Uamuzi wa jana wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujitoa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na
maendeleo (Chadema), wananchi kadhaa wametoa maoni tofauti kuhusiana na
uamuzi wa mwanasiasa huyo.
MAKAMU RAIS TEC
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu
Severine Niwemugizi, alisema hatua ya Lowassa ni ukomavu wa vyama vya
siasa nchini hasa vya upinzani kuwa mtu yoyote anaweza kuhama na
kujiunga na chama chochote.
“Tafsiri ni kuwa ameona CCM haikumtendea haki na kama binadamu
yeyote ana haki ya kuchukua hatua kama binadamu mwingine, mtu anapoona
hajatendewa haki kama binadamu uamuzi ni wake kuondoka kama wengine
wanavyobadilisha vyama, hatushangai ni jambo linatokea kwa wengi siyo la
pekee sana,” alisema na kuongeza:
“Tafsiri nyingine ni ukomavu wa vyama vyote vinaendelea kukua
kiasiasa, kusema vyama vya upinzani havijakomaa siyo kweli, kama
kiongozi wa juu anaweza kuona chama cha upinzani ni mbadala, wasiendelee
kushambuliana kwenye majukwa.”
Askofu Niwemugizi alisema Lowassa siyo wa kwanza kukihama chama
tawala kwani kuna nchi nyingi hata marais wanahama vyama vyao waliwahi
kuhama, hivyo ni ukomavu wa demokrasia nchini.
Alisema anaamini Lowassa ataleta ushindani mkubwa, kwani mchuano
utakuwa mkali kwa kuwa watanzania wengi wanamuunga mkono huku Mgombea wa
CCM, Dk. John Magufuli, naye anaungwa mkono.
“Matarajio ya umma ni makubwa, tunachoomba kusiwe na rafu kila mmoja awe muungwana wakati wa kampeni,” alisema.
Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda, alisema hata katibu Mkuu
wa zamani wa CCM, Hayati Horace Kolimba, alikihama chama hicho, hivyo ni
jambo la kawaida na ni haki yake.
“Kuhama Chama ni haki ya kidemokrasia ya kila mtu, kama unaona
mfumo unakubana katika chama ulipo haufai unaweza kuhama ukaenda mahali
ambapo unaona ni sahihi, hilo siyo jambo baya,” alisema Akitanda.
Mwenyekiti wa Alliance For Democratic Change (ADC), Said Miraaj,
alisema kabla ya kurejesha mfumo wa vyama vingi ilikuwa ngumu kuhama
chama, lakini baada ya kurejeshwa mfumo huo ilimpa uhuru kila mtu
kujiunga na chama anachotaka.
Alisema alichokifanya Lowassa siyo kitu cha ajabu kwa kuwa hata
wengine waliopita walishawahi kufanya hivyo kwa kuwa ni haki ya kila
mtu kujiunga na chama chochote anachoona kinamfaa.
Alisema wapo waanzilishi katika vyama mbalimbali waliovihama vyama
vyao licha ya kwamba walivianzisha na kwamba asilimia 80 ya wanzilishi
wa vyama hivyo walivihama.
Mwenyekiti wa Chama Cha United Peoples Democratic Party (UPDP),
Fahmi Dovutwa, alisema uamuzi wa Lowassa siyo mbaya kwa kuwa ana haki ya
kufanya hivyo.
“Mimi sioni ubaya kwa Lowassa kuhamia Chadema kwa kuwa ni haki yake
ya kidemokrasia, wala sioni ubaya Chadema kumpokea kwa kuwa ndiyo kazi
ya chama cha siasa kuongeza wanachama,” alisema Dovutwa na kuongeza:
“Labda kaona hapo alipokuwa hawezi kutimiza malengo yake na huko
alikoenda atatimiza malengo siyo mbaya , mimi naona alichofanya ni
sahihi.”
DK. Bana Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na
Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (UDSM), Dk. Benson Bana,
alisema ni haki ya kila Mtanzania kuhama au kuchagua chama anachoona
kinamfaa.
Alisema maamuzi ya Lowassa ni haki yake ya kidemokrasia, hivyo maamuzi yake yanahitaji kuheshimiwa.
“Naona yuko sawa, lakini kama kweli atahamia Ukawa bado naona
atakuwa amekwenda kwa ajili ya kupata madaraka iwapo atateuliwa na Ukawa
kugombea urais,” alisema Dk. Bana.
Alieleza kuwa Lowassa atakuwa sahihi endapo atakuwa amejiunga
Chadema kwa sababu ya kushawishika na sera za Chadema kwa malengo ya
kuzitumia na kukijenga chama, lakini si kwenda huko na kupewa nafasi ya
kugombea urais.
Alieleza kuwakama Ukawa wanaweza kumsimamisha kuwania nafasi hiyo
kubwa wanajifedhehesha na kuwaaminisha Watanzania kuwa Lowassa ni mkubwa
kuliko taasisi zilizounda Ukawa.
“Akiwania urais inatupa ukakasi kwani haiwezekani taasisi zote
zikamsimamisha mtu mmoja pekee ambaye hakuwepo katika umoja huo,
itamaanisha kuwa amezinunua taasisi zote hizi. Pia Ukawa wasishangae
kuitwa CCM namba mbili kwani sasa watamsimamisha mgombea anayetokana na
CCM,” alisema Dk. Bana.
KIJO BISIMBA
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.
Hellen-Kijo Bisimba, alisema kitendo cha Lowassa kujiunga na Chadema
hakimaamishi kuwa kweli ana wito wa kuwatumikia Watanzania.
Alieleza kuwa kama Lowassa kweli alikuwa na dhamira ya dhati ya
kuwasaidia Watanzania, angefanya hivyo akiwa ndani ya chama chake.
“Chama alichotoka Lowassa hakiendani kabisa na sera za chama
anachokwenda, sasa anawezaje kwenda huko na kupewa madaraka badala ya
kuwa mwanachama kwanza?” alihoji na kuendelea: “Huku ni kutafuta
madaraka.”
“Kama Lowassa atapatiwa nafasi hiyo ni wazi kuwa kimwili atakuwa
na umoja huo, lakini akili na mawazo yake yatakuwa bado yako CCM kwani
lengo na dhamira yake ni kupata uongozi na atakuwa hajaachana na itikadi
za chama chake,” alisema.
NICOLAUS MGAYA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni