzigo tu kitandani tena Malaya wa kutupwa wewe na huyo rafiki
yako Frank mnanitukana, kumbuka nilikuokota mimi nilikuokota Deeees
niliku…..okotaaa….leo hii unanitupa kwa kishindo, nilikuokota wewe nikiwa
nikiwa peke yangu, kwa uamuzi wangu nikatumia pesa zangu mimi mwenyewe!!!
lakini unashirikiana na rafiki zako kunitupa Desmund….Desmu…..Desmuuu kweliiii
wanifanyia hivi kweli mimi yaani….aaargh!!!” hii haikuzuilika sasa, vifaa
vikawekwa kando nikachukua jukumu la kumbembeleza, alilia kwa sauti kuu sauti
ilishtua sana, kuna mengi moyo wa huyu dada ulibeba hakika.
Mimi nikazidi kuumizwa na hii simulizi na kwa mara
ya kwanza nikatamani kumwona huyo Desmund ili nimfikishe katika vyombo vya dola
kwa unyama huu, japo simulizi ilikuwa nusunusu bado. Japo kwa matukio hayo tu
ningeweza kumfikisha pabaya, walau kwa kalamu na karatasi ningemfanya dunia
aione chungu na mahali pasipokuwa salama kabisa.
KUMBE!!!!!
MOJA: Mama yake Nadia alimlaani vikali kiasi
kile!!! Je ni laana inaishi??
MBILI: Familia ilimtamkia kuwa inamchukia, na
wamekaa kimya moja kwa moja ama??
TATU: Desmund na FRANK!! Jina jipya tena huyu naye
anamuitaje mke wa mtu Malaya???
NNE: Desmund na kiingereza….hapa niliweka nukuu ili
niwe nacheka mwenyewe…hajui ‘boy na girl’ zina maana gani. Huenda elimu ndogo
nayo ilichangia.
TANO: Desmund akamkuta msichana ana bikra halafu analeta
dharau…bikra zilivyokuwa hadimu!!!
SITA: Hivi wapo wapi hawa akina Desmund mpumbavu na
Frank mshenzi?? Swali hili nililihitaji jibu lake sana.
“NADIA…..USILIE NADIA……nipo kwa ajili yamko”
niliyasema maneno yale kimoyomoyo huku nikiogopa asiweze kunisikia maana bila
shaka alikuwa akiwachukia wanaume wote na mimi nikiwemo…..
Maoni 1 :
Uwii story inaskitisha hii..
Chapisha Maoni