Mkurugenzi wa Tamwa , Valerie Msoka katika taarifa yake amelaani vitendo vinavyofanywa na baadhi ya waandishi wa habari pia wakiwemo watu ambao hawana taalamu ya uandishi kupiga picha za matukio ya ukatili wa kijinsia bila kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya habari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo moja ya matukio yaliyofanyika hivi karibuni ni picha za kutisha zilizomuhusisha mwanamke mmoja kutoka Tarime aliyeunguzwa sehemu za siri na mumewe kwa kukutwa na shilingi 2,000 anazotuhumiwa kuhongwa, picha hizo zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii Julai 13 mwaka huu.
Kufuatia tukio hilo taasisi na mashirika ya kiraia yamevitaka vyombo husika kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anakamatwa na sheria ichukue mkondo wake kwasababu vitendo vya aina hiyo vikiachiwa bila kushughulikiwa jamii bora isiyo na ukatili wa kijinsia haiwezi kufikiwa. Aidha Mashirika ya kiraia yanaamini kuwa matukio matukio ya ukatili yanapopigwa picha hususani yanapohusisha sehemu za siri za mwanamke ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wito umetolewa kwa waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma ya habari iwe ya kutoa habari au elimu kwa lengo la kujenga uelewa katika kupambana na madhara yanayotokana na ukatili wa kijinsia ndani ya jamii na taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni