Pages

Jumatatu, Juni 24, 2013

SIMULIZI YA ..BADO MIMI.....SURA YA ,.......24......

 
 ILIPOISHIA
Pale kitandani nilikuwa nimelala na mdogo wangu Renata alishtuka kutoka usingizini na kunitizama huku akifikicha macho yake na kusema "Dada Kandida, mimi naogopa, naogopa Dada Kandida" Nilimshika mikono kwani alikuwa akitetemeka sana na kumuuliza "Unaogopa nini Renata? Mimi nipo na wewe" Renata alianza kulia na kusema "Kuna mtu anataka kunichoma na kisu, umemuona Dada" Nilijua Renata alikuwa ameota ndoto mbaya nilianza kumbembeleza ili apate usingizi.JE NINI KITAENDELEA ....USIKOSE ...SURA ...YA.... 24.....
 
INAPOENDELEA
Nilikuwa nambembeleza Renata pale kitandani, baadaye usingizi ulimpitia nakulala fofofo.Ilipofika asubuhi niliamka na kwenda kuandaa kifungua kinywa. Wakati huo Renata alikuwa bado amelala, nilipoona muda unazidi kwenda ilinibidi niende kumuamsha "Renata,Renata, umesahau kuwa huu ni muda wa kwenda shule? Embu nyanyuka hapo kitandani  haraka ujiandae." Huku akiwa anajivuta taratibu kwa sauti ya unyonge akasema "Dada mimi kichwa kinaniuma" Nilihisi labda ameanza uvivu, lakini haikuwa tabia ya Renata kukataa kwenda shule.Nilisogea karibu na kumshika kwenye mwili  wake alikuwa na joto kali sana. 
 
Baada ya kuona ile hali ikanibidi nifanye haraka ili nimpeleke Hospitali. "Renata atakuwa anaumwa Malaria, sasa itabidi nimpeleke hospitalini haraka, kwasababu kama itakuwa ni Malaria itabidi apatiwe matibabu haraka kwani huu ugonjwa huwa ni hatari sana" Niljianda haraka na kumuandaa Renata kisha nikampeleka katika zahanati iliyokuwepo maeneo ya pale nyumbani.
 
Baada ya Daktari kumpima kweli aligundulika anayo Malaria. "Umefanya vyema kumleta mtoto Hospitali mapema, baada ya kugundua tu atakuwa na dalili za Malaria. Kwani inakuwa rahisi zaidi katika matibabu" Alisema Daktari. Tulipewa dawa  na kuruhusiwa, kwahiyo Renata alianza dozi ya dawa za Malaria. Baada ya siku mbili tatu Renata hali yake ikiwa inaendelea kuwa nzuri kiafya. Charito alikuja nyumbani akiwa pamoja na mchungaji kuja kumjulia hali mgonjwa.
 
Tulikuwa tumeketi pamoja pale sebuleni na Renata alikuwa chumbani amepumzika. Charito akasema "Kandida, naweza kwenda chumbani kumuona Renata?" Huku nikionyesha tabasamu pana nikasema "Bila shaka, Charito ingia tu mlango wa kushoto" Charito alinyanyuka na kuelekea chumbani kwa Renata.

Tukiwa pale Sebuleni  mchungaji akasema "Pole sana kwa kuuguza Kandida, lakini ni vyema kufanya maombi kila wakati msijisahau kumshirikisha Mungu katika kila jambo" Nilikuwa namsikiliza mchungaji kwa umakini  "Ni kweli mchungaji, kwani kwa takribani kama siku mbli tatu nimekuwa nikiota ndoto za kutisha sana....na " 
 Nikiwa naendelea kuzungumza Mchungaji alinikatisha na kusema .
 
"Unapoota ndoto mbaya, fahamu kuwa hayo ni majaribu, unachotakiwa kufanya ni maombi na kila kitu kitaenda salama" Tuliendelea na mazungumzo wakati huo Charito alikuwa chumbani na Renata. Baada ya muda kidogo nilinyanyuka na kwenda kuwatizama. Nilipofika nilimkuta Renata akiwa amelala na Charito alikuwa ameketi kwa pembeni akimtizama. " Jamani huyu mtoto leo amelala muda mrefu nahisi hizi dawa zinamchosha sana" Charito alitabasamu na kusema "Usijali Kandida hali ya Renata itakuwa salama" Tukiwa  tunazungumza Renata alishtuka kutoka usingizini huku  akimtizama Charito kwa umakini. 

Nilimtizama alionekana kuchoka sana, huku macho yakionekana  kulegea mithili ya mtu aliyekula kungu. "Renata, vipi hali yako, wageni wamekuja kukujulia hali" Alinyanyuka na kuketi kitandani huku akimtizama Charito bila kutoa macho yake, ilinibidi nishangae na kusema "Wewe, Renata mbona unamuangalia Charito, kama vile haumjui, tena haujamsalimia" Kwa sauti ya kigugumizi akamsalimia Charito "Shikamoo shemeji...halafu dada,,,,mbona..." Kabla hajazungumza chochote Charito alimkatisha na kusema "Renata tumekuletea zawadi, biskuti, matunda  pamoja na juisi, unatakiwa kula sana matunda lakini pia usilale sana, inabidi uwe unafanya mazoezi." Nilimtizama Charito huku nikitabasamu na kusema "Asante sana Charito, inaonekana unaweza kweli kumtunza mgonjwa".

Baadaye Charito na mchungaji waliondoka baada ya kumuona mgonjwa. Usiku tukiwa mezani tunakula chakula Renata alionekana kujiinamia chini bila ya kuzungumza chochote. Tumaini alimtizama na kusema "Mwambie dada Kandida." Nilijua kuna kitu anataka kuniambia nikamuuliza "Renata una matatizo gani? Embu niambie" Alinyamaza kimya bila ya kunijibu na kisha aliondoka na kuelekea chumbani huku akiwa analia sana.
 
 Niliogopa kuona ile hali, ikanibidi nimuulize Tumaini  "Kuna tatizo gani, Tumaini mbona Renata analia?" Tumaini akasema "Mimi ameniambia kuna mtu anataka kumuuwa, akilala usiku" Ilinibidi nishangae na kusema "Ati, unasemaje!hivi wewe Tumaini una akili kweli"Nilinyanyuka na kumfuata Renata alikuwa amejikunyata mithili ya mtu anayesikia baridi nikamsogelea karibu na kumuuliza "Eti kuna mtu anataka kukuuwa?Wewe unajua nini kuhusu kifo?Ile ilikuwa ni ndoto tu mdogo wangu".
 
 Renata kwa sauti ya kigugumizi akasema "Hapana dada, mimi nimemuona huyo mtu leo, amesema lazima atanichukua". Nikamuuliza "Huyo mtu ni nani?" Alikuwa akitizama huku na kule na kusema "Ni Mchungaji Mkombozi, amesema ataniuwa na huwa anakuja na kisu usiku" Nilikuwa kama nimepigwa na butwaa, nilihisi labda Renata Malaria inataka kumpanda kichwani na kusema  "Renata, hiyo ni ndoto tu, pamoja na majaribu ya shetani, usijali mdogo wangu." Aliendelea kulia ikanibidi niwe mkali kidogo ndipo alinyamaza na kwenda kuendelea kula chakula. Nilibaki nikiwaza na nafsi yangu "Inamaana huyu shetani, anataka kumfanya mdogo wangu achanganyikiwe hadi amuone mchungaji Mkombozi kuwa ni mtu mbaya, eeh Mungu naomba utusaidie". Je nini kitaendelea usikose sura ya ....25.....

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

uwiiiiiiiiiiiiii maskin,kumbe wale wachawi wameuvaa uchungaji jmn.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom