MTUNZI: ADELA DALLY KAVISHE
ILIPOISHIA: “Baba Julieth naona tumalize maongezi kwani kesho asubuhi na mapema unatakiwa uwahi sokoni kufungua biashara. Na wewe Julieth kesho ni shule, hebu tukalale.” Alishauri mama Julieth. “Haya Julieth nenda kapumzike ila ukae nayo kichwani yote tuliyozungumza leo.” Alisisitiza Mzee Magesa huku akisimama kuelekea chumbani. “Sawa baba.” Alijibu Julieth.
INAPOENDELEA: Kesho yake
asubuhi waliamka mapema sana. Julieth alijiandaa haraka na kunywa uji
na kuwahi shuleni. Mzee Magesa aliweka mboga zake kwenye mkokoteni
na kuelekea sokoni. Mama Julieth tayari alikwishaanza kupika chapati
kama kawaida yake. “Mke wangu
leo nitachelewa kurudi kwani nikifunga tu biashara itabidi niende
kuchukua vitunguu na nyanya. Ninaomba leo usiku unipikie ugali na
matembele.” Aliomba Mzee Magesa huku akiondoka na toroli lake kuelekea
sokoni.“Haya baba
kazi njema ila sio ndiyo uchelewe sana, halafu usisahau kuleta matunda.”
Aliongea mama Julieth huku akimsindikiza kwa macho.
****************************************************************
Mzee
Magesa alipofika karibu na sokoni akiwa anavuka barabara, ghafla lilitokea
gari likiwa katika mwendo wa kasi ya ajabu na kumgonga. Mzee Magesa
aliumia sana sehemu za kichwani na sehemu mbalimbali na kusababisha
kutoka damu nyingi mdomoni, puani na masikioni.Wasamaria
wema walimkimbilia Mzee Magesa ili kumwahisha Hospitali ya Mkoa
lakini alikufa palepale hata kabla ya kuondoka.
Mashuhuda
wa ajali walijaribu kuchukua namba za gari lakini haikuwa rahisi
kwani halikusimama. Walipiga simu polisi na askari walifika baada ya muda wa
kama dakika ishirini hivi. Baada ya kuwahoji walioshuhudia ajali ile
waliuchukua mwili wa Mzee Magesa na kuondoka. Baada ya
askari kuupeleka mwili wa marehemu Hospitali ya Mkoa askari wawili
walikwenda kutoa taarifa nyumbani kwake. Walipofika walimkuta mama
Julieth katika biashara yake ya chapati. “Habari
yako mama.” Askari mmoja alisalimia. “Nzuri tu
karibuni.” Alijibu mama Julieth na kuwakaribisha akidhani ni
wateja
wake wa chapati.
“Mbona
mnazunguka nimeuliza hali yake iko vipi?” Mama Julieth aliendelea
kuhoji zaidi huku ametoa macho mithili ya panya aliyebanwa kwenye
mtego wa chuma. Wale
askari wakatazamana kwa sekunde chache kisha mmoja wao akatamka. “Wewe ni
mwanamke lakini tunakusihi ujikaze kiume.” Akamwangalia usoni mama
Julieth kisha akaendelea.
Mume wako
yupo katika Hospitali ya Mkoa katika chumba cha …” “Wagonjwa
mahututi?” Mama Julieth alimalizia sentensi akiwa kama aliyechanganyikiwa. Askari
kuona hali ya kuchanganyikiwa kwa mama Julieth akaamua
kumdanganya.
“Ndiyo
mama yupo ICU. (Intensive Care Unit)” Alifafanua Askari. “ICU? Ndo
wapi huko mbona unanichanganya.” Alihoji mama Julieth. Samahani
mama ninamaanisha yupo chumba cha wagonjwa
mahututi anafanyiwa
uchunguzi wa kina. Kisha mama
Julieth aliwaomba wale askari ajitayarishe ili aongozane nao. Baada ya
dakika kama tano hivi mama Julieth alikuwa tayari kuelekea kumwona Mzee Magesa. Walipofika askari mmoja aliwaambia wasubiri
kidogo nje ili akamwombe daktari ruhusa ya kumwona mgonjwa.
Askari
mmoja alibaki na mama Julieth katika chumba cha mapokezi huku yule
mwenzie akiingia katika chumba cha daktari ambaye ndiye aliyepokea mwili wa
Mzee Magesa na kuthibitisha kitaalamu kwamba kweli Mzee Magesa
alikuwa amekufa. Daktari
aliposikia kutoka kwa askari kwamba mke wa marehemu amekuja alimwambia
akamwite. Haraka askari alitoka nje na kuwakuta wakimsubiri kwa hamu
na kutoa ishara ya kumfuata. Wote walielekea ofisini kwa daktari. “Karibuni
mkae kwenye viti”. Daktari alitamka kisha akaendelea huku akimwangalia
kwa makini yule mama. Kwa bahati mbaya alifikiri wale askari
walikwisha mwambia kuhusu kifo cha Mzee Magesa.
“Pole sana
mama mwili wa mumeo upo katika chumba cha …..? Kabla ya
kumaliza kusema mama Julieth alianguka chini na kupoteza fahamu. Haraka
wale askari walimbeba Mama Julieth na kumwingiza katika chumba
maalumu ambako alipata huduma na kupata fahamu baada ya saa 3. Kisha
daktari aliwaomba wale askari kumsindikiza mama Julieth nyumbani
kwake. NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA .......3................
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni