Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema Tanzania ina
sera nzuri ya kuwawezesha Watanzania, wakiwamo vijana kujikwamua katika
hali duni za maisha, lakini haitekelezwi.
Alisema hayo katika uzinduzi wa programu ya Airtel Fursa, jana jijini Dar es Salaam.
Dk. Mengi alisema sera ya kuwezesha wananchi ya mwaka 2004 nchini
ni nzuri, lakini inaishia katika maneno majukwaani, vinginevyo ingeweza
kuwafikisha mbali Watanzania katika kuboresha maisha yao.
“Sera ya kuwawezesha wananchi ipo. Ni nzuri sana. Ingeshughulikiwa
kivitendo, wangekuwa mbali. Lakini leo sera ya kuwawezesha wananchi
inaishia katika maneno majukwaani,” alisema Dk. Mengi.
Aliwataka vijana kufanya kazi kwa bidii na kuwa na ndoto kubwa siyo
kwa kutaka kufanana na matajiri walioanza, bali kuwa na malengo zaidi
yao.
Alisema ili vijana wafanikiwe katika hilo, wanapaswa kuwa na macho
yanayoona fursa, kujiamini, kutojiona wadogo, kwani katika umri walionao
wanaweza kuwa matajiri.
Dk.
Mengi alisema hakuna aliyezaliwa kuwa wa pili, lakini baadhi ya
viongozi wanaona hivyo kwani fursa zinapotokea zinaenda kwa watu wa nje
mbali na kuwapo kwa sera hiyo.
“Vijana wengi wanashindwa kuanzia wapi. Kinachotakiwa ni kuwa na
macho yanayoona fursa. Mahali pa kuanzia ni kuwa na ndoto kubwa...ndoto
kubwa huanza na kidogo na kujua unakotaka kwenda,” alisema Dk. Mengi.
Mkurugenzi wa Airtel Tanzania, Sunil Colaso, alisema Tanzania ni
moja ya nchi inayokua kwa kasi kiuchumi, huku asilimia kubwa ikiwa ni
vijana, ambao wanahitaji kuwezeshwa kufikia malengo yao na kuwaandaa
kuwa wafanyabiashara wakubwa wa baadaye.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Airtel, Balozi Juma Mwapachu,
alimpongeza Dk. Mengi, akisema ni Mtanzania pekee, ambaye yupo mstari wa
mbele kutetea maslahi ya wazalendo na kutiwa moyo na vijana, ambao wapo
tayari kujiwezesha na kuwezeshwa kufanikisha malengo yao.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni