KITABU MALIPO NI HAPAHAPA
MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
ILIPOISHIA....“Wewe
mpumbavu sana tena nisikusikie unasema ni mama yetu, mjinga mkubwa
mama yetu alishafariki na kamwe huyu hawezi kuchukua nafasi ya mama anataka
tu pesa za baba.” Alifoka Jamal huku akimwonyeshea kidole
Aisha.
“Sasa
tufanyeje kaka kwani Baba ndio ameshamwoa.” Alisema Aisha huku akimfunga
Jamal kishikizo cha shati.
“We subiri
utaona nitajua cha kufanya.” Aliongeza Jamal huku akisimamana kumuashiria
Aisha waende ndani. INAPOENDELEA...Jamal na Aisha waliingia na kukaa sebuleni kumsubiri baba yao arudi kutoka kazini. Baba yao alipofika aliwaambia wajiaandae kwa ajili ya sherehe aliyoahidi kumfanyia Jamal. Mikakati ya sherehe ikaanza mama yao mdogo alishughulika na kuhakikisha kwamba kila kitu kinachohusika katika sherehe kinakamilika. Mama mdogo alitengeneza keki nzuri yenye herufi ya J juu yake. Walikula na kunywa. Jamal alivishwa mataji mengi kutoka kwa baba yake, mdogo wake hadi mama mdogo. Kwa ujumla sherehe ilifana sana kwani kila mmoja alimfurahia na kumpongeza Jamal kwa kuhitimu Kidato cha Nne salama.
Baada ya sherehe Aisha alimfuata kaka yake ili kufanya naye maongezi ya
kutathmini jinsi sherehe yake ilivyofana.
“Kaka umeona jinsi ambavyo mama mdogo alivyoandaa sherehe yako? Mimi
naona tuwe naye karibu kama ni mtu mbaya tutafahamu baadaye.” Alisema Aisha huku akimwangalia Jamal.
“Wewe bado mdogo sana, huyu mama ni mjanja sana, lakini hakuna tatizo
tumuheshimu tu kama mke wa baba yetu mimi sina tatizo naye.” Alijibu Jamal huku
akicheka kwa kebehi.
Aisha alifurahi kusikia kaka yake kakubali kuwa karibu na mama yao
mdogo. Siku zilivyozidi kwenda maisha yalikuwa mazuri kwani waliishi vizuri
sana. Jamal na mama yake mdogo walianza
kupatana ingawa mwanzoni ulikuwa ni kama urafiki wa chui na mbuzi. Wakati
mwingine Mama yao mdogo alikuwa anawatoa kwenda kwenye matembezi Jamal na
Aisha. Baba yao alipobaini uhusiano mzuri wa Sophia na watoto wake alifurahi
sana.
Siku za likizo zilipokwisha Aisha alirudi shuleni, alikuwa akiingia Darasa
la Sita. Jamal alibaki nyumbani kwani alikuwa anasubiri matokeo ya Kidato cha Nne.
Baada ya mdogo wake kuondoka pale nyumbani, Jamal alibaki na mama yake mdogo.
Karibu wakati wote Jamal alikuwa na mama yake mdogo akisaidia kufanya kazi
mbalimbali alizopewa. Baba yake yeye muda mwingi alikuwa yupo kazini kwake na
kushughulikia miradi aliyoacha marehemu mke wake.
Kutokana na Jamal kuwa na maelewano mazuri na mama yake mdogo muda
mwingi walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu misha na walikuwa kama marafiki.
Siku moja mama yake mdogo baada ya kunywa chai aliosha vyombo na kukaa sebuleni
akiwa na mawazo mengi moyoni mwake.
“Hivi mimi kwanini niliolewa na huyu mzee? Nikijiangalia bado ni binti
mdogo. Halafu huyu mwanawe ndo rika langu kabisa na ni mzuri sana anapendeza! Sawa
nimemzidi lakini si miaka miwili au mitatu tu? Hivyo bado sisi ni rika moja
kabisa! Natamani sana kuwa na kijana wa umri wa Jamal.” Aliwaza mama mdogo na
kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. USIKOSE SURA YA ....9......
Maoni 2 :
makubwa haya!wacha tuje tuone itakuwaje huko mbele.
ngoja niendeleze kidogo, mamdogo atakuja kumtongoza jamal, na mziki utaanzia hapo dingi siku akibaini
Chapisha Maoni