ILIPOISHIA:
Niliondoka pale
Hospitalini huku machozi yakinibubujika kwa wingi, nilifika nyumbani nikiwa
nimechoka sana lakini Baba alikuwa bado hajarudi kutoka kazini. Baada ya muda
alirudi hali aliyokuwa nayo ilinishangaza kwani alionekana mtu mwenye
wasiwasi sana. Moyoni mwangu mimi nilichokuwa nakiwaza
ni je! Baba atakuwa amefanikiwa kupata hela kwa ajili ya matibabu ya Mama niliamua
kumuuliza “Baba umefanikiwa kupata chochote? Kwani nimetoka hospitalini kumpelekea
Mama chakula hali ya Mama….”
INAPOENDELEA
Kabla sijamalizia kuzungumza Baba alinikatisha “Usijali mwanangu
nimepata pesa za matibabu, kesho asubuhi
na mapema tutakwenda pamoja hospitalini”
Naomba uniwekee maji bafuni nikakoge,
kwani nimechoka sana” Moyoni mwangu nilijisikia
faraja, baada ya Baba kusema amepata
pesa wa ajili ya matibabu ya Mama. Nilinyanyuka haraka na kwenda kumuwekea Baba maji bafuni. Wakati Baba akiwa amekwenda
kuoga mimi niliingia jikoni nikachukua
chakula na kumuandalia mezani.
Nilikuwa najisikia amani moyoni mwangu nilijua sasa Mama yangu atafanyiwa
upasuaji, na haliyake itakuwa nzuri na mimi nitaendelea kwenda shule kama
kawaida. Kwani tokea Mama alipoanza kuumwa, na kuzidiwa ghafla, nilishindwa
kwenda shule. Kwasababu kulikuwa hakuna
mtu mwingine wa kumuhudumia. Baadaye Baba alikula chakula na alikwenda kupumzika .Usiku huo sikupata usingizi kabisa nilitamani kupambazuke ili niwahi kwenda
Hospitalini.
Nilizungumza na nafsi yangu “Mama akipona nitafurahi sana, eeh
Mungu msaidie Mama apone tunamuhitaji sana, wadogo zangu wamekuwa wakilia kila
kukicha kwasababu hawamuoni Mama, na mimi nashindwa kuwaeleza ukweli kuhusu
hali ya Mama.Naomba umsaidie Mungu wangu” Baadaye nilipitiwa na usingizi na
kulala fofofo.
Kesho yake asubuhi na mapema Baba aliamka na kuja kuniamsha tuanze
safari ya kwenda hospitalini. Niliamka
na kuanza kujiandaa, nilibandika chai jikoni na kuwawekea wadogo zangu ambapo
wakiamka wangekunywa chai kwanza na
kwenda shule.
Baada ya kumaliza shughuli mbili tatu ambazo nilikuwa nazifanya
sasa nilikuwa tayari kwa kwenda
Hospitalini. Baba alichukua mkoba wake na
tukaanza kuondoka, kabla ya kutoka mlangoni alisikika mtu akibisha hodi, huku
kukiwa na kama malumbano yanaendelea huko nje. Nilitaka kufungua mlango Baba
alinikataza na kunishika mkono kwa nguvu nisifungue mlango. “Mwanangu sikiliza
nikuambie, chukua huu mkoba ndani kuna kiasi cha shilingi milioni nne na nusu,
Shikilia kwa umakini mwanangu. Chukua taksi
nenda hospitalini utampa Daktari milioni nne kwaajili ya matibabu ya Mama yako.Kiasi cha pesa kitakachobakia kitawasaidia hapa nyumbani”.
Nilishangaa
kumuona Baba katika ile hali ya kuchanganyikiwa “Lakini Baba situnaondoka pamoja mbona sikuelewi
kuna nini?” Baba alinisisistiza na kunitaka niondoke haraka kwa mlango wa
nyuma na yeye angefika baadaye .
Niliondoka haraka na kuelekea kupanda
gari tayari kwa kuelekea hospitalini, nikiwa njiani nilijiuliza maswali mengi
sana. “Wale waliokuwa wanagonga mlango ni kina nani? Mbona Baba ameonekana kuwa na
wasiwasi mwingi. Sijui kutakuwa na matatizo gani nyumbani". Nilifika hospitalini
na kuelekea chumba (wodi ya wagonjwa)alipolazwa Mama “Kandida mwanangu” Ilikuwa ni
sauti ya upole ikiniita nilimsogelea karibu
na kumsalimia “Shikamoo Mama pole Mama nimekuja na hela utafanyiwa upasuaji
utapona usijali Mungu atakusaidia”. Mama alikuwa akitokwa na machozi bila
kuongea chochote.
Alifika muhudumu (nesi)” Hujambo binti” niligeuka na
kumsalimia “Sijambo shikamoo” Yule nesi aliniangalia huku akiwa amenikazia
macho na hata nilipomsalimia hakuniitikia “Hivi wewe kwani huoni mgonjwa amejisaidia haja
kubwa, msaidie kumbadilisha nguo chumba
chote kinatoa harufu kali sana na humu ndani kuna wagonjwa wengi”. Alizungumza yule nesi bila ya huruma, nilijisikia vibaya lakini sikumjibu chochote
nilinyanyuka na kumsogeza Mama taratibu nilimbadilisha nguo zake. Alikuwa hawezi kutoka pale kitandani
ilinibidi nichukue maji na ndoo nakuanza kumfuta kwa kitambaa nilikuwa nalia
kutokana na kumuona Mama yangu alivyokuwa anateseka” Daktari alikuwa akiwahudumia wagonjwa wengine kwa wakati huo.
Baadaye Daktari aliniita, nikaenda katika ofisi yake huku nikiwa
nimeshilikilia ule mkoba uliokuwa na pesa za matibabu kwa umakini. “Hivi wewe
mtoto si nilikuambia ukamwambie Baba yako afanye utaratibu wa pesa ili Mama
yako afanyiwe upasuaji mbona umekuja peke yako?” Aliniuliza Daktari “Baba yangu
anakuja yupo njiani, lakini pesa za matibabu amenipa nikuletee” Daktari
alicheka kidogo “ Yaani Baba yako anakupa pesa wewe! je ungevamiwa na vibaka, hajui kama ni
hatari sana” Aliendelea kuongea “Amekupa kiasi gani cha pesa”? Nilijikuta
nimepata nguvu ya kuzungumza “Daktari hizi hapa pesa zote zimekamilika kwaajili
ya matibabu ya Mama yangu, naomba umsaidie Mama apone” “Kuna karatasi ambazo
Baba yako anatakiwa kuweka sahihi kabla ya kumuingiza mgonjwa katika chumba cha
upasuaji”.
Niliwaza haraka nini cha kumjibu “Mimi nitaweka sahihi Baba
atachelewa kufika kwani kuna matatizo kidogo nyumbani” Yule Daktari
alikubaliana na mimi kutokana na hali ya Mama akaamua kumuandaa kwaajili ya
kufanywiwa upasuaji kwa siku hiyo. Baadaye ilinibidi mimi niondoke kwani nilimsubiri
kwa muda mrefu Baba bila mafanikio.
Nilipofika nyumbani
niliwakuta wadogo zangu wakiwa wamekaa nje, Renata ambaye alikuwa darasa la
tatu na Tumaini alikuwa darasa la kwanza. Waliponiona walinikimbilia huku
wanalia “Dada Kandida,, Dada Kandida Baba , baba, baba”Alikuwa akilia Renata
huku akinivuta katika gauni langu nilishindwa kuelewa Baba amepatwa na kitu
gani? “Renata Baba yuko wapi? Mnalia nini? Baba amefanyaje” Nilimuuliza mdogo
wangu wa kike “Baba amechukuliwa na watu, wamempiga Baba” Nini kinaendelea usikose ......sura ya .....4........
Maoni 5 :
hongera sana Adela unastahili pongezi uko juu story inasisimua sana
mmmmmmh jamani sijui Baba kandida kapatwa na maswaibu gani
hongera Adela simulizi ni nzuri sana . uitucheleweshee nina hamu ya kujua nini kitatokea.
hongera Adela simulizi ni nzuri sana . uitucheleweshee nina hamu ya kujua nini kitatokea.
Dah maskini usichelewe kupost basi.
Chapisha Maoni