SEHEMU YA SABA
Usiku ulipita nikiwa chumbani kwangu nikijiuliza,
wanaume tumelaaniwa ama? Nilikosa jibu kwa sababu na mimi ni mwanaume kama ni
kweli tumelaaniwa basi hata mimi nimelaaniwa pia. Nikakosa kundi la kumweka Desmund, nikakosa kundi
la kuwaweka wale wanaume waliombaka Nadia akiwa katika hali mbaya kabisa
kiafya, nikakosa pia kundi la kumweka Ramadhan Ramso yule mwanaume aliyempa
adhabu Nadia ya kufanya mapenzi hadi kupoteza fahamu eti kisa tu alimkatalia
ombi lake la kuwa naye katika mahusiano. Kisha baadaye akamkubalia.
“Sasa jamaa yeye ni nani hadi anataka kila
anapotongoza akubaliwe?” nilijiuliza. Bado nikakosa jibu, lakini mwisho kwa
shingo upande nikakiri kuwa tupo katika kundi moja lakini tabia
zilitutenganisha!!!
Hilo lilikuwa wazo langu la mwisho. Nikasinzia!!
Nilisikia kama midundo ya ngoma za kizaire, midundo
ambayo haikuwa katika mojawapo ya simu zangu. Halafu mbaya zaidi haikuwa katika
mpangilio maalum.
Nikajigeuza, kuzikwepa zile kelele, lakini mara
zikageuka!! Hazikuwa ngoma za kizaire, bali ulikuwa ni mlango wangu unagongwa!!
Nikasimama wima, nikapekecha macho yangu na
kujifunga taulo kiunoni nikajongea mlangoni nikaufungua malango.
Hah! Alikuwa ni Nadia, alikuwa amebadili nguo
tayari. Alikuwa ameng’ara na bila shaka alikuwa ametoka kuoga.
“Nchi itauzwa wewe!! Unalala hadi dakika hii, saa
tatu sasa.” Alisema huku akionyesha uchangamfu wa hali ya juu. Nikastaajabu,
nilikuwa nimelala sana. Nikatabasamu kisha nikainama na kukiri kuwa nilichoka
sana usiku uliopita.
Nadia akaaniambia yu chumbani kwake, nikaiufunga
mlango nikaoga name nikabadili nguo. Kisha nikamchukua kwa ajili ya kwenda
kupata kifungua kinywa!!
Wakati tunakabidhi funguo mapokezi. Yule muhudumu
akatuuliza iwapo tulihitaji kufanyiwa usafi ama la!
Mimi nikamwambia sikuwa nahitaji usafi Nadia yeye
akamtazama kwa muda bilakusema lolote.
Nikamvuta mkono kando na kumuuliza.
“Nadia,mbona haujamjibu sasa. We unadhani
atachukuliaje hapo…sikia Nadia usiruhusu kila mtu ajue matatizo yako sawa.”
Nilimkemea. Bado hakunijibu kitu, nikajua tayari kuna jambo limemtokea katika
akili yake kama kumbukumbu.
Nikamrudisha chumbani ili asije kusema lolote mbele
ya hadhira, na pia kwa upande wangu ilikuwa nafasi nyingine ya kupata majibu ya
maswali yangu ama kujua zaidi kuhusu Nadia.
Nikamwingiza chumbani kwangu. Nikategesha vifaa
vyangu.
“Mwandishi, sio kwamba nina dharau la! Sio kwamba
nilikosa cha kumjibu yule dada hapana! Lakini niliifikiria dunia isiyokuwa na
huruma. Dunia mbaya! Dunia inayotunza watu wabaya.
Hivi kweli unaweza kuwa mwanadamu mwenye moyo na
damu inayozunguka ukaamua tu kila mara kutumia matatizo ya mtu mwingine
kujinufaisha? Halafu mwisho unaheshimika mbele ya hadhira kama mtu mwema?
Sawa nilijipeleka mwenyewe, na nilihitaji sana
kuipata nauli ya kwenda Musoma. Sikuwa na raha ndo maana nikaenda pale.
Ningekuwa na raha wala nisingeweza kuingia katika kazi hiyo.
Wakati mwingine ni heri ufe katika tatizo moja
kuliko kuteseka katika matatizo mbalimbali ambayo kila moja lina uzito mkubwa
kuliko lile lililopita.
Duniani kuna matusi na kuna wakutukanwa, ujue
mabaamedi tunadharauliwa sana, yaani mwanmaume anakushika makalio anakutukania
mama yako lakini ole wako umjibu na achukie!! Eti mmiliki wa baa anadai ni
utovu wa nidhamu kumjibu hovyo mteja. Lakini nisingeweza kudhalilisha utu
wangu. Nisingeweza hata kidogo kujiuza tena kwa wanaume ninaowachukia.
Mtu unafanikiwa kumtoroka mteja na vishawishi vyake
halafu bosi nunayemuheshimu anadiriki kukufanyia ubaya!!
Sikujua kama yule bosi ninayemuheshimu angeweza
kunitenda vile, mimi nilijiuona nina msimamo sana na wateja walilifahamu hilo,
wewe nitukane nishike matako utakavyo lakini hunipati ng’o, hiyo ndo ilikuwa
kauli mbiu yangu.
Nitakufungulia chupa, ukitapika nitadeki ukivunja
chupa nitaokota lakini usitegemee nitakunyenyekea katika mwili wangu.
Nilikuwa nimejiwekea kiapo kuwa sitashiriki na
wanaume tena, nia yangu kuu ilikuwa kufanikiwa kufikisha nauli ya kwenda Musoma
kumkabili Desmund ambaye kuna maswali kadhaa nilitakiwa kupata majibu kutoka
kwake. Maana Jadida alivyoenda mara ya kwanza hakupata majibu sahihi, na hata
kabla hajajipanga kwenda mara ya pili akabakwa na kuuwawa.
Kutokana na msimamo wangu bosi wangu akanipandisha
cheo, nikatokea kuwa baamedi, nikawekwa kaunta. Huku napo nilikuwa makini sana
na pia mwepesi katika kuhudumia wateja. Bosi alikuwa akivutiwa na utendaji wangu
wa kazi haswaa.
Siku moja bosi alitoa udhuru kuwa anaumwa, na
ilikuwa lazima kukabidhi mahesabu jioni, nisingeruhusiwa kulala na pesa ya
bosi.
Bosi akapigiwa simu, akampa maelekezo bwana mmoja
anipeleke nyumbani kwake kukabidhi zile pesa.
Mimi sikuwa na shaka hata kidogo, nikaamini kuwa
bosi alikuwa mgonjwa. Majira ya saa nne huyo bwana akanipeleka nyumbani kwa
huyo bosi.
Nilipofika tu sebuleni nilitambua kuwa bosi alikuwa
anaishi na familia yake. Picha ukutani zilimwonyesha akiwa na familia, lakini
sikusikia hata kelele mle ndani. Bosi akajikongoja kutoka chumbani akiwa na
bukta, akaketi huku akijinyoosha viungo nikatoa heshima yangu na kisha kuweka
daftari na pesa mezani, tukaanza kupiga mahesabu. Lakini tofauti na siku
nyingine bosi wangu alikuwa hana umakini kabisa, nikakiri kuwa bosi alikuwa
anaumwa.
Lakini haikuwa hivyo, bosi hakuwa mgonjwa bali
ulikuwa mtego tu. Mara akaniomba nimwongoze chumbani kwake akalale kwani
kizunguzungu kilikuwa kimemzidia, mimi kama mwanadamu nikafanya alivyoniomba.
Nikamshika mkono mmoja na bega nikamkongoja hadi katika chumba chake.
Tulipofika nikadhani atajilaza kitandani lakini
badal;a yake akafunga mlango.
“Nadia, ni kweli naumwa…..lakini naumwa ugonjwa wa
mapenzi.” Bosi alizungumza huku akionyesha uimara. Nikaduwaa maana sikutegemea
jambo hili.
“Hivi Nadia kweli,muda wote huo haujui kama
nakupenda. Mimi nimekutoa kwa wale walevi, nimekuweka sehemu yenye pesa, hujui
tu kama nakuhitaji, nafasi yako nimewanyikakina Farida, Jeni ambao umewakuta
nimekuweka wewe hujajua tu kuwa nakupenda Nadia.” Alinibembeleza huku nikiwa
sijielewi bado kama ni ndoto ama vipi? .
Mara akanikumbatia yule mwanaume aliyekuwa
ametanuka kifua chake na kitambi kikiwa kinachungulia.
Nilijaribu kujitetea mwandishi, nilimsihi sana
lakini hakunielewa hata kidogo. Alikuwa katika matamanio ya hali ya juu.
Nikiwa bado katika kujitetea akanirusha kitandani.
Mwanaume ni mwanaume tu, ana nguvu na akiamua jambo
mkiwa wawili hashindwi kamwe!!
Sijui niseme bosi alinibaka la! Hakunibaka,
nilikubali yaishe. Maana tulilala naye hadi asubuhi, nikaoga naye huku kila
mara nikona aibu kuitazama picha ya mkewe ambayo ni kama ilikuwa ikinitazama
nikifanya uchafu na mumewe pale kitandani.
“Sijapenda iwe hivi mama!!! Nisamehe.” Niliiambia
ile picha wakati bosi ameenda kuoga.
Aliporejea alikuwa anatabasamu na kuniambia siku
inayofuata nisiende kazini, na atatoa taarifa kuwa sitaenda, nilikubali huku
nikijiahidi kuwa nitafanya kila niwezalo nipate kiasi fulani cha pesa nyumbani
kwa bosi huyo na kisha nitaacha kazi mara moja. Nikiacha kazi nitasafiri
kuelekea Musoma kutimiza azma ambayo haikumalizwa na Jadida.
Kilichokuja kutokea majira ya saa sita mchana ndipo
kilitokea kituko cha mwaka ambacho kiliyarejesha majonzi lakini kama hiyo
haitoshi niliandika historia nyingine.
Bosi alinikuta nikiwa sebuleni nikiwa nimejifunga
kanga za mkewe nikiwa natazama luninga huku nikiyafikiria maisha yangu kwa
ujumla. Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimeketi kwa utulivu katika nyumba kubwa.
Nikiwa na mtu ambaye namuamini pia.
Nikiwa kimada rasmi!!
“Nadia!” nilisikia sauti ikiniita kutoka chumbani.
Nikatambua ni bosi, nikaacha kutazama luninga
nikakimbilia chumbani.
Nilikutana na macho makali sana yakinitazama,
alikuwa ni bosi lakini huyu alikuwa ana hasira sana sikujkua nimemkosea nini
ama kuna nini kimetokea, alikuwa na bukta yake.
“Nadia wewe, wewe…..ni wa kuniletea mimi
kisonono!!” aliniuliza huku akitetemeka midomo.
Nikastaajabu bila kujua nini cha kujibu.
“Kumbe unapiga umalaya kimya kimya na kujifanya
wewe msafi sana. Nadia Malaya wewe…” alishindwa kuendelea akanivamia akanipiga
kibao usoni, sijui ilikuwaje lakini kanga ilifunguka nikabaki uchi, akanikamata
na kuanza kunichapa na mkanda, nikajitahidi kuomba msamaha lakini hakunielewa.
Alinipiga hadi nikatambua kuwa nikiendelea kuvumilia huyu mtu ataniua. Alikuwa
ana mkono mzito sana.
Na huu ulikuwa unyanyasaji wa hali ya juu sana,
yaani amenilaghai mwenyewe kufanya naye mapenzi, sikuwa na wazo la kuwa na
mwanaume. Nikajiweka mbali nao. Sikatai kuwa yawezekana nilimuambukiza huo
ugonjwa lakini alinilazimisha mwenyewe kufanya naye mapenzi.
Nilimsihi pia kutumia kinga lakini yeye mwenyewe
akanibiashia akalazimisha kila alichotaka kiwe. Kajiambukiza ama
nimemwambukiza? Nilijiuliza!!!
Nikapata jawabu kuwa yule mwanaume ananionea.
Ni hapa nilipoukumbuka ukaidi wa Jadida!!
Nikayakumbuka mabavu yake aliyokuwa akiwawekea wanaume!
Kwa mara ya kwanza nikaamua kujitetea, lakini
katika kujitetea kwangu nikafanya jambo dogo lililozua balaa huku
likinihamasisha kufanya zaidi na zaidi.
Nilijikusanya mwili mzima, kisha kwa kichwa kichwa
kama kondoo nikamvamia yule mwanaume nikiwa nimeyaunganisha meno yangu.
Nikamchota mithili ya ng’ombe nikamtupa mbali.
Kilisikika kishindo mara moja tu na kimya
kikatanda!!
Mwandishi nilikuwa sijawahi kuona maiti, hivi kumbe
kufa ni sekunde tu, bosi alijibamiza kichwa chake katika marumaru pale ndani.
Kimya kile kilikuwa kimya cha milele!!
Nilitoweka pale nikiwa nimetaharuki, nisijue nini
cha kufanya. Nikavaa nguo zangu vyema, nikatoweka pale ndani huku nikiuruka
mwili wa yule mwanaume!!
Hali ilikuwa ya hatari. Hatua kwa hatua hadi nje!!
Nilisikia uzito fulani katika sketi yangu,
sikumbuki niliweka nini hapo awali. Nilipojipekua nikakutana n’na kibunda cha
pesa.
Bila shaka yule bosi aliniwekea maksudi kama
shukrani kwa penzi nililompa. Na hii ni kabla hajagundua kama nimemwambukiza
kisonono. Niliondoka mbio mbio baada ya kutoka nje.
Nilirejea nyumbani kwa Chausiku majira ya usiku
sana, huyu ndiye msichana ambaye alikuwa akinihifadhi katika chumba chake huku
akiwa anafanya kazi katika baa nyingine jirani na ile niliyokuwa nafanya mimi.
“We Nadia wewe…..umemfanya nini tena bosi wako?”
aliniuliza huku akiwa na hofu tele.
“Kwani nini?” nilijifanya sijui lolote.
“Bosi wako si amekutwa amekufa wewe..na wanadai
kuna uwezekano kuwa ulilala kwake mwenzangu…mbona kazi sasa.” Alinieleza kwa
sauti ya kunong’oneza, kisha akaendelea.
“Nadia mimi dada yako nambie nini kimetokea.”
Alinisihi.
“Dada Chausiku mi nimemsukuma tu alitaka kunibaka,
kanipiga sasa dada kanipiga kidogo aniue nikajitetea kwa kumsukuma mimi sikuua
dada!!!” nilimweleza huku nikiwa nalia.
“Nadia, cha msingi wewe ondoka hapa Mwanza, mimi na
wewe ni maskini. Na unafahamu hatuna cha kuwabishia wale wenye pesa, Nadia
nilikukuta ukiwa na msiba mzito siku nakuchukua tafadhali sitaki nilie tena
ukihukumiwa kwenda jela. Ondoka Nadia ondoka!!!” alinisihi dada yule. Kisha
akaingia ndani akatoka na kikopo chake cha kuhifadhia pesa. Akakifungua na
kutoa pesa aliyokuwa amehifadhi shilingi elfu ishirini akanipatia.
Nilimtazama, sikuichukua ile pesa nikamkumbatia kwa
nguvu, nikahisi upendo mwingine ukitoweka kwangu, nikajipekua katika sketi
yangu nikalifungua lile burungutu. Nikatoa noti nne nyekundu nikampatia.
Akazikataa na kuniambia kuwa nilikuwa ninayo safari ndefu sana mbele yangu.
Akanisihi niende kwa amani…..nililia sana!!
Baada ya siku mbili, Nadia nilikuwa natafutwa kwa
kosa la kuua!!
Nikaingia rasmi katika safari nyingine ya maisha ya
kikimbizi, yaani ukimbizi katika nchi yangu huru kabisa!!!!
Lakini ningefanya nini iwapo nimelaaniwa!!!
Nina njaa naomba twende kula” alimaliza
Nadia….akafuta machozi!!
Nilipata mshtuko kusikia kuwa kumbe Nadia aliwahi
kupata kesi ya mauaji!! Laiti angekuwa amemuua Desmund wala nisingeshtuka,
kumbe aliua katika jiji ambalo yupo kwa sasa. Mwanza!!! Lakini hakupanga kuua.
Halafu kumbe Jadida aliwahi kwenda Musoma…harakati
zipi zilimpeleka dada huyo ambaye ni marehemu tayari. USIKOSE NINI KITAENDELEA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni