Alhamisi, Novemba 29, 2012

SIMULIZI YA MAMA MDOGO ........SURA YA ...17.......


MTUNZI ADELA DALLY KAVISHE
Baada ya muda mfupi baba yake akiwa ameongozana na mama yake mdogo walifika pale hospitali na kuingia ndani katika chumba alichokuwepo Jamal. Baba yake alipomwona katika hali ile roho ya imani ilimjia. “Masikini kijana wangu ndiyo amekuwa hivi siwezi kuamini dokta naomba umsaidie apone.” Baba Jamal alimwambia daktari. Wakati huo mama yake mdogo machozi yalikuwa yakimtoka kwa uchungu. “Daktari fanya lolote na kwa gharama yoyote Jamal apone.” Alisisitiza  mama mdogo.

INAPOENDELEA “Hakuna shaka kijana atapona wala msijali tatizo lake ni dogo sana. Vipimo vinaonyesha Jamal ana matatizo mawili. Moja anatatizo la kisaikolojia na la pili ni utumiaji wa dawa za kulevya. Matatizo haya yote yanatibika bila wasiwasi. Ila naomba ushirikiano.”Alieleza daktari. “Sawa daktari!” Waliitikia kwa pamoja Baba Jamal na mama mdogo. “Naona mnaitikia tu, je mmeelewa maana ya ushirikiano?” Aliuliza daktari. Baba Jamal na mama mdogo walitazamana kwa sekundi kadhaa, kisha baba Jamal alijibu kuwa inaeleweka na kumwomba daktari aendelee kumtibu Jamal wamejiandaa barabara.

Jamal aliendelea kutibiwa na alipozinduka na kujikuta yupo hospitalini alitaka kutoroka lakini madaktari walimshika kwa nguvu na kumfunga kamba. Jamal alilia sana pale kitandani na kuomba wamfungue. Baba yake alifika na kumsogelea huku akimshika usoni. “Mwanangu una matatizo gani? Nakuomba utulie upate matibabu.” Baba Jamal alimsihi Jamal. Jamal kumwona tu baba yake akasema kwa uchungu.

“Baba nisamehe! Baba naomba unisamehe! Nimekukosea sana baba!” Alilia Jamal na kupiga kelele. “Nimeshakusamehe mwanangu wewe tulia kwanza upone halafu twende nyumbani nakupenda sana mwanangu.” Alijibu baba Jamal. Daktari alifika na kumchoma Jamal sindano ya usingizi akalala. Siku ya pili Jamal alikuwa amepata nafuu kidogo ingawa bado alikuwa anashtuka na kuongea mambo yasiyoeleweka. Baba yake na mama mdogo walifika kumwona na kufurahi sana kusikia maendeleo mazuri ya afya ya Jamal. Baada ya wiki moja Jamal alikuwa ametulia. Siku moja baba yake alipokwenda hospitali Jamal alimwomba baba yake kuwa ana maongezi naye ya faragha kwani kulikuwa na mambo anataka kumwambia.


“Baba samahani ninashida na wewe.” Alisema Jamal. “Sawa mwanangu kwani huwezi kusubiri hadi upone na kuruhusiwa?” Aliuliza baba Jamal. “Hapana baba naomba unisikilize sasa hivi, kwani kuna jambo kubwa nimekukosea, nisamehe baba yangu nimekutendea kosa kubwa sana.” Jamal alianza kumwambia baba yake jambo linalomsumbua, lakini ghafla daktari alifika na kumwambia baba Jamal kuwa mgonjwa anaweza kuondoka kwani tayari hali yake ilikuwa ni nzuri.

“Sasa umepona mwanangu twende nyumbani tutaongea zaidi na mdogo wako anakuja likizo leo atafurahi sana kukuona.” Aliongea baba Jamal kwa furaha kubwa. Kwa hiyo Jamal alishindwa kumuelezea chochote baba yake kwa wakati ule walikusanya vitu na kuelekea katika gari la baba yake aina ya Range Rover na kuelekea moja kwa moja nyumbani. Akiwa njiani Jamal aliwaza ataanzaje kumwambia baba yake kuhusu mambo yote waliyokuwa wakiyafanya na mama yake mdogo hadi akazaa naye.

“Ni lazima nimueleze baba ukweli. Mungu nisaidie nimetenda dhambi kubwa sana katika maisha yangu.” Aliwaza Jamal. Walipofika nyumbani walimkuta mama mdogo ambaye aliwapokea kwa furaha na alikuwa ameandaa chakula kitamu siku hiyo kwa ajili ya Jamal. Walikaa na kula pamoja. Hata hivyo Jamal bado alikuwa hana raha kabisa. Alionekana mtu mwenye mawazo sana. Basi baada ya kula alikwenda chumbani kwake kupumzika huku akitafakari.

Ilipofika jioni muda wa saa moja hivi, Aisha alifika kutoka shuleni baada ya kufunga kwa ajili ya likizo ya mwezi wa kumi na mbili. Aisha alipomwona kaka yake alimrukia na kumbatia kwa nguvu. “Yaani kaka masomo ya chuo ni magumu sana? Mbona umepungua hivi?” Aliuliza Aisha huku amemshika Jamal mkono. “Kaka yako alikuwa anumwa Aisha, ila kwa sasa hali yake inaendelea vizuri hana tatizo.” Alitamka baba Jamal.

“Oh! Jamani kaka polee!” Aliongea Aisha kwa huruma huku akimshika Jamal  kichwa. Baada ya chakula cha usiku wote wakiwa wamekaa sebuleni Jamal aliwaomba wanyamaze kwani alikuwa na kitu cha kuwaambia na wote wakatii. Ilikuwa ni usiku uliotulia, usiku wa kihistoria, usiku ambao hakuna aliyejua kama Jamal angekuwa na akili timamu tena. Baada ya ombi la Jamal la kunyamaza kila mtu alikuwa kimya, baba, mama mdogo, Aisha wala Rama. Wote walikuwa kimya. Baba Jamal akifikiri pengine Jamal anataka kuanza matatizo yake tena. Aisha alibaki akimwangalia sana Jamal na kutabasamu muda wote.

“Baba nashukuru sana kwa kunipeleka hospitali na sasa nimepona.” Alivunja ukimya Jamal kwa kuanza kuongea. “Usijali mwanangu huo ni wajibu wangu alimradi upo salama tunamshukuru Mungu sasa utaendelea na masomo yako vizuri.” Alijibu baba Jamal. “Lakini baba kuna kitu nataka nikwambie.” Alitamka Jamal huku akimwangalia baba yake. “Sawa sema tu ni kitu gani hicho?” Aliuliza baba Jamal. “Ni kile kitu nilichotaka kukwambia kule hospitali halafu daktari akanikatisha.” Alijibu Jamal. “Sawa nakumbuka, lakini hukusema.” Aliongeza baba Jamal. Kisha Jamal aliinamisha kichwa chini kwa muda kama vile kuna kitu anatafakari. 

Akasogea karibu na baba yake akapiga magoti mbele yake huku machozi yakimtoka. “Baba nimekukosea sana! Nimetenda dhambi kubwa mbele za Mungu pia. Nisipotubu dhambi hii sitapona nitateseka maisha yangu yote…”
Jamal aliongea kwa huruma na huzuni kubwa. Baba yake alimsikiliza Jamal kwa makini na huku mama yake mdogo akimwangalia na kuwaza moyoni mwake ni nini anataka kusema Jamal. Aliingiwa na hofu kubwa sana. JE NINI KINAENDELEA USIKOSE SURA YA .......18..........

Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom