Na. Freddy Macha |
Kuna siku nilikuwa dukani nikikagua nazi kwa ajili ya kula.
Nikawa nikiitikisa tikisa na kuidonoa kwa fedha, kuufahamu mlio wake.
Wazungu watatu kando walinitazama wakiona kama muujiza. Nikawaambia ule
ni ufundi rasmi wa Kiafrika. Sasa wakaniomba niwasaidie kukagua nazi
zao. Moja ya sifa za mzungu ndiyo hiyo. Kama hajui, hataona aibu
kuuliza. Utamwona mjinga mjinga kumbe mwenzio, yuko shule. Iko siku
utamshangaa hata kitabu atakiandika kuhusu elimu ile. Wewe utabaki vile
vile. Waafrika tuna tatizo la kutoweka kumbukumbu na taarifa. Mambo yetu
mengi yameishia tu vichakani. Elimu na busara za zamani Afrika zinaanza
kupotea kutokana na siye kuwa wavivu kuhimiza kumbukumbu, kimaandishi.
Wajukuu wetu watajifunza wapi?
Mwaka 2007 Rais Jakaya Kikwete alihutubia
Watanzania hapa London akagusia kadhia ya wanajeshi, maana yeye
kitaaluma ndiko alikoanzia. Akasema huwa jeshi huchagua vijana kwa kuwa
bado wana moto na afya. Ujana ni wakati muhimu sana. Ndiyo maana
ukichunguza hawa magaidi, wote hunasa vijana. Ukitazama wakimbizi
wanaofia majini kwenye Bahari ya Mediterranean, takriban wote ni vijana.
Waafrika walioshambuliwa na wenyeji kule Afrika Kusini, wengi wao
vijana.
Kawaida mtoto asipokuwa na wa kumwongoza, hugeuka
mwizi au yatima. Vijana ndiyo wanaoongoza mabadiliko (au maasi) ya
kijamii duniani. Hivyo matatizo yanayoonekana ni dalili ya tu ya tunda
au nazi kutokuwa sawa ndani. Kujua chanzo cha dalili ni kulifahamu
tunda. Askari wanapotumwa kupiga au kuua, hupalilia tu hasira, chuki na
uhasama.
Mwanzo wa wiki hii msemaji wa Shirika la Uhamiaji
la Kimataifa (IOM), mjini Geneva, Uswisi, Joel Millman alisema hadi sasa
Waafrika na Waarabu 1,727 wamefariki wakivuka Bahari ya Mediterranean
kuingia Ulaya. Akasisitiza idadi hii ni mara 10 zaidi ya mwaka jana.
Mwaka 2013 ni watu 600 tu waliokufa maji; wakafikia 4,000 mwaka 2014.
Makisio ya Millman ni vifo 30,000 mwisho wa 2015. Iko kazi.
Ingawa lawama kwa Jumuiya ya Ulaya kutofanya zaidi
kuwaokoa wakimbizi zimekuwa nyingi, ilitangazwa kuwa kiasi cha
wakimbizi 11,000 walifaulu kutua Italia. Walipokewa na askari, wasamaria
wema, wanahabari na hata mfanyabiashara mmoja aliyejitolea kuigeuza
hoteli yake kuwa stara ya muda mfupi. Miongoni mwa wakimbizi hawa
wanaokimbia vita, umaskini na tafrani (kutoka ukanda wa Sahel, Arabuni
na Afrika Mashariki) ni kina mama waja wazito, wasichana vigoli, watoto
wadogo, vijana, wanaume kwa wanawake.
Oktoba 2014, mwandishi na mkalimani maarufu wa
Kiitaliano, Aldo Busi, alisema ameacha kula samaki. “Siku hizi sinunui
tena samaki kutoka Bahari ya Mediterrenean shauri naogopa samaki hawa
wamekula maiti za Walibya, Wasyria, Wasomali na Wairaki. Mimi si mla
watu. Ninakula samaki waliofugwa au kutoka Bahari ya Atlantic.”
Wiki iliyopita BBC ilimwonyesha mwanahabari wake
mweusi, Reggie Yates, akishiriki maandamano ya kundi la weupe linalopiga
wageni nchini Urusi. Yates alionyesha namna moja ya makundi haya
yanavyofanya mazoezi ya viungo na visu. Mkimbizi wa Kikongo aliyehojiwa
alikiri kukatwa tumboni, bahati nzuri hakufariki. Na nchini Ugiriki,
chama cha mafashisti, Golden Dawn, kimekuwa kikipiga na kuua wahamiaji
tangu kilipoundwa miaka 30 iliyopita. Mwaka 2012 Golden Dawn
ilishambulia sehemu wanayoishi Watanzania mjini Athens.
Juma lililopita eneo la Durban, Afrika Kusini,
lilikuwa na makonzi kwa wageni. Kati ya waliohasimiwa walikuwa
Watanzania wawili. Baada ya rabsha hizi, Rais Jacob Zuma aliahirisha
ziara yake barani Asia kusimamia tatizo. Hadi makala hii ikiandikwa
wageni 5,000 walitazamiwa kuondoka Afrika Kusini, huku jeshi la nchi
likitoa ulinzi.
Siyo mara ya kwanza kwa wenyeji kuwahasidi wageni
Afrika Kusini. Mwaka 2008, mashambulizi ya wahamiaji kwenye jimbo la
Alexandria, kaskazini mashariki ya Johannesburg, yalisababisha vifo vya
watu wawili na majeruhi 40. Hatimaye wenyeji 200 walitiwa nguvuni kwa
hatia za kubaka, wizi, kuua, na uharibifu wa mali ya umma.
Wiki jana, Waziri Mkuu wa Ethiopia, HaileMariam
Desalegn alilalamika kwa niaba ya Waafrika wote. “Tulichangia harakati
za Afrika Kusini dhidi ya makaburu, hivyo ni vyema uwepo uhuru wa kila
Mwafrika kwenda popote atakako ili mradi havunji sheria.”
Ama kweli shukrani ya punda ni mateke.
Tukija Afrika Mashariki.
Baada ya mauaji ya Garissa, serikali ya Kenya
ilitangaza kufunga kambi ya wakimbizi wa Kisomali iliyoko Daadab,
mpakani na Kenya. Msemaji wa shirika huria la kuhudumia na kutibu bure
duniani, Medecines Sans Frontiers, Bw Kenneth Lavelle alilaumu kufungwa
kwa kambi hiyo kuwa kutawaathiri sana maskini na wanaohitaji msaada.
Mpigania haki za binadamu toka Kenya Onyonga Oloo naye alikashifu
kitendo akasisitiza lazima Kenya itimize masharti ya kanuni za kimataifa
na kibiashara.
Tunafahamu kwanini kambi imefungwa. Ni jitihada za
serikali ya Kenya kupambana na ugaidi wa Al Shabaab. Jitihada nyingine
zimekuwa ni kufunga mpaka wake na Somalia kwa kujenga ukuta mrefu
utakaozuia magaidi hao kuua Wakenya.
Mifano hii michache inatufanya tujiulize kwanini watu hukimbia kwao kwenda kuishi kwingine?
Tunajuaje kuwa tunda limeoza ndani? Nini dalili za mvua?
Kundi la Al Shabaab lilitokana na hali ya uasi na
serikali dhaifu baada ya aliyekuwa Rais wa Somalia, Siad Barre,
kung’olewa mwaka 1991; akafariki 1995.
Tukio la wananchi wa Kilombero wiki jana kufichua
waliokisiwa kuwa wafuasi wa Al Shaabab kwenye msikiti wa kata ya Kidatu
na kumpiga mmoja wao (kama mwizi) kumeshangiliwa sana hasa na watoa
maoni kutoka Kenya, gazeti la The Citizen.
Watanzania tuna historia ya kuunga mkono mapambano
ya haki na kutetea wakimbizi duniani. Mbali na wapigania uhuru,
tulisaidia kumnyofoa nduli Idi Amin mwaka 1979.
Mtoa maoni Maina: “ Kazi nzuri Tanzania. Pambana
na mdudu huyu mharibifu kabla ya imani zake za enzi za watu wa mawe
hazijazagaa.”
Mtoa maoni, Oluoch :“Kazi njema jamaa zangu. Na hawa viumbe watumiwe kuwataja wenzao wanaojificha misikitini.”
Kitendo cha wananchi wa Kilombero ni mfano wa
kuigwa na wote. Ikiwa kila mwananchi atakuwa na msimamo thabiti kulinda
nchi yetu tutaendelea kudumisha Tanzania ya amani. Hata tukiwa maskini
kiasi gani, tusisahau tunaheshimika miaka mingi kwa maarifa ya kulijua
tunda.
-London, 21 Aprili, 2015 Bpepe: gmacha52@gmail.com CHANZO MWANANCHI
Maoni 1 :
Wow sijui nisemaje. Nahisi kama nimepelekwa shule. Kweli watanzania tuendelee na kazi ya kulitambua tunda.
Chapisha Maoni