Alhamisi, Desemba 13, 2012

SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA SEHEMU YA .........8..........



ILIPOISHIA
Baada ya siku kadhaa kupita hakukuwa na mabadiliko yoyote ila matatizo yalizidi kila siku ilikuwa ni ugomvi. Miezi kadhaa ilipita bila Julieth kuwa na mawasiliano na wazazi wake kwani alikuwa hana simu, hivyo ilikuwa vigumu kujua hata wazazi wake walikuwa wanaendeleaje. Kwa kweli maisha yalikuwa magumu sana. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wamiezi saba lakini John alikuwa hajali. 

INAPOENDELEA

Siku moja John alimwambia Julieth kwamba siku zake za kuondoka zinahesabika. Ilikuwa ni yapata kama saa mbili usiku wakati Julieth akiandaa chakula cha jioni. John alifika na kumwita Julieth. “We mwehu si ulikuwa unataka uende nyumbani kwenu sasa muda wako umefika unaweza ukaondoka muda wowote nakupa wiki mbili tu.” Aliongea John kwa maneno ya kutukana. “Lakini si ulisema tutakwenda wote? Hebu niangalie na hali hii kweli ndiyo niende nyumbani mwenyewe. Afadhali nisubiri hadi nijifungue ndiyo niende nyumbani.

 “Wewe una kichaa nini hivi hapa ni kwako? Tena sikiliza kwa makini nataka uondoke uende popote unapopajua hata ukifa shauri yako. Kwanza hata hiyo mimba si yangu. Kwa hadhi yangu siwezi kuwa na mke kama wewe. Kwa taarifa yako mimi nina mke na mtoto na siku si nyingi anarudi sitaki aje akutane na kinyago kama wewe humu ndani.” John alitukana na kuongea kwa kebehi na dharau. Akiwa amejiinamia Julieth alisikiliza yale maneno na kuhisi kama ni ndoto.

Kabla hajazungumza lolote John aliondoka na kumwacha akiwa na mawazo sana na kushindwa kuelewa mwenziwe ana matatizo gani. Baada ya wiki moja kupita tokea John alalame na kutukana wakati Julieth akiwa amekaa sebuleni mara John aliingia na kupita pale sebuleni kama hajamwona kisha aliingia ndani na kurudi na mabegi ya nguo na kumtupia huku akimfukuza Julieth aondoke na kwenda kwao.

“Kuanzia muda huu ninavyoongea sitaki kukuona katika nyumba yangu tena. Kama kuna kitu nimesahau kukitoa ukakitoe sasa hivi sitaki kukuona hapa mke wangu karibu atarudi.” Aliongea John kama mtu aliyepagawa. “Jamani mimi nitakwenda wapi na hii mimba? John uliniambia unanipenda kweli leo unanifanyia hivi? Nakuomba kama nimekukosea unisamehe unajua hali halisi ya maisha yangu nitafanyaje mimi kama unanifukuza? Je, maisha yangu yatakuwaje? Aliuliza Julieth kwa uchungu huku machozi yakimtoka kama mtoto mdogo.


“Mbona siku uliponitoa kwetu ulionyesha kunipenda sana, halafu ukamwambia na mama….” Kabla Julieth hajamaliza kuongea machozi yalimtiririka mashavuni kama vile kamwagiwa maji kichwani. “Mimi nikupende wewe! Mjinga sana, nimekwambia ondoka kabla sijakuua.John ”Alimfukuza Julieth na kutupa mabegi yake nje. Ilikuwa jioni
yapata saa kumi na moja, Julieth alilia sana huku akiwa hajui atakwenda wapi. Aliondoka na kwenda nyumba ya jirani kidogo ambapo alikuwa anakaa rafiki yake aliyeitwa mama Janeth na kumsimulia mkasa mzima.

“Pole sana rafiki yangu wanaume wa siku hizi ndivyo walivyo, mimi nitakusaidia ulale leo, halafu kesho uende tu nyumbani kwenu Arusha. Nitakupa hela kidogo.” Mama Janeth alimwonea huruma na kumfariji. “Asante sana mama Janeth kwani hapa nilipo sijui ningefanyaje.” Alishukuru sana Julieth na kwenda kulala baada ya kuonyeshwa sehemu ya kupumzika. Usiku akiwa amelala mara akaanza kuumwa uchungu wa kujifungua, wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba. Mama Janeth alimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ambako alipelekwa moja kwa moja chumba cha kujifungulia. 

Muuguzi wa zamu alimwambia mama Janeth aende nyumbani na awahi kuleta chai asubuhi. Julieth alijifungua salama watoto mapacha mmoja wa kike na mwingine wa kiume. Mama Janethi alipokuja asubuhi alifurahi sana kuona mgonjwa wake amepata watoto mapacha bila matatizo, aliwashukuru sana wauguzi na kuwapa shilingi elfu ishirini kama shukurani na kwa furaha aliyokuwa nayo. Julieth alijifungua kabla ya miezi tisa kutokana na misukosuko aliyokumbana nayo. Hata hivyo Julieth ilibidi aendelee kukaa pale hospitalini kwa muda wa miezi miwili huku akipewa huduma zote na mama Janeth.

Baada ya miezi miwili Julieth aliruhusiwa kurudi nyumbani. Alikaa kwa mama Janeth kwa muda wa mwezi mmoja akiwa anamuhudumia ili apone vizuri. Hali ya Julieth pamoja na watoto iliendelea kuwa nzuri. Siku moja wakiwa wamekaa sebuleni baada ya kula chakula cha jioni mama Janeth na Julieth walikuwa na maongezi kuhusu John. “Hivi Julieth, kwa nini usirudi kwa John labda akikuona na watoto atakupokea.” Alishauri mama Janeth. “Mama Janeth John amebadilika sana si yule wa siku zile, amekuwa mkali
kama mbogo aliyejeruhiwa. Ninaogopa sana asijeniumiza na pengine hata kuua wanangu.” Julieth alijibu.

“Hapana jaribu kwenda na watoto kwani anajua kuwa umeshajifungua ingawa anaona aibu ataanza vipi kuja kuwaona.” Mama Janeth aliendelea kutoa ushauri. “Sawa! Hebu nijaribu kwenda na watoto kwani kama unavyosema akiwaona watoto pengine atapunguza hasira.” Alijibu Julieth. Huku akiwa amewabeba watoto wake aliondoka kuelekea kwa John. 

Alipofika alikuwa na wasiwasi mkubwa akifikiria jinsi atakavyokabiliana na uso wa John baada ya kuachana kwa takribani miezi mitatu. Alisogea jirani, akagonga taratibu na kusubiri afunguliwe. Mara mlango ulifungulwa na mwanamke mwenye uso wa kujiamini kisha akaanza kumsemesha Julieth: “Habari za leo dada! Alisalimia. “Salama dada yangu! Habari za hapa?” Alijibu na kuuliza Julieth. “Karibu dada nikusaidie nini?” Aliuliza bila hata kujibu swali aliloulizwa.Julieth alishtuka sana na kuingiwa na hofu kubwa kumwona yule mwanamke aliyefungua mlango. USIKOSE SURA YA 9...........

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

hi adela, hadithi imekuwa tamu kweli hadi sikutamani iishe jamani naisubiri kwa hamu ili nijue mwisho wa Julieth, asante sana usitukatesha jamani

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom