KITABU MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI ADELA KAVISHE
Ilipoishia,,,,Alipofika katika ofisi za utawala aliwaeleza walimu hali halisi kuhusu
kuugua kwa mama yake. Walimu walimwita Jamal. Baada ya Jamal kumwona baba yake alishtuka kwani haikuwa kawaida yake
kwenda kumtembelea shuleni.
Inapoendelea,,,,“Shikamoo baba!” Aliamkia Jamal
“Marahaba mwanangu!” Aliitika Mzee Said.
“Baba karibu sana shuleni kwetu.” Alisema Jamal huku akimwangalia baba
yake kwa furaha ya kutembelewa.
“Asante mwanangu, je,
unaendeleaje na masomo?” Alijibu na kuuliza Mzee Said.
“Vizuri baba, tunajiandaa na mitihani ya kumaliza muhula, je, hawajambo
nyumbani?” Alijibu na kuuliza Jamal.
“Hawajambo kiasi ila mama yako anaumwa kidogo na angefurahi sana kama
ungekwenda kumwona halafu utarudi kuendelea na maandalizi yako ya mtihani.”
Alisema Mzee Said.
“Haiwezekani baba kumbuka hii ni mitihani ya kumaliza Kidato cha Tatu
hivyo ninahitaji kuwa na muda wa kutosha kujiandaa.” Alijibu Jamal
Ni kweli lakini kwa sababu mama yako mwenyewe ameomba kukuona huna budi
kwenda angalau ukamwone tu leo kisha kesho utarudi kuendelea na hayo
matayarisho ya mtihani. Haya nenda ukajiandae nishakuombea ruhusa kwa walimu.”
Alishauri baba yake.
Jamali aliondoka kuelekea bwenini kujiandaa huku akiwaza kuna nini mbona
baba yake anasisitiza sana. Alichukua
begi lake dogo na kuongozana na baba yake hadi nyumbani. Walipofika tu
walimkuta Aisha nje ambaye alimkimbilia Jamal na kumpokea begi kisha kumshika
mkono.
“Shikamoo kaka Jamal” Aliamkia Aisha akimwongoza ndani.
“Mama anaumwa hawezi kutoka kitandani analia tu!” Alisema Aisha huku
akionyesha wasiwasi mkubwa.
Jamal alimsikiliza mdogo wake lakini hakumjibu chochote aliingia
chumbani na kumkuta mamake akiwa amelala kitandani.
“Shikamoo mama!” Aliamkia Jamal.
“Marahaba mwanangu nimefurahi kukuona baba!” Alimwitikia mama yake kwa
sauti ya chini sana na ya upole.
“Unaumwa nini mama yangu?”
Aliuliza Jamal huku akimwangalia Mama
yake.
Mama yake alikuwa amebadilika sana rangi ya ngozi yake ilififia na
kuonekana mweusi na alikuwa amepungua sana. Jamal akalia kwa uchungu huku
akitaka kujua mama yake anaumwa nini.
“Usilie mwanangu wewe ni kijana
mkubwa kwa sasa mimi naumwa sana mwanangu kuna vitu nilikuwa nataka kukwambia,
naomba unisikilize kwa umakini.” Aliongea mama yake kwa sauti ya chini sana.
"Nakusikiliza mama ongea tu.” Jamal alisema huku amemshika mkono
mama yake.
Wakati huo wote pale chumbani walikuwa wawili tu, baba yake pamoja na
mdogo wake walikuwa wamekaa sebuleni na wageni. Ndipo mama yake alipoanza kumwambia
Jamal alichomwitia.
“Mwanangu nakuomba usome kwa bidii naamni utamsaidia sana mdogo wako
katika masomo yake na pia mali zote zilizopo hapa ni za kwangu kampuni zote
mbili na nyumba ambazo zipo kimara Mbezi ambazo zina wapangaji zote ni zangu pamoja
na nyumba hii tunayoishi. Mimi nilikutana na baba yako nikiwa tayari
nimeshajiendeleza sana kimaisha na
nilimsaidia hadi akapata kazi Wizara ya Kilimo na baadaye tukawa tunashirikiana
pamoja katika kazi zangu, nimekwambia hivi ili ujue hizi mali ni zako wewe na
mdogo wako naomba msome kwa bidii.” Kabla hajaendelea kuongea Jamal alimkatisha.
“Lakini mama kwa nini unaongea hivyo? Twende hospitali mama utapona tu
mama bado tunakuhitaji.” Huku akiwa analia Jamal alimtaka mama yake aende
hospitali.
“Mwanangu nakupenda sana wewe pamoja na mdogo wako naamini Mungu
atawasaidia mimi siwezi kupona naumwa kansa ya kizazi na imefika katika hatua
mbaya sana, naomba usilie ningependa kuona mkifurahi muda huu ambao tuko pamoja.”
Alisema mama Jamal huku akiwa anatabasamu na kumfuta machozi mtoto wake na
kumshika mkono. Mama yake alikuwa
anapata maumivu makali sana kwa wakati huo. Nini kinaendelea usikose sura ya ...4...Unaweza kuagiza kitabu cha MALIPO NI HAPAHAPA kusoma simulizi hii.
Maoni 1 :
jmn imenitoa chozi,i wish nipate icho kitabu sema ndo niko uku ughaibuni!ongera kwa kz nzuri
Chapisha Maoni