ILIPOISHIA
Baada ya hapo
nikabeba kilicho changu na kuingia katika mitaa ya Tukuyu nikiwa na shilingi
elfu tano tu!!
Pesa
niliyoipata baada ya mama Aswile kuiangusha akijaribu kukabiliana na mimi!!
Jonas
mgongoni, kibegi kidogo mkononi!!
Nikaingia
katika mitaa yenye baridi kali. Sina ndugu wala rafiki!!.........USIKOSE SEHEMU YA 21
INAPOENDELEA
Sikuwa
nafahamu ni wapi natakiwqa kwenda muda huo, na hapo nikaanza kuona muda ukienda
kwa kasi sana. Ilikuwa asubuhi mara ikawa mchana, bado nilikuwa katika kiza
kinene bila jibu sahihi.Mida ya saa
nane mchana Jonas akaanza kulia huku akiwa mgongoni.
Njaa!!
Nikawaza. Nikamgeuzia kifuani na kuanza kumbembeleza lakini hakubembelezeka,
nikatamani angeweza kusema nini kinamtokea nitafute njia ya kumtibia lakini
hakuweza kusema na badala yake alikuwa analia tu. Nikalazimika kuingia katika
banda la mama lishe, nikaomba huduma ya chakula, nikapatiwa wali na maharage.
Jonas akakataa kula badala yake akaendelea kulia kwa fujo na kuwa kero kwa
wateja wengine.
Hapa nikalazimika kutoka naye nje huku ule wali nikiulipia bila
kuula hata kidogo, ningeanza vipi kula wakati Jonas alikuwa analia? Yule mama
alinifuata nje na kuniuliza nini kimemsibu mtoto, nikamweleza kuwa nilihisi ni
njaa lakini ajabu hataki kula hata hicho chakula. Yule mama akampima joto kwa
kutumia mikono yake na kisha akanieleza kuwa mtoto alikuwa amechemka sana
nijaribu kumpeleka hospitali ama la nimpatie dawa za kutuliza maumivu.
Hilo la
hospitali lilikuwa zito sana kwa sababu nilikuwa na shilingi 5000 tu, sasa
ingetosha vipi gharama za hospitali tena kwa mgonjwa asiyefahamika magonjwa
yake. Nikaamua kushika la pili, nikanunua dawa za kutuliza maumivu,
nikazikoroga katika maji kishas tukasaidiana na yule mama kumywesha Jonas,
alisumbua sana lakini alimeza.
Baada ya saa
zima Jonas hakuwa akilia tena na alikuwa amejilaza katika mikono yangu. Mama wa
kufikia ambaye hajui hata kesho yake na sasa ana mtoto mikononi mwake.
Ngoja ngoja,
tafakari tafakari hatimaye usiku ukafika
akili ikiwa imeganda tu nikishindwa kufikiri hata kidogo ni kitu gani natakiwa
kufanya.
Si kwamba
hawakuwepo watu ambao ningeweza kuwakabili na kunipa hifadhi ya siku mbili
tatu, hofu yangu ilikuwa usalama wangu katika wilaya hiyo. Hao watu niliokuwa
nafahamiana nao walikuwa wakimfahamu mzee Aswile na familia yake, hivyo ilikuwa
kazi nyepesi sana kuweza kuzisikia tetesi za shambulio langu dhidi ya familia
ile. Na ningejuaje huenda nilikuwa natafutwa??
Ningekuwa
mimi kama mimi ningejitoa muhanga lakini Jonas!! Jonas aliniumiza sana kichwa.
Laiti kama ningeamua kujisalimisha huko kisha nikakamatwa, bila shaka Jonas
angebaki katika familia ya mama Aswile! Familia ambayo inamuita yeye
mwanaharamu. Angeishi vipi, kama wakati mtetezi wake nilipokuwa naye waliweza
kumuita mwanaharamu na kumzaba vibao, je wakati ambao sipo kabisa nini
kingejiri kama sio kumuua kabisa.
Hapana!!
Siwezi kurudi nyuma. Nikafikia uamuzi huo. Nikasimama na kuelekea stendi ya
mabasi ya pale Tukuyu, nikatafuta kona moja nikajiegesha huku Jonas akiwa
salama kifuani kwangu.Sijui hata
nilikuwa nawaza nini hadi kufika pale stendi. Lakini ni sehemu pekee ambayo
niliamini kuwa hapatakuwa na bughuza za hapa na pale, maana nikiwa na begi
langu ningeweza kusingizia kuwa mimi ni abiria.
Baridi
ilikuwa kali sana majira ya saa tatu usiku, meno ya Jonas yakawa yanagongana
mdomoni, matumbo yake yakawa yanaunguruma. Nikajisemea nafsini kuwa yule mtoto
yupo katika mateso makuu, alinikumbatia kwa nguvu sana lakini sijui kama
alipata alichokuwa akikitafuta.
Joto!!
Hakulipata joto kwani mwili wangu wote ulikuwa wa baridi pia. Nilimsikitikia
sana, nikajaribu kujiuliza tena na tena ni kitu gani naweza kufanya kupambana
na hali hii. Nilitazama huku na kule, kisha nikavamiwa na wazo moja kuwa iwapo
nitaleta lelemama Jonas atanifia kifuani.
Wazo la kifo
likanigutusha kutoka pale chini, nikasimama wima, nikampigapiga Jonas mgongoni,
akakohoa kisha akasema neno moja likaniumiza.
“Ataaka
babuuu!!”
Chozi
likanidondoka, nikaujua uchungu anaopitia Jonas kwa kumkosa mzee Aswile lakini
nami pia nilikuwa katika uchungu mkubwa kwani laiti kama mzee Aswile angekuwepo
ningekuwa natabasamu tena. Na ningekuwa nimemkumbatia Jonas huku tukiwa
tumejifunika blangeti zito.
Lakini sasa
nilikuwa stendi na mawazo yangu yakiwa yameganda.
Suala la kifo
cha Jonas likanichangamsha na kunitia hofu kwa wakati mmoja. Na hapa
nikakumbuka sehemu moja ambapo naweza kujaribu kukimbilia. Nikamkumbuka
Stephano.” Nadia akasita kuzungumza kisha akanitazama na kuniuliza swali.
“Stephano…jina
zuri eeeh!!” nikatikisa kichwa kukubaliana naye.
“….ni heri
uwe na jina baya lakini matendo yako yawe mazuri kuliko kuwa na jina baya
linaloficha matendo yako….alikuwa anaitwa Mchungaji Stephano na wengi walimuita
mtu wa Mungu. Alikuwa anajitolea sana kwakweli, alikuwa akihubiri basi watu
wote kimya na alikuwa anagusa samba nafsi. Mara yangu ya kwanza kumfahamu
nilienda na akina Monica watoto wa mzee Aswile, ujue pale nyumbani ni mimi peke
yangu nilikuwa muislamu, tena muislamu jina tu maana sikuwa nakumbuka hata
mwezi mtukufu ni upi, sikumbuki mara ya mwisho kukanyaga msikiti ni lini. Kwa
kifupi nilikuwa muislamu wa kale, hivyo ilipotokea familia ile inaenda katika
ibada nami nilijumuika nao mara moja moja ninapokuwa najisikia, sikuwahi
kulazimishwa kubadili dini hata siku moja. Na pia hakuna aliyewahi kuniuliza
kwanini siendi msikitini.
Nilipohudhuria kongamano hili ndipo nilimfahamu
mchungaji Stephano, alikuja kuisalimia familia nzima ya mzee Aswile na hapo
akatambulishwa kwangu. Alikuwa mchangamfu tena mwenye utani sana, haukuwa utani
wa kukera, nilipomwambia mimi ni muislam akaniambia tushindane kuomba dua,
aisee yule ni zaidi ya muislamu yaani kila aya ninayoifahamu mimi na yeye
anaijua. Lakini mbaya zaidi alikuwa anazijua hata nisizozifahamu mimi. Ukaribu
wetu ukaanzia hapa.
“Mariam
wakristo na waislamu ni watoto wa baba mmoja, usisite kuhudhuria ibada kisa
wewe ni muislamu, hakuna anayeutukana uislamu katika ibada na vilevile hakuna
mwenye haki ya kuutukana ukristu misikitini sisi ni watoto wa baba mmoja Mariam, usibaki nyumbani mpweke.”
Mchungaji aliniambia maneo yale yakaniingia na tangu wakati ule nikawa nikipata
hamu ya kusikiliza kwaya nahudhuria kanisani, na kila nilipohudhuria mchungaji
Stephano alikuwa akizungumza nami.
Sikuwahi
kujutia hata siku moja kuhudhuria katika ibada zao.
Kanisa lao
lilikuwa maeneo ya Uyole! Na siku ya kutimiza miaka miwili tangu awe mchungaji
tulipata nafasi ya kwenda kwake kusheherekea na familia yake nyumba yake
ilikuwa jirani na maeneo ya Uyole. Nilipakumbuka vyema.
Jina la
mchungaji huyu likawa jina sahihi kabisa kwa wakati ule, kama aliweza kunielewa
vyema tangu nikiwa kwa mzee Aswile na kwa kuwa alikuwa mtu wa kujitolea basi
huyu alikuwa mtu sahihi kabisa wa kumweleza matatizo yangu.
Nikaingia
stendi, sasa nilikuwqa abiria kweli.
“Mbeya mjini
ya mwisho, Uyole Sai, Ilomba, Mama John, Soweto……mbeya mjini ya mwisho
gariii..” nilisikia sauti ya mpiga debe akiinadi gari aliyokuwa anasimamia.
Nikaingia
garini nikiwa nimembeba Jonas aliyekuwa usingizini nusu na nusu macho!!
Gari
likapakia kwa takribani nusu saa, na hapo likaondoka kwa mwendo wa kusuasua
likiokota abiria hapa na pale.
Saa tano
usiku tulikuwa Uyole, nikashuka baada ya kulipa nauli.
Sasa
nikabakiwa na shilingi elfu mbili tu!
Giza lilikuwa
limetanda na bado baridi iliendelea kupiga, mji ulikuwa umetulia sana. Lakini
niliendelea kusonga mbele hadi nikaifikia nyumba niliyoamini kuwa aliishi
mchungaji Stephano. Niligonga geti mara nyingi sana, na hatimaye nikamsikia mtu
akiligusagusa.
“We nani?”
sauti inayounguruma kutoka usingizini ilisema nami. Nikajitambulisha lakini
hakunielewa, nikasema mimi ni muumini wa kanisa la mchungaji Stephano, hapo
sasa aliweza kufungua geti.
“Unamtakia
nini usiku huu.”
“Mtoto
amezidiwa nahitaji huduma yake…” nilidanganya, hapa mlinzi akatilia maanani na
kunikaribisha ndani. Kwa jinsi tulivyokuwa tunatetemeka hata angekuwa nani
lazima angeamini nilichokuwa nasema. Mlizi akaelekea mlangoni, akanyanyua
mkonga wa simu akaanza kusikiliza nikaisikia ikiita kwa ndani maana ulikuwa ni
usiku ilisikika vyema. Simu ikapokelewa wakazungumza kwa dakika kadhaa kisha
akaushusha mkonga chini na kungojea.
Baada ya kama
robo saa akatoka mchungaji kijana, Stephano. Nikamkimbilia na kumwangukia
kifuani mimi na Jonas, akaizungusha mikono yake nikalipata lile joto la upendo.
Akanikaribisha
ndani sebuleni, nikaingia huku nikiwa nalia kilio cha kwikwi, akaniuliza
kulikoni. Huku akiwa ananitazama katika
hali ya kutia matumaini na upendo mkuu.USIKOSE SEHEMU YA 22
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni