Pages

Alhamisi, Juni 27, 2013

SIMULIZI...BADO MIMI...SURA YA.....25......... ILIPOISHIA
Aliendelea kulia ikanibidi niwe mkali kidogo ndipo alinyamaza na kwenda kuendelea kula chakula. Nilibaki nikiwaza na nafsi yangu "Inamaana huyu shetani, anataka kumfanya mdogo wangu achanganyikiwe hadi amuone mchungaji Mkombozi kuwa ni mtu mbaya, eeh Mungu naomba utusaidie". Je nini kitaendelea usikose sura ya ....25.....

INAPOENDELEA
Baadaye usiku kabla ya kulala, tulifanya maombi kwa kusali pamoja na wadogo zangu. Nilijaribu kumliwaza Renata ambaye alionekana kuwa katika wakati mgumu, kwani alikuwa akiogopa sana kulala "Renata, usiogope chochote Mungu yupo pamoja nasi, unachokiona katika ndoto ni majaribu tu ya shetani lakini kwa nguvu za Mungu yatashindwa, sasa unaweza kulala vizuri usiwe na hofu yoyote".

 Huku akiwa ananitizama alikuwa anaonekana kuwa na hofu sana, niliendelea kumbembeleza huku nikimuimbia wimbo mzuri "Mungu wetu ni mwema, Mungu wetu anatupenda, yeye atatulinda maisha yetu yote, Nampenda Mungu katika maisha yangu, yeye ananipenda atanilinda na mabaya. Sina hofu tena mimi nipo na Mungu. Nasema Mungu ni mwema, Mungu wetu anatupenda,  yeye atulinda maisha yetu yote." Wakati nikiwa naimba Renata alipitiwa na usingizi na kulala fofofo.

Kesho yake asubuhi kama kawaida nilikuwa nikiendela na shughuli zangu za kawaida niliamka mapema na kujiandaa kwenda Dukani, siku hiyo ilikuwa ni siku ya jumamosi hivyo wadogo zangu walikuwa nyumbani hawakwenda shule. Baadaye niliondoka na kuelekea dukani kwangu nikiwa kazini nilikuwa na mawazo sana "Hivi ni kitu gani ambacho kinataka kuitokea familia yangu, mbona nimekuwa na hofu sana moyoni, kwani nimekuwa nikiota ndoto za ajabu, lakini pia mdogo wangu Renata amekuwa akiota ndoto za ajabu sijui nini kinataka kutokea jamani eeh Mungu nisaidie" Nilikuwa nawaza sana, siku hiyo nilikuwa sina furaha kabisa.

Baadaye nilitoka kazini na kuelekea kanisani kwenye maombi kabla ya kwenda nyumbani. Nikiwa kanisani tulikuwa pamoja na Charito.Tulifanya maombi pamoja na baadaye alinisindikiza hadi nyumbani. Nilipofika nyumbani niliwakuta wadogo zangu wakiwa wameketi sebuleni wakitizama tamthilia iliyokuwa inaonyeshwa kwenye televisheni. "Hamjambo watoto wazuri" Aliwasalimia Charito "Hatujambo shikamoo shemeji" Ilisikika sauti ya Tumaini zaidi kuliko ya Renata iliyokuwa ikisikika kwa mbali nilimtizama na kusema "Vipi hali yako Renata,  natumaini hakuna tatizo" Renata alinitizama bila ya kuzungumza chochote.


Baadaye niliingia jikoni na kuandaa chakula cha usiku.Siku hiyo tulikula pamoja na Charito. Baada  ya kumaliza kula chakula cha usiku Charito aliondoka, nilimsindikiza hadi kwenye gari lake  huku tukiwa tunaendelea na mazungumzo "Unajuwa Kandida mimi nafikiri ni vyema tungefanya haraka kufunga ndoa, kwani nafikiri itakuwa ni vyema tukiishi pamoja" Huku tukiwa tumesimama pembezoni mwa gari la Charito nikasema "Hakuna tatizo, Charito, mimi nakusikiliza wewe,.. lakini mimi nilikuwa sitaki kwenda kuishi katika ile nyumba ya Mama Bilionea".

 Charito alinisikiliza kisha akacheka na kusema "Unaogopa nini Kandida, kwani wewe umempokea Mungu na hata na hivyo nyumba ile imebarikiwa hakuna nguvu yoyote ya giza katika nyumba ile tena. Nakusihi usiogope chochote Mungu yupo pamoja nasi" Nilimsikiliza Charito, baadaye tulielewana na kutokana na kwamba nilikuwa nikimuamini Mungu basi na mimi nilikubali  baada ya kufunga ndoa tutaishi pamoja katika ile nyumba ya Mama Bilionea.

Baada ya wiki moja  mikakati ya kufunga ndoa yangu na Charito ilizidi kupamba moto. Hatimaye zilibaki siku chache ili tufunge pingu za maisha. Siku hiyo nilikuwa nipo chumbani nikilitizama gauni langu zuri ambalo nililiandaa kwa ajili ya kulivaa siku hiyo ya harusi. Nikiwa nalitizama huku nikizungumza na nafsi yangu "Naamini siku hiyo nitapendeza sana jamani, gauni langu ni zuri sana, na pia nafurahi kuolewa na kijana ninayempenda" Nikiwa nawaza nilishtuka Renata akilivuta lile gauni "Hivi, wewe Renata una matatizo gani, unajua hii nguo yangu ni safi, halafu unaivuta na mikono yako sijui kama itakuwa ni misafi, wewe mtoto siku hizi umekuwa na kiburi sana" Renata alinitizama na kusema "Dada mimi simpendi Shemeji Charito, usiolewe naye".

 Nilimtizama Renata na kuwaza "Hivi wewe mtoto wa darasa la nne unajua nini kuhusu ndoa, kwanini haumpendi shemeji yako?" Renata huku akiwa amekunja sura mithili ya mtu mwenye hasira kali akasema " Dada Kandida, mimi simpendi shemeji sitaki tuishi naye" Nilimshika mkono Renata na kusema "Sikiliza nikuambie mdogo wangu, ni tabia mbaya kumchukia mtu bila sababu, na hata Mungu hapendi hivyo, na tena nisikusikie hata siku moja unamwambia shemeji yako kuwa humpendi, unanisikia  Renata?" . Renata alijitoa katika mikono yangu na kuondoka bila ya kunijibu chochote. Nilibaki niwaza na nafsi yangu "Hivi huyu mtoto nahisi atakuwa na mapepo jamani, mbona amekuwa na kiburi hivi, yaani  hawa watoto  bila ya kuwachapa wanakosa maadili".

Tabia ya Renata ilikuwa ikibadilika kila siku, lakini mimi sikumjali sana kwasababu nilikuwa nikimuona bado ni mtoto mdogo. Ilikuwa imebaki siku moja kesho yake ndiyo nifunge ndoa, usiku nilikuwa nimelala huku nikiwa na mawazo yaliyokuwa yameambatana na furaha na kiwewe cha kufunga ndoa. "Kesho ni siku yangu ya muhimu sana katika maisha yangu, eeh Mungu nisaidie nimalize salama, hatimaye na mimi nitakuwa Mama katika nyumba yangu na Charito". Nilikuwa nikiwaza na baadaye nilipitiwa na usingizi mzito sana. Nikiwa usingizini ilinijia ndoto ya ajabu nilimuona Baba yangu na Mama yangu, wakiwa pamoja huku wakiwa wameinama bila yakuonyesha sura zao, nilijisogeza karibu na kuita kwa nguvu "Baba, Baba, Mama ,Mama , Mamaaaa".

 Niliita kwa sauti lakini hawakuzungumza chochote ila waliinua sura zao, ambapo walionekana kutokwa na machozi ya damu katika paji la uso, huku damu nyingi zikibubujika. Nilikuwa kama nimechanganyikiwa nilianza kuwafuta  machozi yale, bila ya mafanikio kwani damu ilikuwa ni nyingi sana. Ilikuwa ni ndoto ya kutisha ghafla nilishtuka kutoka usingizini baada ya mdogo wangu Renata kuniamsha "Dada, simu yako inaita muda mrefu, umelala"Nilishtuka nakujitizama mikono yangu kama ilikuwa na damu, lakini haikuwa na damu yoyote "Mungu wangu hii ni ndoto mbaya sana" Nilikuwa na hofu kubwa huku jasho likinitoka kwa wingi ilikuwa tayari ni majira ya saa moja asubuhi" JE NINI KITAENDELEA....USIKOSE SURA YA.......26.........

 

Maoni 5 :

Bila jina alisema ...

hili nalo libishi linaniboa badala yakumsikiliza mdgo wake,muhache yakamkute kaniboa

emu-three alisema ...

Duh, natamani iendelee tupo pamoja mpendwa, usinichoke kwa kupiga hodi kwako mara kwa mara, ukijaliwa karibu na kwangu

toto ya Jak alisema ...

Jaman Renatha....cjui ndo shetani

Bila jina alisema ...

Renata kaoneshwa tabia za Charito ambazo wewe huzijui. Endelea kumbishia na kumuona mtoto yatakukuta makubwa na utakosa wa kumlilia. Achana na charito c mtu mzuri

Adela Dally Kavishe alisema ...

PAMOJA SANA WADAU

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

share bottom