ILIPOISHIA
“Gari ya mama ileee.” Tukiwa nje yule mtoto alinionyesha kwa kidole gari iliyokuwa inaingia pale shuleni. Akimaanisha ni ya mama yake, nikazidisha mwendo na kukata kona mbili tatu. Sikutaka kupoteza muda zaidi, nikafanya nilichopanga, nikampa yule mtoto pipi, akaidaka na kuitupia mdomoni, baada ya dakika ishirini nilikuwa nimetoa kanga na alikuwa mgongoni kwangu kama mwanangu wa kumzaa vile amelala hoi. Hatua ya kwanza ilikuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.USIKOSE MWISHO WA SIMULIZI HII
INAPOENDELEA
Alipokuja
kustuka alikuwa kitandani, nikamchukua na kumwogesha aliniuliza maswali
nikamjibu vyema na kumtaka awe mtulivu kabisa.Alilala
Musoma na sasa ameamka akiwa jijini Mwanza. Harakati zangu zilienda kwa usahihi
sana.
Nia yangu ya
kumnyanyasa Desmund na mkewe kimawazo ilikuwa inatimia sasa, nilijua
watahangaika sana na mwisho watajiona hawana thamani yoyote katika maisha yao.
Namba ya Desmund ilikuwa kichwani mwangu na bado sikutaka kuwasiliana naye. Cha
muhimu zaidi nilitaka ateseke hadi nafsi yangu iridhike.” Nadia akakomea hapa,
uchovu ulikuwa umemshika akaaga na kwenda chumbani mwake. Mimi nilipojilaza
kidogo nikapitiwa na usingizi kwa sababu usiku kucha nililala kwa kujibana sana katika kochi.
Nilikuwa
naamini sasa mwisho wa simulizi unakaribia kwa sababu tayari Desmund alishaanza
kuguswa pabaya.
Nikasubiri
kwa hamu kabisa siku ambayo Nadia ataendelea kusimulia ili nijue aliishia wapi
katika harakati zake hizo.
Nilikuja
kushtuka mchana jua likiwa kali kabisa, nilitaka kwenda chumbani mwa Nadia
lakini nikasita na kuamua kupiga simu ya chumbani mwake, iliita bila kupokelewa.
Nikajua na yeye atakuwa katika dimbwi la usingizi mzito kabisa kama mimi
nikapuuzia na kuendelea kulala.
Majira ya
jioni nikapata cha kuingia chumbani mwa Nadia. Ni kumchukua twende kupata
chakula na pia kujiandaa kwa safari ya kwenda jijini Dar es salaam kwa ajili ya
kumtimizia ndoto zake za kuwa huru tena na mwenye furaha.
Nilifika
nikakigonga chumba chake lakini hakujibu kitu, hii haikuwa kawaida ya Nadia
hata kidogo, nikaamua kufungua, kitasa kikafunguka vizuri tu!! Kuingia chumbani
hapakuwa na mtu. Lakini kitandani palikuwa na ujumbe mfupi.
“Nimetoka
kidogo!!” ujumbe huu ulinishangaza, yawezekana vipi Nadia kutoka peke yake
katika jiji hilo la Mwanza tangu nifike naye pale, hapa nikapata walakini.
Nikajiuliza nichukue hatua gani lakini sikupata namna ya kufanya. Mara macho
yangu yakakutana na rekoda yangu!!
Nikaduwaa imefika vipi pale ndani, wasiwasi
ukaniingia maana hadi ninaposinzia ilikuwa katika chumba changu.
Nikaichukua
na kutazama, nikakuta kuna kitu kimeongezeka katika ile reekoda, mara ya mwisho
nilikuwa nimerekoda kwa masaa nane, lakini sasa yalikuwa masaa tisa. Hivyo kuna
jambo la ziada.
HAKIKA katika
maisha unatakiwa kujifunza na kukubaliana na ukweli kuwa moyo wa mtu ni fumbo
gumu kabisa, fumbo lisilofumbuliwa kirahisi. Kuna jambo Nadia alikuwa
amelihifadhi katika moyo wake ambalo sikulijua na mbaya zaidi ulikuwa mpango
wake wa siku nyingi.
Nikaiwasha
ile rekoda kuanzia pale nilipoishia yaani saa moja nyuma.
Nikakutana na
sauti ileile ya Nadia.
“Gerlad Iron!
Mwandishi mpole, msikivu muelewa mnyeyekevu na mwenye huruma, natamani sana
moyo wako ungeukata kidogo na kuwagawia akina Desmund maana wapo wengi duniani.
Naamini unahitaji sana kunisaidia huku ukihitaji pia kujua kila kitu kuhusu
mimi. Lakini sina maana hata ukinisaidia mimi.
Mara ya
mwisho kuzungumza nawe nilichoka ghafla kwa sababu tu sipendi kabisa kukumbuka
kilichokuja kutokea katika maisha yangu! Sitaki kukumbuka machungu na maasi
yangu.
Ni kweli
nilifanikiwa kumteka mtoto wa Desmund na kumuhifadhi jijini Mwanza, hiyo kwangu
ilikuwa hatua kubwa Desmund alitetemeka kama mtoto mdogo na bado hakujua kama
ni mimi nahusika, baada ya kumweka mtoto Mwanza nyumbani kwa dada yangu
aliyekuwa akiishi na Jonas niliamua kurejea Musoma tenma kwenda kukabiliana na
Desmund, hakika walikuwa wamefadhaika sana na duka lilifunguliwa na yule kijana
wa kichaga, mkewe Desmund hakugusa
kabisa pale, nilipoonana na yule mchaga alinieleza kuwa kale katoto kamepotea
katika njia za kishirikina, nilitabasamu huku nikiyasikitikia mawazo yao.
Nikiwa Musoma nilikutana na kundi moja la wahuni likijiita WEST LAWAMA,
nilizungumza nao vyema, hawa nikawaagiza kijijini kwao Desmund kule alipokuwa
anaishi mama yake, huku nilihitaji jambo moja tu la kuiteketeza akili ya
Desmund zaid, nilihitaji waichome ile nyumba. Hilo halikuwa na shida hata
kidogo biashara ilienda vizuri sana, Desmund akazidi kupagawa. Bado nilienda mbele
zaidi kutuliza kidonda changu moyoni, nikawaagiza wapeleleze ni wapi nyumbani
kwa mke wa Desmund, upesi wakapapata, nikawalipa na huku wakateketeza, bahati
mbaya kwake na bahati nzuri kwangu, wadogo zake mke wa Desmund wawili
waliteketea katika moto. Sikuwa na huruma hata kidogo maana nimelaniwa,
nisingeweza kukusimulia haya nikiwa nakutazama maana mimi ni zaidi ya shetani
kwa malipo haya, malipo yaliyokuwa yakinifariji moyo wangu.
Baada ya hapo
nikaenda nyumbani kwa Desmund mida ambayo nilijua kabisa kuwa hayuipo nyumbani,
nikaacha ujumbe kwa mlinzi kuwa ‘AKIJA MWAMBIE MWENYE NYUMA ALIKUJA’, nadhani
aliupata ujumbe ule na bado akaupuuzia ni hapo nikampa tena pigo jingine, pesa
niliyokuwanayo zaidi ya kula na kulala haikuwa na kazi nyingine ile, hivyo nikaendelea
kuitumia vilivyo. Mdogo wake Desmund wa kiume aliyekuwa akiishi naye
akacharangwa mapanga vibaya sana lakini hawakumuua, nami nilitaka iwe hivyo.
Wakamuachia ujumbe kuwa mwenye mali anataka mali zake. Ujumbe alioufikisha kwa
kaka yake bila shaka.
Diwani
akazidi kukonda, diwani akapagawa. Nikaifurahia hali hiyo.
Mwandishi,
ujue sikupanga kabisa kumdhuru Desmund wala mkewe baada ya adhabu hiyo, badala
yake nilitaka anipe mali zangu hata nusu nijiondokee kwenda ninapojua lakini si
kumdhuru, nilikuwa nina tatizo la kuwa na huruma sana. Hiyo ilikuwa mbaya sana
kwangu.
Lakini mawazo
yalibadilika ghafla na kujikuta nikifanya kitu nisichokitarajia hata kidogo.
Siku hiyo
niliamua kwenda nyumbani kwa Desmund siku niliyoamini kuwa alikuwepo nyumbani
yeye na mkewe. Niliingia hadi ndani
baada ya mlinzi kuambniwa aniruhusu. Nikaingia katika nyumba ya Desmund na
mkewe, walikuwa wameketi wakiwa wanatazama luninga lakini hawakuwa wameitilia
maanani sana.
Desmund
alishtuka sana kuniona nikiwa pale, alitaka kupiga mayowe lakini nikawahi
kumwambia akae kimya.
“Maonyo yangu
unayapata ama huyapati.” Nilimweleza na kisha kabla hajafanya lolote
nikamuonya, “Ukithubutu kuleta ujuaji wako, nyumba hii itachomwa moto dakika
hii na utafia humu ndani wewe na hiki kikaragosi chako.” Niliongea kwa ujasiri
sana na wote walitetemeka.
“Nadia
tafadhali nakuomba sema chochote nitakupa, lakini unipe mwanangu Nadia.”
Alinisihi kwa sauti ya huruma sana.
“Mali zangu
unanipa ama hunipi wakati huu, ama ndo hunijui tena mimi ni nani.’ Nilimuuliza
bado nikiwa nimesimama.
“Nadia nakupa
kila kitu utakachotaka.” Aliendelea kunisihi kwa huruma.
“Desmund
naondoka muda huu nitarejea baada ya siku tatu, nahitaji nikute nyumba hii ipo
mnadani, uiuze, vitu vya dukani uviuze, gari uliuze na bila shaka haitakuwa
chini ya miloni miambili mezani. Nitaichukua hiyo na utampata mtoto wako,
lakini vinginevyo, nitaanza na kile kiuchafu chako nitanyonga, halafu wewe na
huyu mjinga mwenzio nita..” kabla sijamaliza kuongea yule mwanamke akaja
kunikabili kwa jazba akilalamika eti nimemtusi sana. Pole yake hakujua mimi ni
wa aina gani kwa wakati huo, alikutana na teke moja maridhawa akaangukia kwenye
viti huko akatokwa na yowe la hofu, Desmund akamkanya asiniguse. Nikaondoka na
kuahidi kurejea baada ya siku hizo tatu.
Niliondoka
pale na kuchukua mabasi kwa safari ya Mwanza, kila abiria alikuwa akizungumzia
habari ambayo nilikuwa siijui lakini nilipolikanyaga jiji ndipo nikaamini laana
yangu inashambulia hadi watu wasiohusika.
Jiji la
Mwanza lilikuwa limekumbwa na mafuriko, nyumba ziliezuliwqa na nyingine
kusombwa na maji, hali ilikuwa mbaya. Sikuishughulisha akili yangu kuwaza juu
ya familia yangu kwa wakati huo, yaani Jonas na Desmund Jr. lakini akili
ilichanganyikiwa baada ya kukuta eneo alilokuwa akiishi yule dada na wale
watoto nyumba zikiwa zimemezwa na maji. Nilifanikiwa kuonana na jamaa yake yule
dada.
“Mvua
imeondoka na dada yangu jamaniii…” aliugulia, nikakosa la kusema.
“Na vile
vitoto masikini vimekufa vikiwa vimekumbatiana naye, jamani aah!! Dada weee!!” alianza
kulia, nikaungana naye kwa uchungu mkubwa, nikiwa nimepagawa kabisa nakujiuliza
kama ni kweli nayasikia maneno yale ama la!! Nilikuwa naota….hapakuwa na ndoto
pale hali ilikuwa halisi kabisa. Nikaongozana na yule kijana hadi Bugando
mochwari tukajieleza na kisha tukaonyeshwa maiti zile. Hakika alikuwa ni Jonas
na yule mwingine alikuwa ni Desmund jr.
Mwandishi
sikuwahi kushikwa na uchungu wa moja kwa moja moyoni namna ile katika misiba
lakini msiba huu ulinichanganya na kujina mimi sina haki ya kuishi kabisa,
nilijiona niliyelaaniwa na laana yangu inaishi nami. Nikaamua kurejea Musoma
baada ya kuwazika watoto wale, nikamkabili Desmund, alikuwa ndani ya nyumba
ileile lakini milioni mia mbili zilikuwepo mezani.
Nikahitaji
kujua ni kipi chanzo zcha yeye kunitenda vile hadi kunisababishia laana.
Desmund
alinisimulia mkasa juu ya baba yake
mzazi alivyodhulumiwa mali na mzee wa kiarabu, akaelezea juu ya mzee huyo
kumuua baba yake mzazi mbele ya macho yake yeye akiwa bado mdogo, hali hiyo
ikamfanya awe na chuki na ngozi hii, baada ya kuamua kuendelea na maisha
akaajiliwa na mwarabu huku napo akajikuta anateswa sana huku akizidi kupoteza
uelekeao wa maisha, hiyo haikuwa simulizi pekee bali akaenda mbali zaidi na
kunieleza juu ya kifo cha dada yake ambaye aliolewa na mwarabu licha ya yeye
kumzuia, dada akayavumilia mengi ya ndoa lakini siku ya kukata roho akamweleza
Desmund kuwa yule mwarabu alikuwa anamlawiti mara kwa mara, hivyo anakufa kwa
sababu alikuwa anatendwa vibaya. Nilijisikia vibaya kumwona Desmund akliwa
analia kwa uchungu huku akiikumbatia picha ya dada yake lakini nilijikaza
nisidondoshe machozi kwani ungekuwa udhaifu wa hali ya juu.
Desmund
akakiri kuwa alivurugwa akili kabisa na ngozi hiyo na hata ndugu zake na
marafiki wa karibu walijikuta wakiichukia ngozi ile. Naam!! Desmund akanichukia
na mimi na kuamua kutulizia maumivu yake huku. Nilimwelewa Desmund na sikutaka
kumweleza zaidi juu ya upendo wangu kwake katika kipindi hicho. Sasa alikuwa
amechelewa sana kunitaka radhi, nikambana na maswali juu ya nani alimuua Danny
yule askari, akajibaraguza lakini baadaye akakiri kuwa angeweza kumdhuru mtu
yeyote ambaye angeweza kunitetea, hivyo Danny alikosea kunitetea. Desmund
alimuua Danny. Hasira zikanichemka nilipokikumbuka kifo cha Danny mtetezi wangu.
Hapa sasa
nikaamua kufanya nililotaka kufanya, nikamkabili Desmund aliyekonda klidhaifu
kabisa nikachomoa kisu changu na kukisukumiza katika mbavu zake, aliga kelele
nikawa kumziba mdomo. Niliona mwanaume huyu hakufaa kuishi hata kidogo na
sikutaka kuwa na udhaifu kama ule wa Jesca wa kumchekea adui. Aliyefuata baada
ya pale ni mkewe, huyu alipoingia ndani tu nikamkaba, hata sikutumia kisu,
nilimnyonga hadi akapoteza uhai. Nafsi yangu ikapata ahueni. Wataishi vipi watu
hawa wabaya wakati kitoto kisichojua lolote kimekufa huko Mwanza kwa makosa ya
wazazi wao.
Nikaunganisha
safari yangu moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee Matata, nikamuulizia hakuwa
anapatikana tena hapo, lakini si hapo tu hata ulimwenguni hakuwa anapatikana,
mzee Matata alikuwa marehemu, alikufa kwa kupigwa risasi. Waliompiga
hawakujulikana.
Wamenisaidia
hao!! Nilijisemea na kujiaminisha kuwa ni mzee huyu aliyeniteka na kunitupa
katika dimbwi la kuwa msafirishaji wa madawa ya kulevya .
Nilipomaliza
hapo, nilikuwa nimechakaa nafsi na sikujua kabisa kama nilikuwa nina chochote
cha kufanya duniani, milioni mia mbili hazikuwa na maana yoyote kwangu
nikaziacha nyumbani kwa Desmund.
Nikaondoka
kwa nia moja tu ya kujiua, na hapo ndipo nikakutana nawe kichakani usiku ule
mkiwa mmeharibikiwa damu, ukanisihi sana hadi nikaamua kufuatana nanyi, hakika
unayo lugha ya ushawishi sana, uliweza kunibadili mawazo yangu, umeweza
kunifanya mtu mwingine tena na kujikuta natabasamu mara kwa mara. Uliponichukua
sikuamini kama nitakuamini hata kidogo, lakini umekuwa wa pekee sana kwangu,
lakini kitu kimoja tu, sihitaji twende wote Dar es salaam mimi nina mikosi
sitaki kukuambukiza mikosi yangu, sitaki maafa yaliyolikumba jiji la Mwanza
yahamie pia Dar es salaam, hii yatosha.
Wewe ni
mshauri mzuri sana tena mwenye ushawishi sasa nahofia kuwa katika maamuzi haya
ningekushirikisha lazima ungeyabadili mawazo yangu tu hiyo lazima ingetokea.
Ni kweli
labda kuna maswali yako mengi sijayajibu, hii yote labda ni kwa sababu ya
uchovu wa akili na msongo wa mawazo vilevile, kama utabaki na maswali naamini
hautapata nafasi ya kuyasikia nikiyajibu, si kwamba hatutaonana tena ama labda
niseme si kwamba hautaniona tena bali utaniona lakini hakika sitakuwa tayari
kusema lolote lile. Najua wewe ni bingwa wa kusihi na kubembeleza lakini
sitabembelezeka katika hilo niliyokueleza yanatosha sana, yasambaze katika
dunia, mimi Nadia nimekubali kuwa mfano kwa wasichana na wanadamu wenzangu
usiogope kusema ukweli kama nililawitiwa, usifiche juu ya shughuli za
usafirishaji madawa kuwa muwazi kama nilivyokuwa muwazi kwako. Gerlad Iron baki
na sauti hii milele, iishi sauti hii kizazi hadi kizazi, tone la chozi langu
wasimulie wahangaikaji wa dunia, kwikwi yangu iwe funzo kwao na amani ya bwana
iwe nawe G katika lolote lile utakalofanya na limpendeze Mungu!!! Uwe na amani.
Tutaonana inshalah!!”
Sauti ya
Nadia ilimaliza na ule ukawa mwisho wa kurekodi, nilivaa viatu vyangu upesi
upesi huku nikiamini kuwa natakiwa kwenda mahali lakini ni wapi ningeenda,
nikawa mnyonge na kukaa chini tena. Nikajipa moyo kuwa huenda Nadia atarudi
jioni. Hadi kufikia saa kumi na mbili bado mambo yalikuwa yaleyale. Lakini saa
moja Nadia alirejea!!
Hakika
alirejea chumbani lakini katika namna ambayo alikuwa ameahidi, hakuwa Nadia
ninayeweza kumshika na kumliwaza bali alikuwa Nadia katika luninga akiwa
ametulia tuli waandishi wa habari wakimpiga picha.
Nadia alikuwa
amejinyonga!!!
Niliishiwa
nguvu nikabaki kukodoa macho tu..mwandishi yule aliyeisoma habari hiyo kwa
majonzi alipiga nyundo ya mwisho kwa kusema kuwa, marehemu aliacha ujumbe mfupi
sana wenye majina mawili.
“Nadia
Gerlad”, hapo nikazidi kusisimka na kupagawa zaidi. Lakini sikuwa na ujanja
kifo hakina mbadala, alikufa na inabaki hivyo kuwa alikufa.
Kumbe Nadia
alipanga kujiua!! Nilijiuliza lakini nani angenijibu!! Hakuna wa kunijibu!!
Nikapitiwa na
usingizi, kesho yake nikaamkia kituo cha polisi kutoa taarifa kuwa Nadia ni
dada yangu!! Wakanielewa na nikapewa ruhusa ya kuuchukua mwili.
Nilifanikiwa kuuchukua
na kufuata hatua zote, Nadia akasafirishwa kuelekea jijini Dar es salaam,
familia yangu ambayo ilikuwa na taarifa tayari iliupokea mwili wa Nadia, kisha
mimi nilifika siku moja baadaye. Nadia akazikwa kwa heshima zote kama ndugu
katika familia yetu.
Kampuni
iliyoniajiri ilijumuika nasi katika msiba huu huku kila mmoja akingojea kusikia
ni kitu gani nilivuna kwa miezi yote hiyo tangu nikutane na Nadia.
Baada ya siku
arobaini, niliibuka hadharani nikiwa na kila kitu kuhusiana na Nadia, sauti na
baadhi ya picha.
Kila mwenye
moyo wa nyama aliposikia juu ya Nadia alitokwa na machozi. Wengi walijifunza
kutokana na simulizi ya Nadia
Kuna kipindi
nilikuwa najiuliza hivi ni kweli nilikutana na Nadia, na hapo nikajikuta
naisikiliza sauti yake tena na tena huku nikizitazama picha zake nilizowahi
kumpiga.
Mwisho
nikaibuka na kitabu kikubwa cha simulizi nilichokipa jina la USILIE
NADIA…kitabu kilichokuwa maalumu kwa msichana aliyesota ulimwenguni kupigania
haki yake na mwisho akatoweka akiwa amelipiza kisasi!!!
NADIA
BARGHASH!!! Aliyeishi pia kwa jina la MARIAM
na baadaye MAMA JONAS huku akiamua kufa kwa jina la NADIA GERLAD!!!!
MWISHOOO!!!
WADAU MAONI YENU NI MUHIMU SANA ILI TUWEZE KUBORESHA UWANJA HUU
Maoni 3 :
Kazi nzuri sana, simulizi ni tamu sana. ni vizuri ungetoa kitabu ili kila mtu asome inafundisha sana. Asante sana mwandishi
Mhh Nadia,...kwanza nikushukuru kwa kutupa simulizi hili na mwengine, kwani muda na kufikiri ni gharama, pili nikupo hongera, kwani pamoja na hayo umeweza KUCHAPA vitabu kitu ambacho wengine bado kinatupa shida, narudia tena kusema HONGERA MPENDWA, na TUPO PAMOJA
hongera della kwa story nzr, inahuzunisha sana, kama unaweza tafuta wasanii wakubwa wa hapa tz watengenezee filam ya ii stor yako mana ina mafundisho mazuri,
asante sana, tupe na nyngne ila zisiwe za kichawi bana
Chapisha Maoni