Desmund alinishangaa sana hadi
nami nikaanza kujishangaa kuwa huenda ni kweli nimemfananisha. Nikaanza kugwaya
na kumsikililiza kwa makini kila neno alilokuwa anasema.
Lakini kutokana na kuduwaa kule niliishia kuona tu
mdomo wake ukichezacheza bila kusikia ni kitu gani alikuwa akisema. Pia macho
yangu yaliishuhudia hasira kali kutoka machoni mwake. Macho yalikuwa mekundu na
alinyesha chuki ya waziwazi, sijui kwanini niliendelea kuamini yule ni Desmund
na wala sijamfananisha, japo nilikuwa naelekea kukata tamaa sikufikia hatua ya
kumkwepa niliendelea kumkabiri.
Ile hali ya kuamini kuwa yule aliyepo mbele yangu
ni Deus ilinifanya nishikwe na donge zito kooni, donge ambalo lilinikera na
kunifanya nisipumue vizuri. Nilipojaribu kumeza mate ili kulilainisha, uso
wangu ukachafuka kwa machozi.
Macho yakaikosa nuru na nikashindwa kabisa kuona
mbele kulikoni. Nikawa naona kama ukungu na mara badala ya kuwa kiwiliwili
kimoja cha Desmund, sasa vikaongezeka na kuwa viwili. Sikujua kile kingine ni
cha nani.
Kile kiwiliwili kipya kikaanza kunisogelea huku
kikiwa katika mavazi ya kanga. Kabla sijakitambua kikanibamiza na kitu kizito
usoni. Maumivu niliyoyapata hayasimuliki, nikapangusa machozi
na mara nikakutana ana kwa ana na yule mke wa Desmund. Mwanamke aliyejifanya ni
dada yake Desmund, nikamheshimu na kumtunza vyema jijini Mwanza lakini baadaye
nakuja kugundua ni mke wa mume wangu!!
Desmund!!
Mshtuko nilioupata ukanifanya damu ichemke sana na
mara nikahisi mchuruziko puani, nilipojishika na kutazama nilikuwa natokwa
damu. Yule mwanamke alivyonibamiza na kitu kizito usoni, kisha nikakumbwa na
mshtuko.
Sasa nilikuwa natokwa damu!! Yule mwanamke kuna
maneno aliyokuwa anaongea kwa kikabila, baadhi niliyatambua kuwa ni matusi, kwa
sasa hayana haja ya kukweleza maana nitakuwa kama nakutukana mwandishi katika
kabila usiyoijua.
Niliyavumilia yote lakini akavuka mipaka
akanitukania na mama yangu wa kunizaa, yule mama aliyezikwa tayari huku akiniachia
laana kuwa hanipendi. Sasa watu waliosababisha niuone uchungu wa laana
wanamtukana marehemu mama yangu.
Mwandishi!! Kama nilivyokueleza awali kuwa huenda
Jadida aliniachia roho yake ya ujasiri na ukatili. Nilimvamia yule mama mwenye
mwili kunipita mimi, hakutarajia ujio ule, nilimshika nywele zake ndefu,
nikazivuta. Alipiga yowe kubwa. Nadhani unafahamu maumivu yanayopatikana
ukivutwa nywele. Desmund akanivamia pale na kuanza kunipiga ngumi mgongoni
lakini sikumwachia mkewe yule, nikazidi kuongeza nguvu.
Naam! Nikaridhika hatimaye, nywele zikakatika!!
Nikawa nimemnyoa bila kutumia mkasi. Nikamwachia
akaanguka chini kama mzigo.
Mwandishi, nikiwa sijui hili wala lile, mara
niliona kundi la watu lililokuwa likishuhudia ugomvi ule likitawanyika. Mara
nikamwona mbwa mkubwa aklielekezwa kunishambulia. Si mbwa aliyenifadhaisha la!
Ni mtu aliyekuwa anamwelekeza kufanya vile.
Ni mama yake Desmund!! Yule mama aliyeugua sana
Desmund akakata tamaa kuwa lazima mama yake atakufa, nikachukua ada yangu ya
chuo kwa penzi langu kwa Desmund na familia yake nikaamua kumuhudumia mama hadi
akapona. Desmund na mama yake wakasema mimi ni Mungu wao, nikakataa wasiniite
hivyo. Mama yule akadai kuwa hatanisahau kamwe katika maisha yake, nikafurahi
kuwa nimepata mama mkwe anayenipenda kwa dhati, kisha akaongezea kwa kumkanya
Desmund akimwambia kuwa ‘ole wake aje kuniacha siku moja’. Sasa yule mama
ambaye nilishatambua kuwa alikuwa mnafiki mkubwa alikuwa ameshikilia mbwa na
akiielekeza kuja kwangu. Anaielekeza kuja kunifanyia shambulizi mimi Nadia
Mungu wake katika shida iliyomkumba. Sasa ni adui yake nikiwa mimi nina shida.
Mwanadamu!! Usimtendee mtu wema ukatarajia
atakulipa wema vilevile, moyo wa mwanadamu una siri nzito. Mdomo wake
unadanganya na sura yake inashawishi na anaweza kutokwa machozi, sauti yake ya
upole ikikulaghai kuwa ana uchungu sana nawe ukasema huyu ndiye sahihi!! Kumbe
ule moyo usioonekana unakukejeli na kukutukana matusi mazito!! Eeh! Mwenyezi
Mungu ungenionyesha muujiza.
Hapo nikajikuta nimefanya kosa kubwa kupindukia,
nilisimama na kujaribu kukimbia. Yule mama aliyekuwa na uso wenye hasira kali
alimuachia yule mbwa!!
Mbwa akatii amri ya bosi wake!!
Desmund badala ya kumzuia yule mbwa yeye
akamsisistiza, yaani Desmund akafurahia mimi kukimbizwa na mbwa! Desmund akatoa
tabasamu kali mimi kudhalilika katika kijiji nisichokijua.
Sijui kwanini Mungu aliniruhusu kugeuka na
kumtazama Desmund jinsi alivyokuwa ananicheka!! Maana nilizidisha chuki dhidi
yake, badala ya kumkimbia mbwa nikataka kumkimbilia Desmund! Kabla sijamfikia
yeye mara mbwa akanirukia na kunitupa chini.
Neno la mwisho kulisikia tena kwa sauti ya
Desmund!!!
“Huyu Chokoraa sijui katoka wapi maskini wee!!”
Desmund akaniita mimi chokoraa na hatambui wapi
nilipotoka!!
Huenda alikuwa sahihi kabisa, kama marafiki zangu
niliosoma nao hawakunikubali tena wakadai nina majini, familia yangu ilinikataa
na mama akanilaani.
Naam!! Hakik nilikuwa chokoraa, lakini kuwa
chokoraa mbele ya Desmund ni uongo uliotukuka. Sikuwa chokoraa, alijua kabisa
maovu aliyonifanyia.
Mara yule mbwa akakutanisha meno yake makali katika
paja langu!! Na hapo ndipo kiza kikatanda, kabla nuru haijatoweka nililiona
tabasamu la dharau kutoka kwa Desmund!!
Kilio cha mbwa nacho kikasikika, bila shaka alikuwa
anafurahia paja!
Kisha kimya!! Sikujua nilipoteza fahamu kwa muda
gani.
Nilipozinduka nilikuwa nina pingu mkononi. Kila
mmoja alikuwa ananizomea, lazima kuna kitu walikuwa wameambiwa aidha na Desmund
ama mama mkwe wangu yule mnafiki. Walinizomea huku wakicheka haswa!!
Wakati huu nilikuwa katika mkeka, mtu pekee ambaye
nilimwona kuwa mkarimu alikuwa ni nesi, ambaye bila shaka ndiye aliyenifunga
bandeji katika kovu langu pajani.
Kovu la kung’atwa na mbwa!!
“Samahani dada nahitaji kuondoka hapa.” Nilimweleza
yule nesi.
“Oooh!! Huwezi kuondoka dada wanadai hapo kabla
umewahi kuwa na kichaa cha mbwa ni vyema twende hospitali kwanza, halafu na
hawa polisi wanahitaji kuzungumza na wewe.” Aliniambia kwa upole sana.
“Nesi, sijawahi kuugua ugonjwa wa hivyo mimi.”
“Usijali dada utakuwa salama muda si mrefu!!”
“Na mbona wananizomea viumbe hawa sasa.”
“Eti ulivua nguo zako ndipo wakakushikishia mbwa
maana ulitaka kuleta hatari msibani, ulitaka kufukua kaburi. Yawezekana ukichaa
ulipanda, lakini usijali mrembo kila kitu kitakuwa sawa mama eeh!” nesi aliendelea
kunieleza vitu ambavyo vilikuwa kama simulizi tu maana nilikuwa na akili zangu
timamu na nilikuwa najua chanzo cha yote yaliyotokea.
“Nesi mimi ni mzima tafadhali niamini!!”
“Hapana binti, usingeweza kumng’oa yule mama nywele
zake kwa kutumia mikono. Na kama hiyo haitoshi yule mbwa usingeweza kumvunja
miguu yake kwa nguvu za kawaida.
Alipoongelea mambo haya nikakumbuka kile kilio cha
mbwa kabla sijapoteza fahamu, kumbe hakuwa akilia bure. Katika tapatapa yangu
nilimkamata miguu yake, hatimaye nikaivunja. Lakini eti haya yote ni kwa
ukichaa wangu.
Mimi Nadia baada ya kuzushiwa kuwa nina majini,
sasa Napata kesi kuwa nina ukichaa wa mbwa!!
Baada ya muda likafika gari la wagonjwa,
nikakimbizwa Musoma mjini hospitali.
Kama utani vile, ile hospitali ambayo ilishindwa
kumtibu Desmund alipovunjika miguu nami nikaingizwa humo.
Baada ya juma moja la matibabu. Nikahamishiwa
katika jengo jingine la serikali.
Rumande!!
Nikashikiliwa kwa kosa la kufanya vurugu msibani
kisha nikajeruhi na baadaye kutishia kuua. Aliyelalamika kutishiwa kuuwawa
alienda kwa jina la Desmund!!
Maajabu!! Huyu Desmund aliyenikataa kuwa hanijui,
akachekelea niking’atwa na mbwa sasa anadai tena mimi nimetishia kumuua!!
Desmund!! Sikutaka kuamini kama familia yao ilikuwa na roho za kawaida, kila
baya wananirushia mimi!!
Kila nilipotaka kuilaani familia yao nikakumbuka
kuwa laana ya mama ilikuwa inaishi. Laana ya mama ikanifanya niishi kama
kivuli, kivuli kisichopata muda wa kupumzika. Kila dakika kila sekunde nikawa
mtu wa majanga!!
Nilipokelewa rumande majira ya saa moja usiku,
tangu nesi anipatie chakula ile asubuhi nilikuwa sijapata chakula tena.
Nikapokelewa katika selo ya wanawake, nikakutana na wababe. Usiku ule nikalazwa
mbele ya mlango wa choo. Choo kichafu na kinachonuka, kumbuka ile bandeji
ilikuwa haijatolewa na nilikuwa na maumivu bado lakini yote haya hakuna
aliyejali. Nikaingizwa kule, katika siku nilizohisi kuwa dunia nzima imenilalia
ni hiyo!! Nilijaribu kutoa machozi yanifariji lakini hata yenyewe hayakutoka.
Kidonda, njaa, kisha nalazwa chooni!!
Mungu msamehe Desmund! Msamehe mama yake, lakini
Mungu usisahau kukilaani kizazi chake, ishushe laana yako Mungu! Ni wewe
ulisema tusihukumu lakini hebu nipe nafasi ya upendeleo, nihukumie kizazi
hiki..kiteseke kisha kimlaani Desmund, mama yake na yule mwanaharamu
mkewe!!”….hapa Nadia akasita kidogo kusimulia, akajifuta machozi, alikuwa
anatetemeka haswa, bila shaka ni hasira. Maana kwa simulizi yake hii hata mimi
nilijikuta namchukia mtu nisiyemjua hata sura yake. Desmund!! Hakika nilimchukia
mwanaume huyo, kisha nikajilaani kwa sababu hata mimi nilikuwa mwanaume!!.
Nadia alipomaliza kujifuta machozi na kupenga
kamasi akaendelea kusimulia.
“Nikabaki rumande nikiingoja siku yangu ya kusomewa
mashtaka. Hakuna mtu aliyeniletea chakula, nilikuwa mtu wa kudowea vya wenzangu
kila leo. Majira ya saa tisa nakula ugali na maharage mabovu!!
Mwandishi!! Hakuna kitu kama uhuru, ni heri uwe na
mateso mtaani lakini usifungwe mahali kama nilipokuwa uukose uhuru. Mbaya zaidi
sikuwa na kosa lolote sasa. Lakini nani atanitetea, sina ndugu wala rafiki!!
Ukimya wangu nikaona hauna maana hata kidogo.
Katika kusoma kwangu niliwahi kusikia kuhusu haki za mahabusu. Nikaamua
kunyanyua mdomo wangu na kuanza kumuita kila afande anayepita.
Nilipoona sisikilizwi nikaanza kupiga kelele kila
sekunde!! Nilitaka kuijua hatma yangu.
Hatimaye kelele zangu zikasikiwa na askari
mpelelezi aitwaye Daniel ama walivyozoea kumuita kwa jina la afande Dany.”
Nadia akakaa kimya kwa muda kisha akasema neno lililoniacha njia panda na kugundua
kuwa binti huyu amepitia mengi,
“Mungu amsamehe Dany kwa maovu yake, ampe kibali
kwa mema aliyotenda na kama itabidi basi alazwe pema peponi!!......Dany maskini
yaani alikuwa bado hata hajapata mtoto jamani, dah!! Sijui mama yake
alijisikiaje baada ya kifo chake, yaani haya maisha haya. Mwandishi naomba
nilale siwezi kusema zaidi kwa wakati huu.” Nadia akanyamaza na hakuendelea
kuzungumza.
Nikabaki kujiuliza maswali magumu.
MOJA. Kama Nadia alikamatwa kwa kesi ile, ilikuwaje
akatoka?
MBILI: DANNY ni nani na mbona Nadi anadai kuwa ni
marehemu tayari..
TATU: Harakati za Nadia kudai haki yake ziliishia
wapi??
USIKOSE SEHEMU YA 12. Wadau mniwie radhi kwa simulizi kuchelewa kutokana na mattizo kidogo ambayo yapo nje ya uwezo ila kwasasa mtaendelea kupata uhondo hadi mwisho wa simulizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni