Nadia alilala hatimaye, nikamsaidia kuviondoa viatu vyake
miguuni nikamfunika shuka kisha nikaishusha na neti ili asisumbuliwe na wadudu
warukao iwapo watatokea. Nilimtazama binti yule aliyekuwa amefumba macho, uso
wake ukiwa mwekundu na machozi yaliyomtoka muda mfupi uliopita yakiacha
michirizi.Nilitikisa kichwa huku mengi yakipita katika kichwa changu!!
Ni kipi kilimfanya hadi kila hatua anayopita akutane na mikasa mizito kiasi
hiki.
Japo mimi nilikuwa sijwahi kutokewa na msala kama huu lakini
nilikiri kuwa kama ningevaa viatu vya Nadia na kuwa yeye. Kwa haya magumu
aliyopitia bila shaka ningekuwa nilishajikatia tamaa kitambo kirefu na labda
hata ningekuwa nilishajifia huko kwa kujiua.
Lakini Nadia alikuwa anaishi na alikuwa akiusimulia mkasa huo
ambao ulimweka katika nafasi ambayo alikuwa sasa. Nafasi ya mjutaji!!
Hakika alikuwa mwanamke wa aina yake binti huyu!!
Nilitafakari sana na usingizi ulinipitia baadaye sana usiku!!
Majira ya saa tatu na nusu asubuhi nilikuwa katika chumba cha
Nadia tena, siku hii nilimkuta akiwa amemaliza kujiandaa, tulikuwa na safari ya
kwenda katika hifadhi ndogo ya ‘SAA NANE’ iliyopo jijini Mwanza.
Tulitaka tuwahi kwenda ili tuwahi kurudi.
“Leo umejitahidi kuwahi!” alinambia.
“Aah! Leo nimeota ndoto mbaya nilikuwa nakimbizwa, sasa
nikajikwaa, ile nainuka nikimbie tena nd’o nainuka kitandani.” Nilimtania tu
lakini akastajabu…
“Eheee…umenikumbusha umenikumbusha…” alisema huku
akijilazimisha kukumbuka jambo fulani…hapo nikatambua kuna maelezo marefu
yanataka kutoka katika kinywa chake, nikabofya kifaa changu cha kurekodia
kilichokuwa mfukoni.
“Nini tena Nadia au na wewe umeota unakimbizwa…” nilidadisi.
“Hapana kaka huenda kweli ni Desmund alimuua jamani!! Desmund
atakuwa alimuua..”
“Nani tena Nadia….” Nilimuuliza swali kimakosa, sikutakiwa
kumuuliza, lakini haikuleta madhara yoyote kwani huenda hata hakunisikia.
“Ujue jana nimegundua kitu ambacho nilijiuliza siku nyingi
sana, huenda yeye Desmund aligoma kabisa kukiri lakini nilibaki na imani hiyo
kuwa ni yeye alimuua Danny yule askari mpelelezi. Maskini Danny, sawa alikuwa
na mabaya yake lakini kwa nini Desmund alimuua kwa kuniibia siri kidogo tu
isiyokuwa na mantiki?
Jana nilikwambia nilivyokuwa nimewekwa rumande bila kutolewa
kwa ajili ya mahojiano, nilikwambia jina kama Danny hivi. Yah! Danny!! Bila
yeye nadhani ningeweza kuishia kuhamishwa rumande na kiha kutupwa gerezani bila
kosa lolote, Danny alinitoa rumande na kuamua kunihoji, alinihoji kama mtu
anayejua kitu fulani, alinihoji maswali mengi sana, nami kwa kuwa sikuwa na
njia nyingine bali kusema ukweli nikamweleza juu ya hila ninayofanyiwa na
Desmund na familia yake kwa ujumla. Danny alinisikiliza huku kila baada ya
dakika kadhaa akiandika nukuu anazozijua yeye.
Baada ya mahojiano aliniambia kauli nzito. “Binti, kwanini
usijiweke mbali na Desmund. Jiweke mbali naye yule atakusumbua sana, kila mtu
mweupe anayejaribu kumgusa kwa sasa anaishia pabaya. Desmund hapendi wahindi,
hapendi waarabu na anayo haki ya kuwachukia. Wewe jiweke mbali naye tu!!
“Lakini alikuwa mume wangu!!” niliingilia kati.
“Kuwa mume wako ama bwana yako kwa sasa haina maana, tuachie
sisi tunaomjua Desmund na historia yake, cha muhimu kwa sasa jiweke mbali naye.
Kulingana na maelezo yako, umenijeruhi sana kama ni mateso yametosha na
hautakiwi kutumikia kifungo kisichokuwa na jina wala hukumu. Mimi nitakusaidia,
lakini ukitoka hapa potea mbali kabisa. Maana Desmund hakupendi hata kidogo na
nina kuhakikishia kuwa ukifa hataumia hata kidogo. Hawapendi waarabu kwa sababu
zake za miaka mingi ambazo yeye anaziita sababu za msingi!! Tumejaribu
kumshauri lakini hataki kubadili msimamo.” Maelezo ya askari yule
yalinichanganya sana, nikabaki kuduwaa. Desmund na umasikini wote ule
niliomkuta nao ana kisa gani na wahindi na waarabu. Kumbe tangu siku ya kwanza
alikuwa ananichukia!! Nilibaki kuduwaa.
Nikataka kuuliza swali lakini afande Danny akanikata
kidomodomo kuwa ule haukuwa wakati wa maswali!
Akanirudisha rumande bila kunieleza jambop jingine la ziada.
Baada ya dakika kadhaa nikaletewa chai nzito ya maziwa, nikawagawia rafiki
zangu wa wakati ule ndani ya selo. Mimi sikuweza kunywa chochote.
Usiku ambao sikufahamu ni saa ngapi mlango wa mahabusu
ukafunguliwa, nikaitwa jina nikaitika. Nikatolewa nje ya ile mahabusu!! Safari
hii hakuwa Danny bali askari mwingine tu ambaye sikuwahi kumjua jina lake.
Aliponifikisha nje nikiwa pekupeku vilevile nilikutana na gari
ndogo ikinisubiri. Mlango ukafunguliwa nikaingia mle ndani. Gari ikaondolewa!!
Taa ya ndani ilipowashwa nikagundua kuwa dereva ni Danny.
Moja kwa moja tukafika mtaa uitwao ‘Kariakoo’ hukohuko Musoma.
Hapa ndipo Danny aliongea mara ya kwanza akiniambia chanzo cha mtaa ule kuitwa
Kariakoo.
Baada ya dakika chache nyingine tukafika nyumbani kwa Danny.
Vilikuwa ni vyumba viwili vilivyoungana, choo na bafu vilikuwa
nje.
Kitu cha kwanza baada ya kufika kwa askari huyu nilitakiwa
kuoga, lakini bado sikutakiwa kwenda nje. Aliniletea maji katika ndoo na beseni
kubwa akaniambia niogee ndani ya beseni, japo nilikuwa naona aibu nilioga.
“Safisha masikio hayo vizuri binti!!” Danny alinisisitiza
kutokea chumba cha pili. Baada ya chakula, nikamsihi Danny anieleze chanzo kidogo tu
kwanini Desmund alikuwa akiwachukia watu weupe. Nilitamani sana kujua ili
niamini kuwa Desmund yu sahihi ama la!!
“Umechoka sana binti! Kesho siingii kazini, nitakusimulia
asubuhi sawa!!” alinijibu huku akipiga mwayo!! Sikuwa na kipingamizi,
nikamkubalia. Akanipa gogoro tukapangua viti nikalitandaza chini. Akaniletea
mashuka.
“Unajua bila kumshirikisha mama yangu walaah nisingeweza
kukutoa kule, mama yangu amelizwa na historia yako Ameumizwa na machungu yote
uliyopitia na mwisho amenipa kibali cha kukusaidia, mama yangu ni kila kitu
kwangu na mimi ni kila kitu kwake. Mimi mtoto wa ngama.” Alinambia huku
akitabasamu.
“Mtoto wa ngama nd’o nini?”
“Mimi ni mtoto pekee na yeye nd’o mama pekee.” Alinijibu tena.
Moyo wangu ulikuwa wa baridi sana katika namna ya utulivu,
nilitamani sana kumuona mama huyo awezaye kuumizwa na maisha ya mtu ambaye
hajawahi kumuona kamwe. Hakika ilishangaza hali hiyo. Danny akaniambia
tutaongea mengi asubuhi. Lakini alipoona sijaridhika akachukua simu yake,
akabonyeza namba kadhaa, alivyozungumza kwa kudeka nikajua anaongea na mama
yake. Akanipa nami nikamsalimia, sauti ya mama yule ilikuwa ya ukarimu sana.
Nikatamani kumuona siku moja.
Sasa niliridhika na nikatabasamu!!!
Nikajitupa katika godoro na baada ya muda kidogo nikasinzia!!
Baadaye nikahisi kama ndoto, kuna kitu kilikuwa kinanipapasa
matakoni. Nikawa nahisi ni ndoto nami napuuzia, nikazidi kupapaswa, safari hii
nikaunyanyua mkono na kupeleka mahali nilipohisi ule mpapaso!!
Nikakutana na mkono ukinipapasa. Nikataka kupiga kelele
nikakutana mara nikazibwa mdomo wangu, nilijua kuwa Danny anataka kunibaka,
Danny alikuwa naye anataka kunitendea unyama ambao kama ni kweli basi mama yake
mzazi alikuwa anaulaani. Nikajaribu kufurukuta lakini haikuwezekana.
Hakika alikuwa Danny, mara akanisogelea masikioni.
Wanaume!! Wanaume na tamaa!! nililalamika kimya kimya huku
nikimtazama.
Kumbe nd’o maana alikuwa anasisitiza nioshe masikio
vizuri…shenzi kabisa!!
Ajabu!! Mawazo yangu yalikuwa batili. Danny hakuingiza ulimi
wake masikioni mwangu. Badala yake aliongea kwa sauti ya kunong’ona.
“Kuna watu nje…….simama njoo huku.” Sauti yake ilimaanisha.
Sasa nikawa kimya, nikajiziba mdomo mwenyewe.
Danny akanipakata hadi katika chumba alichokuwa amelala.
Akaniamuru kwa vitendo niingie uvunguni!!
Nikatii!!!
Nikiwa uvunguni nikasikia mlango unagongwa!! Danny akaondoka
kuelekea kule mlango ulipogongwa.
“Msichana yupo wapi kijana!!” sauti nzito iliuliza.
“Mi sijui msichana gani kwani?” sauti ya Danny ikajibu.
Hapo halikuulizwa swali kwa muda nikasikia kukurukakara, na
mara Danny akasikika analia. Bila shaka alikuwa anatembezewa kipigo kikali.
Walimpiga huku wakianza tena kumuuliza kuhusu msichana ambaye
bila shaka ni mimi, lakini ajabu Danny hakuwaambia. Nilikuwa natetemeka, mikojo
ikizidi kulowanisha chupi yangu nikiwa chini ya kitanda uvunguni. Nilijua kuwa
lazima Danny akizidiwa atanitaja na safari hii nadhani nd’o nilikuwa naenda
kufa.
“Nasema nasema….” Nilimsikia Danny akisema huku sauti
ikimkwamakwama.
“Yupo wapi msichana sema upesi.”
“Nimemsafirisha kwenda kwao…” alidanganya. Nami uvunguni hali
ikiwa tete!!
“Unataka mama yako aKute kichwa chako mlangoni kwake” sauti
ilimuuliza.
“Haki ya Mungu nawaambia….nimemsafirisha kwenda Mwanza.”
Alisisitiza Danny.
“Kijana yaani umemtoa usiku huu halafu unasema umempeleka
Mwanza….unatutania sivyo. Ayubu hebu na wewe mtanie.”
Hapo nikasikia kilio kikuu kutoka kwa Danny kisha kimya
kikatanda baada ya kishindo.
“Mpumbavu huyu atakuwa amemuhifadhi kwa mama yake. Watoto
wengine kujitafutia vifo maksudi tu!!” kauli hiyo ikanipagawisha. Ina maana
Danny amekufa kwa sababu yangu!! Danny amekufa akinitetea, kwanini hakusema tu
waniue…Danny alikuwa anategemewa na taifa na mbaya zaidi hakuwa hata na
mtoto..niliumia sana. Mara nikawa kimya tena baada ya watu wale kuingia mle
chumbani, sijui walichukua nini lakini niliwasikia wakivuruga vitu huku na
kule. Kisha wakatoweka!!
Niliendelea kudumu uvunguni kwa nusu saa nyingine kisha
nikatoka nikiwa natetemeka sana. Niliamini kuwa nimemuua Danny iwapo nitamkuta
akiwa mfu!!!
Haswaa!! Haikuhitaji elimu ya utabibu kutambua kuwa Danny ni
mfu, inanilazimu kukueleza mwandishi ili upate picha alivyokuwa lakini
vinginevyo sitaki kukumbuka picha ile. Danny alikuwa amepasuliwa kichwa chake
bila shaka kwa panga nililolikuta pale chini, nondo ilipenya katika tumbo lake
na utumbo ulikuwa nje. Mwandishi niliumia kumtazama Danny niliumia sana, yaani
wakamkata na mikono yote miwili…..aaaah!! Danny!! Kwanini sasa ulinisaidia mimi
nisiyekuwa na umuhimu!! Na ni akina nani sasa waliokuja kukuua Danny!!....sasa
kama laana mama alinipa mimi mbona wapate majanga na hawa wengine eeh!! Mama
niambie hivi ulinilaani mimi ama uliwalaani hata wanaohitaji kunisaidia, mama
ongea nami sasa eeh!! Sema nami…nife sasa kama ni hivyo…niue nije huko
unieleze!!” Hapa Nadia akaanza kuomboleza kwa sauti ya juu. Nikamkabili
nikauzungusha mkono wangu begani mwake na kuanza kumbembeleza
“Nadia haya mambo hutokea, binadamu hatufanani licha tu ya
kutokamilika ambayo ni kwetu sote lakini kumbuka kila mtu ana roho yake, USILIE
NADIA hayo yametokea tayari na yamepita, USILIE NADIA..tena kuhusu mama acha
kukufuru, mwache apumzike….” niliendelea kumsihi.
Sasa akatulia kidogo kisha akiwa anabubujikwa machozi bado
akaweza kumalizia maelezo yake.
“Kabla ya kulala Danny aliweka simu yake katika chaji kisha akaitia
katika mfuko wa suruali yake. Akaitundika palepale sebuleni nilipokuwa
nimelala.
Akili yangu ikafanya kazi upesi, nikaamini kuwa wauaji
walikuwa wakimtambua Danny vizuri na hata mama yake walikuwa wanamtambua. Sasa
kama walikuwa wanamtambua mama yake pia. Bila shaka walikuwa wameenda kumuuliza
pia na yeye kama hana jibu wanamua vilevile.
Nilichukua simu ya Danny,nikabofya kitufe cha kupigia.
“La Mujer De Mi Vida” nikajikuta natabasamu mwenyewe, kwa
sababu nilikuwa mtazamaji mzuri sana wa tamthilia hivyo nikaelewa maana kuwa
alimaanisha ‘Mwanamke wa maisha yangu!’….nikapiga namba hiyo.
Iliita kwa muda mrefu sana kisha ikapokelewa.
“We Danny nawe…nini sasa..” alilalamika mama.
“Mama ni mimi Nadia, kuna tatizo mama jihadhari huko usiwe
peke yako kuna watu wabaya mama wanakuja huko..” nilimweleza.
“Unasema?” aliuliza sasa akiwa makini.
Nikataka kumweleza tena simu ikaishiwa salio.
Nikasubiri anipigie!! Hakupiga!!
Nikatazama saa ya ukutani ilikuwa saa nane na nusu usiku!!
Nikayacha maiti ya Danny ndani, nikapekua pesa nikazipata kiasi kidogo.
Nikaondoka na simu yake.
Majira ya saa tisa usiku nilikuwa nazagaa huku na kule ndani
ya mji wa Musoma bila kuelewa ni kitu gani natakiwa kufanya…
Hapa nikakiri kuwa hakika Nadia mimi nilikuwa nimelaaniwa
Mji ukazidi kuwa mchungu!!!........nilifanikiwa kupata salio
baadaye kabisa lakini mama hakuwa akipatikana tena…chozi la uchungu likanitoka,
nayapigania maisha yangu, naipigania haki yangu, mali zangu za halali, mali
nilizozivuna na Desmund kwa sababu tu ya mapenzi yangu kwake!! Leo hii
nachukiwa kila pande, nimetengwa na sasa nasababisha vifo, Danny amekufa
akinitetea, sijui kuhusu mama mwenye upendo uliopitiliza mama aliyenipenda hata
bila kuniona!!...Desmund, Desmund mapenzi yangu yooote niliyokupa umenitenda
hivi Desmund….kweli umeamua kunifanya niwe mkimbizi kiasi hiki Desmund ambaye
sijawahi hata kukutukana sijawahi kukulaumu Desmund, Des niliyekunyenyekea
licha ya kuwa nakuzidi kwa kila kitu…leo unaniita Chokoraa na nisiyefaa katyika
jamii, unawatuma watu waniue mimi Desmund!!” kikafuata kilio kikuu huenda
kupita vyote, Nadia alilia sana, alilia akiomboleza juu ya kifo cha Danny na
kuhusu mama asiyejua kama alikufa ama la!! Lakini Nadia aliamini kuwa walimuua.
Nadia alilia kinyakyusa!! Alilia huku akilaani katika namna ya kuimba!!
“Nadia, mimi nipo upende wako na sitakusaliti, ni mimi na wewe
tunajua wapi tulipokutana amini kuwa …”
“Shhhhhhh!!!! Wote ninyi ni wale wale..” alinikaripia.
Nikatambua kuwa hii ni hasira iliyopitiliza. Nikaamua kumuacha Nadia alie
akimaliza apumzike na huenda anaweza kusema nami tena, maana kwa hali
aliyokuwanayo angeweza kunipiga hata makofi!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni