Jumatatu, Novemba 03, 2014

MWISHO WA SIMULIZI YA BADO MIMI SEHEMU YA 36.

ILIPOISHIA
Baadaye nilizinduka na kujikuta nikiwa nyumbani ambapo pembeni yangu alikuwepo Charito mume wangu nilijikuta naanza kulia kwa uchungu sana “Masikini mdogo wangu, Renata wangu  jamani, inaniuma sana mdogo wangu, tulikuwa tunakunywa chai pamoja asubuhi, yalaiti ningekushika mkono usitoke nje, mdogo wangu moyo wangu unaumia sana jamani”  Nililia sana kwani nilikuwa siamini kama Renata amefariki, Charito alijitahidi kunibembeleza na kusema “ Nyamaza mke wangu usilie mke wangu, yote hiyo ni mipango ya Mungu, sisi tulimpenda lakini Mungu kampenda zaidi” USIKOSE SEHEMU YA 36

INAPOENDELEA 
Ilikuwa ni vilio na simanzi, na amani ilitoweka kabisa moyoni mwangu nilihisi kama ni ndoto lakini haikuwa ni ndoto, nililia sana kwa uchungu na  kupoteza fahamu mara kwa mara, ndugu jamaa na marafiki walikusanyika pamoja na baadhi yao walijitahidi kunibembeleza bila mafanikio, Siku hiyo nilikuwa katika wakati mgumu sana, Charito pamoja na Mchungaji Mkombozi ndiyo walikuwa wakipanga taratibu za mazishi, pamoja na siku ya kumpumzisha marehemu katika makazi yake ya milele.Ambapo kutokana na mwili wa Renata kuwa na majeraha makubwa sana katika paji la uso, ilitakiwa asichelewe kuzikwa hivyo kutokana na taratibu zilizopangwa wakasema kesho yake atazikwa.

 Hali yangu kwa wakati huo ilizidi kuwa mbaya kwani wakati wote nilikuwa nikiishiwa nguvu, mwili wa marehemu ulikuwa umekwisha pelekwa hospitalini  kwa siku hiyo, ilipofika majira ya usiku nilikuwa nimechoka sana, hivyo charito alinishika mkono na kunisindikiza chumbani nikapumzike, mdogo wangu Tumaini alinifuata, na kutaka kupumzika pamoja na mimi, tukiwa pale kitandani niliendelea kulia, huku Tumaini akinishika mkono na kusema “Dada Kandida usilie, kwani shemeji Charito amempeleka Renata hospitalini, kesho atarudi akiwa amepona, usilie dada, Renata atapona yupo pamoja nasi”.


 Nilimtizama Tumaini kwa macho yaliyojaa simanzi na kumkumbatia kwa uchungu huku nikiendelea kulia bila ya kumjibu chochote huku machozi yakidondoka bila kuisha, baadaye nilijikuta nikipotelea kwenye usingizi bila ya kujijua, ulikuwa ni usiku mzito nikiwa usingini nilimuona Mama Bilionea akiwa anakuja huku akiwa anacheka kicheko cha ajabu sana.

 “Hahahahahahahah, hahahahahahah, Kandida mwanangu Kandidaaaa, kiongozi makini wa hekalu la Bilionea, hahahahahahahahaha, hongera sana sasa umefikia kiwango kikubwa sana, wewe ni malikia wa Bilionea, hahahahahahaha akiwa anaendelea kucheka, taratibu nilimuona Mama na Baba yangu  mzazi wakiwa wanasogea, huku Mama akiwa amemshika mkono Renata wote walikuwa wakinitizama huku nyuso zao zikiwa zimetawala machozi ya damu, nilijisogeza taratibu na kuanza kuwaita bila ya mafanikio, niliendelea kuita kwa sauti kali sana jina la Renata “Mamaaaaa, Renataaaaaa, Mamaaaa, Renataaaa, Tumaini alishtuka na kunishika mkono.

 “Dada Kandidaa, kuna nini Renata yuko wapi" Nilishtuka kutoka usingizini na kumtizama Tumaini alikuwa anatetemeka na jasho lilikuwa likimbubujika mithili ya mtu aliyemwagiwa maji, “Dada Kandida nimemuona Mama na Baba na Renata, dada wanalia machozi ya damu dada mimi naogopa nimewaita lakini hawakunijibu chochote” Nilimtizama Tumaini huku moyoni mwangu nikiwaza “Inamaana Tumaini alikuwa anaota ndoto ileile ambayo nilikuwa nikiota mimi Mungu wangu Mama Bilionea anaimaliza familia yangu, eeh Mungu nisaidie niweze kuondoka katika nguvu hizi za giza” Nilikuwa na wasiwasi sana siku hiyo nilitizama muda ilikuwa ni saa tisa za usiku, nilimkumbatia mdogo wangu Tumaini ambaye alikuwa na wasiwasi sana huku nikimbembeleza asiwe na hofu “Tumaini hiyo ni ndoto tu mdogo wangu usiogope inabidi tulale kwani kwa sasa ni usiku sana” Nilikuwa na hofu lakini ilinibidi niwe jasiri kwasababu ya Tumainijapokuwa kwa wakati huo nilikuwa naogopa sana.

Kesho yake taratibu za mazishi ziliendelea na baadaye mwili wa marehemu ulienda kuchukuliwa kutoka hospitalini, ambapo baada ya mwili wa marehemu kufika Mchungaji Mkombozi alianza kufanya mahubiri na baadaye watu walipata nafasi ya kuaga mwili wa marehemu kwa mara ya mwisho,  “Renata mdogo wangu, jamani kwaninini umetuacha, nani atacheza na Tumaini, eeh Mungu wangu naumia sana,Renata ni kweli umetutoka, amka mdogo wangu amka” Nilikuwa nikimshika kwenye paji la uso huku nikilia kwa uchungu sana nguvu ziliniishia na kupoteza fahamu, baada ya kumtizama mdogo wangu kwa mara ya mwisho.

Nilipozinduka sasa tayari mwili wa marehemu ulikuwa ndiyo unapelekwa kupumzishwa katika makazi ya milele, ambapo mdogo wangu alizikwa karibu na alipozikwa Baba na Mama yangu. Baada ya kumaliza taratibu zote ndugu jamaa na marafiki walitawanyika.

Maisha yaliendelea baada ya mwezi mmoja tangu mdogo wangu atangulie mbele ya haki. Siku moja nilikuwa nimekwenda dukani, ndipo nilipokutana na mchungaji James ambaye aliniita na kisha kunijulia hali “Habari yako Kandida ni muda mrefu hatujaonana, ulisema kuwa ungefika kanisani lakini sijawahi kukuona, vipi nyumbani mnaendeleaje?” Aliniuliza mchungaji nilimtizama huku moyoni mwangu nikiwa na simanzi kubwa kwani nilimkumbuka sana Renata baada ya kukutana na mchungaji James machozi yalianza kunidondoka huku nikiwa nimenyamaza kimya nikimtizama Mchungaji James ambaye  alikuwa hana taarifa za msiba, Mchungaji alinitizama na kisha akaniuliza tena “Vipi Kandida, una matatizo gani, mbona unalia kuna nini, embu nyamaza halafu unieleze nini kimekusibu” Nilijifuta machozi na kitambaa kisha nikasema “Mchungaji, Renata alifariki kutokana na ajali ya kugongwa na gari, ni mwezi mmoja sasa umepita, samahani nilishindwa hata kukufahamisha, kwani nilikuwa nimechanganyikiwa sana”

 Mchungaji alinyamaza kimya kidogo na kisha akasema “Unasemaje Kandida, ati Renata amefariki? Mungu wangu eeh Mungu ipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi, alikuwa mtoto  mwenye heshima na akili sana, pole Kandida usijali Mungu yupo pamoja nawe”  Mchungaji alinisihi nisilie niendelee kumuombea Renata pamoja na familia yangu alinisihi niende katika kanisa analohubiri ili nikafanye maombi, nilikubali kuwa nitajihidi niweze kwenda. Baadaye tuliagana na mchungaji aliendelea na safari zake.

Niliporudi nyumbani nilimkuta Tumaini akiwa amelala chumbani kwake na wakati huo ilikuwa ni saa sita mchana, nilimsogelea na kusema “Tumaini, embu amka mdogo wangu haiwezekani ukalala hadi muda huu” Nilimshika mkono wake ulikuwa na baridi kali sana alinitizama nakusema “Dada nasikia baridi sana, siwezi kwenda shule” Nilishangaa kuona hali ile na moja kwa moja nikasema “Unaumwa nini tena jamani,Eeeh Mungu wangu embu twende hospitali haraka” Yaani Tumaini alikuwa hana nguvu kabisa ilinibidi nimbebe mgongoni na kwenda kumpeleka kwenye gari na kwa wakati huo mume wangu Charito alikuwa hayupo.

Tulipofika hospitali moja kwa moja Daktari alichukua vipimo vya Tumaini na baadaye alimpa kitanda ili apumzike na hivyo siku hiyo hatukuruhusiwa kwani kutokana na hali ya Tumaini ilibidi alazwe pale hospitalini. Nilishindwa kuelewa Tumaini anaumwa nini kwani hata majibu ya daktari yalionyesha alikuwa haumwi chochote, nilijihisi kama nataka kuchanganyikiwa moyoni mwangu nilikuwa na hofu sana ya kumpoteza mdogo wangu “Mungu wangu ni kitu gani hiki tena kimempata mdogo wangu eeh Mungu nisaidie ni vyema niende kwa mchungaji James muda huu, Niliondoka pale hospitalini na kumuacha Tumaini akiendelea na matibabu na moja kwa moja nilienda hadi katika kanisa analohubiri mchungaji James, nikiwa njiani niliwaza.

 “Hapana siwezi kwenda kwa mchungaji Mkombozi na hili jambo siwezi kabisa kumshirikisha Charito najua hawezi kukubaliana na mimi, na sasa ni vyema nikamuona Mchungaji James anisaidie” Nilipofika pale kanisani niliona watu wengi wakiwa wamejikusanya wakifanya maombi nilisogea huku nikitizama huku na kule nilipofika karibu mchungaji aliniona na kushangaa huku akisema “Kandida, ni wewe,nimefurahi umepata muda jioni ya leo kuja kujumuika pamoja nasi karibu sana”.

 Nilianza kumueleza mchungaji hali halisi ya kile kichotokea alinitizama na kusema “Kandida huu ni wakati wako kumkabidhi Mungu maisha yako Mungu wa kweli ambaye atakutoa katika nguvu za giza, sasa tunakwenda kufanya maombi nakuangamiza nguvu zote zilizozunguka maisha yako. “Mchungaji naomba unisaidie mdogo wangu apone,naogopa sana sijui nitafanya nini nikimpoteza mdogo wangu, kwani inaonekana Mama Bilionea anataka kuiangamiza familia yangu yote yaani naona Bado mimi, yaani bado mimi na mdogo wangu Tumaini.

Nilikuwa nalia sana kwa uchungu mchungaji alinishika mkono kisha alinisogeza karibu na  nilijumuika na baadhi ya waumini kisha wakaanza maombi. “Nimepewa mamlaka yakukutoa mapepo kwa jina la Yesu, na ninayaondosha, yakiondoka yasirudi tena kwako, na ninausafisha mwili wako kwa damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani, ukawe huru wewe pamoja na familia yako, Mungu wetu wa kweli nakuomba ukaiponye familia hii nakemea mizimu yote, mapepo yote yakuache huru, na uponyaji ufanyike kwa mtoto aliye, hospitalini mapepo yashindwe na kumuacha huru”.

 Alikemea mchungaji na mimi nguvu ziliniishia nilianza kugaragara chini na kuanza kulia kwa sauti ya ajabu huku nikisema “Bado mimi, bado mimi, nimesema sitoki, sitoki lazima niwachukue wote, Kandika ni kiongozi wetu katika hekalu la bilionea, lazima abaki kwetu hawezi kuwa huru” Mchungaji aliendelea kukemea “Nautuma moto ukaangamize hekalu la bilionea, moto moto, katika jina la Yesu hamna mamlaka katika maisha ya mwanamke huyu nasema mkateketee wote kizazi cha Bilionea”.

 Mchungaji aliendelea kusali wakati huohuo pale kanisani alifika Mchungaji Mkombozi na Charito. sikujua walikuwa wametokea wapi ila nguvu zilikuwa zimeniishia na nilikuwa sijielewi Mchungaji aliendeleza maombi na sasa Mchungaji alizidisha maombi, baadaye maombi yalielekezwa kumkemea mchungaji Mkombozi na Charito ambao walikuwa na nguvu kali za giza walianza kusema “Wewe ni nani unayeingilia maisha ya watu tunaomba utuache, mimi ni mtumishi wa hekalu la Bilionea, na huyu ni mwenzangu mtoto wa Mama Bilionea anaitwa Chande, hutuwezi wewe kwenda zako mjinga mkubwa” Mchungaji James aliendelea kufanya maombi bila ya kuwasikiliza ghafla wote walianza kulalamika “Moto unaninichoma, moto unaunguza, naondoka naondoka sirudi tena naondoka naondoka” Walikuwa wakilalamika na sasa walikimbia na kuondoka kusikojulikana.

Nilikuwa kama nimepigwa butwaa baada ya kuona hali ile na pia kumbe siku zote nilikuwa nimeolewa na mtoto wa Mama Bilionea ambaye ni Chande, na Mchungaji Mkombozi alikuwa ni mtumishi wa shetani? yaani alikuwa mchungaji feki. Nililia huku nikimshukuru Mungu kwa kila jambo “Ewe Mungu nakushukuru, nakuomba uniongoze katika maisha yangu”Baadaye niliongozana na Mchungaji James hadi hospitalini ambapo tulimkuta Tumaini akiwa anaendelea vizuri na aliponiona alinikimbilia na kunikumbatia niliendelea kumshukuru sana Mungu. Tuliondoka na kuongozana na mchngaji James hadi nyumbani kwake na alitupatia chumba cha kupumzika nilijisikia huru sana na baadaye usingizi ulinipitia kutokana na uchovu “Nilimuona Mama yangu, Baba yangu pamoja na mdogo wangu Renata wakiwa wamevaa mavazi ya rangi nyeupe huku nyuso zao zikionyesha kuwa na  furaha sana, siku hiyo walizungumza na mimi na Mama akasema.

 “Mwanangu asante sana kwa kutuokoa kutoka kwenye kikombe cha mateso, sasa tumekuwa huru tunaimba na kufurahi na Mungu wetu wa kweli, kila la heri katika maisha yako tunakupenda sana Kandida” Nilikuwa ndotoni lakini niliposhtuka nilimshukuru sana Mungu na moyo wangu ulifurahi sana na sikuwa na hofu yoyote kwani ndoto ile niliiona ni njema kwangu.Na tangu siku hiyo nilikuwa huru katika maisha yangu na sasa niliondoka kabisa katika nyumba ya Mama Bilionea na kurudi nyumbani kwetu Mmbagala kuishi pamoja na mdogo wangu Tumaini maisha yaliyojaa amani upendo na furaha. Baada ya miezi sita kupita Mungu alinibariki nikapata mchumba na kuolewa Maisha yanaendelea vizuri na sasa nimebarikiwa kupata mtoto wa kike ambaye anaitwa Renata jina la marehemu mdogo wangu.
                        ****************MWISHO***************

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom