Jumatano, Juni 03, 2015

Lowassa, Wasira, Mwandosya, Makongoro kuchukua fomu leo.

Makada watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo watafungua pazia kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
 
Leo ndiyo siku ya kwanza ya uchukuaji fomu ndani ya CCM kwa ajili ya kurithi nafasi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye anang’atuka kwa mujibu wa katiba ya nchi.
 
Makada watakaochukua fomu hizo leo baada ya kutangaza nia kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Charles  Makongoro Nyerere.
 
Makada hao watatangulia kuchukua fomu hizo huku chama hicho kikitoa masharti makali yanayotakiwa kufuatwa na wagombea.
 
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM wa Idara ya Oganizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatibu, alisema makada watano wataanza kufungua pazia la uchukuaji fomu leo katika makao makuu CCM mjini Dodoma.
 
Alisema katika utaratibu huo, Prof. Mwandosya ndiye atakayekuwa wa kwanza kuchukua fomu saa 4:00 asubuhi akifuatiwa na Wasira.
 
Dk. Khatibu alisema Lowassa atakuwa wa tatu kuchukua fomu hiyo saa 7:00 mchana, akifuatiwa na Balozi Amina saa 8:30 na Nyerere atafunga dimba kwa leo.
 
Alisema ratiba ya uchukuaji fomu hiyo haikupangwa kwa kufuata umaarufu au cheo cha mtu ndani ya chama na serikali bali umezingatia mgombea kuwahi kutoa taarifa katika chama kwamba anataka kuchukua fomu.
 
UCHUKUAJI FOMU Z’BAR
Kwa upande wa Zanzibar, alisema wagombea wanaowania urais wa Zanzibar watachukulia fomu katika ofisi za CCM na wale wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watachukulia mjini Dodoma.
 
“Kama mgombea hawezi kufika Dodoma basi hawezi kuwa Rais, wagombea wajitokeze kwa muda uliopangwa   kuchukua fomu, hatuwezi kukaa hapa mwezi mzima kuwasubiri wao,” alisema.
 
YALIYOMO KATIKA FOMU
Alisema fomu zitakazotolewa ambazo zitatakiwa kujazwa zitakuwa na maelezo binafsi ya mgombea na fomu ya orodha ya wadhamini 450 kama taratibu, kanuni na sheria zinavyoelekeza. 
 
 “Wadhamini wa mgombea hawatakiwi kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama na hawatakiwi kudhamini zaidi ya mgombea mmoja, fomu hizi kabla ya kuzirejesha zinatakiwa zipigwe mhuri na Katibu wa CCM wa wilaya anayotoka mgombea,’’ alisema. Aliongeza fomu hizo zitatolewa katika ofisi ya sekretarieti chini ya usimamizi wake (Khatibu) ambaye amepewa kazi hiyo na chama.
 
MASHARTI KWA WAGOMBEA
Alisema kila mgombea atatakiwa kuingia katika ofisi za kuchukulia fomu akiwa na familia yake ndugu na jamaa wasiozidi 10 na pamoja na Sh. milioni moja ambazo ni gharama za kuchukulia fomu. Alisema baada ya kuchukua fomu, kila mgombea atapewa muda wa saa moja na nusu kuwapo ndani ya jengo la CCM na kuzungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Nec na baada ya hapo atatakiwa kuondoka kupisha mwezake.
 
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema wakati wa kutoa fomu aliwataka makada hao kuzingatia kanuni na taratibu za chama ikiwa ni pamoja na kuzisoma ili wasifanye kinyume cha taratibu na kwamba mbwembwe za aina yoyote haziruhusiwi.
 
“Tusingependa kuona wale wanaokuja kuchukua fomu na kuzirejesha wanakuja kwa mbwembwe, hatutaki sherehe wala madoido, safari hii kosa moja goli moja,” alisema.
 
Hadi kufikia jana idadi ya makada wa CCM waliotangaza nia ya kuwania urais hadharani ni Lowassa, Wasira, Mwigulu Nchemba, Prof, Mwandosya, Nyerere na Balozi Amina, Titus Kamani, Prof. Sospeter Muhongo, Balozi Ali Abeid Karume,  Luhana Mpina na Frederick Sumaye na Lazaro Nyalandu.
 
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM, kazi ya uchukuaji na kurejesha fomu itakamika Julai 2, mwaka huu na kufuatiwa na vikao vya chama vya uteuzi wa kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM kupambana na wagombe wa vyama vya upinzani. Mgombea wa CCM atapatikana Julai 12, mwaka huu baada ya kupitishwa na mkutano mkuu utakaoanza Julai 11.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeshatangaza rasmi kuwa uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 25, mwaka huu kwa ajili ya kuchagua Rais, wabunge na madiwani.
 
Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu Jumamosi ijayo atahutubia wananchi rasmi akiwa mkoani Singida  kabla ya kuelekea Dodoma kuchukuwa fomu ya kuwania urais.
 
Nyalandu ambaye amekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa miaka kumi sasa, pia atatumia mkutano huo wa hadhara utakaorushwa hewani moja kwa moja na vituo vya televisheni vya EATV, STAR TV na  ITV kusikiliza  hoja mbalimbali  kutoka kwa wananchi pamoja na kujibu maswali yao mbalimbali.
 
Nyalandu alishatangaza nia ya kuwania urais mapema mwaka huu jimboni kwake mkoani Singida.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom