Pages

Jumatano, Mei 22, 2013

SIMULIZI.....BADO MIMI.... SURA YA .....15.......... ILIPOISHIA
Wewe Kandida mbona umeanza kuwa mtoto ambaye ni muongo?usiwe na tabia mbaya mwanangu si unajua Mama yako nakupenda sana, huwezi kwenda nyumbani usiku huu". Alinijibu Mama Bilionea. Huku nikiwa natafuta njia ya kutoroka nilisikia kitu kikinisukuma kwa kishindo kikali sana. Ghafla nilianguka chini na hata nilipoamka mazingira niliyoyaona yalikuwa tofauti kabisa.Mama Bilionea sikumuona tena ila kulikuwa na watu wengi sana katika hilo eneo. .......JE NINI KITAENDELEA USIKOSE SURA YA..........15.....

INAPOENDELEA
Nilitizama huku na kule, lakini sikumfahamu hata mtu mmoja katika lile eneo. Kulikuwa na watu wengi sana,kwa kukadiria ni zaidi ya watu wapatao mia tano. nilishindwa kuelewa imekuwaje nimefika eneo hili na tena katika mazingira ya ajabu. Ilikuwa ni sehemu ambayo hakuna nyumba hata moja zaidi ya miti huku kila mtu akionekana anafanya kazi zake wengine walikuwa wanaimba lakini sauti zao zilikuwa hazisikiki, na wengine walikuwa wakipepeta pumba katika nyungo kubwa.Nilimuona Mama mmoja akiwa ameketi pembeni yangu huku akiwa ameinama  kama kuna vitu anaokota pale chini."Huku ni wapi tena jamani?Mbona sielewi, na hawa watu wote wametokea wapi na mbona hakuna nyumba yoyote nikitizama naona miti, inamaana hawa watu wanalala juu ya miti?"

Nilikuwa najiuliza maswali mengi huku taratibu nikiwa najisogeza karibu na yule Mama aliyekuwa ameinama huku akiokota vitu ambavyo sikuvielewa ni vitu gani. "Shikamoo Mama, samahani nilikuwa naomba kuuliza hapa ni wapi?" Yule Mama alinitizama na kuendelea na kazi aliyokuwa akiifanya bila ya kunijibu chochote nilijitahidi kumuuliza lakini hakunijibu kabisa niliamua kusogea na kutafuta watu wengine ambao ningewauliza kwani nia yangu nilikuwa nataka kufahamu hapa nilipo ni wapi?Kila niliyekuwa namuuliza hakunijibu chochote, alinitizama na kuendelea na mambo yake.

Nikiwa naendelea kuzunguka huku na kule nilikutana na kijana mmoja ambaye alionekana kuwa tofauti na wengine, kabla hata sijamuuliza chochote alinitizama na kunisemesha "Wewe ni mgeni maeneo haya?" Huku nikiwa namtizama nilimjibu "Ndiyo,sielewi haya mazingira, nisaidie kaka yangu kwani hapa ni wapi?" Yule kaka akacheka "Hahahahaha umewezaje kufika huku ukiwa na uwezo wa kuongea, kwani wote unaowaona hapa ni watu waliokufa duniani, na pia hawazungumzi wala hawamtambui mtu yeyote au kusikia chochote zaidi ya kumsikiliza malkia pekee. Kwani wewe umetokea wapi?" Sikutaka kuamini kile alichokuwa anakisema yule kaka nilihisi kama nipo ndotoni "Mungu wangu, inamaana mimi nimekufa, Mama Bilionea amenitoa kafara?" Nikiwa nawaza yule kaka akaniuliza  tena "Wewe ni nani? Umetokea wapi?".


Huku nikiwa natetemeka kwa sauti iliyo nakigugumizi nikasema "Mimi nilikuwa nyumbani, nashangaa nimefikaje huku kwani hata Mama Bilionea simuoni na tulikuwa naye pamoja na......." Kabla hata sijamaliza kuongea yule kaka alinikatiza "Kumbe wewe ni Kandida, karibu sana, ndiyo maana umekuja ukiwa hai. Mimi naitwa Chande ni mtoto wa kwanza wa Mama Bilionea,nilikuja huku tokea nikiwa na umri wa mwaka mmoja"Bado nilikuwa sielewi kwani Mama Bilionea aliniambia hakubahatika kupata mtoto "Mtoto wa Mama Bilionea? Siamini jamani,inamaana wewe ulifikaje huku?" Nilimuuliza Chande "Siwezi kukumbuka kwani nilikuwa mdogo sana, na pia mambo mengine siwezi kukueleza kwani wewe bado uko hai na unaweza kurudi duniani na mambo yote ya humu huwa ni siri".

Baada ya Chande kuniambia kuwa mimi naweza kurudi duniani nikamuuliza "Ninawezaje kutoka katika hili eneo kwani hata njia ya kutokea siijui ilipo" hahahahahahahaha kilikuwa ni kicheko kutoka kwa Chande "Siyo rahisi kutoka humu ndani ya hekalu kama unavyofikiria, ni lazima ukubali masharti ya Bibi Bilionea ndipo atakuruhusu urudi duniani" Nilishindwa kuelewa "Masharti ya Bibi Bilionea? Yuko wapi huyo Bibi" nilimuuliza huku nikiwa na shauku la kumuona huyo Bibi ili anirudishe duniani, niliogopa sana yale mazingira na pia  nilikuwa naiwaza familia yangu, nilimuhofia Mama Bilionea kutokana na njama zake za kutaka kumtoa kafara Mama yangu.

Chande alinitizama na kusema "Bibi yupo mbali kidogo, inabidi tutembee hadi kwenye mkuyu wa Bibi, na leo siyo siku nzuri kwani tunaweza kukutana na wadudu wakakudhuru" Maneno yake yalizidi kunikatisha tamaa na kuniweka katika wakati mgumu sana kwani mimi nia yangu ilikuwa niweze kutoka katika lile eneo "Eee Mungu nisaidie nitoke huku kwenye hili shamba la misukule wa Mama Bilionea." Nilikuwa nawaza huku nikumuomba sana Mungu anisaidie "Inamaana Chande hakuna njia nyingine ya kwenda kwa Bibi Bilionea" 

Huku akinitizama akasema "Hakuna njia nyingine labda uwe umekufa itakuwa rahisi zaidi kumuona Bibi Bilionea" Nilizidi kuchanganyikiwa kwani maisha yangu yalikuwa hatarini. Tukiwa tunaendelea kuzungumza Chande akaniambia "Huu ni wakati wa kwenda kula, unaweza kujumuika pamoja na mimi" Moyoni mwangu nikajiuliza "Mbona sioni mazingira ambayo chakula kinaweza kupikwa, ni chakula gani hicho" Wakati nikiwa natafakari huku nikitizama huku na kule ghafla pembeni yangu alipita Baba yangu mzazi Mzee Kitali, nilihisi labda macho yangu yananidanganya nikamtizama kwa umakini kweli alikuwa ni Baba yangu "Baba baba, babaaa , ni mimi mtoto wako Kandida" 

Nilimuita kwa sauti kali sana lakini hakunigeukia wala kuzungumza chochote aliendelea na safari yake. Nilitaka kumkimbilia ili nimshike  mkono, lakini Chande alinikataza "Sikiliza nikuambie Kandida, huyo Mzee hawezi kukusikia kwani tayari amekuwa msukule kamili na tayari amekatwa ulimi hivyo hawezi kuzungumza wala hakutambui." Tena kuwa makini usije ukamgusa anaweza kukudhuru" Machozi yalinibubujika nguvu ziliniishia nikajikuta nimekaa chini huku nikijikunyata kama mtu anayehisi baridi kali nililia sana "Eeeh Mungu nisaidie nitoke eneo hili, Masikini Baba yangu yalaiti ningelijua kuwa Mama  Bilionea ni mtumwa wa Shetani, yote haya yasingenikuta mimi pamoja na familia yangu.Mateso gani haya jamani, sijui nini hatima ya maisha yangu." Je.....NINI KITAENDELEA USIKOSE ....SURA YA 16.........


Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

eeeeeh sitk kuamin mna ni mtiani mwingne huo anaupata,yani Adela ninavyopitia humu kila sekunde hacha tu,big up mamy

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom