Jumanne, Februari 03, 2015

SEHEMU YA KWANZA SIMULIZI "NIMEPATA NJIA"



Ulikuwa ni usiku wa manane majira ya saa nane na nusu, ambapo Mzee Jengo alikuwa amepumzika kitandani akiwa na mtoto wake wa kiume ambaye alikuwa anaitwa Rony.Alikuwa ni kijana mdogo mwenye umri  kati ya miaka nane au tisa, Usiku huo hali ya Mzee Jengo ilikuwa si nzuri kwani alianza kujisikia vibaya ghafla kiasi kwamba hata alipojaribu kunyanyuka alishindwa. Kutokana na maumivu makali aliyokuwa akiyasikia aliamua kumuamsha mtoto wake, taratibu alinyoosha mkono na kuanza kumvuta Ronyhuku akizungumza kwa sauti ya unyonge sana.


 “Rony, Rony …..aaaaa…amka ukamwambie ….dada mimi naumwa, Rony mwanangu nenda kamwite dada yako najisikia vibaya sana” Alikuwa akizungumza kwa shida sana, lakini Rony alimsikia, na kwa haraka aliamka huku akiwa anafikicha macho yake kutokana na kushtuka kutoka usingizini, alimtizama baba yake, na moja kwa moja alishuka kutoka kitandani huku akiwa anamuuliza Baba yake, “Baba unaumwa nini,  nani atakupeleka hospitali Baba,”.


 Rony alikuwa akiongea huku akimtizama Baba yake ambaye alikuwa akimuonyesha ishara aende kumuita dada yake, kwani hali yake ilizidi kuwa mbaya. Rony alikuwa bado ni mtoto mdogo lakini kutokana na hali ya Baba yake ilivyokuwa alishtuka sana na sasa alienda moja kwa moja katika chumba cha dada yake na aligonga mlango kwa nguvu huku akisema “Dada Ritha, Dadaaaa, Dada fungua mlango, Baba anaumwa, njoo Baba anakuita, fungua mlango Dada”


 Rita alikuwa amelala usingizi mzito sana kiasi kwamba ilimchukua muda mrefu Rony kumuita, na sasa chumba cha pili ambapo kulikuwa na kijana wa kazi alimsikia Rony akiita alitoka ndani haraka  “Wewe, mbona unapiga kelele, kunanini, nenda kalale tizama huu ni usiku wa manane” Rony alimtizama huku akionekana kuwa na wasiwasi akasema “Baba amenituma nimuite Dada Ritha  ampeleke hospitali, Baba anaumwa sana”.

 Yule kijana alinyamaza kimya kidogo, na wakati huo Ritha naye alifungua mlango na kumsikiliza Rony, “Jamani Rony, nenda kalale, utakuwa unaota wewe mtoto, usiku huu unasema Baba anaumwa mbona alikuwa mzima na usiku ule wa saa mbili tulikuwa tumekaa naye anazungumza hana tatizo lolote, embu nenda kalale utakuwa unaota”.

 Aliongea Ritha huku akiwa amemshika mdogo wake na kumrudisha chumbani kwa Baba yake aende kulala, alipofika pale chumbani, Rony aliingia huku akisema “Baba, dada Ritha huyu hapa, Baba, Babaaaa, Dada Ritha, Baba anatoka damu mdomoni” Ilikuwa ni sauti kali ya Rony baada yakumuona Baba yake akiwa amelala huku amengata ulimi, na macho akiwa hajayafumba, masikini Mzee Jengo kumbe alikuwa amekwishfariki.

Watoto walilia sana wasijue nini chakufanya, na Yule kijana wa kazi haraka alikimbia kuwaita majirani ili waje kutoa msaaada na kwa wakati huo aliwapigia simu baadhi ya ndugu wa karibu wa marehemu na kuwapa taarifa. Ndugu na majirani walifika haraka nakuanza kusaidiana kumuweka vizuri mzee Jengo, watoto walikuwa wakilia sana kwa sauti kali, zilizojaa simanzi.

 Ritha alikuwa amelala chini huku akigaragara na kusema "Baba, jamani Baba kweli umeondoka na kutuacha, hapana baba, haiwezekani kwaniniunatuacha peke yetu tafadhali baba nakuomba uamke, hatuwezi kuishi bila wewe, tizama sasa nani atakaa na sisi, jamani wewe ndiyo ulikuwa baba na pia ndiyo mama kwetu , uwiiiii Mungu wangu kwanini yote haya yametokea".

 Alikuwa akilia sana na machozi yalimtiririka mithili ya mtu aliyemwagiwa maji kichwani. na moja kati ya majirani aliyekuwa anaitwa Mzee Sindimba alisogea na kumfariji "Pole sana mwanangu naomba ujikaze tizama unavyolia sana wadogo zako wanajisikia vibaya zaidi, vumilia mwanangu kazi ya Mungu haina makosa, vumilia mwanangu.
Aliongea Mzee Sindimba huku akimnyanyua Ritha kutoka pale kibarazani alipokuwa akilia na kugaragara. Baadaye majira ya saa kumi na moja kasorobo alfajiri mwili wa marehemu Mzee Jengo ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali, vilio na simanzi ziliendelea huku Rony akiwa anamtizama dada yake alikuwa akilia nakusema "Dada kwanini baba amekuwa hivyo, inamaana hawezi tena kuongea, dada Baba aliniambia atanipeleka shule, inamaana hanipeleki tena, kwanini Baba yangu anatoka damu, halafu wanambeba  na kumuweka kwenye gari, dada mimi namtaka Baba yangu".

 Aliongea Rony kwa uchungu sana dada yake alishindwa kumjibu chochote alimkumbatia na kuendelea kulia kwa uchungu. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU YA PILI SIMULIZI HII ITAKUJIA KILA SIKU YA JUMANNE NA SIKU YA IJUMAA HAPAHAPA KWENYE BLOG YETU.

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom