SIMULIZI HII IPO KATIKA KITABU CHA MALIPO NI HAPAHAPA
Ilipoishia “Juliusi we ni mwanamume mzuri sana nafurahi kuwa pamoja na wewe haijawahi kunitokea nikamwamini mwanaume kwa haraka kama ilivyo kwako nimekupenda naomba usiniache.” Esta aliizungumza maneno huku akiwa anamshika katika paji la uso naye James taratibu alinyanyuka na kuanza kumbusu Esta bila hata ya kuzungumza lolote huku akimkumbatia na baadaye walilala usingizi wa pono.
Inavyoendelea.........Ilipofika asubuhi Esta aliamka na kwenda kuoga wakati James alikuwa bado amelala usingizi mzito. Baada ya Esta kutoka bafuni alikaa katikasofa lililokuwa pale chumbani huku akiwa anamsubiri James aamke.
“Mmh sijawahi kupenda kiasi hiki huyu mwanamume sijamfahamu vizuri
ni siku moja tu lakini nimempenda sana naamini atakuwa ni mwanamume
wa maisha yangu.” Aliwaza Esta huku akimwangalia James.
Wakati akiwa anaendelea kuwaza mara ghafla James aliamka kutoka
usingizini na kukaa pale kitandani huku akionekana kuchoka sana.
“Habari za asubuhi Juliasi mpenzi wangu umelala sana”. Esta alimsalimia
James.
“Jana nilikuwa nimekunywa pombe nyingi sana vipi unaweza ukaondoka
tu muda huu usijali mimi nipo sawa tu.” Alijibu James.
“Sawa mpenzi mimi nitaondoka kwani hata hivyo nilikuwa na kazi ya
muhimu naifuatilia ila naamini usiku tutakuwa pamoja nataka tuzungumze
zaidi.” Esta alisema huku akiwa ananyanyuka na kumsogelea James kisha
kumbusu na kuchukua mkoba wake kuondoka kwa furaha sana. James
alichukua waleti yake na kutoa kiasi cha shilingi laki moja na kumkabidhi
Esta.
“Nimefanya nini mimi nimemsaliti mpenzi wangu Upendo itabidi niwe
makini sana hiki kitu asikifahamu vinginevyo itakuwa balaa.” Aliwaza
James baada tu ya Esta kuondoka.
Basi James alinyanyuka na kwenda kuoga na baadaye aliendelea na kazi
zake kama kawaida. Ilipofika jioni Esta alimpigia simu James na kutaka
kuonana naye. James alimtaka Esta aende hotelini usiku ili waendelee na
huo mchezo huku James akiwa anafanya kwa siri Upendo asijue.
Ilipita kama miezi miwili hivi James akiwa bado yupo Arusha akiwa
anaendelea na shughuli zake na bado akiwa na uhusiano wa kimapenzi
kwa siri na Esta.
Huko Dar es Salaam Upendo alikuwa mpweke sana kwani alikuwa
amemaliza mitihani ila hakwenda Morogoro alibaki Dar es Salaam na
alikuwa akiishi katika nyumba ya James Kinondoni. Wakati wote walikuwa
wakiwasiliana na mpenzi wake vizuri. James alitakiwa kukaa Arusha kwa
muda wa miezi minne ndio shughuli zake zitakuwa zimekamilika, kwa
hiyo alikuwa akimtaka Upendo avumilie na waendelee na mikakati ya
kufunga ndoa ili punde akirudi tu wafunge ndoa.
Upendo aliendelea na mikakati ya harusi huku akishirikiana na wazazi
wake pamoja ili kuandaa sherehe ya kumuaga Upendo. Akiwa katika
mikakati ya harusi alimpigia simu mdogo wake ili kumjulisha mambo
yanavyoendelea.
Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa lakini baadaye ilipokelewa.
“He! We Eliza mbona umechelewa kupokea simu?” Aliuliza Upendo.
“Mh dada samahani nilikuwa bafuni, ehe niambie.” Alijibu Eliza.
“Ndugu yangu natamani ungekuja huku unisaidie katika mipango ya
harusi yangu vipi mnafunga lini chuo?” Aliuliza Upendo.
“Makubwa! Kweli mapenzi yamepamba moto ndio unaolewa na huyo
shemeji hata simjui jamani?” Alihamaki Eliza.
“Wewe nawe! Utakuja kumwona siku ikifika. Kwanza yupo huko Arusha
lakini ametingwa sana sijui kama mtaweza kuonana.” Alisema Upendo.
“Hee! Jamani kweli shemeji yangu yupo huku halafu huniambii? Vibaya
hivyo dada yangu, sasa kuhusiana na mimi kuja huko kukusaidia hiyo
mipango yako ya harusi kwa sasa itakuwa vigumu kwani najiandaa na
mitihani itakayoanza mwezi ujao.” Alijibu Eliza.
“Jamani Eliza mwenzio natamani ungekuwepo ila hakuna tatizo kwani
masomo nayo ni muhimu. Mh mdogo wangu hebu niambie sijapata
shemeji mmasai huko?” Aliuliza Upendo huku akicheka.
“Mmh! mwenzangu nimepata mchumba nampenda sana, mambo yakiwa
sawa nitakufahamisha.” Alijibu Eliza.
Basi waliendelea kuzungumza na baadaye kila mmoja aliendelea na
mambo yake.
James kipindi chote akiwa Arusha alikuwa akimsaliti Upendo na kustarehe
na Esta. Baada ya siku kadhaa kupita hatimaye siku za James kurudi Dar
es Salaam zilikaribia. Esta alimfuata James hotelini ili kuzungumza naye
kuhusiana na hatma ya uhusiano wao watakapokuwa mbali.
“Juliasi karibu utaondoka kwenda Dar hivi kweli utanikumbuka? Na jinsi
warembo walivyo wengi huko Dar?” Aliuliza Esta huku akimpapasa uso
James.
“Hapana siwezi kukuacha mpenzi wangu tutawasiliana usijali. Arusha
nitakuja hata wewe utakuwa unakuja Dar es Salaam.” Alijibu James huku
akimbusu Esta katika shavu la upande wa kushoto.
“Sawa hakuna tatizo mimi naomba tuendelee kuwasiliana nakupenda sana
mpenzi wangu.” Alijibu Esta huku akiwa amemkumbatia na kumbusu
James. Nini kinaendelea usikose sura ya 7......................
Maoni 1 :
mhhhhhhh usaliti mbya jmn!yn upendo kajituliza mwenzie ndo vile tena.
Chapisha Maoni