Alhamisi, Novemba 29, 2012

HIVI NINI KIFANYIKE KUMALIZA MATUKIO YA UKATILI AMBAYO YAMEKUWA YAKITOKEA MARA KWA MARA HUKO SHINYANGA MWANAMKE AUAWA KINYAMA

Ikiwa bado tupo katika maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili kwa wanawake  huko Shinyanga mkazi wa  kijiji cha Ibingo kata ya Samuye  Bibi Salu Charles mwenye umri wa miaka 50 ameuawa nyumbani kwake kwa kupigwa risasi kichwani  na kisha mwili wake kukatwakatwa mapanga kwa imani za kishirikina 

Tukio hilo ambalo limetokea ambapo marehemu akiwa amelala na mumewe usiku huo nyumbani kwao, walifika watu wawili nyumbani hapo na kuwagongea wakiomba maji ya kunywa , Baada ya kuwafungulia na kuwapa maji hayo  hawakuyanywa na badala yake waliyamwaga, baada ya kumwaga maji hayo waliomba kusaidiwa pampu ili wajaze upepo kwenye magurudumu ya baiskeli waliyokuwa wakiitumia kama usafiri uliowafikisha nyumbani hapo , Lakini mume wa marehemu aliwajibu alikuwa hana pampu  hivyo alienda nao kuwambea kwa shemeji yake aliyeitwa Emmanuel Daudi.

Wakiwa  njiani kama hatua kumi na tano kutoka nyumbani hapo. Marehemu Salu alimsihi mumewe awaelekeze  wanapoweza kupata pampu hiyo na kumtaka arudi nyumbani 

Baada ya kusikia hivyo watu hao walifyatua risasi hewani na kusababisha Ntugwa ambaye ni mume wa marehemu kukimbia huku hao watu wakarudi nyumbani kwa yule mume wa marehemu , walipofika walimkuta marehemu Salu nje akimsubiri mume wake, wakamuhoji kwanini hakukimbia baada ya kusikia mlio wa risasi walizopiga hewani  lakini marehemu hakujibu chochote ndipo walipoamua kumpiga risaisi kichwani na kufa papo hapo kisha kuukatakata mwili wake  kwa mapanga na kutoroka kwa kutumia  baiskeli. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusisistiza kuwa  linaendelea na kufanya uchunguzi  ili kuwabaini waliohusika nayo .

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kitongoji cha Mwamagushi Bw. Onesmo Kisinza Matukio ya mauaji kwa kutumia silaha mbalimbali za moto na za kienyeji  yamekuwa yakitokea takribani mara moja kila baada ya miezi miwili katika kijiji hicho amesema mauaji hayo yamekuwa yakiwalenga wanawake wenye umri wa miaka 45 na 80 kwa imani za kishirikina  na kuzua  hofu kwa rika hilo.


Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom