Jumatano, Mei 23, 2012

SIMULIZI YA MAMA MDOGO SURA YA ...6.....


 KITABU MALIPO NI HAPAHAPA kwa wanaohitaji kutumiwa au maelekezo  kukipata tuwasiliane kupitia kavisheadela@yahoo.com au +255652343430 upate kusoma simulizi ya MAMA MDOGO,,DADA YANGU NA ILIYOBEBA JINA YA KITABU MALIPO NI HAPAHAPA

 ILIPOISHIA,,,,“Mama yangu! Huyu hawezi kuwa mama yangu hata siku moja. Mama yangu hawezi kurithiwa na mtu yeyote yule, halafu baba, mbona huyu msichana hata hamlingani anaonekana ni msichana mdogo sana huoni anaweza kuwa hata mtoto wako?” Alihoji Jamal  huku akionekana kuwa na hasira sana.

 INAPOENDELEA ,,,“Sikiliza nikwambie Jamal, mimi ni baba yako huwezi ukanijibu maneno ya kashfa kiasi hicho. Sasa upende usipende huyu ni mama yako kwa sababu mimi ndiye niliyeamua sawa?” Alifoka Mzee Said huku akimwangalia Sophia.
“Mke wangu huyu ni kijana wangu anaitwa Jamal ametoka shule anaumwa sasa hebu ni mpeleke hospitali na kesho atarudi shuleni.” Alitamka Mzee Said huku akisimama.
“Hapana baba shule narudi muda huu sintolala hapa nina kazi nyingi za kujisomea shuleni.” Alijibu Jamal huku akisimama na kuondoka bila hata ya kuagana vizuri na baba yake.
 “Lakini Jamal si ndio umefika muda huu ungesubiri kidogo ili nikuandalie chakula.” Alihoji Sophia huku akimsogelea Jamal.
Jamal aligeuka na kumtazama Sophia kisha alitoka nje bila kusema chochote na kuondoka. Baba yake alimwita lakini Jamal alijifanya kama hasikii.


Alipofika shuleni alionekana mwingi wa mawazo, alikaa pembeni mwa mti uliokuwa karibu na darasa alilokuwa akisoma.
“Hivi kwa nini baba ameamua kuoa hata mwaka haujaisha tangu mama alipofariki? Isitoshe mwanamke aliyemwoa ni msichana mdogo tu? Na sidhani kama kweli yule msichana amempenda baba yetu kwa dhati, naona kampendea hela tu. Mimi siwezi kukubali hata kidogo, najua hizi ni mali za mama yangu mzazi, lakini kwa sasa zipo mikononi kwa baba sijui nifanyeje.” Aliwaza sana bila kujua nini cha kufanya.
Mwisho alifikiria kwamba hawezi kumzuia baba yake asioe kwani ameshaamua. Kwa hiyo aliendelea na masomo yake huku akiwa anawasiliana na mdogo wake kwa barua, lakini hakumwambia chochote kuhusu baba yake kuoa mke mwingine. Hatimaye Jamal alimaliza mitihani ya Kidato cha Nne na kurudi nyumbani kuanza maisha mapya.


Akiwa nyumbani baba yake alipanga kumfanyia sherehe ya kumaliza Kidato cha Nne pindi tu mdogo wake atakaporudi kutoka shule kwani shule aliyokuwa anasoma bado walikuwa hawajafunga. Maisha ya Jamal akiwa nyumbani yalikuwa ni ya upweke sana, alikosa raha kila alipomwona yule mama yake mdogo na hakuwa na muda naye hata kidogo.  Sophia alijitahidi kuwa karibu naye lakini Jamal hakutaka kabisa.

Siku moja Jamal alitoka katika matembezi na kuchelewa kurudi nyumbani, ilikuwa ni saa tatu za usiku. Alimkuta baba yake pamoja na mama yake mdogo wamekaa sebuleni.
 “Shikamoo baba!” Aliamkia Jamal
 “Umetokea wapi usiku huu, unarudi muda unaotaka siku hizi?” Aliuliza Mzee Said kwa hasira bila hata kujibu salamu.
“Nilikuwa na marafiki zangu samahani kwa kuchelewa.” Alijibu Jamal huku akimuomba baba yake radhi na kuondoka.USIKOSE SURA  YA ....7....

Maoni 3 :

lyna wa ukweee alisema ...

mhhhhhhh yn yazd kunoga duh!jmn jamal mana uyo baba hashaanza kubadilika taratibu.

emuthree alisema ...

Haya haya simulinzi njoo utamua kolea, twipo pamoja, .........

DAVID JERMOS alisema ...

ahhhhhhhhhhhh,adela upele umefika kwa mkunaji mbona unanikata kucha ingali upele badu upo!!!!

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom