Jumanne, Agosti 11, 2015

Kashfa, matusi viepukwe kuelekea Uchaguzi Mkuu.



Zimebaki takriban siku 73 tu kuanzia leo kabla ya kufikia Oktoba 25 wakati Watanzania wote waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura watakapopata nafasi ya kuchagua viongozi watakakuwa madarakani kwa miaka mitano ijayo.
 
Uchaguzi huo utakaokuwa wa tano tangu kuanza kufuatwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, utatoa fursa ya kupatikana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na pia madiwani.
 
Hakika, hiki ni kipindi muhimu kwa mustakabali wa taifa kwani kwa namna yoyote ile, kufanyika kwa uchaguzi unaozingatia sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea kutatimiza ndoto ya walio wengi ya kuendelea kuwa na taifa linalojivunia tunu za amani na utulivu. Kinyume chake, kama uchaguzi utavurugika kwa namna yoyote ile, ni wazi kuwa taifa litawekwa njiapanda. Amani na utulivu tunavyojivunia sasa vitakuwa shakani. Na hili halipaswi kutokea.
 
Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kwamba sasa kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kinabaki kuwa salama na kamwe hakiwi sababu ya kuiweka nchi njiapanda.
 
Sisi tunatambua kuwa hivi sasa, tayari wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vyenye usajili wa kudumu wameshajiweka hadharani na wengine wameshapitishwa na vyama vyao ili kuwania nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi.
 
Kadhalika, inafahamika vilevile kuwa siku rasmi ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu bado haijawadia. Kwa mujibu wa ratiba ya Nec, ifikapo Agosti 22 ndipo kila chama kitapata ruhusa rasmi ya kuanza kunadi wagombea wake kwa kila nafasi. Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa ratiba hiyo, ni ukweli ulio wazi kuwa karibu kila chama kimeanza harakati za awali kwa nia ya kujiweka sawa.
 
Nipashe tunatambua kuwa katika kipindi hiki cha kuwapo kwa harakati za kujiweka sawa, kuna baadhi ya wanasiasa wameanza kucheza 'faulo'.  Wanakiuka kanuni za msingi za kuheshimiana na kujali utu wa kila mmoja, bila kujali itikadi zao. Mathalan, wapo wanaoacha wajibu wao wa kuvijenga vyama vyao ili vitambulike zaidi kwa umma na mwishowe kujirahisishia kazi wakati wa kampeni na badala yake kugeukia vijembe, matusi na kashfa dhidi ya wapinzani wao. Hili halipaswi kuachwa. Kuna kila sababu ya kulikemea kwa nguvu zote ili hatimaye mchakato huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ukamilishwe kwa amani na utulivu.
 
Kwa mfano, sisi tunaona kwamba haipendezi hata kidogo kuona mgombea mtarajiwa wa chama kimoja akitoa maneno ya kashfa na hata kuwatusi washindani wake kutoka ndani na nje ya chama chake. Bali, tunaamini kwamba ni vizuri zaidi kwa kila anayetarajia kugombea baada ya majina kuidhinishwa na Nec Agosti 21 ajitahidi kueleza mazuri yake na ya chama chake ili kujijengea mazingira ya kufahamika na umma kabla ya kuanza kwa kampeni. 
 
Tunasisitiza jambo hili kutokana na ukweli kuwa hivi sasa, taifa linakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji majibu ya msingi kutoka kwa wote wenye ndoto za kushika madaraka, kwa maana ya kuanzia urais hadi udiwani. Hivyo, badala ya wagombea watarajiwa kutoleana matusi na kashfa kwenye majukwaa ya kisiasa, ni vyema kwa kila mmoja kufikiria mara mbili juu ya namna ya kushughulikia kuwapo kwa uhaba wa maji, changamoto za elimu, miundombinu ya barabara na afya. Wajikite pia katika kuzungumzia tatizo la ukosefu wa ajira na pia ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima. Kwa kufanya hivyo, ni wazi kwamba kashfa na matusi miongoni mwao havitapata nafasi. Na ndivyo inavyopaswa kuwa. 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom