Alhamisi, Aprili 25, 2013

SIMULIZI .....BADO MIMI.......SURA YA .....7.....



 ILIPOISHIA:Wakati wote nilikuwa namsikiliza Daktari kwa umakini nilihisi kama kuchanganyikiwa, baada ya kusikia alichokisema Daktari "Eti India, Mungu wangu haiwezekani jamani nani atatusaidia pesa za kumpeleka Mama India" Mama Bilionea alinisihi nitulie kwanza kwasababu nilikuwa kama nimechanganyikiwa. Baadaye Daktari alitupatia dawa nyingi sana na kusema kuwa zitamsaidia Mama kutuliza maumivu lakini inabidi ipatikane pesa kiasi cha shilingi milioni tisa, ili Mama akafanyiwe upasuaji India. Je Mama Bilionea atamsaidia Kandida?.Usikose SURA YA.......7..........

INAPOENDELEA
Nilikuwa katika wakati mgumu sana, kwasababu sikujua nini hatima ya maisha ya familia yangu. "Baba yangu yupo anatumikia kifungo Gerezani, Mama anaumwa, Kinahitajika kiasi cha shilingi milioni tisa ili akafanyiwe upasuaji India. Mimi bado ni msichana mdogo nikijiangalia nina majukumu ya kulea familia sielewi nini kitatokea katika maisha yangu. Na kama nisingekutana na Mama Bilionea Mama yangu si angekufa pale nyumbani" Niliwaza sana na machozi yalikuwa yakinibubujika bila kuisha ijapokuwa Mama Bilionea alijitahidi kunibembeleza.

Baadaye Daktari alituruhusu tuondoke na Mama kwani zile dawa alizompa zilimsaidia kutuliza maumivu makali aliyokuwa akiyasikia. Hali yake ilionekana kuwa njema, lakini sasa alikuwa ni mtumwa wa dawa, kwani kila siku alitakiwa kumeza dawa hizo kwaajili ya kutuliza maumivu. Dawa hizo zilikuwa zinauzwa kwa gharama kubwa kama asingekuwepo Mama Bilionea nisingeweza kuzinunua. Kila wiki alitakiwa kununua dawa za shilingi laki moja.Mama Bilionea alinunua dawa za mwezi mzima nilimshukuru sana kwa moyo wake wa kujitolea.Mama aliendelea kutumia dawa ijapokuwa Daktari alitusisitiza itafutwe hela haraka Mama akafanyiwe upasuaji kwani   baadaye tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi.

Tukiwa nyumbani Mama alikuwa katika hali ya kawaida kwani zile dawa zilimsaidia sana, na kwa wakati wote huo hakutaka Baba afahamu chochote kuhusu hali yake.Ikiwa imepita wiki moja tokea Mama atoke Hospitalini, Mama Bilionea alikuja nyumbani kutujulia hali, tulifurahi sana kwani alikuwa ni mtu wa muhimu sana kwetu. "Karibu Mama Bilionea karibu sana" Mama alimkaribisha na waliketi pamoja kwenye mkeka huku mimi nikiwa jikoni naandaa chakula.Baadaye Mama Bilionea alimwambia Mama kuwa,  anichukue mimi nikamsaidie kazi za nyumbani kwake na atakuwa ananilipa mshahara mzuri. Mama alishukuru sana "Sijui hata nikushukuru vipi umetusaidia sana, nakushukuru sana Mungu atakuzidishia" Ilikuwa ni sauti ya Mama ambaye aliongea kwa furaha.


Baada ya Mama kuniambia kuwa sasa nitaenda kuishi kwa Mama Bilionea na kumsaidia kazi mbalimbali nilifurahi lakini pia nilikuwa na wasiwasi "Lakini Mama hapa nyumbani nani atakusaidia kazi na wewe hali yako haitabiriki" Mama alinijibu huku akionyesha kutokuwa na wasiwasi wowote. "Mwanangu usiwe na shaka mimi hali yangu inaendelea vizuri, dawa ninazotumia zinanisaidia sana wewe nenda kafanye kazi, na tena Mama Bilionea ameniambia kila siku ya jumamosi na jumapili utakuwa unakuja kulala hapa nyumbani, kwahiyo hakuna tatizo." Aliongea Mama huku akiwa na matumaini makubwa. Sikuwa na kipingamizi nilikubali ombi la Mama Bilionea kwani sasa nilijua naweza kuisaidia familia yangu bila matatizo yoyote ijapokuwa mawazo yangu yote yalikuwa ni juu ya matibabu ya Mama na Baba yangu siku atakayoachiwa huru kutoka gerezani.

Maisha yalibadilika nilihamia kwa Mama Bilionea maeneo ya Mikocheni katika jumba la kifahari lililosheheni vitu vya thamani. Nilikuwa nashangaa kila nilichokuwa nakiona, kwasababu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika nyumba ya kifahari kiasi kile. Kila nilichokiona mbele yangu kilikuwa nikigeni kwangu. "Karibu Kandida jisikie huru, hapa ni nyumbani kwangu" Bado nilikuwa nashangaa kiasi kwamba nilijiona mchafu hata kukalia masofa yaliyokuwa yanaonekana yakisasa "Mama Bilionea nyumba yako ni kubwa sana,unaishi mwenyewe na watoto wako?" Niliuliza swali ambapo Mama Bilionea alinyamaza kidogo na kunijibu "Naishi peke yangu na wafanyakazi wangu wapo vijana wanne, kwa bahati mbaya sikubahatika kupata mtoto katika maisha yangu" Nilimuonea sana huruma kwani alionekana tajiri na mwenye pesa nyingi lakini kumbe alikuwa hana mtoto "Lakini kwasasa nimepata mtoto ambaye ni wewe mwanangu Kandida".Aliongea Mama Bilionea huku akinishika mkono na kunipeleka kunionyesha chumba nitakachokuwa nalala.

Kilikuwa ni chumba kizuri sana, ilinibidi nianze kufundishwa kutumia kila kitu kwasababu nilikuwa sijui chochote, lakini Mama Bilionea alinionyesha upendo wa hali ya juu kwani hata kazi niliyokuwa natakiwa kuifanya sikuiona muda mwingi nilikuwa nikiangalia video, niliishi kama mtoto wake wa kumzaa na alikuwa akinipa pesa nyingi sana.JE NINI KINAENDELEA ....USIKOSE SURA YA ....8...





Hakuna maoni:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom