Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo BADO MIMI. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo BADO MIMI. Onyesha machapisho yote

Jumatatu, Julai 22, 2013

SIMULIZI YA ...BADO MIMI...SEHEMU YA ....28......



 ILIPOISHIA
Nilikuwa nawaza huku Renata akinitikisa mkono kwa nguvu na kunivuta “Dada twende tukamtafute Tumaini, twende dada” Wakati huo Charito alikuwa amesimama pembeni na kusema “Inawezekanaje mlinzi alikuwepo hapa getini halafu mtoto anakimbia anashindwa kumrudisha, sasa atakuwa amekimbilia wapi, si unajua Dar es salaam ni kubwa” Alisema Charito huku akiwa anaelekea kumtafuta mlinzi na mimi nikawaza kuwa hawezekani Tumaini akawa ameenda  sehemu ya mbali labda atakuwa maeneo ya karibu, haraka nilitoka nje na kuanza kuwauliza majirani JE NINI KITAENDELEA USIKOSE...... SEHEMU YA........28.........

INAPOENDELEA
Nilizunguka huku na kule kumtafuta Tumaini bila ya mafanikio. kwani kila jirani nileyekuwa nikimuulizaa alisema hakumuona Tumaini.Nilikuwa na mawazo sana huku nikiwa na hisia labda Tumaini anaweza kupotea kabisa au hata kugongwa na gari.Wazo la kwenda kuripoti kituo cha polisi sikuwa nalo kabisa kichwani niliendelea kuzunguka huku na kule na machozi yalikuwa yakinilengalenga kutokana na hofu ya kuwa naweza nisimpate mdogo wangu.
 
Kwa wakati huo mume wangu naye alikuwa akizunguka kumtafuta Tumaini.Yalipita masaa kama matatu huku tukimtafuta Tumaini bila ya mafanikio ilinibidi nirudi nyumbani huku mawazo yangu yakinipelekea kuwa yawezekana Tumaini akarudi mwenyewe.

Nilipofika nyumbani nilimkuta mume wangu  akiwa ameketi sebuleni pamoja na Renata "Vipi jamani, inamaana Tumaini hajarudi nyumbani" Charito alinitizama na kusema "Nimehangaika sana kumtafuta huku na kule bila ya mafanikio nilifikiri labda wewe utakuwa umempata, sasa sijui atakuwa ameelekea wapi" Wakati Charito akiwa anazungumza Renata alimtizama Charito  na kusema kwa sauti iliyojaa hasira kali "Wewe shemeji unajua wapi ameenda Tumaini, sema yuko wapi mdogo wangu?".

Jumatatu, Julai 15, 2013

SIMULIZI....BADO MIMI......SEHEMU YA .....27........


ILIPOISHIA
Nilimshika  mikono huku nikimbembeleza kwasababu alikuwa na hofu sana nilimchukua na kwenda naye sebuleni kisha nikamuuliza taratibu. Kilichonishangaza Renata alinisimulia ndoto aliyokuwa anaiota ilikuwa inafanana vilevile na ndoto ya kutisha niliyokuwa nikiota.Nikiwa na hofu kubwa  na wasiwasi Charito alinitizama na kusema "Usiwe na wasiwasi mke wangu, haya ni majaribu ya shetani, kuwa na imani na Mungu kila kitu kitaenda sawa , usiogope chochote kwani shetani atashindwa kwa nguvu zake Mungu". JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE ....SURA YA ........27...

INAPOENDELEA
Nilikuwa na wasiwasi na mawazo mengi sana kichwani,  na hata kujiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu kwani sikuelewa ni kwanini, maisha yangu yanaendelea kupata majaribu na wakati nimekwisha mpokea Mungu katika maisha yangu. Siku zilienda huku nikiwa naota ndoto za ajabu kila kukicha wakati mwingine nilikuwa nashindwa kulala kabisa, kutokana na hofu.

Siku moja nilikuwa nimeketi sebuleni huku nikiwaza “Hivi  inawezekana hii nyumba ya Mama Bilionea imezindikwa na nguvu za giza ambazo haziwezi kuisha, na sasa mbona tunasali na kukemea nguvu za giza kila siku  kwanini hali hii inajirudia, yaani mimi nimechoka na hii hali, haya ni mateso jamani ni bora nimwambie mume wangu tuondoke katika hii nyumba vinginevyo na wasiwasi linaweza kutokea tatizo”. Nilikuwa na mawazo mengi sana siku hiyo, nikiwa naendelea kuwaza, Renata alikuja na kuketi karibu yangu huku akiwa amenyamaza kimya bila ya kuzungumza chochote.

Nilimtizama  Renata na kusema “Renata mbona upo kimya sana, na tena unaonekana mnyonge vipi una matatizo mdogo wangu?” Renata alinyama kimya kidogo na kisha akanijibu “Dada, hata nikikueleza matatizo niliyonayo, wewe hauniamini, mimi usiku naona vitu vya ajabu, halafu kinachonishangaza wakati mwingine namuona shemeji Charito akija chumbani kwangu usiku huku akionekana kuwa katika umbo la ajabu na pia....” Kabla Renata hajamaliza kuzungumza nilimkatisha na kusema  “Sikiliza nikuambie Renata, hizo ni ndoto tu na hazina maana mbaya, na pia kumbuka kusali kabla ya kulala kwani hayo ni majaribu ya shetani, anaweza kukufanya wewe umchukie  shemeji yako” Renata alinyanyuka kwa hasira pale alipokuwa amekaa na kusogea karibu yangu “Nilijua tu, hauwezi kuniamini lakini dada kumbuka usilolijua ni sawasawa na usiku wa kiza kinene, mimi naongea ukweli na wala siyo ndoto”.

 Nilishangaa kumuona Renata katika hali ile, ikanibidi niwe mkali kidogo “Unajua Renata wewe ni mtoto mdogo sana kuzungumza na mimi kwa sauti kali kiasi hicho, mimi ni dada yako mkubwa na inabidi uniheshimu lakini sasa naona unapoelekea nitakuja kukupiga nikuumize vibaya, sijaipenda kabisa tabia yako, embu toka hapa sitaki kukuona nisije nikakunyofoa huo mdomo wako mchafu.” Renata aliondoka huku akisema “Sawa dada lakini ipo siku utaniamini”.

Alhamisi, Julai 04, 2013

SIMULIZI... BADO MIMI...... SEHEMU YA .....26.........



 ILIPOISHIA
Ilikuwa ni ndoto ya kutisha ghafla nilishtuka kutoka usingizini baada ya mdogo wangu Renata kuniamsha "Dada, simu yako inaita muda mrefu, umelala"Nilishtuka nakujitizama mikono yangu kama ilikuwa na damu, lakini haikuwa na damu yoyote "Mungu wangu hii ni ndoto mbaya sana" Nilikuwa na hofu kubwa huku jasho likinitoka kwa wingi ilikuwa tayari ni majira ya saa moja asubuhi" JE NINI KITAENDELEA....USIKOSE SURA YA.......26......... 

INAPOENDELEA
Ghafla simu iliita kwa mara ya pili. Nilishtuka kwasababu nilikuwa nawaza ile ndoto je itakuwa inamaanisha kitu gani? Renata alinipa simu nami nikaipokea, alikuwa ni Charito "Mambo vipi, inamaana umelala hadi muda huu? Mbona nimepiga simu imeita muda mrefu hivyo?" Alilalamika Charito, na mimi kwa sauti ya unyonge nikasema "Nilikuwa nimepitiwa na usingizi mzito sana, samahani mpenzi" Charito alicheka kidogo nakusema "Angalia tu usije ukasahau na muda wa kwenda kanisani, tafadhali naomba ujiandae mapema" Alisistiza Charito."Usiwe na wasiwasi mpenzi, siwezi kusahau jamani". Baadaye nilinyanyuka pale kitandani huku viungo vya mwili wangu vikiwa vinaniuma sana kutokana na uchovu. Nilianza kwa kufanya mazoezi madogo ya kunyoosha viungo kwa kuruka kamba na baadaye nilienda kukoga na kujiandaa kwaajili ya kwenda saluni.

        Hatimaye muda wa kwenda kanisani ulifika, Lilikuja  gari la kifahari kunichukua. Kabla sijaenda kupanda lile gari mdogo wangu Renata alikuja chumbani na kusimama mlangoni huku akinitizama na kusema "Lakini dada kwanini unakubali kuolewa na Charito?" Nilimtizama na kusema "Hivi wewe Renata una matatizo gani? Unajua leo ni siku yangu ya muhimu sana lakini unataka kunipotezea furaha yangu kwa maneno yako yasiyokuwa na kichwa wala miguu,Embu nenda kamchukue Tumaini tuondoke  kwani tunachelewa kanisani." Renata aliondoka huku akiwa amekunja sura kwa hasira. Nilitoka nje huku nikiwa na majirani zangu na baadhi ya akina dada ambao walikuwa wasimamizi katika harusi yangu.

Alhamisi, Juni 27, 2013

SIMULIZI...BADO MIMI...SURA YA.....25.........



 ILIPOISHIA
Aliendelea kulia ikanibidi niwe mkali kidogo ndipo alinyamaza na kwenda kuendelea kula chakula. Nilibaki nikiwaza na nafsi yangu "Inamaana huyu shetani, anataka kumfanya mdogo wangu achanganyikiwe hadi amuone mchungaji Mkombozi kuwa ni mtu mbaya, eeh Mungu naomba utusaidie". Je nini kitaendelea usikose sura ya ....25.....

INAPOENDELEA
Baadaye usiku kabla ya kulala, tulifanya maombi kwa kusali pamoja na wadogo zangu. Nilijaribu kumliwaza Renata ambaye alionekana kuwa katika wakati mgumu, kwani alikuwa akiogopa sana kulala "Renata, usiogope chochote Mungu yupo pamoja nasi, unachokiona katika ndoto ni majaribu tu ya shetani lakini kwa nguvu za Mungu yatashindwa, sasa unaweza kulala vizuri usiwe na hofu yoyote".

 Huku akiwa ananitizama alikuwa anaonekana kuwa na hofu sana, niliendelea kumbembeleza huku nikimuimbia wimbo mzuri "Mungu wetu ni mwema, Mungu wetu anatupenda, yeye atatulinda maisha yetu yote, Nampenda Mungu katika maisha yangu, yeye ananipenda atanilinda na mabaya. Sina hofu tena mimi nipo na Mungu. Nasema Mungu ni mwema, Mungu wetu anatupenda,  yeye atulinda maisha yetu yote." Wakati nikiwa naimba Renata alipitiwa na usingizi na kulala fofofo.

Kesho yake asubuhi kama kawaida nilikuwa nikiendela na shughuli zangu za kawaida niliamka mapema na kujiandaa kwenda Dukani, siku hiyo ilikuwa ni siku ya jumamosi hivyo wadogo zangu walikuwa nyumbani hawakwenda shule. Baadaye niliondoka na kuelekea dukani kwangu nikiwa kazini nilikuwa na mawazo sana "Hivi ni kitu gani ambacho kinataka kuitokea familia yangu, mbona nimekuwa na hofu sana moyoni, kwani nimekuwa nikiota ndoto za ajabu, lakini pia mdogo wangu Renata amekuwa akiota ndoto za ajabu sijui nini kinataka kutokea jamani eeh Mungu nisaidie" Nilikuwa nawaza sana, siku hiyo nilikuwa sina furaha kabisa.

Baadaye nilitoka kazini na kuelekea kanisani kwenye maombi kabla ya kwenda nyumbani. Nikiwa kanisani tulikuwa pamoja na Charito.Tulifanya maombi pamoja na baadaye alinisindikiza hadi nyumbani. Nilipofika nyumbani niliwakuta wadogo zangu wakiwa wameketi sebuleni wakitizama tamthilia iliyokuwa inaonyeshwa kwenye televisheni. "Hamjambo watoto wazuri" Aliwasalimia Charito "Hatujambo shikamoo shemeji" Ilisikika sauti ya Tumaini zaidi kuliko ya Renata iliyokuwa ikisikika kwa mbali nilimtizama na kusema "Vipi hali yako Renata,  natumaini hakuna tatizo" Renata alinitizama bila ya kuzungumza chochote.

Jumatatu, Juni 24, 2013

SIMULIZI YA ..BADO MIMI.....SURA YA ,.......24......

 
 ILIPOISHIA
Pale kitandani nilikuwa nimelala na mdogo wangu Renata alishtuka kutoka usingizini na kunitizama huku akifikicha macho yake na kusema "Dada Kandida, mimi naogopa, naogopa Dada Kandida" Nilimshika mikono kwani alikuwa akitetemeka sana na kumuuliza "Unaogopa nini Renata? Mimi nipo na wewe" Renata alianza kulia na kusema "Kuna mtu anataka kunichoma na kisu, umemuona Dada" Nilijua Renata alikuwa ameota ndoto mbaya nilianza kumbembeleza ili apate usingizi.JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE ...SURA ...YA.... 24.....
 
INAPOENDELEA
Nilikuwa nambembeleza Renata pale kitandani, baadaye usingizi ulimpitia nakulala fofofo.Ilipofika asubuhi niliamka na kwenda kuandaa kifungua kinywa. Wakati huo Renata alikuwa bado amelala, nilipoona muda unazidi kwenda ilinibidi niende kumuamsha "Renata,Renata, umesahau kuwa huu ni muda wa kwenda shule? Embu nyanyuka hapo kitandani  haraka ujiandae." Huku akiwa anajivuta taratibu kwa sauti ya unyonge akasema "Dada mimi kichwa kinaniuma" Nilihisi labda ameanza uvivu, lakini haikuwa tabia ya Renata kukataa kwenda shule.Nilisogea karibu na kumshika kwenye mwili  wake alikuwa na joto kali sana. 
 
Baada ya kuona ile hali ikanibidi nifanye haraka ili nimpeleke Hospitali. "Renata atakuwa anaumwa Malaria, sasa itabidi nimpeleke hospitalini haraka, kwasababu kama itakuwa ni Malaria itabidi apatiwe matibabu haraka kwani huu ugonjwa huwa ni hatari sana" Niljianda haraka na kumuandaa Renata kisha nikampeleka katika zahanati iliyokuwepo maeneo ya pale nyumbani.
 
Baada ya Daktari kumpima kweli aligundulika anayo Malaria. "Umefanya vyema kumleta mtoto Hospitali mapema, baada ya kugundua tu atakuwa na dalili za Malaria. Kwani inakuwa rahisi zaidi katika matibabu" Alisema Daktari. Tulipewa dawa  na kuruhusiwa, kwahiyo Renata alianza dozi ya dawa za Malaria. Baada ya siku mbili tatu Renata hali yake ikiwa inaendelea kuwa nzuri kiafya. Charito alikuja nyumbani akiwa pamoja na mchungaji kuja kumjulia hali mgonjwa.
 
Tulikuwa tumeketi pamoja pale sebuleni na Renata alikuwa chumbani amepumzika. Charito akasema "Kandida, naweza kwenda chumbani kumuona Renata?" Huku nikionyesha tabasamu pana nikasema "Bila shaka, Charito ingia tu mlango wa kushoto" Charito alinyanyuka na kuelekea chumbani kwa Renata.

Jumatatu, Juni 10, 2013

SIMULIZI...BADO MIMI....SURA YA .....20.......

 ILIPOISHIA
Ngozi ya mwili wake ilionekana kubadilika katika upande mmoja wa mwili wake ilionekana kuwa na ngozi ya ajabu kama magamaba ya nyoka, ilikuwa ni ngozi ya kutisha sana, niliogopa na kutetemeka huku nikiwa kama nataka nitimue mbio, Mama Bilionea aliniita “Usiogope Kandida naomba uketi unisikilize mwanangu”  Nilisogea huku nikiwa siamini kile ninachokiona “Mama Bilionea umepatwa na kitu gani, mbona ngozi yako inabadilika”.Yaani nilikuwa nahisi kama nataka kuzimia kwasababu sikujua ni kitu gani kinataka kutokea kwa muda ule. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA......20.....

INAPOENDELEA
Nilijisogeza kwambali kidogo, huku nikiwa na jikunyata kwa kuogopa kile nilichokuwa nakiona. Mama Bilionea kwa sauti ya upole akasema “Kandida wakati wangu umefika, narudi nyumbani kwa Mama yangu Bibi Bilionea, naimani utathamini nakuenzi hekalu la Bilionea siku zote za maisha yako, naomba uchukue huu mfuko” Huku akiwa ananionyesha mfuko mkubwa uliokuwa na rangi nyekundu akaniambia humo ndani kuna vitambaa vingi sana na mikufu ya rangi nyekundu. Lakini pia kuna kitabu ambacho kitakusaidia kukuongoza katika kukamilisha kazi za Bilionea, Maisha yako yatakuwa mazuri sana,  kama tu utafuata masharti yalipo katika kitabu”.

 Sikuamini kile nilichokuwa nakisikia inamaana Mama Bilionea alikuwa ananirithisha mikoba yake. “Lakini Mama sintoweza kumtoa kafara mtu yeyote nakuomba usiniachie mimi tafadhali, niruhusu tu niondoke.” Mama Bilionea alikohoa kidogo na kusema “Hapana haiwezekani, wewe tayari jina lako lipo katika hekalu la Bilionea na tayari ulishasaini mkataba kwa kutoa kafara ya Baba yako ni vigumu kutoka katika maisha ya Bilionea labda uwe umekufa” Akiwa anaendelea kuzungumza hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Nilikuwa naogopa sana kwa jinsi Mama Bilionea alivyokuwa akibadilika, huku akiwa anaendelea kusema “Kandida kitambaa na  mkufu utakuwa unampa mtu ambaye umeoteshwa kuwa tunahitaji kafara kutoka kwake, usiogope siyo kila wakati  utatoa kafara ni mpaka atakapokuambia Bibi Bilionea na pia yeyote atakayeniulizia mwambie nilihamia nje ya nchi. Kwani mwili wangu hautoonekana, nakutakia maisha mema Kandida” Nilikuwa bado sijielewi nikahisi labda naota lakini haikuwa ndoto “Mama Bilionea Mimi sintoweza kabisa kufanya hivyo tafadhali nakuomba uniruhusu niondoke.”

Jumatatu, Juni 03, 2013

SIMULIZI .....BADO MIMI....SURA YA .....18


ILIPOISHIA
Baada ya kumaliza kuongea  ghafla  niliona giza kali sana bila ya kuona mwanga wowote niliogopa huku nikipapasa huku na kule bila ya kushika chochote "Bibi Bilionea usiniuwe jamani nakuomba usiniuwe"  Nilizungumza bila ya kujielewa nguvu zilikuwa zinaniishia taratibu baadaye sauti ilinikauka kabisa sikuweza tena kuzungumza. JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA ....18........

INAPOENDELEA
Baadaye  nilizinduka, na kidogo nikaanza kuona mwanga kwa mbali nilikuwa  kama mtu mwenye matatizo ya macho, nilifikicha macho yangu huku nikitizama kwa umakini nishangaa kujikuta nipo nyumbani kwa Mama Bilionea tena chumbani kwangu ambapo huwa nalala "Mmmmh inamaana nilikuwa naota au? Haiwezekani jamani mbona....kama...."Nilikuwa naongea mwenyewe bila kujielewa nimefikaje pale kwa Mama Bilionea nilisikia sauti ikinisemesha "Haikuwa ndoto Kandida,kila kitu kilikuwa ni kweli.

 Naimani sasa umejua ni kwa kiasi gani nakupenda hadi nimekuchagua uwe mrithi wangu. Vinginevyo usingeweza kurudi hapa lazima ungekufa hakuna mtu anayekwenda kwenye hekalu la Bilionea nakurudi akiwa hai." Alikuwa akizungumza Mama Bilionea huku akinitizama, Mimi nilikuwa nimeketi kitandani huku nikionekana kuwa na wasiwasi sana kutokana na mambo yote yaliyonitokea. Nilikuwa nimechoka sana kwani kwa muda wote niliokuwa katika hekalu la Bilionea nilikuwa sijala kitu chochote.Niliongea kwa sauti ndogo na ya upole "Mama Bilionea, kwanini umenichagua mimi, naomba usiimalize familia yangu".

"Hahahahahahahahah" Alicheka Mama Bilionea huku akinisogelea taratibu pale kitandani   na kunishika usoni huku akiinua shingo yangu kwa kunishika kidevu  changu kwa mkono wake "Hivi wewe Kandida, unajua nini maana ya Maisha, Wewe ni Binti mrembo sana nashindwa kuelewa ni kwanini unakuwa mgumu kufahamu  mambo yote haya ni kwa faida yako.Halafu kuhusu familia Mama yako ni mgonjwa na amepelekwa Hospitali."Nilihisi kuishiwa nguvu baada ya Mama Bilionea kuniambia kuwa Mama yangu yupo Hospitalini "Mungu wangu Mama Bilionea umeamua kumtoa kafara Mama yangu, tafadhali nakuomba usimuuwe Mama yangu" Nilinyanuka na kupiga magoti chini huku nikimuomba Mama Bilionea.

 "Hivi Kandida unasahau kuwa Mama yako ana matatizo ya uvimbe tumboni? Sasa nashangaa unasema nimemtoa kafara. Hata na hivyo kutokana na tatizo alilonalo Mama yako hawezi kupona."Mwili ulikuwa ukinitetemeka kwa hasira huku nikilia kwa uchungu nikasema "Mama Bilionea kwanini unaitesa familia yangu, kwanini mimi jamani, hata kama Mama yangu ni mgonjwa ni bora nijue Mama yangu amefariki kwa kuugua kuliko kumtoa kafara, unaitesa familia yangu Mama Bilionea". 

Jumatatu, Mei 27, 2013

SIMULIZI......BADO MIMI ..SURA YA ......16.......



 ILIPOISHIA
Machozi yalinibubujika nguvu ziliniishia nikajikuta nimekaa chini huku nikijikunyata kama mtu anayehisi baridi kali nililia sana "Eeeh Mungu nisaidie nitoke eneo hili, Masikini Baba yangu yalaiti ningelijua kuwa Mama  Bilionea ni mtumwa wa Shetani, yote haya yasingenikuta mimi pamoja na familia yangu.Mateso gani haya jamani, sijui nini hatima ya maisha yangu." Je.....NINI KITAENDELEA USIKOSE ....SURA YA 16.........

 INAPOENDELEA
Kwa wakati wote huo nilikuwa nahisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa ndoto, niliumia sana moyoni kumuona Baba yangu katika hali aliyokuwa nayo. Alikuwa amevaa nguo zimechanika huku nywele zake zikiwa ndefu bila ya kupitishwa kitana.Uso wake ulikuwa umepoteza nuru ya maisha nilikuwa nikimtizama anapoelekea lakini baadaye sikumuona tena. Moyoni mwangu niliwaza "Eeeh Mungu nakuomba unisaide, Mama Bilionea anataka kuiangamiza familia yangu ili aje kutufanya misukule. 

Nawezaje kutoroka eneo hili? Nataka nikamuokoe Mama yangu jamani". Nikiwa nawaza Chande alinisemesha "Kandida nimekuambia huu ni muda wa kwenda kula unaweza kujumuika pamoja na mimi lakini sikuelewi, sizani kama upo sahihi kutoa machozi eneo hili. Kwani hapa watu huwa hawalii unaweza kupatwa na chochote kibaya. Na ikiwezekana unaweza  usitoke kabisa eneo hili maisha yako yote ukaishi  katika hekalu la Bibi Bilionea". 

Nilinyanyuka pale chini huku nikiwa najifuta machozi yaliyokuwa yakibubujika katika paji la uso wangu na kusema "Chande naomba unisaidie niondoke katika hili hekalu,siwezi kubaki huku" Chande alinitizama kwa kunikazia macho "Nimekuambia huu ni muda wa kwenda kula, na pia kuhusu kuondoka katika hili hekalu ni mpaka utakapoonana na Bibi Bilionea"Aliongea kwa sauti kali kuonyesha msisitizo. Tuliongozana hadi katika eneo ambalo watu wote walikuwa wameketi huku wakila chakula ambacho kilikuwa ni pumba pamoja na damu ambayo sikujua wameipata wapi damu ya binadamu. nilishindwa kuamini ninanchokiona mbele yangu kwani zile pumba zilikuwa zimemwagwa chini na huku kila mmoja akiwa ameshikilia kikombe cha ajabu kilichokuwa na damu "Natamani hii ingekuwa ni ndoto jamani, haya ninanyoyaona yanatisha sana" .

Jumatano, Mei 22, 2013

SIMULIZI.....BADO MIMI.... SURA YA .....15..........



 ILIPOISHIA
Wewe Kandida mbona umeanza kuwa mtoto ambaye ni muongo?usiwe na tabia mbaya mwanangu si unajua Mama yako nakupenda sana, huwezi kwenda nyumbani usiku huu". Alinijibu Mama Bilionea. Huku nikiwa natafuta njia ya kutoroka nilisikia kitu kikinisukuma kwa kishindo kikali sana. Ghafla nilianguka chini na hata nilipoamka mazingira niliyoyaona yalikuwa tofauti kabisa.Mama Bilionea sikumuona tena ila kulikuwa na watu wengi sana katika hilo eneo. .......JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA..........15.....

INAPOENDELEA
Nilitizama huku na kule, lakini sikumfahamu hata mtu mmoja katika lile eneo. Kulikuwa na watu wengi sana,kwa kukadiria ni zaidi ya watu wapatao mia tano. nilishindwa kuelewa imekuwaje nimefika eneo hili na tena katika mazingira ya ajabu. Ilikuwa ni sehemu ambayo hakuna nyumba hata moja zaidi ya miti huku kila mtu akionekana anafanya kazi zake wengine walikuwa wanaimba lakini sauti zao zilikuwa hazisikiki, na wengine walikuwa wakipepeta pumba katika nyungo kubwa.Nilimuona Mama mmoja akiwa ameketi pembeni yangu huku akiwa ameinama  kama kuna vitu anaokota pale chini."Huku ni wapi tena jamani?Mbona sielewi, na hawa watu wote wametokea wapi na mbona hakuna nyumba yoyote nikitizama naona miti, inamaana hawa watu wanalala juu ya miti?"

Nilikuwa najiuliza maswali mengi huku taratibu nikiwa najisogeza karibu na yule Mama aliyekuwa ameinama huku akiokota vitu ambavyo sikuvielewa ni vitu gani. "Shikamoo Mama, samahani nilikuwa naomba kuuliza hapa ni wapi?" Yule Mama alinitizama na kuendelea na kazi aliyokuwa akiifanya bila ya kunijibu chochote nilijitahidi kumuuliza lakini hakunijibu kabisa niliamua kusogea na kutafuta watu wengine ambao ningewauliza kwani nia yangu nilikuwa nataka kufahamu hapa nilipo ni wapi?Kila niliyekuwa namuuliza hakunijibu chochote, alinitizama na kuendelea na mambo yake.

Nikiwa naendelea kuzunguka huku na kule nilikutana na kijana mmoja ambaye alionekana kuwa tofauti na wengine, kabla hata sijamuuliza chochote alinitizama na kunisemesha "Wewe ni mgeni maeneo haya?" Huku nikiwa namtizama nilimjibu "Ndiyo,sielewi haya mazingira, nisaidie kaka yangu kwani hapa ni wapi?" Yule kaka akacheka "Hahahahaha umewezaje kufika huku ukiwa na uwezo wa kuongea, kwani wote unaowaona hapa ni watu waliokufa duniani, na pia hawazungumzi wala hawamtambui mtu yeyote au kusikia chochote zaidi ya kumsikiliza malkia pekee. Kwani wewe umetokea wapi?" Sikutaka kuamini kile alichokuwa anakisema yule kaka nilihisi kama nipo ndotoni "Mungu wangu, inamaana mimi nimekufa, Mama Bilionea amenitoa kafara?" Nikiwa nawaza yule kaka akaniuliza  tena "Wewe ni nani? Umetokea wapi?".

Jumatatu, Mei 20, 2013

SIMULIZI.......BADO MIMI....SURA YA ....14.......

  ILIPOISHIA
Nilihisi kama nataka kuchanganyikiwa kwa maneno aliyokuwa anazungumza Mzee Temba "Inamaana Mama Bilionea ndiye aliyemuuwa Baba yangu? Mungu wangu akili sasa ndiyo inanifunguka, na yule mchungaji namkumbuka kule hospitalini alisema tumefungwa macho na nguvu za giza. Pia  naikumbuka ile ndoto niliyoota Baba ananiita nimuokoe kabla Mama Bilionea hajanivisha ule mkufu. Huyu Mama ni mchawi eeh Mungu nisaidie nitafanya nini mimi, Mzee Temba naomba unisaidie. .......JE NINI KITATOKEA ...USIKOSE SURA YA 14.......
  
INAPOENDELEA
"Sijui nini hatima ya maisha yangu" Nilikuwa katika wakati mgumu sana huku nikimtizama Mzee Temba "Sikiliza nikuambie binti yangu, jambo la kufanya wewe rudi nyumbani kwa Mama Bilionea na uishi bila ya kuogopa chochote. Na wakati huo ukiwa unapanga ni namna gani unaweza kuondoka. Kwani kwa sasa hata ukisema unaenda nyumbani kwenu Mmbagala, anaweza kuja kukufuata kwani si anapafahamu?" Alikuwa akinishauri Mzee Temba huku mimi nikiwa nimekodoa macho mithili ya mjusi aliyebanwa kwenye mlango, "Lakini mimi naogopa sana, sizani kwama naweza kurudi ndani ya ile nyumba.Ukweli mimi siwezi Mzee Temba".

Aliendelea kunishauri nirudi ila nifanye juu chini yule Mama asigundue chochote kama mimi nimekwisha fahamu tabia yake. Baadaye ilinibidi nimsikilize Mzee Temba alichonishauri na kunyanyuka kuelekea nyumbani huku nikiwa na mawazo sana "Eeeh Mungu naaomba unisimamie, hapa nilipo sijui nini kitatokea katika maisha yangu. Huyu Mama si ataniuwa mimi." Nikiwa natembea taratibu ghafla nilisikia mlio wa honi ya gari "piiiii,piiiiii,piiiiii".

 Kutokana na mawazo niliyokuwa nayo nilikuwa nikisikia mlio wa honi kwa mbali, "Wewe Kandida una matatizo gani? Kama ningelikuwa katika mwendo wa kasi si ningekugonga na gari" Aliongea kwa sauti ya ukali Mama Bilionea aliyekuwa anaendesha lile gari. Niligeuka na kubaki nikimtizama bila ya kuzungumza chochote "Ehee umetoka wapi? Na mbona haujachana nywele na nguo inaonekana haijanyooshwa, hivi una kichaa? Embu panda ndani ya gari twende" Aliongea huku akinitizama kuanzia chini mpaka juu.

Kwa sauti ya upole na iliyojaa wasiwasi mwingi huku nikijikaza nisionekane kama nina tatizo lolote nikasema "Samahani Mama nilikuja dukani mara moja kununua dawa kichwa kinaniuma" Huku nikiwa napanda ndani ya gari la kifahari la Mama Bilionea "Sasa kama unaumwa si unasema mwanangu, pole sana ila siku nyingine kuwa makini unapotembea barabarani kwani unaweza kugongwa na gari, pikipiki na hata baiskeli." Nilikuwa kimya huku moyoni nikiwaza "Yaani huyu Mama ni muuaji mkubwa, anajifanya mpole tena mwenye huruma kumbe nia yake ni kuimaliza familia yangu! Tena naomba Mungu asikumbuke kama sijauvaa ule mkufu".

 Hatimaye tulifika nyumbani, huku Mama Bilionea akielekea chumbani kwake. Na mimi nikiwa natembea kwa kuogopa nilifungua mlango wa chumba changu.  Huku macho yangu moja kwa moja nikiyaelekeza juu ya kitanda, ambapo kulikuwa na kile kitambaa chekundu na ule mkufu.

Niliingia kwa ujasiri wa ajabu huku moyoni nikisali "Mungu nisaidie, ni wewe pekee nakutegemea sina mtu mwingine nisaidie Mungu wangu" Nilivuta lile shuka pale kitandani na kulifunga pamoja na vile vitu bila hata ya kuvishika, na kuviweka ndani ya kabati. kisha nikalifunga kabati na ufunguo. Baada ya hapo nilichukua shuka lingine na kutandika pale kitandani. Nilikuwa na hofu nyingi sana kwani siku hiyo sikuwa na amani hata kidogo. Baadaye nilienda sebuleni na kula  chakula cha usiku pamoja na Mama Bilionea. Nilikuwa  nikijikaza sana asielewe chochote. Haraka baada ya kumaliza chakula nilimuaga  Mama Bilionea kuwa nakwenda kupumzika.

Jumatatu, Mei 13, 2013

SIMULIZI ....BADO MIMI ....SURA YA .........12..........

 ILIPOISHIA
Baadaye nilipitiwa na usingi, nikiwa nimelala niliota ndoto ya ajabu sana. Nilikuwa namuona Baba yangu akiniita "Mwanangu Kandida njoo, niokoe, njoo niokoe,,usiniache huku shimoni, toka huko ulipo njoo nateseka sana" Ilikuwa ni sauti ya Baba nikiisikia nikiwa ndotoni" Wakati nikiwa najaribu kumsogelea Baba niliona kitambaa chekundu kikimwaga damu. Wakati wote huo ilikuwa ni ndoto nilishtuka sana na kuita kwa nguvu "Baba, Babaaaaaa" Mama Bilionea alishtuka na kuja chumbani kwangu kwani sauti yangu ilikuwa kali sana.............NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA .....12,,.........

INAPOENDELEA
 Nilikuwa natetemeka kama mtu aliyekuwa anahisi baridi kali, huku jasho likinibubujika kwa wingi mithili ya maji yakitiririka usoni. Mama Bilionea aligonga mlango wa chumbani kwangu "Kuna nini wewe Kandida, mbona unapiga kelele usiku  wa manane?" Nilinyanyuka haraka kitandani nakuelekea kufungua mlango "Mama nilikuwa naota ndoto mbaya sana, hapa nilipo naogopa hata kulala peke yangu." Mama Bilionea aliingia chumbani na kuketi kitandani kwangu "Inamaana ndoto ndiyo inakufanya upige kelele kiasi hicho?Ni ndoto gani hiyo?"

 Aliuliza Mama Bilionea huku akiwa ananitizama "Nimeota Baba yangu ananiita nimsaidie lakini ......"Mama Bilionea alikuwa amenikazia macho kabla sijamaliza kuzungumza akasema "Unajua wewe mtoto una mambo ya ajabu sana, ule mkufu niliokupa uuvae  uko wapi? na mbona haujauvaa?" Nilishangaa kumuona Mama Bilionea akiwa mkali kidogo huku akinisisitiza nivae mkufu wa dhahabu alionipa. "Mkufu nimeuweka kwenye kabati kwani sikuona kama ni vyema nikilala huku nikiwa nimeuvaa".

Mama Bilionea alifungua kabati na kunitaka nivae ule mkufu niliuchukua na kuuvaa "Sikiliza nikuambie Kandida huo mkufu ni zawadi nzuri sana kwani utakusaidia usiote tena ndoto za ajabu. Hakikisha unauvaa wakati wote, tizama mimi nimevaa mkufu huu unafanana na wako unanisaidia sana,  ukinisikiliza utaishi vizuri sana lakini tatizo watoto wa siku hizi mkiambiwa mfanye jambo fulani haufanyi ila unafanya vile unavyotaka wewe. Hakikisha huo mkufu unauvaa na usiutoe hata siku moja nadhani tumeelewana." Alinisisitiza Mama Bilionea huku nikiwa namsikiliza kwa umakini "Sawa Mama nimekuelewa, naomba unisamehe kwani sikujua kama huu mkufu natakiwa niuvae hata wakati wakulala, na tena kama utanisaidia nisiote ndoto za ajabu, nakuahidi siwezi kuuvua kamwe." Mama Bilionea alinisihi nilale kwani ilikuwa ni saa nane za usiku. 

Baada ya kuvaa ule mkufu nilijisikia tofauti kwani sikuwa na hofu yoyote nilipanda kitandani na kulala mpaka asubuhi kulipambazuka. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kwangu kwani ni siku ambayo Mama Bilionea angenipeleka katika Duka langu ambalo nilikuwa na hamu sana ya kwenda kuliona.Nilifanya kazi ndogo ndogo za pale nyumbani na baadaye Mama Bilionea alinipeleka dukani kwangu maeneo ya Mwenge karibu na kituo cha daladala. 

Lilikuwa ni duka kubwa sana kuliko nilivyotarajia kwani kwa wakati wote nilifikiri lingekuwa duka dogo. Duka lilikuwa na vipodozi vya aina mbalimbali pamoja na wafanyakazi wanne. Mama Bilionea alinitambulisha "Vijana leo nimemleta bosi wenu ili mfahamiane" Mmoja kati ya wale vijana alinitizama na kusema "Karibu sana bosi tumefurahi kukufahamu mimi naitwa John". Alijitambulisha yule kijana "Asante sana John usijali tutashirikiana pamoja, nawategemea sana katika kuimarisha hii biashara."

Jumatatu, Aprili 29, 2013

SIMULIZI .....BADO MIMI ........SURA YA ....8.......


ILIPOISHIA:
Kilikuwa ni chumba kizuri sana, ilinibidi nianze kufundishwa kutumia kila kitu kwasababu nilikuwa sijui chochote, lakini Mama Bilionea alinionyesha upendo wa hali ya juu kwani hata kazi niliyokuwa natakiwa kuifanya sikuiona muda mwingi nilikuwa nikiangalia video, niliishi kama mtoto wake wa kumzaa na alikuwa akinipa pesa nyingi sana.JE NINI KINAENDELEA ....USIKOSE SURA YA ....8...

INAPOENDELEA
Baada ya mwezi mmoja nikiwa naendelea kuishi na Mama Bilionea. Maisha yangu yalibadilika kwani nilikuwa sina matatizo yoyote. Ijapokuwa tatizo kubwa lilokuwa moyoni mwangu  ni kuhusu Mama yangu kwenda kutibiwa India, na Baba yangu aachiwe huru  kutoka gerezani.Siku moja nilikuwa nimejipumzisha sebuleni huku nikiwa nazungumza na nafsi yangu "Maisha yangu yana msalaba mzito sana, hapa nilipo naishi maisha ya kifahari lakini sijui nini hatima ya Mama yangu na hata Baba yangu. Kama ikiwezekana Mama Bilionea angenikopesha kiasi cha pesa ili nimpeleke Mama India akatibiwe. Halafu mimi nitamfanyia kazi zake bila  ya kunilipa chochote sijui atakubali?" Nilikuwa nikiwaza nakujiuliza maswali mengi sana bila ya kupata majibu.

Mama Bilionea alifika muda huo akiwa anatokea katika shughuli zake za kila siku. "Haujambo Kandida, habari za hapa nyumbani" Ilikuwa ni sauti ya Mama Bilionea ambayo nilihisi kuisikia kwa mbali lakini kutokana na mawazo niliyokuwa nayo nilikuwa kimya kana kwamba sikumsikia akinisalimia "Wewe mtoto, unawaza nini? Mbona nakusalimia umekaa kimya?" Mama Bilionea alizungumza kwa sauti kali kidogo "Shikamoo Mama, samahani nilikuwa sijakusikia, nilipitiwa kidogo Mama" Nilinyanyuka huku nikiwa naongea kwa sauti iliyo na kigugumizi".

 Mama Bilionea alinisihi niketi "Una matatizo gani, si nilishakuambia kama kuna tatizo lolote usisite kuniambia".Baada ya Mama Bilionea kuniambia nimueleze matatizo niliyonayo, niliamua kumueleza kila kitu kwamba nahitaji anisaidie kiasi cha pesa kwaajili ya matibabu ya Mama na siku zote nitaendelea kufanya kazi katika nyumba yake bila malipo. "Kandida mwanangu usijali kuhusu hali ya Mama yako mimi nitakusaidia" nilijihisi kupata faraja moyoni mwangu "Asante sana Mama Mungu atakuzidishia.

Alhamisi, Aprili 25, 2013

SIMULIZI .....BADO MIMI.......SURA YA .....7.....



 ILIPOISHIA:Wakati wote nilikuwa namsikiliza Daktari kwa umakini nilihisi kama kuchanganyikiwa, baada ya kusikia alichokisema Daktari "Eti India, Mungu wangu haiwezekani jamani nani atatusaidia pesa za kumpeleka Mama India" Mama Bilionea alinisihi nitulie kwanza kwasababu nilikuwa kama nimechanganyikiwa. Baadaye Daktari alitupatia dawa nyingi sana na kusema kuwa zitamsaidia Mama kutuliza maumivu lakini inabidi ipatikane pesa kiasi cha shilingi milioni tisa, ili Mama akafanyiwe upasuaji India. Je Mama Bilionea atamsaidia Kandida?.Usikose SURA YA.......7..........

INAPOENDELEA
Nilikuwa katika wakati mgumu sana, kwasababu sikujua nini hatima ya maisha ya familia yangu. "Baba yangu yupo anatumikia kifungo Gerezani, Mama anaumwa, Kinahitajika kiasi cha shilingi milioni tisa ili akafanyiwe upasuaji India. Mimi bado ni msichana mdogo nikijiangalia nina majukumu ya kulea familia sielewi nini kitatokea katika maisha yangu. Na kama nisingekutana na Mama Bilionea Mama yangu si angekufa pale nyumbani" Niliwaza sana na machozi yalikuwa yakinibubujika bila kuisha ijapokuwa Mama Bilionea alijitahidi kunibembeleza.

Baadaye Daktari alituruhusu tuondoke na Mama kwani zile dawa alizompa zilimsaidia kutuliza maumivu makali aliyokuwa akiyasikia. Hali yake ilionekana kuwa njema, lakini sasa alikuwa ni mtumwa wa dawa, kwani kila siku alitakiwa kumeza dawa hizo kwaajili ya kutuliza maumivu. Dawa hizo zilikuwa zinauzwa kwa gharama kubwa kama asingekuwepo Mama Bilionea nisingeweza kuzinunua. Kila wiki alitakiwa kununua dawa za shilingi laki moja.Mama Bilionea alinunua dawa za mwezi mzima nilimshukuru sana kwa moyo wake wa kujitolea.Mama aliendelea kutumia dawa ijapokuwa Daktari alitusisitiza itafutwe hela haraka Mama akafanyiwe upasuaji kwani   baadaye tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi.

Tukiwa nyumbani Mama alikuwa katika hali ya kawaida kwani zile dawa zilimsaidia sana, na kwa wakati wote huo hakutaka Baba afahamu chochote kuhusu hali yake.Ikiwa imepita wiki moja tokea Mama atoke Hospitalini, Mama Bilionea alikuja nyumbani kutujulia hali, tulifurahi sana kwani alikuwa ni mtu wa muhimu sana kwetu. "Karibu Mama Bilionea karibu sana" Mama alimkaribisha na waliketi pamoja kwenye mkeka huku mimi nikiwa jikoni naandaa chakula.Baadaye Mama Bilionea alimwambia Mama kuwa,  anichukue mimi nikamsaidie kazi za nyumbani kwake na atakuwa ananilipa mshahara mzuri. Mama alishukuru sana "Sijui hata nikushukuru vipi umetusaidia sana, nakushukuru sana Mungu atakuzidishia" Ilikuwa ni sauti ya Mama ambaye aliongea kwa furaha.

Alhamisi, Aprili 18, 2013

SIMULIZI ...BADO MIMI..... SURA YA ....5.......



ILIPOISHIA:
Maisha yaliendela hali ya Mama ilikuwa ni njema aliweza kuandaa chakula na kumpelekea Baba gerezani mara kwa mara. Kwa upande wangu nilikuwa nimekaa nyumbani kwa kipindi kirefu bila kwenda shule.Kutokana na hali ya pale nyumbani Mama aliniambia  hawezi kunilipia ada ya shule kwahiyo ilinibidi nibaki nyumbani , ijapokuwa nilitamani sana kusoma lakini kutokana na hali halisi ya maisha ya pale nyumbani sikuwa na namna nyingine yoyote.Nini kitaendelea usikose sura ya ......5..........

INAPOENDELEA
Katika maisha yangu nilitamani sana na mimi ningeendelea  na Shule. Nilijaribu kuwasiliana na shangazi yangu ili aweze kunisaidia. Lakini ilishindikana kwani aliniiambia anayo majukumu ya kuwasomesha watoto wake. Ilinibidi nikubaliane na hali halisi ya maisha kwamba sintoendelea tena na masomo, na elimu yangu ya sekondari ndiyo imeishia kidato cha pili.Nikiwa nyumbani nilianza kumsaidia Mama katika biashara ya kuuza mbogamboga na matunda, nilikuwa nikiamka asubuhi na mapema na kwenda kufanya biashara.

Katika kufanya biashara hii ya kuuza matunda, nilijuana na watu mbalimbali kwasababu nilikuwa nikiwauzia matunda watu katika maeneo mbalimbali. Siku moja nikiwa njiani nauza matunda  ambapo kulikuwa na mvua  ikinyesha, huku maji yakiwa yamejaa kwenye madimbwi ya barabarani. Lilipita gari moja aina ya Vitara na dereva aliyekuwa anaendesha alikuwa akiendesha kwa kasi sana.Gari lilipita kwa mwendo kasi wa ajabu, karibu  na miguu yangu,  Kulikuwa na shimo dogo lililojaa maji yale maji yalinirukia na kunichafua nguo zangu zote.

 Kutokana mshtuko matunda yangu yote yalimwagika na kuingia katika dimbwi la maji, nilihuzunika sana. "Mama yangu! nini tena hiki, inamaana huyu dereva hanioni hadi kanimwagia maji kiasi hiki, nitafanya nini mimi matunda yote yamemwagika sijui nitamueleza nini Mama " Nilijikuta machozi yakinitoka huku nikiinama kuokota matunda niliyodondosha katika maji yale machafu.Lile gari liliondoka bila hata ya kusimama.

Jumapili, Aprili 07, 2013

SIMULIZI YA .....BADO MIMI.... SURA YA ....4.......


ILIPOISHIA
Nilipofika nyumbani niliwakuta wadogo zangu wakiwa wamekaa nje, Renata ambaye alikuwa darasa la tatu na Tumaini alikuwa darasa la kwanza. Waliponiona walinikimbilia huku wanalia “Dada Kandida,, Dada Kandida Baba , baba, baba”Alikuwa akilia Renata huku akinivuta katika gauni langu nilishindwa kuelewa Baba amepatwa na kitu gani? “Renata Baba yuko wapi? Mnalia nini? Baba amefanyaje” Nilimuuliza mdogo wangu wa kike “Baba amechukuliwa na watu, wamempiga Baba”

INAPOENDELEA

Baba amechukuliwa na watu, wamempiga Baba” Alinijibu kwa sauti yenye  kigugumizi, Nilihisi kuchanganyikiwa kwani sikuamini kile alichokuwa anakisema mdogo wangu. Nilikimbia na kuelekea kwa Mama Keku kabla hata sijafika Mama Keku aliniita “Kandida nipo huku njoo” alikuwa ameketi jikoni kwake akiandaa chakula. Nilisogea huku nikiwa na shauku la  kutaka kujua Baba yangu ameenda wapi?"
 Karibu uketi mwanangu, aliongea Mama Keku huku mimi nikiwa namuangalia "Mama Keku Baba yangu amepatwa na kitu gani?" Mama Keku alijaribu kuniliwaza na baadaye akaamua kunieleza hali halisi ya kile kilichotokea.

 “Kandida wewe ni msichana mkubwa, fikiria Mama yako na wadogo zako wanakutegemea wewe. Baba yako amepelekwa Polisi” akiwa anaendelea kuongea yale maneno nilihisi kama yananichanganya kichwa changu kabisa. “Ati unasema Baba yangu amepelekwa Polisi, amefanya nini? Baba yangu eeh Mungu balaa gani hili jamani mbona tunateseka hivi” Nijikuta nimekaa chini huku nikilia kwa sauti  Mama Keku alijitahidi sana kunibembeleza lakini sikutaka kumsikia.Niliamua kuchukua maamuzi ya haraka na kwenda hadi kituo cha polisi.

“Wewe binti una matatizo gani? Unalia nini?” Ilikuwa ni sauti ya Askari ambaye nilimkuta pale kwenye mapokezi ya kituo cha polisi “Namtaka Baba yangu jamani, namtaka Baba yangu” Yule askari akaniuliza “Binti sasa unavyolia sikuelewi unamtaka Baba yako yuko wapi? ametekwa? au amefanyaje” Nilikuwa nalia kwa uchungu “Baba yangu amekamatwa na Polisi, na Mama yangu amelazwa hospitalini sisi tutabaki na nani? Namtaka Baba yangu” Kulikuwa na askari mwingine kwa pembeni ambaye alikuwa ni mwanamke alinichukua na kuanza kunibembeleza huku akinisihi ninyamaze na kumuelezea taratibu. 

Jumanne, Aprili 02, 2013

SIMULIZI TAMU YA KUSISIMUA..... BADO MIMI ......SURA YA ....3......



 ILIPOISHIA:
Niliondoka pale Hospitalini huku machozi yakinibubujika kwa wingi,  nilifika nyumbani nikiwa nimechoka sana lakini Baba alikuwa bado hajarudi kutoka kazini. Baada ya muda alirudi hali aliyokuwa nayo ilinishangaza kwani alionekana mtu mwenye wasiwasi  sana. Moyoni mwangu mimi nilichokuwa nakiwaza  ni je! Baba atakuwa amefanikiwa kupata hela kwa ajili ya matibabu ya Mama niliamua kumuuliza “Baba umefanikiwa kupata chochote? Kwani nimetoka hospitalini  kumpelekea Mama chakula hali ya Mama….”

INAPOENDELEA  
Kabla sijamalizia kuzungumza Baba alinikatisha “Usijali mwanangu nimepata pesa  za matibabu, kesho asubuhi na mapema tutakwenda  pamoja hospitalini” Naomba  uniwekee maji bafuni nikakoge, kwani  nimechoka sana” Moyoni mwangu nilijisikia faraja,  baada ya Baba kusema amepata pesa wa ajili ya matibabu ya Mama. Nilinyanyuka haraka na kwenda  kumuwekea Baba  maji bafuni. Wakati Baba akiwa amekwenda kuoga mimi  niliingia jikoni nikachukua chakula na kumuandalia  mezani.

  Nilikuwa najisikia amani moyoni  mwangu nilijua sasa Mama yangu atafanyiwa upasuaji, na haliyake itakuwa nzuri na mimi nitaendelea kwenda shule kama kawaida. Kwani tokea Mama alipoanza kuumwa, na kuzidiwa ghafla, nilishindwa kwenda shule. Kwasababu  kulikuwa hakuna mtu mwingine wa kumuhudumia. Baadaye Baba alikula chakula na  alikwenda  kupumzika .Usiku huo sikupata usingizi kabisa  nilitamani kupambazuke ili niwahi kwenda Hospitalini.

Nilizungumza na nafsi yangu “Mama akipona nitafurahi sana, eeh Mungu msaidie Mama apone tunamuhitaji sana, wadogo zangu wamekuwa wakilia kila kukicha kwasababu hawamuoni Mama, na mimi nashindwa kuwaeleza ukweli kuhusu hali ya Mama.Naomba umsaidie Mungu wangu” Baadaye nilipitiwa na usingizi na kulala fofofo.

Kesho yake asubuhi na mapema Baba aliamka na kuja kuniamsha tuanze safari ya kwenda hospitalini.  Niliamka na kuanza kujiandaa, nilibandika chai jikoni na kuwawekea wadogo zangu ambapo wakiamka wangekunywa chai  kwanza na kwenda shule. 

Baada ya kumaliza shughuli mbili tatu ambazo nilikuwa nazifanya sasa nilikuwa tayari  kwa kwenda Hospitalini. Baba alichukua mkoba wake na tukaanza kuondoka, kabla ya kutoka mlangoni alisikika mtu akibisha hodi, huku kukiwa na kama malumbano yanaendelea huko nje. Nilitaka kufungua mlango Baba alinikataza na kunishika mkono kwa nguvu nisifungue mlango. “Mwanangu sikiliza nikuambie, chukua huu mkoba ndani kuna kiasi cha shilingi milioni nne na nusu, Shikilia kwa umakini mwanangu. Chukua taksi  nenda hospitalini utampa Daktari milioni nne kwaajili ya matibabu  ya Mama yako.Kiasi cha pesa kitakachobakia  kitawasaidia hapa nyumbani”.

Jumanne, Machi 26, 2013

SIMULIZI YA KUSISIMUA,,, BADO MIMI SURA YA .......1......

“Napata  maumivu makali sana jamani naombeni mnisaidie nateseka sana eeh Mungu wangu” ilikuwa ni sauti ya  Mama kutoka chumbani niliinuka na kukimbilia ndani huku nikimwangalia Mama kwa huzuni kutokana na maumivu ya tumbo aliyokuwa akiyasikia nilisogea karibu “Pole mama twende nikupeleke Hospitali” Alijivuta kidogo na kuinua uso wake huku akinitazama “Mwanangu baba yako yuko wapi”  Nilimshika mama mkono “Baba ametoka ameenda kazini”.

 Kutokana na hali aliyokuwa nayo Mama nilitamani kumsaidia lakini sikuwa na namna kwani maumivu aliyokuwa anayapata yalikuwa makali sana “Kandida mwanangu naomba umtafute Baba yako anipeleke hospitalini” Baba yangu alikuwa ni mfanyakazi katika kiwanda cha plastiki na Mama alikuwa hana kazi nikiwa ni mtoto wa kwanza katika familia yetu na wadogo zangu wawili ambao wote walikuwa wakisoma shule ya msingi wakati huo mimi nilikuwa kidato cha pili pale nyumbani hakukuwa na mtu yeyote zaidi yangu na Mama alikuwa ni mgonjwa, hali ya mama yangu ilizidi kuwa mbaya ikanibidi nikimbie kwenda kumuita jirani yetu anayeitwa  Mama Keku.

“Mama keku ,Mama keku” Niliita kwa sauti kubwa iliyojaa wasiwasi mwingi “hee kuna nini Kandida  mbona  unaita kwa sauti kali hivyo” Alinijibu mama keku  huku akitoka chumbani kwake wakati huo machozi yalikuwa yakinibubujika kwa wingi “Mama yangu anaumwa, Mama yangu anakufa jamani naomba uje umsaidie tumpeleke hospitali” Niliongea kama nimechanganyikiwa. 

“Sasa mbona sikuelewi,  inamaana amezidiwa yuko na nani nyumbani? Embu twende haraka ukilia haisadii chochote” Tuliondoka haraka nyumbani kwa Mama Keku na kuelekea chumbani kwa mama yangu safari hii tulimkuta Mama akiwa kimya huku macho yakiwa yamemjaa machozi na hata tulipomuita hakuzungumza lolote “Mama yangu jamani Mama uwiiiiiii nisaidie mimi Mama yangu” Nililia kwa uchungu nikijua Mama yangu atakuwa amefariki Mama Keku alitoka nje haraka kwaajili ya kwenda kutafuta usafiri wa kumpeleka Mama hospitali .

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom