Alhamisi, Machi 08, 2012

SIMULIZI YA DADA YANGU SURA YA ...2......

Kesho yake asubuhi na mapema Mama yake Upendo alimwamsha na kumshauri Upendo ajiandae kwani safari ingeanza saa nne asubuhi. Eliza siku hiyo hakwenda shule ili amsindikize dada yake.  Walikunywa chai kwa pamoja na tayari baba yao alikuwa amejiandaa kwa safari. Waliondoka na usafiri wao binafsi hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumwacha Upendo. Upendo alimwaga mama yake na mdogo wake akiwa na huzuni kutokana na kuanza maisha mapya. Upendo alipangiwa kuishi katika hosteli za mabibo ambazo zipo kandokando ya barabara ya Mandela upande wa kulia kutokea Ubungo kuelekea Buguruni.

Akiwa chuoni Upendo alikutana na watu mbalimbali. Alijitahidi sana kusoma kwa bidii akiwa na uwezo mzuri darasani aliweza kufaulu vizuri mitihani yake.

Eliza naye alimaliza Kidato cha Sita na kupangiwa kwenda kusoma Chuo cha Njiro Mkoa wa Arusha wakati huo Upendo alikuwa amebakiza mwaka mmoja ili amalize Chuo. Upendo aliishi vizuri na alipendwa sana na wanafunzi kutokana na juhudi zake katika masomo na tabia yake nzuri aliyokuwa nayo, hivyo alikuwa na marafiki wengi na pia walimu walimpenda sana.

Wakati akikaribia kumaliza chuo Upendo alipata rafiki wa kiume aliyeitwa James ambaye  alikuwa ni mfanyabiashara. James naye alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma lakini aliamua kufanya kazi zake binafsi kutokana na ajira kuwa ngumu. Kadiri siku zilivyozidi kwenda urafiki wa James na Upendo ulikua na kuimarika sana kiasi kwamba watu waliokuwa wakiwaona pamoja walijua ni mke na mume.

Siku moja James akiwa amekaa nyumbani kwake maeneo ya Kinondoni aligubikwa na wazo zito kuhusu Upendo.
“Mimi na Upendo ni marafiki wakubwa sana na huyu binti ni msichana ambaye anajiheshimu sana tokea nilipomfahamu, nimempenda sana kutoka moyoni mwangu natamani awe mama wa watoto wangu. Kwa vile sijawakuhi kumtamkia lolote juu ya suala la mapenzi kwa kipindi chote cha kufahamiana kwetu, nahisi nikimdokeza tu pengine anaweza akachukia.” Aliwaza James huku akitamani kumwambia Upendo kuhusu alilonalo moyoni mwake.

Zilipita siku kadhaa kila James akionana na Upendo akawa anataka kumwambia lakini alikuwa anasita. Siku moja alipanga kumtoa Upendo ili kwenda naye  sehemu tulivu apate fursa nzuri na adimu ya kumwambia Upendo juu ya mapenzi aliyonayo moyoni mwake.

Ilikuwa siku ya Ijumaa James aliyopanga kumtoa Upendo jioni yake kwenda katika matembezi. Alipomweleza Upendo juu ya azima yake ya kutoka naye alikubali bila pingamizi. Ilipofika jioni ya saa kumi na mbili hivi James alikwenda  Hosteli ya Mabibo na gari yake aina ya Benzi kumchukua Upendo. Alipofika Hosteli block A chumba namba 228 alimkuta Upendo akiwa tayari amejitayarisha kwa ajili ya matembezi ya jioni. Upendo alivalia vazi la kutokea jioni ambalo lilimkaa barabara likionyesha vizuri jinsi Mungu alivyompendelea kimaumbile. Alipendeza sana kiasi kwamba James alijiona ni mwanamume mwenye bahati kama angefanikiwa kumpata kimapenzi.


James aliendesha gari kuelekea Sinza eneo liitwalo Madukani katika Mgahawa uitwao “Fast Food and Take Away” ambao ulikuwa na utulivu na hali ya hewa nzuri. Walichagua sehemu nzuri na kwenda kukaa pamoja. James alimpa Upendo uhuru wa kuagiza chochote alichopenda kula na kunywa. Waliletewa vinywaji na kuanza kunywa huku wakisubiri chakula. Muda wote mapigo ya moyo wa James yalikwenda mbio akiwaza namna ya kuanza kumwambia Upendo suala la mapenzi. Baada ya kama dakika ishirini hivi za maongezi ya kawaida James aliamua kumwaga sera zake.
“Upendo umependeza sana leo hilo gauni ulilovaa limekupendeza sana.” James alianza kwa kumsifia Upendo.
“Asante James mbona hata wewe umependeza.” Wote wakacheka na kugonganisha mikono.  

James alivuta kiti chake na kusogea karibu na Upendo huku moyo wake ukiwa bado unamdunda macho yakiwa na rangi nyekundu kwa hofu ya kumwambia Upendo kuwa anampenda.  James alijikaza na kumshika Upendo mkono.
“Upendo kuna kitu kinanisumbua sana moyoni mwangu, kitu hicho kimekuwa kinanitesa kwa muda mrefu sana tangu tufahamiane.” Aliongea James huku midomo ikimtetemeka kidogo.
“James! Ni kitu gani hicho jamani?” Aliuliza Upendo kwa sauti ya mahaba na macho yake ya kurembua.
“Ni kitu cha kawaida sana lakini…”
“Lakini nini?” Alimkatisha Upendo akiwa ananyanyua glasi ya soda na kuinywa huku akimwangalia James usoni.
“Nitakwambia kitu hicho jioni hii ya leo ingawa kitu hicho kinaweza kuharibu au kuboresha urafiki wetu.” Aliongea James kwa kujihami ili apate ujasiri wa kusema.

“We sema tu James, ni jambo gani hilo ambalo unasita kuniambia wakati kuna mambo mengi sana tumekwishaongea mimi na wewe tangia tufahamiane.” Upendo aliongea kana kwamba anampa uhuru wa kusema linalomsumbua James.
“Upendo! Aliita James kwa sauti ya chini sana huku akijitahidi kuyakwepa macho ya Upendo.
Abee!” Aliitikia Upendo.

“Ahhm! Tangu tufahamiane nimetokea kukupenda zaidi ya urafiki tulionao.” James alitulia kidogo huku safari hii akimwangalia Upendo usoni. Kabla Upendo hajasema kitu James aliendelea kumwaga sera zake huku Upendo akiwa kimya.
“Ningependa uwe mpenzi wangu na baadaye Mungu akitujalia uwe mama wa watoto wangu.” Aliongea James akimkazia macho Upendo. 
Upendo aliyekuwa ametulia akimsikiliza aliutoa mkono wake mikononi mwa James ambaye alikuwa amemshika, huku akiinama na kuminyaminya vidole vyake kwa aibu.
“Mh! We James! Ina maana hadi sasa hauna mwanamke kijana mzuri kama wewe acha hizo bwana mbona si kitu cha kawaida.” Alihoji Upendo.

Ni kweli Upendo lazima utafikiria hivyo, ila nakwambia ukweli kutoka moyoni mwangu, sina mwanamke yeyote. Ila niliwahi kuwa na mpenzi zamani kidogo tukakorofishana na kwa sasa ameolewa. Nilikuwa nampenda sana ila aliniumiza moyo wangu nikajikuta sitamani kuwa na mwanamke tena maishani mwangu. Lakini tulipoanza urafiki mimi na wewe nimegundua kuwa nahitaji kuyaanza maisha yangu upya. Nimekupenda sana Upendo nipe nafasi katika moyo wako.” Alibembeleza James.
“Je, kwa sasa huyo aliyekuwa mpenzi wako anaishi wapi?” Aliuliza Upendo.
Alikuwa anaishi hapahapa Dar lakini baada ya kuolewa alihamia Mbeya na mume wake.
“Mmmh!! Hapana James kwa sasa, naona tuendelee kuwa marafiki, ila nitakujibu kuhusu ombi lako siku yoyote.” Alimjibu Upendo huku akitafakari kitu. Je nini kitaendelea usikose sura ya ...3....

Maoni 1 :

Elizabeth Wanjiru alisema ...

love it cant wait for part 3

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom