Pages

Jumamosi, Aprili 04, 2015

EMBU SOMA UCHAMBUZI HUU "Wanawake bado wanaathiriwa na hali ya utegemezi kwa wanaume."

Tangu enzi na enzi wanawake wamekuwa wakichukuliwa kama wasaidizi wa wanaume na wamekuwa hawahusishwi kwenye nafasi mbalimbali, hasa zile kubwa serikalini, hata kwenye madhehebu mbalimbali ya dini. Ingawa katika nchi zilizoendelea kama za Ulaya na Marekani, wamepiga hatua kubwa katika kupunguza pengo la jinsi, hata wao hawajaufikia usawa kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana hadi leo hajatokea rais mwanamke Marekani kati ya marais 44.
Uingereza ni hivi karibuni tu ndiyo tumesikia akichaguliwa askofu wa kwanza mwanamke kutoka Kanisa la Anglikana.
 Kwenye mihimili mikuu ya dola bado uwakilishi wa wanawake ni mdogo na katika utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na Umoja wa Mabunge (IPU) unabaini kuwa wanawake wengi pia wamekuwa waoga wa kuthubutu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na hasa za kisiasa.

Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu, hakuna mwanamke hata mmoja ambaye amejitokeza hadharani. Waliojitokeza na kutangaza hadharani ni zaidi ya watano na hakuna mwanamke hata mmoja. Hali hii inatokea wakati wapo wanawake wengi wenye uwezo na elimu ya vyuo vikuu.
Marais wanawake Afrika ni Joyce Banda wa Malawi na Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia. Hawa wanabaki kuwa mifano pekee ya wanawake mashuhuri waliopambana bila kuogopa dhidi ya mfumo dume na hatimaye wakaweza kuwa marais.
Kwenye nyanja za kiuchumi, wanawake pia bado wako nyuma na hususan kwenye umiliki wa biashara kubwa na viwanda, ingawa kwenye uzalishaji ngazi ya chini, inasemekana wao ndiyo wazalishaji wakubwa.
 Wanawake bado wanaathiriwa na hali ya utegemezi kwa wanaume.
Wengi hupata wakati mgumu kuyakabili maisha, inapotokea kufiwa na waume zao ingawa ni wazalishaji wakubwa. Hii inaonyesha kuwa  wameendelea kubakia tegemezi kwenye kufanya uamuzi na kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
Wanawake wanakumbwa na changamoto nyingi na hasa vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa kwenye ndoa kama kupigwa, kukeketwa, kutengwa au kunyanyaswa kwa sababu ya kutozaa au kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi.
Wanawake wazee pia wanauawa kwa imani za kishirikina na hasa wale wenye macho mekundu.
Matukio ya ndoa na mimba za utotoni bado yameshamiri na yamekuwa kikwazo kwa watoto wa kike kupata elimu, yote hayo yamekuwa yakisababishwa na ujinga pamoja na umaskini.

Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa mimba na ndoa za utotoni kwa mujibu wa shirika la haki za binadamu duniani.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) katika miezi ya karibuni  waliendesha kampeni dhidi ya ndoa na mimba za utotoni. Hii iliandamana pamoja na kupinga ukeketwaji wa wasichana kwenye mikoa ya kanda ya ziwa.
Sababu nyingine inayosababisha kuendelea kwa mimba na ndoa za utotoni ni kasoro zilizopo kwenye sheria ya ndoa ya mwaka 1971.
Katika sheria hiyo, licha ya kutaja umri wa kuolewa kuwa ni miaka 18, sheria imeruhusu mtoto wa miaka 15 na 14 kuolewa kwa idhini ya wazazi na mahakama, kinyume na sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inasema; ‘Mtoto ni yule mwenye umri ulio chini ya miaka 18 na haruhusiwi kuolewa.’
Inabidi sheria ya ndoa iangaliwe upya ili tufanye kama wenzetu wa Malawi ambao hivi karibuni wamepitisha sheria inayopiga marufuku mtoto aliye na umri wa chini ya miaka 18 kuolewa na atakayekiuka atapewa adhabu kali.
Tumaini Munale  ni mkufunzi Chuo cha Ualimu Bunda TC. (0755554694) 
CHANZO MWANANCHI

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom