Hatua ya serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi kwa kuzuia
wizara, taasisi na mashirika ya umma kukutana katika hoteli kwa shughuli
mbalimbali za kikazi, imeanza kuleta athari chungu huku baadhi ya
wamiliki wa hoteli wakisema wameathirika kimapato na sasa wako mbioni
kupunguza wafanyakazi.
Kadhalika, baadhi ya wasomi wamesema licha ya dhamira nzuri ya
serikali katika kuhakikisha inabana matumizi ili fedha zitakazopatikana
zielekezwe katika miradi ya maendeleo, bado kuna haja ya kuangalia kwa
umakini athari zake. Pia wameonya kuwa sekta ya hoteli ikiyumba
itaathiri wajasiriamali wengi na sekta binafsi kwa ujumla.
Baada ya kuapishwa na kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana,
Rais Dk. John Magufuli ilitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi
yasiyo ya lazima ili kuipa nguvu ya kuwatumikia wananchi.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni ni kupiga marufuku vikao vya
kazi vya taasisi na mashirika ya umma kufanyika hotelini, kufanyika kwa
hafla za kupongezana, kuadhimisha wiki mbalimbali zikiwamo za maji na
Siku ya Ukimwi, warsha, semina, makongamano, mikutano na mafunzo.
Zingine ambazo sasa zinaelezwa kuathiri baadhi ya wajasiriamali na
sekta binafsi ni pamoja na kufutwa kwa sherehe mbalimbali ikiwamo ya
Uhuru, maadhimisho ya kitaifa na kimataifa yaliyokuwa yakiwalazimu
wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi kutua Tanzania au kusafiri kutoka
mkoa mmoja kwenda mwingine.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa tangu kutolewa
kwa agizo la serikali kuzuia hafla, vikao na shughuli za serikali kwenye
kumbi za hoteli, karibu hoteli zote hazijapata mikutano wala shughuli
yoyote kutoka kweye taasisi za umma, mashirika wala wizara.
CHAMA CHA WENYE HOTELI
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT),
Latifa Sykes, alisema sekta ya hoteli ni moja ya maeneo yanayoajiri
watu wengi kwa sababu ya kuangalia wageni na kushughulikia matukio
mbalimbali, ikiwamo mikutano.
“Kitu kitakachotokea na ambacho kwa sasa kinatokea ni kwamba hoteli
za mjini ambazo zilikuwa zikipokea mikutano mingi, sasa zitapunguza
wafanyakazi,” alisema.
Alisema mbali na kupunguzwa kwa watu na pato la hoteli hizo
kupungua, kutaathiri pia serikali kwa sababu ilikuwa ikipata kodi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya ongezeko la thamani (VAT).
“Lazima tuwe makini na tujue kila hatua ina matokeo yake. Kwenye
hii ya kupunguza mikutano, matokeo yake ni kupungua kwa mapato
yaliyokuwa yalipwe serikalini na hakuna tena sababu ya kuwa na
wafanyakazi wengi.
“Tunamuunga mkono Rais kwenye kubana matumizi mabaya ya serikali
lakini ni vyema akaangalia hatua za utekelezaji zisiathiri uchumi na
biashara zinazosaidia ukusanyaji wa kodi,” alisema.
HALI HALISI
Ofisa Mauzo wa hoteli ya Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro
Kempinsk), Godlove Mlaki, aliiambia Nipashe kuwa agizo la Rais Magufuli
halijawaathiri sana kwa sababu hawategemei mikutano pekee ya serikali na
taasisi zake kwa kuwa hoteli yao ni ya hadhi ya kimataifa.
Alisema athari ya moja kwa moja waliyopata kutokana na uamuzi wa
serikali ni kukosa wateja ambao kwa kawaida huwapata wakati wa
maadhimisho ya siku ya Uhuru, Desemba 9 ya kila mwaka.
Wakati wa sherehe za kitaifa, ikiwamo Uhuru, wageni mbalimbali
ambao hualikwa kutoka nje ya nchi wakiwamo na marais na wafanyabishara,
hufika kwa wingi nchini na kusaidia kuingiza fedha za kigeni kutokana
na kulala kwenye hoteli na huduma zingine wanazohitaji katika siku zote
wanazokuwapo nchini.
Mlaki alisema kutofanyika kwa sherehe za Uhuru kuliwakosesha fedha
nyingi kwa sababu awali hoteli yao ilikuwa ikipokea wageni kutoka nje
waliokuwa wakialikwa kuhudhuria sherehe hizo.
Alisema hoteli hiyo yenye kumbi 10 za mikutano, wateja wake wakubwa
walikuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na wastani
wa mikutano waliyokuwa wakifanya kwa mwezi ilikuwa ikifikia 19.
Alisema kuna wakati walikuwa wakipata mikutano ya siku mbili hadi sita mfululizo kutoka serikalini.
“Toka mwaka jana Desemba hadi Januari hatujapata (kuandaa) mikutano yoyote kutoka serikalini,” alisema Mlaki.
Mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, alisema mbali na wateja
wananaotaka kumbi za mikutano, hata baadhi ya maaofisa wa serikali
waliokuwa wakifika hapo ili kupata kifungua kinywa na chakula cha
mchana, siku hizi hawapo tena.
Akifafanua juu ya ugeni wa marais waliokuwa wakifika kuhudhuria
shehere za kitaifa, alisema: “Wakija marais wawili tu kwa mfano, ukiweka
na walinzi wao, utakuta umeshafanya biashara ya zaidi ya vyumba 30,
hapo hujaweka chakula na vinywaji. Kwa hiyo ile ni biashara kubwa sana
kwetu,” alisema.
Katika hoteli ya Bahari Beach, Meneja anayehusika na kukodisha
kumbi, Robert Vitus, alisema wameathirika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa
tangu kutolewa agizo la kuzuiwa kwa vikao na mikutano hotelini,
hawajawahi kupata wateja kutoka serikalini.
Alisema hivi sasa wateja wanaowapata zaidi ni wale wanaotoka katika taasisi na kampuni binafsi pekee.
"Kwa ujumla, siku zote wateja wetu wakuu ni wale wanaotoka katika
taasisi binafsi na wengine kutoka nje ya nchi. Watu wa serikalini kwa
kiasi fulani walikuwa wateja wetu, japo si kama ilivyo kwa hawa wengine.
Hivi sasa, hata hao asilimia ndogo ya wateja kutoka serikalini
hatuwapati tena," aliongeza.
Meneja Masoko wa Hoteli ya Blue Pearl iliyoko Ubungo, Abdul
Sheikh, alisema kutokana na serikali kuacha kufanya mikutano kwenye
hoteli yao, baadhi ya wafanyakazi wamekosa kazi za kufanya.
“Yaani hakuna kabisa biashara siku hizi kulinganisha na ilivyokuwa
awali ambapo kumbi zote zilikuwa zinajaa. Sasa hivi ni kama
ulivyotukuta, hakuna kazi, kuanzia asubuhi hadi jioni, ni hivi hivi tu
tunakaa” alisema Sheikh.
WASOMI WANENA
Mtafiti wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Profesa Haji Semboja, alisema ingawa hoteli kadhaa zitakuwa zimeingia
katika msukosuko wa kiuchumi, bado kuna haja kwa serikali kuangalia
ushirikiano mkubwa wa maendeleo baina ya sekta binafsi na ya umma katika
kukuza pato la nchi.
Alisema kadri anavyoona, agizo la Rais Magufuli, moja kwa moja
halikulenga kusitisha mikutano mikubwa yenye idadi ya watu zaidi ya 200
hadi 500, bali ile midogo ambayo haikuwa na ulazima wa kufanyika katika
kumbi za hoteli kwa lengo la kuokoa rasilimali fedha ambayo inaweza
kufanya jambo mbadala.
“Kuyumba
kiuchumi kwa hoteli hizo huenda kumechangiwa na uelewa mdogo wa tabia
za Waswahili, ambao wanajumuisha kila kitu na kusababisha hofu
iliyochangia kuyumba kiuchumi kwa sekta binafsi ambayo ni miongoni mwa
mihimili muhimu ya serikali hasa katika uchangiaji wa uchumi wa ndani,”
alisema.
Mkurugenzi wa Sera wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein
Kamote, alisema katika nchi yoyote serikali ni muhimili wa kwanza wa
ununuzi wa bidhaa na huduma, hivyo inavyobana sana matumizi yake
itasababisha kuathirika kwa sekta mbalimbali na kusababisha uchumi mkuu
kushindwa kukua.
“Kubana bajeti ni jambo la kawaida, ila ibane na kuachia ili kutoa
ushirikiano mzuri kwa sababu inaweza kusababisha madhara kwa sekta
iliyodhamiria kuibana. Tunajua inaweza kubana na fedha zile zikatumika
katika sekta nyingine kama elimu au afya,” alisema Kamote.
Alisema ni vigumu hoteli nyingi kumudu kujiendesha bila kupata
mteja muhimu ambaye ni serikali, hasa kwa sababu serikali imeanza kwenye
eneo linalogusa sekta ya utalii ambayo ni kitovu kikubwa cha uchumi.
Alisema huenda ajira nyingi kwa wafanyakazi wa hoteli zikapungua
huku wengi wasijue la kufanya na kujikuta wakiangukia katika kundi la
wazururaji au shughuli haramu kama za utapeli.
IKULU YAFUNGUKA
Kaimu Mkurugenzi, Kurugenzi ya Mawasiliano Ofisi ya Rais Ikulu,
Gerson Msigwa, alisema kuyumba kiuchumi kwa hoteli nchini kutokana na
agizo la Rais Magufuli si kazi ya serikali na wala agizo hilo haliwezi
kubadilishwa.
Alisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo kwa dhumuni la kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima kwa serikali na kuwataka Watanzania wote
wapenda maendeleo wamuunge mkono katika suala hilo.
“Wizara zilikuwa zinatumia pesa nyingi sana kukodi kumbi kwa saa
kadhaa wakati kuna kumbi katika wizara zao. Sasa kuyumba kiuchumi au
kukosa wateja katika hoteli hiyo si kazi ya Ikulu,” alisema Msigwa.
Alisema hoteli zinapaswa kuwa wabunifu wa kupata fedha zaidi na si
kutegemea wizara au taasisi kwenda kufanya mikutano katika hoteli zao.
Imeandaliwa na Gwamaka Alipipi, Fredy Azzah, Elizabeth Zaya na Efracia Massawe.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni