Pages

Alhamisi, Julai 04, 2013

SIMULIZI... BADO MIMI...... SEHEMU YA .....26......... ILIPOISHIA
Ilikuwa ni ndoto ya kutisha ghafla nilishtuka kutoka usingizini baada ya mdogo wangu Renata kuniamsha "Dada, simu yako inaita muda mrefu, umelala"Nilishtuka nakujitizama mikono yangu kama ilikuwa na damu, lakini haikuwa na damu yoyote "Mungu wangu hii ni ndoto mbaya sana" Nilikuwa na hofu kubwa huku jasho likinitoka kwa wingi ilikuwa tayari ni majira ya saa moja asubuhi" JE NINI KITAENDELEA....USIKOSE SURA YA.......26......... 

INAPOENDELEA
Ghafla simu iliita kwa mara ya pili. Nilishtuka kwasababu nilikuwa nawaza ile ndoto je itakuwa inamaanisha kitu gani? Renata alinipa simu nami nikaipokea, alikuwa ni Charito "Mambo vipi, inamaana umelala hadi muda huu? Mbona nimepiga simu imeita muda mrefu hivyo?" Alilalamika Charito, na mimi kwa sauti ya unyonge nikasema "Nilikuwa nimepitiwa na usingizi mzito sana, samahani mpenzi" Charito alicheka kidogo nakusema "Angalia tu usije ukasahau na muda wa kwenda kanisani, tafadhali naomba ujiandae mapema" Alisistiza Charito."Usiwe na wasiwasi mpenzi, siwezi kusahau jamani". Baadaye nilinyanyuka pale kitandani huku viungo vya mwili wangu vikiwa vinaniuma sana kutokana na uchovu. Nilianza kwa kufanya mazoezi madogo ya kunyoosha viungo kwa kuruka kamba na baadaye nilienda kukoga na kujiandaa kwaajili ya kwenda saluni.

        Hatimaye muda wa kwenda kanisani ulifika, Lilikuja  gari la kifahari kunichukua. Kabla sijaenda kupanda lile gari mdogo wangu Renata alikuja chumbani na kusimama mlangoni huku akinitizama na kusema "Lakini dada kwanini unakubali kuolewa na Charito?" Nilimtizama na kusema "Hivi wewe Renata una matatizo gani? Unajua leo ni siku yangu ya muhimu sana lakini unataka kunipotezea furaha yangu kwa maneno yako yasiyokuwa na kichwa wala miguu,Embu nenda kamchukue Tumaini tuondoke  kwani tunachelewa kanisani." Renata aliondoka huku akiwa amekunja sura kwa hasira. Nilitoka nje huku nikiwa na majirani zangu na baadhi ya akina dada ambao walikuwa wasimamizi katika harusi yangu.


 Tukiwa tunaelekea kanisani mawazo ya ile ndoto yalinijia nikawa nazungumza na nafsi yangu "Yaani ile ndoto ni ya kutisha sana, sijui inamaanisha kitu gani?Au Mama Bilionea anaendelea kuwatesa wazazi wangu" Nilikuwa nawaza huku nikimuomba  Mungu anisaidie nisahau.Baadaye tulifika Kanisani  watu walikuwa wengi sana walikuwa wamependeza na  rangi ya njano ambayo ndiyo ilikuwa ni rangi ya sare ya harusi. Baada ya muda kama wa dakika tano  Charito  alifika alikuwa amependeza sana  na suti aliyokuwa ameivaa, nilimtizama  na kuonyesha tabasamu pana katika paji la uso wangu.

Baadaye kidogo wote tuliingia kanisani na  mchungaji aliingia na sasa tulikuwa tayari kwaajili ya kufunga pingu za maisha.Moyoni mwangu nilikuwa na furaha sana,  muda wa pete ulifika Charito alianza kunivalisha mimi "Mwenzangu pokea pete hii, iwe ishara ya mapendo yangu kwako mpaka kifo kitakapotutenganisha." Alisema Charito huku akionekana kutabasamu na kunitizama kwa macho yaliyoonyesha kuwa nahisia kali za mapendo. Baada ya Charito kumaliza mchungaji aligeuka upande wangu nakunipa  pete na kisha alinitaka  niseme maneno yale aliyosema Charito. Wakati nikiwa nimeishika ile pete, nilikuwa nahisi kutetemeka na hofu ilinijia, nilikuwa kimya bila ya kusema chochote.

 Niligeuka huku na kule huku kijasho chembamba kikiwa kinanitoka kwenye paji la uso. Nilipotizama upande wa mlango wa kanisa  kwa mbali nilimuona Mama bilionea akiwa amevalia gauni la rangi nyekundu, huku akionekana kutabasamu. Nilihisi labda nilikuwa sioni vizuri ilinibidi nianze kuyafikicha macho yangu huku nikitizama kwa umakini zaidi. Wakati nikiwa naendelea kushangaa Charito alisemesha "Kandida vipi, mbona kama una wasiwasi mpenzi" Nilikuwa natizama pale mlangoni, niliogopa sana. Huku nikiwa kama nimepigwa na butwaa ghafla sikumuona tena Mama Bilionea.

Niliwaza moyoni mwangu "Eeeh Mungu ni kweli nimemuona Mama Bilionea au ni macho yangu yananidanganya?" Hapana embu nijikaze kwani hawa watu wote hapa kanisani wanaweza kuhisi labda nimekuwa kichaa"Nilikuwa nimeishika ile pete mkononi huku nikitetemeka na sauti ilikuwa imejaa kigugumizi nilitamka yale maneno na kumvisha pete Charito.

Kwani kwa muda mchache watu wote walikuwa wananitazama wakisubiri nimvishe pete Charito. Baada ya kumvisha pete nilijikuta machozi yakinibubujika huku nikijiuliza  "Kwanini hii hali imenitokea muda huu,kwani nilikuwa najisikia vibaya sana huku nikiwa na wasiwasi mwingi. Vifijo na nderemo vilitawala baada ya kuvishana pete watu waliimba kwa furaha "Anameremeta, anameremeta, Charito anameremeta, anameremeta na  Kandida anameremeta, anameremeta" Watu walikuwa wakiimba kwa furaha na baadaye tulielekea katika tafrija fupi iliyofanyika katika ukumbi uliokuwepo palepale kanisani. Tukiwa katika sherehe nilikuwa katika hali ya kawaida tulifurahi kwa pamoja.

        Baada ya wiki mbili kupita tokea tufunge pingu za maisha tuliikuwa tunaishi maisha ya amani na upendo. Na sasa nilikuwa nimehamia katika ile nyumba ya Mama Bilionea na kuishi pamoja na Charito.Sikuwa na wasiwasi kwani nilikuwa nikimuamini Mungu wangu.Maisha yaliendelea siku moja ambapo  ilikuwa  ni siku ya jumatano usiku tukiwa tumelala,  niliota ndoto ya kutisha  sana. Nilikuwa nikihisi kuwa nimelala na nyoka mkubwa kwakukadiria alikuwa na ukubwa  kama  wa chatu. Huku nikiwa natetemeka nakutaka kukimbia pembeni nikamwona Mama Bilionea akiwa na yule nyoka.  Nililia kwa uchungu sana huku nikisema  "Mama bilionea, kwanini unanitesa jamani nimechoka niache niwe huru na maisha yangu. Mama Bilionea alicheka kwa sauti ya ajabu. Ghafla nilishtuka kutoka usingizini  huku mwili wote ukiwa umelowa kwa jasho mithili ya mtu aliyekuwa amemwagiwa maji. 

Niligeuka na kutizama pembeni yangu huku nikiwa na wasiwasi, kwa mbali nilisikia sauti ya mdogo wangu Renata akipiga yowe. "Mama nakufa, Mama nakufa, nisaidie jamani, nisaidieeeeeee" Ilikuwa ni sauti ya Renata. Niliogopa sana , nilinyanyuka pale kitandani huku nikimuamsha mume wangu  aliamka  haraka tukaenda hadi chumbani kwa Renata. Mdogo wangu aliniponiona,  alinikumbatia  kwa nguvu huku akiwa analia. "Dada Kandida, mimi naogopa, siwezi kulala mwenyewe, nimemuona nyoka, dada naogopa" Nilimshika  mikono huku nikimbembeleza kwasababu alikuwa na hofu sana nilimchukua na kwenda naye sebuleni kisha nikamuuliza taratibu. Kilichonishangaza Renata alinisimulia ndoto aliyokuwa anaiota ilikuwa inafanana vilevile na ndoto ya kutisha niliyokuwa nikiota.Nikiwa na hofu kubwa  na wasiwasi Charito alinitizama na kusema "Usiwe na wasiwasi mke wangu, haya ni majaribu ya shetani, kuwa na imani na Mungu kila kitu kitaenda sawa , usogope chochote kwani shetani atashindwa kwa nguvu zake Mungu". JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE ....SURA YA ........27.........

Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

Uwiiiiiiii usinambie kaolewa na lichatu?htakuja kumkumbuka mdgo wake mna libishi sana.

Bila jina alisema ...

Acyeckia la mdogo mbelen majuto na mdharau mwiba humchoma. akome kutoshaurika

Bila jina alisema ...

jamani angemsikiliza mdogo wake tu ayo yote yasingetokea

Bila jina alisema ...

jamani angemsikiliza mdogo wake tu ayo yote yasingetokea

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom